Katika Kisiwa cha Nkombo, kilichopo magharibi mwa Rwanda katika Ziwa Kivu, kuna utamaduni
wa kipekee usiokuwepo popote pale nchini Rwanda ambapo wanawake huwaosha
miguu waume zao, kuwapaka mafuta na kuwabeba mgongoni hadi kitandani.
Wanawake
waliozungumza na BBC wanasema utamaduni huo sio kudhalilisha mwanamke
wala mke kunyenyekea mumewe kupindukia bali ni kuonesha upendo.
Wanaume wanasifia sana utamaduni huo kiasi kwamba baada ya ndoa hutoa mahari tena mara nyingi iwezekanavyo.
"Bwana anaporudi nyumbani anakuta umechemsha maji. Unamuosha miguu na
kumpaka mafuta...kwa kuwa kawaida huwa amechoka, unamweka mgongoni hadi
kitandani, Josephine Nyirantibashima aliambia mwandishi wa BBC Yves
Bucyana.
"Mimi binafsi mzee wangu ana miaka 51 na mimi nina 48 nampa huduma hiyo."
Yeyote unayemuuliza katika kisiwa hiki anakusimulia jinsi anavyobeba au kubebwa mgongoni na mme au mkewe:
Rurangwa Jean Damascene ni miongoni mwa wanaume wanaodai kuonja kile wanachotaja kuwa utamu wa utamaduni huo.
"Mimi
kila mara nikienda bafuni mke wangu huwa ananisaidia kunisafisha.
Sijamlazimisha. Yeye mwenyewe anafanya hivyo kwa moyo wake mkunjufu,"
anasema.
"Hata kunibeba mgongoni hadi kitandani nikalala na
kusinzia vizuri sana. Hufanya hivyo mara nyingi. Unajua? Kuna wakati mtu
anakuwa amechoka sana. Kwa hiyo hapa kwetu siyo ajabu kabisa."
Wanawake
katika kijiji hicho waliambia BBC kwamba kuwabembeleza waume zao siyo
kwamba wananyenyekea kupindukia wala kuwaogopa waume zao.
"Mfano mimi nyumbani tuna tatizo la uhaba wa
chakula baada ya mamlaka kufunga shughuli za uvuvi katika ziwa
Kivu,bwana hana kazi kwa sasa, lakini pamoja na hayo nitajitahidi
kumliwaza. Lazima nimbebe mgongoni, siwezi kwenda kinyume na utamaduni
huo ili na yeye asisite kutoa mahari kwetu mara kadhaa," alisema mmoja
wao.
Mahari anayozungumzia yanatolewa na mwanaume hata baada ya ndoa kama ishara ya kuridhika na ndoa yake.
"Alitoa
mahari kwetu mara nne pekee kwa sababu uwezo wake siyo mkubwa. Lakini
bwana kutoa mahari mara kadhaa nyumbani kwa mkewe kunatokana na
utamaduni wetu wa namna tunavyowabembeleza waume zetu. Kawaida huwezi
kuolewa bila bwana kutoa mahari,lakini hata baada ya kuolewa anatoa
mahari mara kadhaa kubainishia familia ya mkewe kuwa walilea vizuri."
Rwanda ni miongoni mwa nchi zilizo mstali wa mbele katika swala la usawa wa jinsia na kuwajali sana wanawake.Wakuu wa makundi ya kidini katika kisiwa hiki wanasema hili ni suala la utamaduni wa wananchi.
Hanyurwa
Jean ni mchungaji wa la Kiangilikana: "Tunapofundisha bi harusi na
bwana harusi watarajiwa hapa kanisani wanatuambia kinagaubaga kuwa huu
ni utamaduni wao. Sio swala la wanawake kulinda ndoa zao zisivunjike,
hapana!."
"Pia sidhani kwamba utamaduni huu unakinzana na masharti ya
usawa wa jinsia, hapana! Utamaduni huu haujawakataza kuheshimiana na
kushirikiana kama mke na mme. nionavyo ni swala la utamaduni kuliko
tunavyofikiria kwamba wanawake wanaogopa waume zao. Huwezi kuwakataza
kufanya hivyo? Ni kama uwakataze kuzungumza lugha zao asilia."
Maafisa
wa serikali wanasema wanawake kuwabeba waume zao mgongoni siyo
utamaduni unaofaa kwa wakati huu lakini kwamba ni vigumu kumkataza mtu
anachokitaka.
Comments
Post a Comment