Featured Post

SPORTPESA KUZIKUTANISHA SIMBA, YANGA NUSU FAINALI



NA MWANDISHI WETU
SIMBA na Yanga zinaweza kukutana katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup inayotarajia kuanza Juni 3, 2018.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana, timu hizo zinaweza kukutana katika hatua hiyo ikiwa zitashinda mechi zao za mtoano kwenye michuano hiyo itakayoshirikisha timu nane, ambapo bingwa wake atapata nafasi ya kwenda kucheza na Everton nchini Uingereza.
Mwaka 2017 Simba na Yanga zilikutana katika fainali ya michuano hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Ratiba kamili ya michuano hiyo inaonyesha kwamba, katika robo fainali Juni 3, Yanga itaanza kumenyana na Kakamega Home Boys ya Kenya kabla ya kuipisha Gor Mahia pia ya Kenya kucheza na JKU ya Zanzibar.
Simba wenyewe watacheza na Kariobangi Sharks ya Kenya Juni 4, wakati AFC Leopards pia ya Kenya itacheza na Singida United Juni 5.
Katika nusu fainali, mshindi baina ya Gor Mahia na JKU atakumbana na mshindi baina ya AFC Leopards na Singida United katika mechi ya kwanza.
Kwenye mechi ya pili, mshindi wa mechi Kakamega Home Boys na Yanga ndiye atakumbana na mshindi baina ya Kariobangi Sharks na Simba.
Mechi zote za nusu fainali zitachezwa Juni 7 wakati mechi ya kumsaka mshindi wa tatu itafanyika Juni 10, siku ambayo fainali itafanyika.

Comments