- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega,
Mpwapwa
BENKI ya vinasaba vya wanyama (gene bank) katika Taasisi ya
Utafiti wa Mifugo Tanzania (Taliri) kituo cha Mpwapwa inaweza kuokolewa ikiwa Serikali
itasitisha kununua ‘mashangingi’ mawili tu.
Uchunguzi umeonyesha kwamba, maabara hiyo ya kisasa imekwama
kwa miaka minne sasa licha ya serikali kuwapaleka wataalam wake kwa mafunzo
katika nchi za Ethiopia na Brazil ili kupata ujuzi wa namna ya kutafiti na
kuhifadhi vinasaba vya mifugo.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, gharama za kununulia vifaa vya
maabara hiyo sasa imefikia Shs. 500 milioni, ikiwa imeongezeka kutoka Shs. 300
milioni zilizokuwa zimekadiriwa awali mwaka 2013.
Gari moja aina ya Toyota Land Cruiser, maarufu kama
‘shangingi’ linagharimu kiasi cha Shs. 300 milioni, hivyo kama bajeti ya
ununuzi wa magari hayo ingepunguzwa magari mawili tu, ingetosheleza kununulia
vifaa vinavyotakiwa kwenye maabara hiyo.
Germanus Bahati Tungu, mtafiti mkongwe na miongoni mwa
waliopatiwa mafunzo Ethiopia na Brazil, anasema kununuliwa kwa vifaa hivyo vya
maabara kungesaidia kuhifadhi mbegu mbalimbali za wanyama, hususan ng’ombe,
mbuzi, nguruwe na kuku wa kienyeji.
Tungu anasema, endapo vifaa hivyo vingepatikana vingesaidia
uzalishaji wa mbegu za kutosha na uhifadhi, hivyo kuiwezesha taasisi hiyo
kusambaza mbegu bora za ng’ombe aina ya Mpwapwa kwa wakulima kwa kupandikiza
mimba kwa ng’ombe wengine kutumia viinitete (embryonic insemination) badala ya kutumia dume.
“Lakini sasa mambo ni magumu katika uzalishaji wa mbegu kwa
sababu hatuna vifaa vya kuhifadhia na siyo rahisi kuzalisha ng’ombe wa kutosha
kwa wakati mmoja kwani kwa kawaida ng’ombe anazaa mara moja tu kwa mwaka,”
anasema Tungu, ambaye huenda mwakani akastaafu kabla hajautumia ujuzi wake
aliousomea kwa gharama za kodi ya wananchi.
Anaongeza: “Nasikitika nitakuwa sijaitendea haki taaluma
yangu, nimepelekwa nje kwa gharama, lakini kama maabara hii ingewezeshwa kwa
kununuliwa vifaa, ujuzi wangu wote ningeutumia kuhakikisha tunaweka vinasaba
vya kutosha.”
Mkurugenzi wa Kituo cha Taliri-Mpwapwa, Dkt. Eliakunda
Kimbi, anasema lengo la kuanzisha benki hiyo ya vinasaba siyo tu kurahisisha
uzalishaji wa mbegu bora za mifugo na kusambaza kwa wakulima, bali pia
kuhifadhi hata mbegu za wanyama za asili.
Anasema, ingawa kituo hicho kinasambaza ng’ombe aina ya
Mpwapwa waliotafitiwa kituoni hapo pamoja na mbuzi bora aina ya Malya Blended
wanaozaa watoto mapacha, lakini pia wanataka kuhifadhi vinasaba vya mbuzi wa
asili kama wanavyofanya hivi sasa ambapo wanao mbuzi kama Gogo White, Newala
Goats na Ujiji Goats (Buha).
Pia wanao ng’ombe wengine wa asili kama Singida White,
Iringa Red na Ufipa ambao wanaendelea kuwafanyia tafiti za kuwahifadhi na
kutathmini uwezo wa mifugo hiyo ya asili.
“Kwa kawaida, hata kama ng’ombe hawa wa asili (Zebu)
wanafanana kama ilivyo kwa mbuzi wa asili, lakini wana tofauti kubwa kutoka
eneo moja na jingine, hivyo ni vyema kuhifadhi vinasaba vyake kwa kuwa aina
nyingi zinatoweka hivi sasa,” anasema Dkt. Kimbi.
Akizungumzia mafanikio ya tafiti ambazo zimekwishafanyika
kituoni hapo, Dkt. Kimbi anasema wametafiti ng’ombe aina ya Mpwapwa wakilenga
kuhifadhi aina hiyo ya koosafu, kuzalisha idadi ya kuwatosheleza kwa ajili ya
wafugaji na kuimarisha kizazi (purity
maintenance and stabilization).
Aidha, anasema wamefanya utafiti kutathmini uwezo wa
uzalishaji wa kuku wa asili kwa kuangalia aina nne za kuku hao ambao ni Kuchi,
Kishingo, Horace na Sasamala.
“Tumefanya utafiti wa majani na mikunde mbalimbali kwa ajili
ya kuongeza upatikanaji wa mbegu za malisho bora kwa wafugaji ambapo kwa sasa
jumla ya aina 80 za malisho zinahifadhiwa katika hifadhi ya vinasaba vya
malisho hapa kituoni,” anasema.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, msimu wa 2015/2016 kituo
hicho kilizalisha kiasi cha malisho (hay) mikate 26,108 ambayo 56% iliuzwa kwa
wafugaji na 44% ilitumika kwa ajili ya mifugo ya kituo.
Kwa zaidi ya miaka 110 kituo hicho cha Mpwapwa, chini ya
majina tofauti, kimekuwa kitovu cha utafiti wa mifugo nchini.
Taasisi hiyo
ilianzishwa na wakoloni wa Kijerumani mwaka 1905, kikiwa kama kituo cha utafiti
wa mifugo ambapo kiliendelea mpaka baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.
Kabla ya
kuhamia katika eneo la Kikombo kilipo hivi sasa, kituo hicho kilinzishwa mwaka
1903 katika Kijiji cha Godegode, takriban kilometa 20 kutoka Mpwapwa mjini.
Sababu za
kuhamishia kituo hicho mjini Mpwapwa, kwa mujibu wa Dkt. Kimbi, ni baada ya Wajerumani
kushuhudia farasi na ng’ombe wengi wakifa kwa magonjwa ambayo hawakuwa wakiyafahamu,
hivyo kuamua kuanza utafiti.
“Baadaye ikagundulika
kwamba wanyama hao walikufa kwa ugonjwa wa Sotoka (Rinderpest), hivyo wakajenga josho la kuogeshea wanyama mwaka 1907.
Josho hilo ndilo kongwe kuliko yote Afrika Mashariki,” anasema Dkt. Kimbi.
Akielezea
historia, Dkt. Kimbi anasema, mwaka 1922 wakoloni Waingereza walianza
kukihudumia kituo hicho na kuanzisha Maabara ya Utafiti wa Magonjwa ya Mifugo (Veterinary Pathology Laboratory).
Kuanzia mwaka
1924 hadi 1929 shughuli kuu za kituo hicho zikawa utafiti wa magonjwa ya Sotoka
na Ndigana (Rinderpest and
Trypanosomiasis), lakini utafiti huo ukawa unafanyika kwa wanyama wote
waliokuwepo kituoni hapo na maeneo ya jirani kwa vile ilionekana magonjwa hayo
yalikuwa yakiwashambulia na wanyama wengine mbali ya farasi.
Zaidi ya dozi
50,000 za kuzuia Sotoka (anti-rinderpest
serum) zilitolewa kila mwaka.
Makao makuu
ya Idara ya Sayansi ya Mifugo na Utunzaji wa Wanyama, kama ilivyojulikana
wakati huo wa ukoloni, ikahamia Mpwapwa kutoka Dar es Salaam mwaka 1929.
Aidha, uboreshaji
wa ng'ombe wa kienyeji wenye asili ya Iringa, Rungwe, Singida na Masailand
ulikuwa umeanza mapema mwaka 1923.
“Kuanzia
mwaka 1930 hadi 1938, utafiti wa utunzaji wa mifugo ulipata sura mpya baada ya
kuletwa mtaalam wa madawa na malisho. Shughuli za uzalishaji wa mifugo
zilipamba zaidi mwaka 1944 baada ya kuteuliwa mtaalam wa vinasaba.
“Taasisi Kuu
ya Mifugo ikaanzishwa mwaka 1951, na wakati huo huo kituo kikaona umuhimu wa
kuiendeleza sekta ya mifugo, hivyo kikaanzisha kituo cha mafunzo ambacho sasa
kinajulikana kama Livestock Training Agency (LITA),” anasema.
Dkt. Kimbi anasema,
makao makuu ya idara hiyo yalirejeshwa Dar es Salaam mwaka 1954 na kumwacha Ofisa
Mkuu wa Mifugo hapo Mpwapwa ambaye alisimamia Maabara ya Utafiti, Kituo Kikuu
cha Uzalishaji, na Utafiti wa Mifugo na Malisho.
Wanyama wa
kufugwa waliokuwepo kituoni hapo walikuwa ng'ombe, nyati, kondoo, mbuzi,
nguruwe, kuku na farasi.
Mnamo mwaka
1962 kulikuwa na mabadiliko ya muundo wa wizara na kukifanya kituo hicho kiitwe
Kituo cha Majaribio ya Mifugo kikiwa kinahusika na mambo ya kilimo, utunzaji wa
mifugo na uvuvi.
Mwaka 1966
Sera ya Maendeleo ya Mifugo iliyopitishwa na Bunge ikiwa inasisitiza umuhimu wa
kueneza ng'ombe wenye ubora wa juu vijijini ilikifanya kituo kikazanie
uzalishaji wa ng'ombe, ambapo sasa kikajulikana kama Kituo cha Uzalishaji wa
Mifugo (Livestock Breeding Station).
Mwishoni mwa
miaka ya 1960 kituo hicho kikaitwa tena Taasisi ya Utafiti na Mafunzo ya Mifugo
kikiegemea zaidi maendeleo ya mifugo.
Kuanzia mwaka
1977 utafiti wa mafunzo na mifugo viligawanywa katika taasisi mbili tofauti,
Taasisi ya Utafiti, ambayo kuanzia Julai 1981 ilijulikana kama Taasisi ya
Uzalishaji na Utafiti wa Mifugo (LPRI) ikiwa chini ya Mkurugenzi na Chuo cha
LITA kikawa chini ya Mkuu wa Chuo. Shirika la Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRO)
lilianza kusimamia taasisi hiyo mwaka 1981 hadi lilipokufa mwaka 1989, na
kuanzia hapo mpaka sasa taasisi hiyo pamoja na chuo viko chini ya Wizara
inayoshughulikia mifugo.
Hivi sasa
taasisi hiyo inajishughulisha na uzalishaji wa ng'ombe aina ya Mpwapwa, Mbuzi
wa Maziwa jamii ya Malya, Kuku wa Kienyeji, Malisho, Lishe, Matibabu ya Mifugo,
na Utoaji wa Elimu kwa Wakulima na Wafugaji.
Comments
Post a Comment