Featured Post

TUKISUJUDIA 'MADILI' TUTAKWENDA KOMBO

Vijana wakishiriki shughuli za kilimo katika kujenga uchumi wa taifa. 


NA ALOYCE NDELEIO
Hivi sasa ni dhahiri kwamba ujenzi wa matabaka umekuwa unamea kwa kasi jambo ambalo limekuwa linawadhoofisha walala hoi na kuwaneemesha wachache kimsingi wakiwa ni wale waliobahatika kuzifikia nyenzo za kuvuna kisicho halali.
Ambao wamekuwa na bahati ya kuzifikia nyenzo hizo ni pamoja na wasomi ambao hivi sasa wamekuwa wanaziacha taaluma zao na kujikita kwenye  masuala ya siasa ambayo yameonekana kuwa ni jiwe rahisi kukanyaga na kuchupia kwenye ulingo huo.

Hawa wameshasahau kauli ambayo iliwahi kutolewa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyoisema miaka mingi kuhusu wale waliobahatika kupata elimu.
Alisema, “Wale wenye bahati ya kupata elimu, wanao wajibu wa kulipa jasho ambalo wengine wamelitolea. Ni sawa na mtu aliyepewa chakula chote katika kijiji chenye njaa, ili apate nguvu za kwenda kuhemea katika sehemu zilizo mbali. Mtu huyu akikipokea chakula hicho, na halafu asiwaletee msaada ndugu zake, basi yeye ni msaliti.”  
Maneno ya msisitizo hapo yapo wazi ‘kulipa jasho ambalo wengine wamelitolea’. Lakini taswira iliyopo hivi sasa badala ya kulipa jasho imekuwa ni kuendelea kuvuna jasho na kwa maana hiyo ‘basi ni wasaliti’.
Mwalimu alikuwa anawalenga wasomi na hususani vijana  kuhusu wajibu wao kwa jamii  na aliwahi kueleza aina ya vijana aliokuwa anataka kuona  kwamba ni “Vijana jeuri na wenye kujiamini; siyo vijana akina ndiyo Bwana … Vijana wenye ujasiri wa kuhoji mfumo wa jamii usioshabihiana na matakwa na matarajio ya jamii.”
Kwa kuwa vijana aliwaona kuwa ndio nguvu kazi ya taifa aliwahi kusema kuwa itakuwa ni kazi bure na ni ubatili mtupu kuwa na taifa lenye silaha kwa maana nyenzo za maendeleo za kisasa lakini vijana wake ni waoga.
Kimsingi nyenzo za maendeleo alizomaanisha ni zile alizobainisha kuwa ili taifa liendelee linahitaji mambo matatu; ardhi na watu, siasa safi na uongozi bora.
 Ukweli unabakia kuwa ardhi ndio mama wa rasilimali zote zilizopo juu ya ardhi ikiwa ni ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo na rasilimali ya misitu, mito na maziwa na hata hivyo zipo nyingine chini ya ardhi haya ndio madini ya kila aina kuanzia almasi, dhahabu, makaa ya mawe, vito kama Tanzanite na aina nyingine nyingi.
Hata hivyo, hili la uongozi bora ndilo linalohitajika zaidi ili kuzisimamia rasilimali zilizopo chini na juu ya ardhi na hali kadhalika kuwa dira ya watu wanaoliunda taifa ili kuharakisha kasi ya maendeleo.
Leo hii baadhi ya vijana wanapohoji umuhimu wa kupata elimu na kuitumia elimu hiyo kwa manufaa ya umma wamekuwa wanaelezwa kuwa ni makuwadi wa wanasiasa wanaopingana na mfumo unaoongoza.
Hali kadhalika akitokea anayeuliza ni kwa jinsi gani jamii imenufaika na rasilimali za madini kutokana na uwekezaji, ni mara chache huelezwa kwa uwazi  na mara nyingine huoneshwa visima vichache vya maji na vyumba vichache vya madarasa ya shule iwe ya msingi au sekondari bila kusahau matundu ya vyoo ikiwa ni ujenzi uliofanywa na wawekezaji kwenye maeneo yanayozunguka migodi.
Linaloshangaza ni zinapotolewa taarifa kwamba kampuni hizo za uwekezaji zinafunga migodi na kuziachia jamii mashimo kama sio mahandaki matupu baada ya kukomba dhahabu yote ilhali mirabaha iliyotolewa kwa serikali ikiwa ni kiduchu. Hapo ndipo mwili unachoka na maungo yanalegea.
Inaweza ikatokea kuhoji na hata kueleza kuwa uwekezaji  unaoendelea kuna mahali umekosa umakini, ni uwekezaji unaotoa taswira kuwa ni usiojali mipaka na umejaa taswira ya uporaji wa rasilimali za taifa na kwamba wapo makuwadi wa utekelezaji huo lakini kitakachotokea ni kwamba wanaohoji hivyo wanaweza kuambiwa kuwa ni wavivu wa kufikiri.
Kuna kipindi ambacho wabunge waliothamini maadili badala ya madili walikuwa wanatetea maslahi ya wanyonge kuliko hata maslahi yao na waliweka wazi mapato yao. Hapa ndipo palipokuwa panaonekana kuwepo kwa siasa safi na uongozi bora.
Leo hii hakuna kiongozi anayekubali kuweka bayana mali zake kutokana na hofu kuwa zitaibuka hoja ni  namna gani alizipata. Hali kadhalika hakuna anayetaka mshahara wake ujulikane. Ndio maana hivi karibuni zimeibuka hoja zinazotaka kufahamu mishahara ya viongozi labda dhamira ya hoja hiyo ni kuona kama inalingana na pato la nchi.
Hoja hapa ni kwamba kuna ubaya gani kuufahamu? Hapa ndipo inaibuka kauli moja ya Mwalimu Nyerere  aliposema na kuweka wazi mshahara wake akisema, “Mnayosema juu ya mishahara ni ya kweli, ni mikubwa mno, mimi na ninyi tumo katika kundi la wanyonyaji. Je, hayo ndiyo mambo nchi hii iliyopigania? Je, juhudi yote tuliyofanya ni kwa sababu ya kuneemesha kikundi cha wanyonyaji huku juu?   
“Mshahara wangu mnajua ni kiasi gani? Shilingi elfu tano kwa mwezi; ni mkubwa mno… Mshahara wangu naupunguza kwa asilimia 20 kuanzia sasa hivi … Nchi hii ya hovyo; mishahara minene mno.”
Kwa kauli hiyo ya Baba wa Taifa aliyoitoa kabla ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha alikuwa amebainisha kuwepo kwa tabaka la walala hoi na walala hai na hivyo kuwepo kwa pengo lililotakiwa kuzibwa.
Ukweli ni kwamba alijaribu kuliziba kwa kutumia maadili ya uongozi na ndio maana aliwahi kulalamika kuwa hata yale mema aliyokuwa ameyaanzisha yalikuwa nayo yametupwa ikiwemo miiko ya uongozi.
Kilichofanya hali hiyo kutokea na kuzikwa kwa maadili hayo ni kuongezeka kwa kasi ya kufufua upigaji dili na hivyo kuongeza kasi ya rushwa, wizi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya madaraka au ofisi za umma, ulafi wa kupindukia, uchoyo, tamaa, kuhodhi kila kitu kinachoonekana machoni na kila aina ya uoza ambao haukuwa kwa maslahi ya taifa.
Hoja inayojitokeza hapa ni kwanini  inakuwa vigumu leo hii kwa wazito kutaja mishahara yao? Ni kwanini leo hii hakuna anayetaja mali alizonazo na kwamba alizipata vipi au kwa njia gani?
Hali kadhalika ni kwanini wazito waziache benki zetu na kuenda kuficha fedha kwenye benki walizoona ni za ‘watu wenye akili’? Je, benki zetu kwa ajili ya makapuku? Sio ajabu kwamba hilo ndilo lilifanya sarafu ya nchi hii kuitwa hela ya madafu.
Kama dhima iliyokuwa imejengwa chini ya maadili ilikuwa ni ya kuwakomboa walala hoi, kuzikwa kwa dhima hiyo nzuri kumewezesha kufufua dhima mpya ya ‘madili’ ambayo itatonesha makovu ya mateso ya unyonywaji, ukandamizaji na kushamirisha hali yao ya kuchumia tumbo pamoja na wategemezi wao. Hawa kila kunapokucha huona afadhali ya jana.
Katika misingi hiyo ina maana kuwa kuna haja ya kubadili mwelekeo kwa kuzingatia hoja ya Rais wa Kwanza wa Ghana Hayati Kwame Nkrumah kwamba kuendelea kukua kwa tabaka la walala hoi kunakuza tabaka la ‘declasse’ ambalo alisema linajumuisha aina yote ile ya wachovu na hata  wale waliokosa maadili ndani ya jamii wakiwemo machangudoa  na kwa hivi sasa linaweza pia kujumuisha mateja.
Lakini akaonya tabaka hilo ni hatari likiendelea kukua kwani ndilo hutumika kuleta mabadiliko ya lazima ndani ya jamii ikiwa ni mikakati ya wao kutaka kuionja na kuifurahia keki ya taifa kama ilivyo kwa wavuna jasho.
Muhimu ni kuamua kuendelea kuyazika maadili na kukumbatia madili au kukumbatia maadili na kutokomeza madili. Hili kwa jinsi hali ilivyo linahitaji maamuzi magumu ili kurejea kwenye mkondo mnyoofu. Je, walala hai watakubali kufanya tafakuri ya jambo hilo?
Jibu la hoja hiyo hivi sasa linaweza kuelezwa kuwa limeshaanza kutoa mwangwi kutokana na utendaji uliopo ambao umekuwa unaangazia maslahi ya umma wote na hata kutoboa maficho ya rasilimali ambako kumefanywa kwa kipindi kirefu na wapiga madili.
Aidha ni katika kipindi hiki inajidhihirisha kuwa wale waliokuwa wanasujudia madili walikuwa wanataka kuipeleka nchi kombo na kinachowakera ni mwangwi wa kusujudia maadili unavyojipenyeza kwa kasi.
CHANZO: TANZANITE

Comments