- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
YEHU mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi
alikuwa miongoni mwa wafalme wa Israel na alitawala baada ya Ahabu katika
Samaria.
Kabla ya kuwa mfalme, yeye ndiye aliyekuwa
jemedari wa jeshi la Israel.
Katika kipindi hicho wafalme waliotangulia
walikuwa wamemuasi Bwana, Mungu wao ambaye aliwakomboa kutoka utumwani Misri,
wakaabudu miungu ya kigeni ambayo Mungu, kwa kinywa cha Nabii Musa,
aliwakataza.
Siku alipoingia tu madarakani, Yehu akaamua
kuuondoa uovu wote ndani ya Israel ambao ulikuwa umemkasirisha Mungu na kulitia
taifa hilo mikononi mwa adui zake.
Aliwafyeka manabii wote wa Baali na Ashera,
miungu ya kigeni iliyokuwa ikiabudiwa, na akawaua manabii na wale wote
waliokuwa wakimwinamia na kumtolea sadaka Baali. Baada ya hapo Mungu akaibariki
Israel tena.
Naam. Hiyo ilikuwa ni miaka mingi nyuma, na
Yehu alitekeleza maagizo ambayo Bwana, Mungu wa Israel alikuwa ameagiza, siyo
kwa makusudi yake.
Leo hii dunia inaendeshwa kwa utawala wa
sheria, wala hawezi kutokea mtawala yeyote akawafyeka watu wake, hata wakosefu,
kwa upanga, bali atawabana kwa sheria zile zilizowekwa.
Tanzania ni taifa ambalo kwa kipindi kirefu
sasa wananchi wake wamekuwa wakiilalamikia serikali yao kwa matendo mengi maovu,
ukiwemo ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Wananchi wanaishi maisha duni wakati
viongozi wenye dhamana wakijilimbikizia mali za umma kwa kutumia nyadhifa zao,
kero ambazo zimesababisha Chama cha Mapinduzi kipate wakati mgumu katika
uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inafafanua vyema kuhusu maadili na miiko ya uongozi, lakini kwa makusudi kabisa
viongozi wetu wamekuwa kama wanaomwinamia Baali na kumtolea sadaka za
kuteketezwa.
Wameiacha hata misingi imara iliyosimika
taifa hili na kuleta heshima, kwa sababu ingawa tuko kwenye mfumo wa vyama
vingi, lakini sidhani kama zile ahadi 10 za mwana Tanu, chama kilichoikomboa
nchi yetu kutoka kwenye makucha ya wakoloni, eti zinaweza zisiwe na maana.
Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni
moja; Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote; Nitajitolea nafsi yangu
kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma; Rushwa ni adui wa haki.
Sitapokea wala kutoa rushwa; Cheo ni dhamana. Sitakitumia cheo changu wala cha
mtu mwingine kwa faida yangu; Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na
kutumia elimu yangu kwa faida ya wote; Nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga
nchi yetu; Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko; Nitakuwa mwanachama
mwaminifu wa Tanu na raia mwema wa Tanganyika na Afrika; na Nitakuwa mtiifu na
mwaminifu kwa Rais wa Serikali ya Tanganyika ndizo ahadi yakini za mwana Tanu
ambazo kipindi kile cha awamu ya kwanza zilijenga nidhamu na kudumisha
uzalendo.
Kwa tafsiri nyingine, ahadi hizi ni kiapo,
na kwenda kinyume chake ni sawa na kuifuata miungu ya kigeni kama walivyofanya
Waisraeli kabla Yehu hajatwaa ufalme mikononi mwa Ahabu na mkewe Yezebeli.
Taifa lilikuwa linaelekea kubaya na
haikushangaza hata baadhi ya watu, kabla ya kumwelewa Dk. Magufuli wakati wa
kampeni, walitamani eti ‘hata kama wangewekewa mbuzi wangeweza kumchagua,
lakini siyo CCM’ ambayo watendaji wachache walikuwa wamekiuka misingi yake.
Kutokana na hali hiyo, Watanzania
walihitaji mabadiliko, na zaidi mtu ambaye angeweza kuleta mabadiliko hayo kwa
kuvaa uso wa Yehu na kuwakamata manabii wote wa Baali ili awakatilie mbali.
Rais Dk. John Magufuli ameingia kwa kasi
kama alivyofanya Yehu, mwana wa Yehoshafati, zamani zile, lakini yeye hatumii
upanga kwa watu ambao wamekwenda kinyume na sheria za nchi na kukiuka maadili
na miiko ya uongozi.
Kitendo cha kuwafurumusha vigogo takriban
100 ndani ya siku 50 tu alizokaa Ikulu kinadhihirisha kwamba Dk. Magufuli siyo
tu amekuja kulikomboa taifa hili kutoka katika makucha ya mafisadi wachache,
bali pia amerudisha imani kwa wananchi kwamba anaweza kusimamia sera za CCM
ambazo zilibaki kwenye makaratasi tu.
Kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu!’
imesaidia kurudisha heshima ya kazi kwa sababu huko nyuma watumishi wa umma
walikuwa wakifanya kazi kwa mazowea bila kujali wanazalisha nini almuradi tu
wanapata mishahara yao.
Mwalimu Julius Nyerere alipata kusema: "...Binadamu hao unaotuona hapa, na hao waliosambaa
dunia nzima wanaishi kwa kazi. Hawana namna nyingine ya kuishi. Wakiacha
kufanya kazi watakufa; hawana namna nyingine; kuishi kwao, na kuendelea kuishi,
lazima wafanye kazi... Lakini binadamu haishi kama farasi. Binadamu haridhiki
kuishi kama farasi au punda; binadamu ana kitu anakiita maendeleo; lazima
aendelee... Wakati mwingine ili kusudi maendeleo haya yaje wana shughuli za
kupigana misasa akili, wanapanuana mawazo tu, nayo ni kazi... nendeni
mkaulizane... kama kazi si kitu cha lazima, kama binadamu anaweza kujikalia tu
hafanyi kazi, akaishi, na maendeleo yakaja bila kazi. Na huyo anayepinga ujamaa
naye ajiulize kama hilo analipinga? Na hilo la kufanya kazi analipinga au kuna
jingine analopinga?"
Wakati wa kampeni Dk. Magufuli aliahidi
kutowafumbia macho mafisadi na wala rushwa, huku akiahidi kuanzisha mahakama
maalum ya kuwashughukilia ‘majizi’ wote.
Suala la kupambana na ufisadi halihitaji
sera wa ilani ya chama, bali uwezo wa kiongozi katika kutoa uamuzi wenye
kuzingatia utawala bora na maadili ya uongozi, ambayo yamemomonyoka kwa kiasi
kikubwa.
“Nawaombeni mnichague kwa sababu mimi ni
maji moto, nipeni urais muone nitakavyowaunguza mafisadi,” alisikika akisema
kwenye kampeni zake. Tayari amekwishawaunguza na kuwababua mafisadi ndani ya
serikali na kasi yake bado inaendelea.
Watanzania walikuwa wanahitaji mabadiliko,
lakini Dk. Magufuli kwa kipindi kifupi amedhihirisha siyo tu mabadiliko, bali
hata maendeleo ya kweli yatapatikana.
Alisema wakati wa kampeni: “Natambua kuwa
Watanzania mnataka maisha mazuri, naahidi kukomesha wizi na rushwa haraka kwa
sababu palipo na rushwa hakuna maendeleo. Haiwezekani mwananchi anaumwa,
anapokwenda hospitali anaambiwa akanunue dawa kwenye duka binafsi lililo jirani
na hospitali… kwa nini duka binafsi liwe na dawa na hospitali ikose dawa, nimejiandaa
kulishughulikia hilo.”
Leo hii anapowabana hao mafisadi na
viongozi wazembe na wabadhilifu, ni dhahiri wapo watu wanaochukia kwa sababu
wananyang’anywa tonge mdomoni.
Kupambana na mafisadi wakubwa siyo jambo
dogo, ndiyo maana hata viongozi wa dini wamesikika wakisema ni lazima Rais
Magufuli aombewe ulinzi – kwa Mungu, kwa sababu kazi anayoifanya ‘imebarikiwa’.
Lakini kwa nini tusubiri mpaka tufuatwe na
‘Yehu’ ndipo tutimize wajibu wetu? Kwa nini tusubiri kuadhiriwa eti tunamwabudu
Baali na Ashera?
Ninaamini kwamba, kila mtu akichapa kazi na
kuzingatia maadili na miiko ya viongozi, tutalijenga taifa letu kuwa lenye
nidhamu ya juu na tutakuwa tumemsaidia Dk. Magufuli.
Kwa kufanya hivyo pia tutaimarisha uzalendo
hata kwa vizazi vyetu, maana Mungu humlaani mtu hata kizazi chake cha nne,
vivyo humbariki mtu hata kizazi chake cha nne!
Wasalaam!
0656-331974
Comments
Post a Comment