Featured Post

SERIKALI YATOA MILIONI 700 KWA VIJANA MWAKA 2017/18

2
 Mwenyekiti wa Jukwaa la vijana walionufaika na mradi wa YEE, Mwajuma Chamkono akichangia hoja wakati wa kikao cha Jukwaa la Vijana Kitaifa cha vijana waliowezeshwa Kiuchumi kupitia mradi huo unaofadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa na Shirika la Plan International – Tanzania.Na Mwandishi Wetu.
Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana imetoa takribani shilingi milioni 700 kwa mwaka wa fedha 2017/18 kwa vijana nchini ili kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kuweza kuepuka utegemezi katika jamii.

Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Vijana - ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Juma Abubakari alipokuwa akifungua kikao cha Jukwaa la Vijana Kitaifa cha vijana waliowezeshwa Kiuchumi kupitia mradi wa YEE unaofadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa na Shirika la Plan International – Tanzania.

Abubakari amesema kuwa mradi huo ni muhimu kwa sababu unaenda sawa na Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2017 ambayo inahimiza suala la uwezeshaji vijana kiuchumi ambapo shirika hilo limejitahidi kushirikiana na Serikali kwa kuwawezesha vijana zaidi ya 10,000 kwa kuwapa stadi za ujasiriamali pamoja na elimu ya ufundi.

“Serikali inawasaidia vijana kwa kuwapa elimu kuhusu Sera, kuwatengea maeneo ya kufanyia biashara zao pamoja na kuwapa mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na asilimia 4 ya mapato ya halmashauri ambayo ni kwa ajili ya vijana hivyo kwa mwaka wa fedha unaoishia tumeshatoa takriban shilingi milioni 700 kwa ajili ya kuwainua vijana,” alisema Abubakari.

Abubakari amefafanua kuwa Serikali kupitia mfuko huo ulianza kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa vijana tangu mwaka 1993 ambapo kuanzia mwaka 2003 hadi 2018 mfuko huo umefanikiwa kutoa jumla ya shilingi bilioni nne kwa vijana nchini.

Ametoa rai kwa vijana hasa waliopata mafunzo kupitia mradi wa YEE kuendelea kujiunga katika vikundi ili waweze kupatiwa mikopo kirahisi pamoja na kuziomba taasisi za fedha  na mabenki kuendelea kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa vijana.

Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa YEE kutoka Shirika la Plan International, Simon Ndembeka amesema katika mradi huo shirika linajivunia kuvuka lengo na   kuwawezesha vijana 10,132 mbali na vijana 9100 waliopanga kuwafikia pamoja na kuhamasisha vijana kuunda vikundi vya uzalishaji mali zaidi ya 849 ambavyo vimepatiwa vitendea kazi vya kuanzia.

Nae Mwenyekiti wa Jukwaa la vijana walionufaika na mradi wa YEE, Mwajuma Chamkono amesema kuwa lengo la jukwaa hilo ni kuishawishi Serikali na wadau wa maendeleo ya vijana kuhusiana na sera, changamoto na fursa za vijana ili kuweza kupata njia mbadala za kuwawezesha vijana kujikwamua.

“Jukwaa hili linapendekeza Serikali na taasisi za fedha zinazoingia mikataba ya utoaji mikopo kwa vijana kuweka bayana masharti na vigezo visivyosababisha vijana kuogopa kuchangamkia fursa ya mikopo kutokana na mkanganyiko wa taarifa”, alisema Bi Mwajuma.

Mradi wa YEE ni wa miaka mitatu ulianza tangu mwaka 2015, unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).  
1
 Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Vijana - ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Juma Abubakari (aliyesimama mbele) akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Jukwaa la Vijana Kitaifa cha vijana waliowezeshwa Kiuchumi kupitia mradi wa YEE unaofadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa na Shirika la Plan International – Tanzania.

Comments