Featured Post

KATIBU TAWALA MOROGORO AWATAKA MAOFISA KILIMO KUONGEZA UZALISHAJI

DSCN9622
Na Andrew Chimesela – Morogoro
Maafisa Kilimo wa Sekretarieti ya Mkoa na Halmashauri za Mkoa wa Morogoro wametakiwa kusimamia na kutoa utalaama wao kwa wakulima kupitia maafisa Ugani ili kuongeza uzalishaji wa mazao Mkoani humo.

Agizo hilo limetolewa Mei 29 mwaka huu na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw. Clifford Tandari alipofanya Kikao na Maafisa wa Kilimo huo kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kilimo za kila Halmashauri na kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji kwa mwaka 2018/2019.
Akifungua Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Tandaria amesema, kila Afisa kilimo ahakikishe anasimamia Maafisa Ugani wake kwenda kwa wakulima kuwafundisha kilimo cha kisasa kwa kuwa wengi wao bado wanalima kilimo cha mazoea jambo linalowakosesha tija katika kilimo.
“sio wakulima waendelee na utaratibu ule ule wa zamani, tuhakikishe wakulima tunaweleza mbegu mpya zilizojitokeza na kuwasimamia kufanya palizi kwa wakati alisema ” alisema Tandari
Tandari amesema endapo watajipanga vizuri katika kuwasimamia Maafisa Ugani kuwafundisha wakulima kilimo cha kisasa na kuondoa kabisa upotevu wa mazao yanayopotea wakati wa kuvuna, upo uhakika wa kuongeza uzalisha wa mazao mara mbili ya matarajio ya mavuno ya mwaka huu ya kupata tani 2,800,000 katika Mkoa.
Aidha, amewataka Maafisa hao kuongeza uzalishaji wa kilimo cha mboga mboga ili kutumia vema fursa iliyojitokeza sasa ya kuwa katikati ya Jiji la Dar es Salaa na Makao Makuu ya Serikali Jiji la Dodoma  ili kuongeza mapato kupitia kilimo hicho hususan Halmashauri za Morogoro, Mvomero na Gairo ambazo ziko kando ya Barabara kuu ya Dar es Salaam – Dodoma.
“Kwa hiyo tunayo fursa, Dodoma sasa hivi mboga mboga zimeisha pale sokoni, inabidi waje watafute huku Morogoro ndio fursa zenyewe hizo, kuna uhaba wa mboga mboga kule Dodoma, sasa sisi tuitumie hii fursa ili tuongeze uzallishaji” alisema Tandari.
Katika hatua nyingine Clifford Tandari amewataka Maafisa hao wa kilimo kutilia mkazo Mkakati ya Pamba, Kahawa na Korosho yanayostawi Mkoani Morogoro ili kuongeza uzalishaji mapato ya Halmashauri kwa kuwa wawekezaji watavutiwa na uwepo wa mazao hayo ambayo ndiyo mali ghafi ya viwanda.
Kuhusu Maafisa Ugani ambao walipata mafunzo muda mrefu wa nyuma na hivyo kukosa Utalaamu ambao unakwenda na wakati (mafunzo rejea) Bw. Tandari amesema yuko katika mazungumzo na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine – SUA ili Maafisa hao waende kupata mafunzo yanayokwenda na wakati ili kuongeza tija kwa wakulima wa maeneo yao.
Mmoja wa Maafisa Kilimo katika kikao hicho Bw. Mohamed Ramadhani ambaye ni Afisa kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero  amesema Halmashauri yao imejipanga kupunguza upotevu wa mavuno wa kati ya asilimia 5 – 40 yanayopotea, kwa kuwa wametambua chanzo cha upotevu huo.
Bw. Mohamed ametaja baadhi ya sababu za upotevu  wa mazao hayo kuwa ni pamoja na wakulima kutopanda mbegu sahihi za mpunga, kutovuna kwa wakati, kuchelewa kutoa mazao shambani baada ya mavuno na kutotumia njia sahihi za kuvuna zao la mpunga.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozaria Rwegasira, amezungumzia changamoto ya viwavi jeshi vamizi waliojitokeza katika msimu huu na kuwahakikishia wakulima kuwa wamejipanga vizuri kukabiliana na tatizo hilo kwa kuwa tayari mafunzo kuhusu kuwazuia wadudu hao yametolewa kupitia ufadhiri wa Benki ya Dunia na sasa yanaendelea kutolewa kwa Maafisa ugani wa ngazi za chini.
DSCN9689

Comments