Featured Post

UKOSEFU WA AJIRA UNAJUMUISHA NINI?


NA ALOYCE NDELEIO
MKAKATI kabambe unaofanywa na Serikali hivi sasa ni kupambana na suala la ukosefu wa ajira na kwa hali hiyo katika shughuli zake za kukuza uchumi imeshaanza kutoa fursa za ajira kupitia shughuli inazozianzisha.
Zipo sekta kadhaa ambazo tayari zimeshatangaza fursa hizo za ajira na hivyo kuleta matumaini kwamba ukosefu wa ajira utapungua  kwani hilo ni ashirio la kwamba uchumi unakua.

Hata hivyo ukosefu wa ajira unajumuisha  mambo kadhaa ambayo mara nyingi yamekuwa hayafahamiki kwa baadhi ya wanajamii.
Ukosefu wa ajira kwa kiwango kikubwa unategemea shughuli za kiuchumi. Ukweli ni kwamba kukua kwa uchumi na ukosefu wa ajira kunaweza kuonekana kama pande mbili za sarafu.
Wakati shughuli za uchumi zikiwa juu, uzalishaji unakuwepo kwa ujumla na watu wengi wanahitaji kuzalisha kiwango kikubwa cha bidhaa na huduma.
Pindi shughuli za uchumi zinapokuwa chini, mashirika yanapunguza wafanyakazi na papo hapo ukosefu wa ajira unakuwa umeongezeka.
Katika mantiki hiyo ni kwamba ukosefu wa ajira unakuwa kwenye mzunguko ikimaanisha kuwa unaoongezeka wakati hali ya uchumi ikiwa chini na hupungua (nafasi za ajira zinakuwepo) pindi uchumi unapokua.
Lakini ukosefu wa ajira  huwa haupungui kufikia ukomo kutokana na kukua kwa uchumi. Huwa ni hali ya kawaida kwa biashara kujaribu kwanza kuziba pengo  kutoka kwenye kuanguka  kwa kuwa na idadi sawa ya wajiriwa kwa ajili ya kufanya kazi nyingi zaidi au kuzalisha bidhaa zaidi ikiwa ni njia ya kuongeza  tija.
Pindi tu  kuziba mwanya huko kunafanyika ndani ya biashara ndipo  wafanyakazi huongezeka. Matokeo yake ni kuwa  ukosefu wa ajira  unaweza kuanza kupungua mara tu uchumi unapoanza kuwa  na ahueni.
Hali hiyo huwa inafanya kazi kinyume pindi uchumi unapoanza kushuka wakati  mashirika au kampuni zinapoanza kupunguza saa za kazi au kupunguza matumizi ya fedha kabla ya wafanyakazi kuondoka.
Ukosefu wa ajira unaanza kuongezeka iwapo tu kupungua kwake hakutadumu kwa muda mrefu. Kwa kuwa kukosekana kwa ajira hutokana na kuchelewa kukua kwa uchumi, hali hiyo hujulikana kama kiashiria cha kuchelewa kwa shughuli za uchumi.
Ni kwa kiasi gani  kiwango cha ukosefu wa ajira ni nyeti kwenye kukua kwa uchumi? Hili linategemea vigezo kadhaa na ambavyo ni muhimu ikiwa ni mazingira ya soko la kazi na usimamizi wake.

Kazi na kukua kwa uchumi
Ni kwa kiasi gani  uhusiano kati ya kukua kwa uchumi na ukosefu ajira unatofautiana? Kama uchumi utakuwa unaendelea kukua je, yawepo matarajio ya kuona ukosefu wa ajira ukitoweka?
Kimsingi hali hiyo haiwezi kuwa hivyo, hata kwenye miaka ya 2000 wakati uchumi wa dunia ukiwa unastawi (hadi kipindi cha mtikisiko wa uchumi ya 2008-09), ukosefu wa ajira duniani ulikuwa umepungua lakini haukufikia kiwango cha ukomo au kufutika kabisa.
Mtazamo huo ulisababisha kuibuka kwa swali la msingi; Je, ukosefu wa ajira  haujawahi kushuka hadi kwenye kiwango cha ukomo (sifuri) au kutoweka kabisa? Jibu linabakia kuwa ni hapana.

Kusafisha soko
Kwa mujibu wa  nadharia za taaluma ya uchumi  kila soko likiwemo soko la kazi au ajira ni lazima liwe na kipindi ambacho kinatakiwa kujisafisha ambapo uhitaji na ugavi unatakiwa kuwa sawa.
Hata hivyo, kuwepo kwa ukosefu wa ajira kunaonesha kwamba masoko ya kazi au ajira duniani kote mahitaji na ugavi unashindwa kufikia kwenye  usawa. Hoja inayoibuka ni kwamba je, masoko ya ajira yataendelea kushindwa?
Mara nyingine huwa ni suala ujira, au kipimo cha kazi siyo kurekebisha usafishaji wa soko. Baadhi ya wafanyakazi, hususani walio na stadi  wanaweza kuwa na viwango vyao vya ujira ambapo chini ya kiwango hicho huwa  hawako tayari kufanya kazi lakini kikiwa ni cha juu kuliko ambacho mwajiri anakadiria mwajiri mwenyewe anakuwa hayuko radhi kulipa.
Kwa upande mwingine ujira ambao mwajiri anakuwa radhi kuulipa  unaweza kuwa wa chini kuliko kima cha chini  kilichowekwa na Serikali  katika kujaribu kuhakikisha kwamba ujira  huo unaweza kuendeleza maisha.
Pindi hali ya kutobadilika kwenye soko la ajira kunaposababisha uhaba wa ajira  hali hiyo hujulikana kuwa ni muundo wa ukosefu wa ajira na wale ambao  kimuundo huwa hawana ajira  hujikuta wakiwa  kwenye lindi la kukosa kazi.
Lakini  kutobadilika kwa  ujira hakuelezei  kwa jumla  uasilia mama wa kukosekana kwa ajira. Baadhi ya kiwango cha ukosefu wa ajira utakuwa unaendelea kuwepo kila siku na hakuna sababu nyingine kila mara kutakuwepo na baadhi ya watu  ambao wako kati ya kazi au wakiwa ndio kwanza wanaanza kutekeleza majukumu yao.
Watu hawa hawana ajira siyo tu kwa sababu kuna uhaba wa ajira kwenye  soko, lakini ni kwa sababu kutafuta ajira kunachukua muda. Hali hiyo ambayo ni ya ukosefu wa ajira inajulikana kama mgongano wa ukosefu wa ajira.

Kupima ukosefu wa ajira
Aidha, siyo watu wote  ambao hawafanyi kazi hawana ajira. Ili kuchukuliwa kwenye takwimu za Serikali za wasio na ajira siyo lazima tu mtu kuwa ameondoka kazini lakini pia awe anatafuta kazi kwa mfano kutuma tena  maombi ya kazi.
Nguvukazi inajumuisha watu walio kazini na wale wanaotafuta kazi. Kiwango cha ukosefu wa ajira ni asilimia ya nguvukazi  inayotafuta kazi. Nguvukazi ni sehemu tu idadi yote ya watu. Uwiano wa nguvukazi dhidi ya umri wa idadi ya watu wanaofanya kazi hujulikana ni kiwango cha ushirikishwaji wa nguvukazi.
Nguvukazi haijumuishi watu walio na umri wa kufanya kazi lakini wanakuwa ama wameajiriwa au wanatafuta kazi  kama vile wanafunzi na waangalizi wa majumbani.
Lakini nguvukazi  pia haijumuishi watu wasio na kazi  ambao wamekuwa kwenye  soko la ajira kwa muda mrefu bila mafanikio  hivyo kwamba walishaacha kutafuta kazi.
Watu hao ambao walishakata tamaa ni sababu mojawapo ya takwimu za ukosefu wa ajira kukadiria isivyo mahitaji ya kweli ya ajira kwenye uchumi.
Aina nyingine ya ukosefu wa ajira uliojificha kwenye takwimu inatoka kwenye kuhesabu mtu asiye na ajira ambaye anafanya kazi yoyote ile kwa malipo au kwa faida kama amejiajiri mwenyewe ndani ya wiki kabla  ya utafiti wa Serikali.
Hali hiyo huficha mahitaji ya wazi kwa watu ambao wanapendelea ajira ya kudumu lakini wanafanya kazi kwa saa chache kwa sababu tu hawawezi kupata ajira za kudumu.
Hata hivyo, haya yote yanajitokeza hivi sasa kwamba upo ukosefu mkubwa wa ajira unatokana na jambo moja tu la msingi kwamba kulikuwepo hujuma katika sekta ya viwanda kutokana na waliovinunua kubadilisha matumizi.
Aina hiyo ya uhujumu uchumi inaweza kueleweka katika mazingira ya kawaida ya kuelezea sababu za ukosefu wa ajira, kwani hujuma hiyo iliwaathiri wazi wazi.

Comments