Featured Post

UTETEZI ENDELEVU WA WANYONGE HULETA TIJA



NA MWANDISHI WETU
“Utajiri wa Tanganyika, bado uko ardhini. Hatuanzi na akiba kubwa ya fedha kama Ghana kwa mfano, iliyoanza nayo ilipopata uhuru wake. Hatuna mkononi fedha walizonazo ndugu zetu wa Nigeria...”
Hiyo ni kauli ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika hotuba ya kwanza mara tu baada ya kuwa Waziri Mkuu baada ya chama cha TANU kupewa ridhaa ya kuunda Baraza la Kwanza la Mawaziri wa Serikali ya Tanganyika mwaka 1961.

Katika hotuba hiyo kimsingi alikuwa anamaanisha kuwa maendeleo ya Watanganyika yatapatikana kwa kutumia rasilimali zilizomo kwenye ardhi na si vinginevyo na kwa kutumiwa kwa busara kwa kuwa jamii kwa jumla ilikuwa maskini.
Katika mazingira hayo, Nyerere alimaanisha kuwa rasilimali ambayo jamii ya Watanganyika inatakiwa kuitumia  kuendesha maisha yao ni ardhi pamoja na rasilimali zilizomo ndani yake.
Upo usemi wa Kiswahili unaosema ‘Ukiona zinduna na ambari yupo nyuma’ tafsiri yake kwa kulinganisha na kauli hiyo ya Baba wa Taifa  ni kwamba haikupita  au haikuwa na ukomo  bali imekuwa na mwendelezo wake kwa kuwepo watu wengine  wenye mawazo kama hayo kama sio wanairithi na kuziongezea mashiko.
Hivyo linapozungumzwa neno rasilimali ni pamoja na ardhi. Hii ni pamoja na mali zilizopo ndani ya ardhi ikiwa ni pamoja na madini. 
Katika mazingira hayo Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Idara ya Sayansi ya Siasa, Dkt. Bashiru Ally  ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliwahi kusema kuwa ardhi inapoporwa na watu wachache ni kupora uhai wa wananchi.
Akizungumza katika mdahalo wa Katiba uliowakutanisha wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu jijini Dar es Salaam hivi karibuni alibainisha kuwa katika mazingira ya hivi sasa kuhusu rasilimali za nchi umekuwepo mpambano kati ya wavuna jasho na wavuja jasho.
Akaongeza kuwa katika mazingira hayo wanyonge wanaoporwa ardhi wakati wao ni tabaka linaloitegemea ardhi kama uhai wa taifa ambao ni wanyonge wa kiuchumi na kisiasa wakiwemo wahunzi, wavuvi, wafugaji, wakulima, wawindaji, warina asali, wakwezi na wasusi ni kuupora uhai wao.
Alisema kuwa katika mwenendo mzima wa kuchukua ardhi kwa ajili ya wawekezaji ni kuwapora maskini uhai wao, kwani ardhi ndio mtaji wao lakini kwa bahati mbaya uwekezaji mwingi umekuwa unalenga  maslahi ya wawekezaji wenyewe badala ya  maslahi ya wanyonge.
Kutokana na hali hiyo, Dkt. Bashiru alisema ipo haja ya kuwepo ulinzi wa kulinda na kuendeleza mapambano dhidi ya utambulisho na uhai wa wanyonge kwani mtaji wa maskini ni ardhi yao.
Aidha, aliongeza kuwa ili kufanikisha hilo ni lazima iwepo Katiba itakayokidhi mahitaji ya Watanzania na hususani wanyonge, katiba itakayojumuisha suala la rasilimali za nchi na hususan ardhi.
Jambo la kutafakari na kuchukua hatua hapa ni kurejea kauli ya Baba wa Taifa ya mwaka 1958 na ambayo ipo kwenye Kitabu chake cha Uhuru na Umoja aliposema, “Katika nchi kama yetu, ambamo Waafrika ni masikini na wageni ni matajiri, kuna uwezekano mkubwa kwamba Mwafrika akiruhusiwa kuiuza ardhi yake katika miaka 80 au 100 ijayo, ardhi yote ya Tanganyika itamilikiwa na matajiri wageni na wenyeji watakuwa watwana.
“Lakini hata kama wageni wasingekuwa matajiri, litaibuka tabaka la Watanganyika matajiri na wajanja. Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana.”
Uendelevu wa kauli ya Mwalimu Nyerere nao unaibukia katika kauli ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli  Septemba mwaka jana mkoani Manyara aliposema, “Nchi hii ni tajiri na historia inazungumza wazi, tukapewa madini ambayo hayapo pengine kokote duniani, tujiulize haya madini yanatusaidia?
“Mungu ametupa madini lakini tunapata shida ndio maana nimefika hapa ila mtu analilia shida, Tanzanite tunayo lakini tunaitumiaje? Tulimkosea nini Mungu? Hilo ndiyo somo langu la leo.”
Alibainisha kuwa kuna uporaji wa rasilimali aliposema, “Tanzania matatizo yetu sio vyama, matatizo yetu ni kwanini tunaibiwa? Wangepewa nchi nyingine, hapa pangekuwa kama Ulaya.”
Ripoti ya Tanzanite iliyoundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Job Ndugai,  ilionesha kuwa rasilimali hiyo haiinufaishi Tanzania ambapo Rais aliongeza,  “Haiwanufaishi hata wananchi wa hapa, pia haiwanufaishi Watanzania. Tanzania inapata asilimia tano, ndio maana nasema tuna changamoto.
“Katika uongozi wangu nimeamua kuongoza hii vita, naomba tusimame pamoja kushinda hii vita. Tanzanite ina eneo la kilometa za mraba 81.99, kuna block (vitalu) zimegawanywa. Tanzanite zinaibwa sana, ni shamba la bibi, nafikiri mabibi waliokufa miaka mingi sana.
“Kuna wawekezaji ambao wana asilimia 50 lakini mali zinasombwa. Nimeamua lile eneo ili tuzuie wizi, block A mpaka D, naagiza JWTZ waanze kulijenga ukuta eneo lote, kazi ifanyike haraka. Wakimaliza wake fence (ukuta) na kamera, kutakuwa na mlango mmoja. Hata kama utameza Tanzanite itaonekana.
Serikali ipate pesa yake na mchimbaji apate pesa yake, tunataka soko la Tanzanite liwe hapa Simanjiro na wala sio Arusha. Wanunuzi wote waje kununua hapa Simanjiro...”
Akaongeza, "Nimeona tuanze na hii hatua, nina hakika watu wa Tanzanite One na wengine watakaa na kutengeneza mkataba wenye faida kwa serikali. Ni lazima tujipange vizuri, hili suala naona sasa linafika mwisho wake.”
Alibainisha kuwa biashara haijazuiliwa lakini inatolewa kwenye biashara ya magendo kuwa biashara halali na kuongeza, “Tuna madini kila mahali lakini majamaa wamekuwa wakisomba tu, tunaendelea kubaki maskini.”
Dhana kuu ya msingi hapa ni kwamba maendeleo ya nchi yoyote ile yanatokana na kiwango cha rasilimali zilizopo ndani yake na jinsi inavyotumia rasilimali hizo kwa ufanisi katika kuboresha maisha ya wananchi wake.


Comments