Featured Post

CHALIWASA YAASWA KUACHA KUSAMBAZA MAJI KWA UPENDELEO

IMG_20180524_162454
Diwani wa Kata ya Miono Juma Mpwimbwi akizungumza wakati wa  mkutano na wananchi Kata ya Miono ,Bagamoyo ,ulioitishwa na Mkuu wa  Mkoa wa  Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo.
IMG_20180524_163217
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ,alhaj Majid Mwanga ,akizungumza wakati wa  mkutano na wananchi,Kata ya Miono ,Bagamoyo ulioitishwa na Mkuu wa  Mkoa wa  Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo.
IMG_20180524_163537
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,akizungumza wakati wa  mkutano na wananchi Kata ya Miono,Bagamoyo.
Picha na Mwamvua Mwinyi
………………
Na Mwamvua Mwinyi, Miono
WAKAZI wa kata ya Miono ,Bagamoyo Mkoani Pwani ,wamemtaka meneja wa Mradi wa Maji Safi Chalinze (CHALIWASA) ,mhandisi Christer Mchomba, kusambaza maji bila upendeleo kwani wanataabika kwa  kipindi kirefu.
Aidha wamemuangukia mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo kuingilia kati tatizo hilo kwa kuangalia namna ya kupunguza kero ya maji inayowakabili pamoja na maeneo mengine ya Bagamoyo na Chalinze.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi hao  , wakati mkuu huyo wa mkoa alipokwenda kuzungumza na wananchi  katika kata hiyo ,Mkuu wa  wilaya ya Bagamoyo ,alhaj Majid Mwanga alisema CHALIWASA hali sio salama.
Alieleza wanashangazwa kuona maeneo ambayo yanasambazwa maji  na mawakala /watu binafsi kwa  niaba ya CHALIWASA kama kijiji cha Hondogo maji hayakosekani kamwe.
Alhaj Mwanga alisema, hata msikitini maji yamekuwa mtihani kupatikana hali inayosababisha kero kwa watumiaji .
“Nikiwa mwakilishi wako wilayani hapa ,nimeshashirikiana na viongozi wa halmashauri, madiwani na Chama Cha Mapinduzi, Tumechukua hatua ya kwanza kumtaka meneja CHALIWASA kuwapelekea taarifa kwanini maji hayasambazwi kwa ratiba”
“Tumefanya kazi ya kutosha ,tumeweka ratiba lakini bado ratiba sio rafiki kwa walaji wa maji si Miono ,Msata ,Kiwangwa ,Chalinze wala Lugoba “; alisisitiza alhaj Mwanga.
Alhaj Mwanga alisema, kilio kikubwa kwa wakazi wa Chalinze ni maji suala ambalo linarudisha nyuma juhudi za kimaendeleo kwa jamii.
Baadhi ya wakazi wa Miono akiwemo Rashid Hemed na Zakia Abdallah walisema, tatizo la  maji  ni  kubwa katika kata  hiyo.
Diwani wa kata ya Miono Juma Mpwimbwi, alisema hali ya mradi mkubwa wa aina hiyo iliyofikia ni mbaya na haileti taswira nzuri kwa jamii.
Alisikitika kutokuwa na maji ya uhakika kwa miaka mingi hali ambayo inakatisha tamaa wananchi.
“Mkuu wa mkoa aingilie kati ama Rais dk.Joh Magufuli aje kujionea labda kauli yake itasaidia kutatua changamoto ya mradi huu:;”Mradi huu sio rafiki tena na jamii  ;” alisisitiza Mpwimbwi.
Akizungumzia  kero hiyo ,Mkuu wa  Mkoa wa  Pwani ,mhandisi Ndikilo ,alisema bado kuna shida ya maji  na ni  lazima kidogo kilichopo kigawanywe ili kila mmoja anufaike.
Alisema inaonekana ratiba na mipango na utaratibu iliyowekwa kwa  wananchi haiheshimiwi .
“Huu  ni mpango wa muda mfupi ,lakini hapa kuna ratiba ambayo haiheshimiwi ,kama ingekuwa inaheshimiwa basi  Miono Kiwangwa wakazi wangekuwa wanajipanga kuchota maji ili kuweka maji ya akiba”
Ndikilo ,alimtaka mhandisi wa CHALIWASA mhandisi Mchomba ,kukutana nae Jumanne Mei 29 mwaka huu ofisini huku akiwa na majibu ya lengo lake la kutofuata utaratibu uliowekwa kusambaza maji  .
Hivi karibuni mhandisi Mchomba ,alifafanua mradi huo una uwezo wa kuzalisha cubic meters za maji 3,000 sawa sawa na lita 300,000 kwa siku .
Alisema lita 15,000 huwa zikipotea njiani wakati wa kusambaza maji hali ambayo wengi wao wanashangaa kuona kuna maeneo ambayo hayakosekani maji.
Mhandisi Mchomba alibainisha ,awali mradi huo ulilenga vijiji 20 na wakazi 100,000 kwasasa vipo vijiji 86 huku wakazi wakifikia zaidi ya 200,000 .#
“Kwa siku CHALIWASA tunazalisha lita laki tatu hadi tano kwa siku za maji, yanayotolewa kwa mgao wa saa 6 kwa kila kijiji ndani ya Chalinze, ikijumuisha na vingine vilivyopo maeneo ya Bagamoyo, Kibaha na Morogoro vijijini,” alisema Mchomba.

Comments