Featured Post

KIM KARDASHIAN AMUOMBA TRUMP AMSAMEHE BIBI ALIYEFUNGWA JELA



Kim Kardashian West amekutana na Rais wa Donald Trump kujadili uwezekano wa msamaha kwa mama mzee na bibi mwenye umri wa miaka 63 ambaye anatumikia kifungo cha maisha jela.

Alice Marie Johnson amekuwa gerezani kwa zaidi ya miongo kadhaa baada ya kupatikana na hatia ya matumizi ya dawa za kulevya kwa mara ya kwanza.
Mkwe wa rais Trump, Jared Kushner, amekuwa pia akizungumza na Bi. Kardashian West juu ya kesi hiyo kwa miezi kadhaa.
Binti yake Johnson ameithibitishia BBCNews kwamba mkutano huo umefanyika.
Baadaye Trump alituma ujumbe wa Twitter kwamba walikuwa na "mkutano mzuri".

Kwa nini Kim Kardashian anajihusisha na kesi hii?
Kwa mara ya kwanza Bi Kim Kardashian ambaye ni nyota wa kipindi cha maisha halisi cha televisheni nchini Marekani aliguswa na video fupi ya Bibi huyo juu ya kesi yake iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii.
Bi Kardashian West aliamua kumuomba wakili wake wa muda mrefu , Shawn Holley, kuiangalia upya kesi yake na akailipa timu ya mawakili wa Bi Johnson.
Nyota huyo wa kipindi maarufu cha televisheni cha ....Keeping up with the Kardashians, pia aliweza kushirikiana na Kushner, mshauri wa ngazi ya juu wa Rais Trump ambaye amekuwa akishinikiza kufanyika kwa mageuzi kwa magereza ya kitaifa.
Muswada wa Kushner unaofahamika kama First Step Act, ambao umetengewa dola milioni $50 kwa ajili ya kusaidia kurekebisha tabia za wafungwa, ulipitishwa na Bunge la Wawakilishi nchini Marekani.
Kwa mujibu wa mabinti zake Johnson, mchakato huo umekwenda haraka kutokana na uhusika wa Bi Kardashian West.
Jumatano pia ni tarehe ya kuzaliwa ya Bi Johnson, ambayo Bi Kim Kardashian West aliikumbuka kupitia ujumbe wake wa Twitter alioutuma leo asubuhi.

Alice Marie Johnson ni nani?

Johnson alihukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha jela kisicho na uwezekano wa msamaha wowote mwaka 1996 kwa mara ya kwanza kwa kosa la matumizi ya madawa ya kulevya ambayo hayakusababisha ghasia.
Alipatikana na hatia ya kutumiwa kama "chambo", cha kusambaza ujumbe baina ya wauzaji na wanunuzi wa dawa za kulevya.
Kulingana na familia na wanaomuunga mkono, Johnson amekuwa mfungwa wa kuigwa ambaye amekuwa akijihusisha sana na mipango mingi gerezani, ikiwemo kufanya kazi katika nyumba ya wagonjwa mahututi katika gereza.
Anatimiza vigezo vyote vya msamaha kwa wafungwa chini ya mradi wa rais wa zamani wa Marekani ulioanzishwa mwaka 2014, lakini alikataliwa msamaha siku kadhaa tu kabla ya muhula wake kumalizika.
"Hii ni mara ya mwisho kuipa familia yangu shauku ya matarajio ya kuisikitisha," Bi Johnson aliiambia BBC wakati huo.
Licha ya hilo, suala la kuingilia kati kwa Bi Kardashian West katika kesi hii linaonekana kuimarisha juhudi za kufunguliwa kwake.
Amy Povah, ambaye ni mmoja wa waasisi wa mradi wa msamaha kwa wafungwa unaofahamika kama CAN-DO ambaye amekuwa akiendesha kampeni ya kufunguliwa kwa Bi Johnson tangu mwaka 2014, amesema kuwa amekwisha kusanya saini 70 kutoka kwa mashirika ambayo yanaunga mkono kuachiliwa kwake pamoja na barua ya kuunga mkono hatua hiyo kutoka kwa mkuu wa zamani wa gereza alimofungiwa Bi Johnston.

Kipi kitarajiwe?
"Binafsi nimekuwa nikimuona kama mtu wa kipekee," amesema Bi Povah. "Si mtu mwenye machungu wala hasira , ni mtu anayekuonyesha matumaini."
Mchakato wa msamaha utategemea maamuzi ya rais , na haijafahamika hadi sasa ikiwa anapanga kutangaza uamuzi wake wakati Bi Kardashian West amemtembelea au la.
Wengi katika mitandao ya kijamii wamekosoa uhusika wa Bi Kardashian West kwa kujifanya mwanaharakati wa mageuzi ya magereza, wakisema kuwa kuna maelfu ya kesi zinazostahili kuchunguzwa kwa karibu, lakini mabinti zake Johnston bado wana matumaini kwamba kwamba kama familia walau hawataendelea kussubiri sana kabla ya kuachiliwa.
"Tunaomba msamaha katika kesi ya mama yetu … ili hatimae machungu tuliyonayo kama familia yamalizike," aliiamnbia BBC Bi Tretessa Johnson.


Comments