Featured Post

TUJIVUNIE FAHARI NA SIYO UZUZU MAMA WA UJINGA



NA ALOYCE NDELEIO
USEMI ambao umekuwa ukitumika kwa siku nyingi ni kwamba Tanzania bado ni nchi changa licha ya kupata uhuru miaka zaidi ya 50 iliyopita.
Lakini uchanga huo umekuwa endelevu mno kiasi kwamba unahitaji lugha au tafsiri nyingine kwamba kushindwa kwake kupiga hatua za maendeleo ni kukwamishwa kukua na hivyo tafsiri sahihi ni kudumaa kwa kipindi chote hicho.

Ili kuikubali tafsiri hiyo kunahitajika marejeo ya kihistoria ili kubaini kilichosababisha udumavu huo.
Ni katika muktadha huo Mwanafalsafa George Santayana aliwahi kuandika “Wale ambao hawawezi kukumbuka walikotoka ni rahisi kwao kurudia makosa.”
Tafsiri yake ni kwamba, wale ambao hawawezi kujifunza kutokana na makosa yaliyotokea mbele ya macho yao hudumaa kwani hubakia na fikra mgando.
Katika kuirejea historia ni kwamba Tanzania ni taifa ambalo katika miaka ya 1960 mpaka miaka ya 1990 lilikuwa likiheshimika sana barani Afrika na ulimwenguni kutokana msingi uliokuwa umewekwa na utawala wa awamu ya kwanza wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Lakini wapo wanaoiona Tanzania katika taswira nyingine kuanzia miaka ya 1990 kipindi ambacho heshima ya Tanzania ilianza kuporomoka.
Wapo waliobahatika kusafiri nje ya nchi na wanasema kufikia miaka ya 2000 mpaka hivi karibuni Tanzania lilikuwa ni taifa lenye kudharauliwa kabisa.
Ilifikia hatua hata ukiwa safarini nje ya nchi unajikuta unajutia kuitwa Mtanzania au kuwa na hati ya kusafiri ya Tanzania. Utapekuliwa sana kuliko raia wa mataifa mengine kwa kuhisiwa kuwa unaweza kuwa na  dawa za kulevya.
Mambo ambayo yalisababisha heshima ya Tanzania kuporomoka ni kama ifuatavyo; mojawapo ni umaskini uliokithiri usioendana na rasilimali.
Hakuna taifa Afrika linaloifikia Tanzania kwa kuwa na rasilimali nyingi, ipo bahari, yapo maziwa makuu, yapo madini, ipo ardhi yenye mabonde yafaayo kwa kilimo, ipo nguvu kazi ya kutosha.
Kadhalika mbali na rasilimali pia Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu hivyo ilitarajiwa kuwa imesonga mbele. Umaskini wa Tanzania unatokana na viongozi na watawala kutowajibika na kuendekeza maslahi binafsi.
Uchambuzi wa kihistoria ukiendelea linabainika jambo jingine, ufisadi. Ufisadi ni jambo ambalo limesababisha heshima ya Tanzania kushuka.
Tanzania chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilikuwa ni Tanzania inayochukia ufisadi.
Siyo kwamba ufisadi haukuwepo kipindi hicho. Ufisadi ulikuwepo ila ulikuwa haujashika hatamu ulikuwa umedumaa. Watu walichukia ufisadi na rushwa. Waliokuwa mafisadi waliishi kwa taabu.
Hali ilibadilika miaka ya karibuni ufisadi ulipochomoza kutoka katika udumavu, ukastawi na kutamalaki. 
Mafisadi na wapiga dili chafu hawa wakaanza kuonekana wajanja. Waliotambulika kuwa ni mafisadi hata nje ya nchi, nyumbani wakawa wanashangiliwa.
Kwa mashangilio na mapambio ile fahari ya heshima ikakanyagwa na uzuzu ambaye ni mama wa ujinga ambao ulisababisha kuwaona watu wanaoingia katika kundi hilo kuwa ni  wenye akili na mwerevu.
Kwa upande mwingine mtu mwadilifu akigeuzwa taswira yake na kuwa  ni mpumbavu, mchovu au lofa.
Ufisadi ndio uliofanya nchi kuingia mikataba ya hasara kwenye rasilimali zetu. Mwalimu Nyerere aliifukuza Kampuni ya uchimbaji madini ya Williamson Diamond ya Mwadui.
Lakini jambo la ajabu yalipokuja makampuni mengine kwa mkataba wa kutupa kabisa yakapokelewa. Ripoti ya makanikia ilibainisha jinsi ambavyo mikataba ilivyotumika kuidumaza nchi.
Jambo jingine ni dawa za kulevya.  Katika miaka ya karibuni kumetokea ongezeko kubwa kwa vijana wa Kitanzania kujihusisha na dawa za kulevya na wengi wameripotiwa kukamatwa sehemu mbalimbali duniani  wakiwa na dawa hizo.
Imefikia hatua kuwa Mtanzania anakaguliwa sana kwenye viwanja vya ndege vya mataifa mengine. Dawa za kulevya zimekuwa zikihusishwa na Watanzania.
Kutokana mlolongo wa matukio ya kukamatwa na dawa za kulevya kwamba wengi wanaokamatwa nje ya nchi wanakuwa wakionekana kutoka Tanzania na hizo dawa unaweza kuamini kuwa nchi imekuwa ni soko kuu la dawa hizo.
Kumbuka kuna raia wa mataifa mengine mfano Nigeria wanaokamatwa ndani ya nchi wakiwa katika harakati za kuondoka wakiwa wamebeba dawa hizo.
Jambo jingine ni suala la elimu. Hili ni suala lisilopingika kwamba elimu ya Tanzania imeshuka. Na hili linahusu ngazi zote kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu. Hali hii imesababisha vijana wengi kukosa kujiamini hasa wanapotafuta masoko ya ajira katika anga za kimataifa.
Mitaala ya elimu imekuwa ikifanyiwa mabadiliko yasiyokuwa na tija ili kuficha uozo katika sekta ya elimu mfano mpango wa madaraja ya ufaulu.
Usimamizi katika sekta ya elimu ni duni kiasi kwamba hakuna ufuatiliaji juu ya kile kinachotolewa kama kipo katika viwango vinavyohitajika. 
Upo mlolongo wa mambo mengi yanayosababisha kushuka kwa heshima ya Tanzania ikiwa ni pamoja na uongozi dhaifu, kukosekana kwa uzalendo na utendaji wa mazoea, kuua viwanda vyetu, ushirikina ambao unahusisha mauaji ya watu wenye albinism ili kupata mafanikio kiuchumi na kisiasa.
Haya yote yanatokana na kukosekana kwa uzalendo na upeo mdogo wa kielimu. Yote haya yametokana na ukosefu wa elimu.
Kama vile faraja imerudi na mikakati ya kuondoa pazia lililoziba fahari ya nchi kwani inaonekana katika kipindi ambacho Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli amekaa madarakani ameonyesha dhamiri ya dhati ya kutaka kurejesha heshima ya Tanzania katika ramani ya ulimwengu.
Raia wa mataifa mengine wameanza kuonyesha kuwa Watanzania tumepata rais bora hata wakitamani aende akaongoze kwao.
Sio kwamba wanaokubali kile kinachotendeka ni mashabiki au wanachama wa CCM lakini wanakubali kuwa  Rais Magufuli anaonesha dira ya kuthubutu kufanya akiwa waziri katika wizara tofauti.
Yupo mtu mmoja aliweka maoni yake akisema, “Baadhi tulikuwa ni watu wa kulalamika sana kutokana na kukatwa kodi wakati kodi hizo hazioneshi manufaa yake.
“Yaani unakatwa kodi, mwanao anatozwa michango mashuleni ambapo pengine kodi ingelitosha kushughulikia matatizo hayo, unatozwa kodi wakati huduma za matibabu hakuna katika hospitali za umma, unatozwa kodi wakati barabara ni mbovu, ilifikia hatua mtu badala ya kufurahia kwamba ni mlipa kodi anaona karaha kulipa hiyo kodi, kwani ni kama unyonyaji.
“Ila kwa hatua alizochukua Rais Magufuli naona fahari kulipa kodi hata kama kodi hiyo itakuwa ni asilimia 18 niko tayari kulipa maana najua kwamba kodi yangu mwanangu ataifaidi kwenye elimu, kwa kodi yangu nitapata huduma za afya bure, kwa kodi yangu itatumika kwenye ujenzi wa barabara, kwa kodi yangu mwanangu atapata mkopo kwa masharti nafuu wakati wa kusoma chuo kikuu.
“Sasa naona fahari ya mimi kuwa Mtanzania, heshima ya Tanzania imerudi. Hivi karibuni nimekuwa nikipokea hongera kutoka marafiki za wa nje ya nchi kwamba wameona Tanzania tumepata rais makini.”
Lakini ukweli utabakia kuwa wanaokinzana na mambo mengi yaliyo katika mkondo sahihi ni wale wale waliokuwa wakiishi kwa utendaji wa mazoea, wakinufaika nao na ambao ulijaa ufisadi, hujuma, unafiki, uzandiki, uzembe, ubinafsi, uongo na ukosefu wa uzalendo.
Watakuwa ni wale waliokuwa wanakwepa uwajibikaji ndani ya jamii na wale waliozigeuza huduma za jamii kuwa mali yao na wana wao badala ya kuwa ni huduma kwa jamii yote.
CHANZO: TANZANITE

Comments