- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
HOTUBA YA WAZIRI WA
MADINI, MHESHIMIWA ANGELLAH JASMINE MBELWA KAIRUKI (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI
MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA WA
2018/19
1.0 UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba,
kufuatia Taarifa iliyowasilishwa leo Bungeni na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini,
Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea, kujadili, na kupitisha Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu, Mpango
na Bajeti ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18.
Aidha, ninaomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa
2018/19.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu,
mwingi wa rehema, kwa
kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana tena. Aidha, ninamshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu Hotuba
ya Bajeti ya Wizara yangu kwa Mwaka wa Fedha wa
2018/19.
3. Mheshimiwa Spika, vilevile, ninakushukuru
kwa kunipa fursa hii adhimu
ya kuwasilisha mbele ya
Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza Bajeti
ya Wizara ya Madini. Kama unavyofahamu
Wizara
hii iliundwa mwezi Oktoba, 2017 baada ya kuvunjwa kwa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini, na hivyo
kufanya bajeti hii kuwa ndiyo ya
kwanza ya Wizara mpya ya Madini. Wizara ya Madini inategemea sana mawazo,
ushauri na maelekezo ya Bunge lako Tukufu ili kuimarisha na kukuza Wizara hii mpya.
4. Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kuniteua kuwa Waziri wa Madini;
Wizara ambayo ni muhimu kwa uchumi wa
Nchi yetu pamoja
na Manaibu wangu,
Mheshimiwa Stanslaus Haroon
Nyongo (Mb.), na Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb.). Tunamuahidi tutatekeleza
maelekezo anayoyatoa kwa ufanisi na uadilifu na tutatekeleza majukumu
yetu vyema na
tutatumia ujuzi na maarifa yote tuliyopewa na Mwenyezi Mungu na tuliyojifunza kusimamia Sekta hii ipasavyo ili Taifa letu linufaike na rasilimali za
madini.
5. Mheshimiwa
Spika, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa
uongozi wake makini katika usimamizi wa rasilimali za nchi.
Sote ni mashahidi wa jinsi uongozi
wake
unavyogusa wananchi wa Tanzania hususan katika matumizi sahihi ya
rasilimali za Taifa katika kuwaletea
maendeleo.
6. Mheshimiwa
Spika, pia ninawashukuru Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia
Suluhu
Hassan
na
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim
Majaliwa Majaliwa (Mb.) kwa miongozo wanayonipatia katika kutekeleza majukumu
yangu kikamilifu.
7. Mheshimiwa Spika,
katika suala hili la usimamizi wa rasilimali za nchi na
hususan katika Sekta ya Madini
ninayoisimamia, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na wewe
binafsi kwa kuunda Kamati ambazo zilishughulikia changamoto zilizopo katika
Sekta ya Madini. Mapendekezo ya Kamati zote yamefanyiwa kazi na baadhi ya mapendekezo mengine yanaendelea kutekelezwa. Nawahakikishia kuwa, Wizara yangu itatekeleza mapendekezo yote
kama yalivyotolewa na Kamati hizo.
8. Mheshimiwa
Spika, vilevile, nikupongeze wewe binafsi, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai (Mb.), Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Naibu
Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb.), na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha Bunge
kwa weledi mkubwa, hekima,
busara na kwa umahiri.
9. Mheshimiwa Spika,
ninachukua fursa hii pia kuwashukuru Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati
na Madini, Mheshimiwa Dunstan Luka
Kitandula (Mb.), Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Mariam Ditopile Mzuzuri (Mb.) na
Wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini, kwa
michango yao mahsusi
wakati wa uchambuzi wa
Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa Mwaka
wa Fedha wa 2017/18 na Mpango na Makadirio ya Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19. Kamati imetoa maoni
mbalimbali na ushauri mzuri unaoboresha
utekelezaji wa majukumu yetu na kuhakikisha Sekta ya Madini inanufaisha Taifa. Napenda kulihakikishia Bunge lako
Tukufu kuwa Wizara ya Madini
itafanya kazi kwa karibu na Kamati hii kwa manufaa na
maslahi ya Taifa.
10. Mheshimiwa Spika, sina budi kuwashukuru
kwa dhati Viongozi
wenzangu wa Wizara ya
Madini Mheshimiwa Stanslaus
Haroon Nyongo
(Mb.), Naibu Waziri,
Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb.),
Naibu Waziri na Profesa Simon Samwel Msanjila, Katibu Mkuu. Viongozi
hawa na Watendaji wote
wa Wizara wananipa
ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yangu na kutekeleza majukumu yao kwa kujituma,
tija na ufanisi. Naahidi Bunge lako kuwa kwa ari na kasi tuliyonayo tutahakikisha
rasilimali za madini zinanufaisha Taifa na mchango wa Sekta ya Madini unaongezeka katika Pato la Taifa, maendeleo ya jamii na kupunguza
umaskini nchini.
11. Mheshimiwa
Spika, napenda kutoa pole
kwa Bunge lako
Tukufu, familia, ndugu, jamaa na
wananchi wa jimbo la Songea
Mjini kwa kuondokewa na mpendwa wao, Mheshimiwa Leonidas Tutubert
Gama (Mb.),
na Jimbo la Buyungu,
Kigoma kwa kuondokewa na mpendwa
wao Mhe. Kasuku Samson Bilago (Mb). Aidha,
naomba kuungana
na Waheshimiwa
Wabunge wenzangu kuwapongeza Mheshimiwa Janet Masaburi kwa kuteuliwa
na Mheshimiwa Rais kuwa
Mbunge, Mheshimiwa Dkt. Godwin Ole Mollel, Mbunge wa Jimbo la Siha, Mheshimiwa
Stephen Lemomo
Kiruswa, Mbunge wa Jimbo la Longido,
Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Mbunge wa Jimbo
la Songea Mjini, Mheshimiwa Justin Joseph Monko,
Mbunge wa Jimbo la
Singida Kaskazini na Mheshimiwa Maulid Said Mtulia, Mbunge wa
Jimbo la Kinondoni, kwa kuchaguliwa na kuwa wawakilishi wa wananchi katika Majimbo hayo. Kuchaguliwa na kuteuliwa kwao ni
kielelezo cha kuaminiwa na
wananchi ili kuwawakilisha ipasavyo katika Bunge hili.
12. Mheshimiwa Spika, napenda kipekee kabisa kuchukua nafasi hii kumshukuru Mume
wangu Mpenzi Balozi Mbelwa Kairuki pamoja na watoto wetu wapendwa kwa
kunivumilia, kuniunga mkono na kuniombea kwa Mwenyezi
Mungu ili niweze kutekeleza
majukumu niliyopewa na Mheshimiwa Rais ya usimamizi wa sekta hii nyeti ya
madini.
13. Mheshimiwa Spika,
baada ya utangulizi huo, naomba sasa kuwasilisha
Taarifa
ya Utekelezaji
wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya
Madini kwa Mwaka wa Fedha
wa 2017/18; na Makadirio ya Mapato na Matumizi
kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19.
2.0 DIRA, DHIMA NA
MAJUKUMU YA WIZARA
Dira na Dhima ya Wizara
14. Mheshimiwa Spika,
Dira ya Wizara
ni kuwa Wizara inayoheshimika
Afrika katika kuendeleza rasilimali za madini ili ziweze
kuchangia kwa ufanisi katika uchumi wa Taifa
na ustawi wa Watanzania. Aidha, Dhima
ya Wizara ni kuzibadili rasilimali
za madini ziweze kuchangia katika
ukuaji wa uchumi
wa Taifa na maendeleo endelevu.
Majukumu ya Wizara
15.
Mheshimiwa Spika,
kulingana na
Hati Idhini (Na.144 ya tarehe 22 Aprili, 2016 iliyofanyiwa marekebisho tarehe 15 Oktoba, 2017, majukumu ya Wizara ya Madini ni: -
(i)
Kubuni, kuandaa na kusimamia Sera, Mikakati
na Mipango ya kuendeleza Sekta ya Madini;
(ii) Kusimamia migodi
na
kuhamasisha
shughuli
za uchimbaji pamoja
na utafutaji wa
madini kwa kutumia tafiti za kijiofizikia na kijiolojia (Geophysical
na Geological surveys);
(iii) Kuratibu na kusimamia uongezaji thamani
madini kwenye biashara ya madini; kukuza ushiriki wa Wazawa (local
content) kwenye shughuli za
utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini nchini;
(iv) Kusimamia na kuratibu shughuli na maendeleo
ya wachimbaji wadogo;
kusimamia Taasisi na
Mamlaka zilizoko chini ya Wizara;
na
(v) Kuratibu na kusimamia maendeleo na utekelezaji wa
majukumu kwa watumishi wa Wizara.
3.0 MAPITIO YA
UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA WA 2017/18
(a) Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa iliyokuwa Wizara ya Nishati
na Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18
16. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18
iliyokuwa Wizara ya Nishati na
Madini iliidhinishiwa Bajeti ya jumla ya shilingi 998,337,759,500. Kati ya fedha hizo, shilingi
938,632,006,000 sawa na asilimia 94 ya Bajeti yote
ilikuwa ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo na shilingi 59,705,753,500, sawa na asilimia 6 ya Bajeti yote ilikuwa ni kwa ajili
ya Matumizi ya Kawaida.
(b) Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa
Fedha wa 2017/18
17. Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka
wa Fedha wa 2017/18 ukiondoa
fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za Sekta ya Nishati, Sekta ya Madini
ambayo sasa inasimamiwa na Wizara
ya Madini, iliidhinishiwa na Bunge lako Tukufu
jumla ya shilingi 52,445,367,000. Kati
ya fedha hizo, shilingi 21,783,000,000 sawa na
asilimia 41.53 ya
Bajeti yote zilikuwa
ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo
na shilingi
30,662,367,000 sawa na asilimia 58.47 ya Bajeti yote zilikuwa ni kwa ajili ya Matumizi
ya Kawaida kwa Wizara na Taasisi zake. Kwa upande wa fedha za Matumizi ya Kawaida, shilingi 13,912,800,000 sawa na asilimia 45.37 zilitengwa kwa ajili ya Matumizi
Mengineyo (O.C) na shilingi 16,749,567,000 sawa na asilimia 54.63 zilitengwa kwa ajili ya Mishahara
(P.E) ya watumishi wa Wizara na Taasisi zilizopo chini yake. Aidha,
Wizara ilipangiwa kukusanya maduhuli ya Serikali ya kiasi cha shilingi
194,663,501,763.
18. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe
31 Machi, 2018 Wizara
ilipokea jumla ya Shilingi
19,173,608,450.31 kutoka Hazina sawa
na
asilimia 36.56 ya
Bajeti yote ya Wizara ya Shilingi
52,445,367,000 kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18. Kati ya fedha zilizopokelewa, Shilingi 834,976,618
ni fedha za Maendeleo sawa na asilimia 3.83 ya bajeti
yote ya Maendeleo ya Shilingi 21,783,000,000. Kwa upande
wa Matumizi ya Kawaida, Shilingi 18,338,631,832.31 zilipokelewa sawa na asilimia 59.81 ya fedha zote za
Matumizi ya Kawaida zilizotengwa ambazo zilikuwa Shilingi 30,662,367,000. Kati ya fedha za Matumizi
ya Kawaida zilizopokelewa Shilingi 8,227,481,851 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (O.C) na Shilingi
10,111,149,981.31 ni kwa ajili
ya Mishahara (P.E)
kwa watumishi wa Wizara
na Taasisi zake.
19. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango na
Bajeti kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18, ulizingatia pamoja na mambo mengine:
Hati Idhini ya kuanzishwa
kwa Wizara ya Madini Namba 144 ya tarehe 22 Aprili,
2016 iliyofanyiwa marekebisho tarehe 15 Oktoba, 2017; Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025; Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka
2015 - 2020; Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21); Malengo
ya Maendeleo Endelevu 2030; Sera ya Madini ya Mwaka 2009; Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 na Kanuni zake.
Vilevile, umezingatia maoni na ushauri wa Kamati Maalum
ya Mheshimiwa Rais ya kuchunguza aina, wingi na thamani ya madini
mbalimbali yaliyopo kwenye mchanga wa madini (Makinikia) unaosafirishwa nje ya nchi iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Hamis Mruma; Kamati Maalum ya Mheshimiwa Rais ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na
mchanga wa madini unaosafirishwa nje ya nchi iliyoongozwa na Profesa Nehemiah Eliakim Osoro; Kamati Maalum ya Spika ya kuchunguza
Biashara ya Tanzanite iliyoongozwa na
Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb.) ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Madini; Kamati Maalum ya Spika ya kuchunguza Biashara
ya Almasi iliyoongozwa na Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb.); na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini.
20. Mheshimiwa Spika,
katika kutekeleza Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha wa
2017/18, maeneo yafuatayo yalipewa kipaumbele: kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Serikali
yatokanayo na rasilimali madini; kudhibiti utoroshaji
wa madini; kuendeleza wachimbaji wadogo na wa kati wa madini; kuhamasisha shughuli
za uongezaji thamani madini; kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na ukaguzi wa
migodi ikiwemo ukaguzi wa afya, usalama, mazingira na uzalishaji wa madini
katika migodi midogo, ya kati na mikubwa; kuendelea kuhamasisha uwekezaji
katika Sekta ya
Madini na kuboresha Sera,
Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali kuhusu rasilimali
madini. Vilevile, kipaumbele
kiliwekwa katika kuimarisha Taasisi
zilizo chini ya Wizara hususan Tume
ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini (MRI),
Kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) na Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji
katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi asilia (TEITI). Maeneo mengine
ya kipaumbele yalikuwa ni
kuwajengea uwezo
watumishi wa Wizara katika
fani mbalimbali pamoja
na kuendelea kuboresha
mazingira ya ofisi.
(c) Ukuaji na Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa
21. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2017, Sekta
ya Madini ilikua
kwa asilimia 17.5
ikilinganishwa na asilimia 11.5 ya Mwaka 2016. Kuongezeka kwa kiwango cha ukuaji wa Sekta ya Madini kulitokana na kuimarishwa kwa udhibiti wa biashara haramu na utoroshwaji wa madini; kuimarishwa kwa ukaguzi na usimamizi katika sehemu za uzalishaji, biashara ya madini; na
usafirishaji wa madini nje ya nchi; kuongezeka
kwa viwango vya mrabaha na kuanzishwa
kwa ada ya ukaguzi wa madini kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yaliyofanyika Mwaka
2017 na Kanuni zake.
22. Mheshimiwa Spika, vilevile, mchango wa Sekta
ya Madini katika Pato la Taifa
umeendelea kuimarika ambapo katika Mwaka 2017 mchango huo ulifikia asilimia 4.8. Kwa upande wa thamani ya mauzo ya
madini nje ya nchi, mauzo yalifikia Dola za Marekani
1,810,697,000 mwaka 2017. Ni matarajio
yetu kuwa thamani ya mauzo itaendelea kuongezeka tena baada
ya kukamilisha mageuzi makubwa ambayo tuliyaanzisha ikiwa ni pamoja na uongezaji thamani
madini ndani ya nchi.
(d) Uzalishaji na Ukusanyaji wa Maduhuli ya
Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18
23. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi
Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya kilo 30,953.59
za dhahabu zilizalishwa na Migodi Mikubwa
na ya Kati ya Bulyanhulu, Buzwagi,
Geita, New Luika,
North Mara na STAMIGOLD na
kusafirishwa nje ya nchi. Vilevile, kilo 2,021.4 za dhahabu zilizalishwa na wachimbaji
wadogo wa madini na wachenjuaji wa
marudio. Aidha, kiasi cha karati
248,083.94 za almasi kilizalishwa katika Mgodi wa Almasi wa Mwadui
(Williamson Diamond Limited) uliopo
Shinyanga, pia kiasi cha karati 43,285.31 kilizalishwa katika Mgodi
wa
El
Hilal na Tanzanite (ghafi) yenye
kilogramu 535.99 ilizalishwa na Mgodi wa TanzaniteOne. Vilevile, kiasi cha kilo 516,408.93 cha
madini mengineyo ya vito kilizalishwa. Kwa upande
wa makaa ya mawe jumla ya
tani 385,352 zilizalishwa kwenye Mgodi wa Ngaka Mkoani Ruvuma.
Aidha, tani 3,125,399 za madini ya ujenzi na viwandani zilizalishwa.
Uzalishaji huu kwa ujumla wake uliiwezesha Serikali kukusanya mrabaha wa Shilingi 175,518,751,221.49.
24. Mheshimiwa Spika, kutokana
na mageuzi ambayo
tumeyafanya, Wizara iliratibu mnada
wa madini ya vito ya tanzanite
uliofanyika tarehe 18 hadi
21 Desemba, 2017. Lengo la mnada huo lilikuwa ni kukuza biashara
ya ushindani baina ya wachimbaji na wauzaji wa madini haya na
wanunuzi wa kimataifa ili kupata bei bora zaidi na ya ushindani kwa njia ya
uwazi na kuwapatia wachimbaji wa madini ya tanzanite
soko la uhakika. Katika
mnada huo, tanzanite yenye uzito wa kilo 47 iliuzwa
kwa jumla ya Dola za Marekani 820,744 sawa na shilingi 1,839,476,075. Mapato yaliyokusanywa na
Serikali ni mrabaha wa shilingi 110,368,564.50, ada ya ukaguzi
shilingi
18,394,760.75 na ushuru wa
huduma
wa shilingi
5,518,428.20.
25. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maduhuli
ya Sekta
ya
Madini,
katika
Mwaka
wa
Fedha
wa
2017/18 Wizara ya
Madini, ilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi 194,663,501,763 na
Bunge lako Tukufu kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vikiwemo mrabaha; ada ya
mwaka; ada za kijiolojia; ada ya uchambuzi wa madini; uchapishaji na uuzaji wa
nyaraka za zabuni; stakabadhi nyinginezo; marejesho
ya fedha za Serikali; tozo mbalimbali zinazotokana na adhabu na ada za ukaguzi. Napenda
kulitaarifu Bunge lako tukufu
kuwa hadi kufikia tarehe 31 Machi,
2018 jumla ya maduhuli ya shilingi 225,006,324,173.21
yalikuwa yamekusanywa. Kiasi
hiki ni sawa
na asilimia
115.59 ya lengo lililowekwa katika Mwaka wa Fedha
wa 2017/18.
26. Mheshimiwa Spika,
ongezeko la makusanyo ya maduhuli limetokana na kuongezeka kwa
viwango vya mrabaha kutoka asilimia
nne hadi sita kwa madini
ya metali, na kutoka asilimia tano hadi sita kwa madini ya vito;
kuanzishwa kwa tozo ya ukaguzi ya
asilimia moja ya mauzo ya madini; usimamizi wa biashara ya madini na kuimarisha
udhibiti wa utoroshwaji wa madini kwa
kushirikiana na wananchi na Vyombo vya
Ulinzi na Usalama.
(e) Udhibiti wa Biashara ya Madini
27. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kufanya ukaguzi wa uzalishaji wa
madini kwenye migodi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata takwimu
sahihi za madini
yanayozalishwa na kuuzwa ndani na nje ya nchi; thamani
halisi ya madini hayo; na mrabaha
stahiki unaopaswa kulipwa. Ukaguzi huo hususan kwenye migodi na mitambo ya
uchenjuaji umekuwa ukifanyika kwa kushirikiana
na Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Kufuatia jitihada hizo, makusanyo ya mrabaha yameongezeka. Kwa mfano, hadi kufikia mwezi
Machi, 2018 Ofisi
ya Madini (Chunya) imeweza
kukusanya
kiasi cha shilingi
718,667,100.41 na Ofisi ya Madini (Mwanza)
kiasi cha
shilingi 9,843,380,762.80 ikilinganishwa na shilingi
416,968,335.28 na shilingi 6,181,589,371.75
zilizokusanywa na Ofisi
hizo kwa Mwaka
wa Fedha wa 2016/17, sawia. Wizara pia
imeanzisha utaratibu mpya wa uombaji
wa vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi, ambapo mchimbaji au mfanyabiashara
wa madini hulazimika kuwasilisha sampuli GST kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara
ili kufahamu ubora stahiki wa sampuli au madini yanayoombewa kibali cha kusafirishwa nje ya nchi. Vilevile, katika kudhibiti shughuli
za uzalishaji na biashara ya madini
ya tanzanite ambayo hupatikana Tanzania
pekee, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ilijenga ukuta wenye mzingo wa
kilomita 24.5 katika Migodi ya Mirerani
kwa lengo la kudhibiti utoroshwaji wa
madini ya tanzanite kwenda nje ya nchi.
28. Mheshimiwa
Spika,
Serikali kupitia Wizara ya Madini ilizuia uingizaji wa madini yanayopatikana
nchini kama vile makaa ya mawe na jasi ili
kuhakikisha madini haya yananunuliwa hapa nchini kwa lengo la kukuza
soko la ndani la madini hayo. Kutokana na udhibiti huo, jumla ya tani 431,029.14 za makaa ya mawe
zenye
thamani
ya
Dola
za
Marekani
18,314,709.53 ziliuzwa hadi kufikia Machi, 2018
ikilinganishwa na tani 429,682.85
zilizouzwa Mwaka wa Fedha wa
2016/17 zenye thamani ya Dola za
Marekani 16,931,162.29. Vilevile, tani
121,186.82 za
jasi zenye thamani
ya Dola za Marekani 3,120,024.09
ziliuzwa kufikia Machi,
2018 ikilinganishwa na tani
181,080.34 zilizouzwa Mwaka wa Fedha wa 2016/17 zenye thamani ya Dola za Marekani 5,283,526.13. Wizara imeanza maandalizi ya uanzishwaji wa masoko
ya madini ya dhahabu na vito ikiwemo
tanzanite, almasi na madini
mengine. Maandalizi haya yanashirikisha Timu ya Wataalamu
na wadau mbalimbali wa biashara ya madini
na Serikali.
29. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha udhibiti dhidi ya utoroshwaji
wa madini, Serikali
imeendelea na mkakati wa kukabiliana na biashara haramu ya madini ambapo
Wizara kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege
(TAA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA) inaendelea kufanya ukaguzi kupitia madawati yaliyopo katika
viwanja vya ndege, Bandari na mipaka
ya nchi. Kufuatia
kaguzi hizo, jumla ya matukio 9 ya
biashara haramu ya madini yenye thamani ya Dola
za Marekani 229,037.85 na shilingi
1,500,000,000 yaliripotiwa kutokea katika
Vituo vya
Kutokea (Exit Points)
nchini katika kipindi
cha Julai,
2017 hadi Aprili, 2018 ikilinganishwa
na
matukio
11 ya biashara
haramu ya madini yenye thamani
ya shilingi 268,700,000 yaliyotokea Mwaka wa Fedha wa 2016/17. Aidha, Serikali imekuwa ikiwafikisha wahusika wa matukio hayo katika Vyombo vya Sheria.
Wizara bado inaona kuna changamoto
ya utoroshwaji wa madini pamoja na
kupungua kwa matukio ya ukamataji kwa watoroshaji
madini. Hivyo, azma ya Wizara ni
kuimarisha udhibiti kwenye mipaka yote ili hatimaye kuondoa kabisa mianya ya
utoroshwaji wa madini nchini.
30. Mheshimiwa Spika, pamoja na uimarishaji
huo, bado kuna changamoto mbalimbali katika udhibiti wa shughuli za madini nchini.
Hivyo, natoa rai na kuwaomba
wadau wote wa Sekta ya Madini na wananchi wote kushiriki katika ulinzi wa
rasilimali madini ili ziweze kuwa na manufaa makubwa zaidi kwa Taifa.
(f ) Ujenzi wa Ukuta kwenye Migodi ya Mirerani
31. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa
mwezi Juni, 2017 uliunda Kamati
Maalum ya Bunge iliyoshughulikia namna shughuli za
uchimbaji na uuzaji wa madini ya tanzanite zinavyofanyika nchini. Kamati hiyo
ilitoa mapendekezo mbalimbali ikiwemo kuwepo kwa mfumo mpya wa udhibiti wa
madini ya tanzanite.
32. Mheshimiwa Spika, kutokana na mapendekezo hayo, tarehe 20 Septemba, 2017 Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli aliliagiza Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kujenga
ukuta kuzunguka eneo la migodi ya tanzanite Mirerani ili kudhibiti utoroshwaji wa madini
hayo. Kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais, Ukuta huo ulianza kujengwa kuanzia tarehe 1 Novemba, 2017 na kukamilika tarehe 15 Februari, 2018 na kuzinduliwa na
Mheshimiwa Rais tarehe 6 Aprili, 2018.
33. Mheshimiwa Spika, kutokana na udhibiti
huo, katika kipindi kifupi cha
miezi mitatu tu cha Januari hadi
Machi 2018, Wizara imefanikiwa
kukusanya mrabaha wa kiasi
cha jumla ya shilingi 714,670,000. Katika kiasi hicho, shilingi 614,670,000 zinatokana na makusanyo kutoka kwa wachimbaji wadogo. Kiasi
hicho kilichokusanywa
kinazidi jumla ya makusanyo ya mrabaha wa miaka
mitatu iliyopita kutoka kwa wachimbaji wadogo. Pia, Bunge
lako Tukufu litapendezwa kufahamu kwamba katika Mwaka 2015 tulikusanya mrabaha
wa shilingi 166,850,000; Mwaka
2016 shilingi 71,860,000; na
Mwaka 2017 shilingi 147,140,000 kutoka kwa wachimbaji wadogo.
(g) Kuimarisha Usalama Migodini
34. Mheshimiwa Spika, pamoja na majukumu
mengine Wizara hii ina
wajibu wa kuhakikisha usalama wa shughuli za uchimbaji migodini. Kwa msingi huo, Wizara
imeendelea kufanya kaguzi
mbalimbali ambapo kwa Mwaka
wa Fedha wa 2017/18 jumla ya leseni za migodi 2,204 zilikaguliwa. Kati ya leseni hizo, 6
ni za uchimbaji mkubwa,
134 za uchimbaji wa kati na 2,064
za uchimbaji mdogo. Wizara pia
iliendelea kufanya uchunguzi wa ajali na matukio yanayotokea migodini kwa lengo
la kubaini changamoto za kiusalama ili kuweza kuzuia matukio ya aina hiyo
katika migodi. Katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, jumla ya ajali 14
ziliripotiwa na kuchunguzwa katika migodi. Uchunguzi huo uliofanyika ulibaini kuwa wachimbaji 33
walifariki dunia; 50 walijeruhiwa, kutibiwa na kuendelea na kazi zao. Matukio
hayo ni kama ifuatavyo: Kanda ya Kati (Singida na Dodoma) matukio 5;
Kanda ya Kaskazini (Arusha, Manyara na Kilimanjaro) matukio 3; Kanda ya Kusini Magharibi (Mbeya, Songwe na Iringa) matukio
2; Kanda ya Kati Magharibi (Shinyanga na Tabora) tukio 1; na Kanda ya Ziwa Victoria Mashariki (Mara na Simiyu) tukio 1. Uchunguzi
wa ajali hizo, ulibaini kuwa chanzo kikubwa cha ajali
hizo ni kutozingatia kanuni za usalama. Kufuatia
uchunguzi huo, ripoti
ziliandaliwa
na wahusika walipewa nakala
ya ripoti husika ili kuboresha usalama
katika maeneo yao na wengine
42 leseni zao
zilisimamishwa hadi
waliporekebisha na kufuata
kanuni za usalama
migodini ambapo jumla ya leseni 38 zilikidhi matakwa
ya kiusalama na kuruhusiwa kuendelea na kazi. Mathalan, katika eneo la Irasanilo - Solemba,
Buhemba shughuli za uchimbaji zilisimamishwa kwa muda wa mwaka mmoja ili kurekebisha kasoro za
kiusalama.
35. Mheshimiwa Spika, kanuni ya 71 ya Kanuni za
Afya, Usalama na Utunzaji wa Mazingira za Mwaka
2010 inaelekeza wachimbaji kutoa taarifa ya kusudio
la kubadilisha teknolojia yoyote katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji na
kuwasilisha taarifa hiyo kwenye Ofisi za Madini. Hata
hivyo, kumekuwa na hulka
ya wachimbaji kutumia teknolojia ya vifaa mbalimbali katika shughuli
za uchimbaji bila kuzingatia uwezo
na ubora wa vifaa hivyo. Hali hii inasababisha uwepo wa ajali nyingi
ambazo zingeweza kuepukika. Mathalan, ajali iliyotokea tarehe 06 Aprili, 2018 Wilayani Bahi, ilisababishwa na winchi inayotumika kubebea
mizigo kutumika kubebea watu. Katika uchunguzi ilibainika kuwa wahusika
walikuwa hawafanyi ukaguzi wa kamba mara kwa mara. Timu yangu ya ukaguzi ilipowahoji wahusika walionusurika kwenye
ajali hiyo, ilibaini kuwa wahusika hao hawakuwa na taarifa kuhusu uwezo
wa winchi husika
kunyanyua mizigo ila yalikuwa ni mazoea ya kutumia chombo
hicho. Natoa rai kwa wachimbaji na wawekezaji wote katika Sekta ya Madini
nchini kufuata maelekezo ya Kanuni za Afya, Usalama na Utunzaji wa Mazingira
zilizopo ili wawe salama katika shughuli zao za uchimbaji.
(h) Kuimarisha Masuala ya Afya Migodini
36. Mheshimiwa Spika, ili kupunguza
athari za kiafya zinazoweza
kuwapata wafanyakazi migodini kutokana na uvutaji wa vumbi na hewa chafu kuzidi
kiwango stahiki kwa muda mrefu; ukaaji
wa muda mrefu kwenye eneo lenye kelele
nyingi; na kutumia vifaa vyenye viwango vya chini kulingana na mahitaji ya eneo husika, Wizara yangu imeimarisha ukaguzi
wa mazingira ya kazi migodini pamoja na kuhamasisha uwepo na matumizi ya vifaa kinga. Ikumbukwe pia, utumiaji wa
vifaa vya kinga ni sehemu ya kuzuia athari za kiafya. Kutotumia vifaa vya kinga
kunaweza kusababisha matatizo ya kiafya kama kuathiri mfumo wa kupumua
au kuambukizana magonjwa
kama Kifua Kikuu (TB) ikizingatiwa kuwa wanafanya kazi
kwenye maeneo yenye changamoto ya ujazo wa hewa. Ukaguzi wa mara kwa mara kuhusiana na utumiaji wa vifaa vya kinga umekuwa ukifanyika migodini.
Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea na utafiti
ili kubaini ukubwa wa changamoto ya TB migodini na kutoa ushauri
wa namna bora ya kujikinga
na maradhi hayo.
37. Mheshimiwa Spika,
kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana,
Ajira na Wenye Ulemavu; na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto tunaendelea kuimarisha ukaguzi wakati
wa kuajiriwa; na upimaji wa afya mara kwa mara kwa wafanyakazi wote wa
migodini. Pia, Wizara inaendelea kuweka utaratibu wa kuchunguza afya wakati mfanyakazi anaacha
au kuachishwa kazi. Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa shughuli
za uchimbaji na uchenjuaji madini zinafanywa kwa kujali afya za wafanyakazi.
(i) Kuimarisha Utunzaji wa Mazingira Migodini na Kwenye Miradi ya
Uchenjuaji Madini
38. Mheshimiwa Spika, Sheria
ya Madini ya Mwaka
2010 pamoja na Marekebisho
yake ya Mwaka 2017 na Kanuni
zake zinasisitiza umuhimu
wa utunzaji wa mazingira. Kama
nilivyoeleza awali, shughuli za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini
zinapaswa kuhakikisha usalama wa watu na mazingira katika maeneo wanayofanyia
kazi. Kwa mujibu wa Kifungu cha 60 cha Sheria ya Madini, moja ya masharti ya
leseni zitolewazo kwa wachimbaji madini ni kutoa tamko la utunzaji wa mazingira ambapo
kwa mchimbaji mdogo hutakiwa
kuwasilisha Mpango wa Utunzaji wa Mazingira (Environmental
Protection Plan) kwa Afisa Madini Mkazi.
Kwa upande wa
uchimbaji wa kati na
mkubwa, wamiliki hutakiwa
kuandaa Tathmini ya Athari za Mazingira
na Mpango wa Kutunza Mazingira (Environmental Impact Assessment (EIA)
and Environmental Management Plan (EMP)). Lengo kuu la kuwa
na maandiko haya
ni kuhakikisha mwenye
mradi anatambua kuwa shughuli
anazofanya zina athari kwa
mazingira na kufahamu
maandalizi yake kwenye utunzaji na uhuishaji wa mazingira ili kuwa rafiki kwa matumizi ya binadamu akiwa
bado anaendelea kuwekeza au anapomaliza uchimbaji katika eneo
husika.
39. Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu inaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Kanuni
ya 177
– 184 za Mwaka 2010 za Uchimbaji Salama, Afya na Utunzaji wa
Mazingira zinazoelekeza migodi kuwa na miundombinu muhimu ya kutupa mabaki ya miamba,
mabwawa ya kutunzia maji na mabaki yenye kemikali yatokanayo na uchenjuaji wa madini (Waste Rocks
Dumps and Tailings Storage Facilities). Katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, Wizara yangu ilimuelekeza mmiliki wa Mgodi
wa Dhahabu wa Nyarugusu kulipa fidia kwa waathirika kutokana na bwawa
la kuhifadhia maji yenye
kemikali zilizotumika kuchenjua madini ya dhahabu kumwaga maji hayo katika
mashamba na kuathiri mazao ya wakulima kutokana
na mvua kubwa kunyesha ndani ya muda mfupi. Licha ya kulipa fidia kwa
waathirika, mmiliki alielekezwa kufanya usanifu mpya wa bwawa hilo ili liweze
kuhimili mvua kubwa pamoja na kuandaa
mpango wa dharura
wa ukusanyaji maji hayo
wakati wa mvua. Pia, Wizara
imeendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maeneo hayo ili kuona
uhimilivu wa miundombinu husika.
40. Mheshimiwa Spika, hali kadhalika, Wizara yangu imeendelea kuhakikisha kuwa migodi
ya madini inapofungwa,
mazingira ya eneo husika yanaachwa katika hali ya usalama. Kwa mujibu wa Kanuni ya 206
ya Kanuni za Madini (Usalama wa Afya Mgodini na Utunzaji wa Mazingira) za Mwaka 2010, Migodi ya kati
na mikubwa inatakiwa kuwasilisha Mpango
wa Ufungaji Migodi (Mine
Closure Plan). Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Kampuni ya ACACIA inayomiliki Migodi ya
dhahabu ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi ilishawasilisha Mpango wake wa
Ufungaji Mgodi na kuweka Hati Fungani ya Mazingira. Pia, Mgodi wa Dhahabu
wa
Geita Gold Mining Limited (GGM) uko kwenye hatua
za kukamilisha utaratibu wa kuweka Hati Fungani. Vilevile, Migodi ya Dangote, TanzaniteOne, New Luika na Williamson Diamonds nayo inakamilisha majadiliano ili kuhakikisha usalama na utunzaji wa mazingira unazingatiwa.
(j) Usimamizi wa Matumizi ya Baruti
41. Mheshimiwa Spika, udhibiti wa matumizi ya baruti kwenye shughuli
mbalimbali zikiwemo za utafutaji wa mafuta na gesi na uchimbaji
wa madini ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa usalama na kwa
madhumuni yaliyokusudiwa uliendelea kufanyika. Katika ukaguzi uliofanywa na Wizara, ilibainika kuwa jumla ya tani 22,474
za baruti na vipande 1,749,203 vya fataki vilitumika kwenye shughuli mbalimbali.
Aidha, jumla ya maghala 37 ya
kuhifadhia baruti na fataki yalikaguliwa katika Mikoa yote
yenye shughuli za uchimbaji wa madini ili kubaini
utunzaji salama kwa mujibu wa matakwa
ya Sheria ya Baruti ya Mwaka
1963 na Kanuni zake.
(k) Uendelezaji wa Wachimbaji Wadogo
42. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kuwa Sekta
ya Madini inatoa ajira kati ya 500,000 na 1,500,000 kutokana na utafiti
uliofanywa na UNEP Mwaka 2012, Wizara
itaendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kujiajiri kupitia Sekta ya Madini kwa
kuwatambua, kuwaendeleza, kuwarasimisha na kuwapatia maeneo ya uchimbaji wa
madini. Vilevile, Wizara itaendelea kuwapatia taarifa
za kijiolojia, kiufundi
na kuwawezesha kupata huduma
za kifedha na masoko. Aidha, Wizara
itaendelea kuwapatia mafunzo
ya
teknolojia na maarifa ya kisasa kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uchimbaji
ili wakue na waweze kuwa wachimbaji wa kati
na wakubwa katika
siku za usoni.
Serikali inaamini kuwa uchimbaji
mdogo siyo hadhi ya kudumu bali
ni hatua ya mpito kuelekea katika uchimbaji wa kati hadi mkubwa. Sababu za
kufanya hivyo zipo wazi kwa kuwa wachimbaji wadogo
endapo watafanikiwa kukua,
mapato yao yanaweza kuwekezwa zaidi kwenye Sekta ya Madini na sekta nyingine nchini na hivyo kuchangia
zaidi kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini, ukuaji
wa uchumi na Pato la Taifa na hatimaye
kuwanufaisha watanzania wengine.
43. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia
GST na STAMICO chini ya Mradi
wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP)
ilikamilisha utafiti wa kina
wa kijiosayansi uliohusisha uchorongaji
na ukadiriaji wa mbale katika maeneo ya wachimbaji wadogo kwenye maeneo sita ya
ujenzi wa Vituo vya Umahiri vya
Katente (Bukombe), Itumbi (Chunya), Kona Z (Tanga),
Kapanda (Mpanda), Buhemba (Musoma) na Kyerwa (Bukoba). Vituo hivyo vitatumika kwa ajili ya mafunzo ya uongezaji thamani
madini na uchimbaji salama pamoja na kuongeza uzalishaji, tija na hivyo
kuongeza mapato kwa wachimbaji wadogo. Ukadiriaji wa mbale umeonesha kuwepo
kwa takriban wakia
47,605 za dhahabu katika
maeneo ya Mpanda
(D – Reef na Kapanda); wakia 10,737.33 za dhahabu
katika eneo la Buhemba;
wakia 46,663 za dhahabu
eneo la Chunya (Itumbi);
na wakia 9,459 za dhahabu katika eneo la
Katente. Aidha, ukadiriaji wa mbale katika maeneo ya Tanga
(Kiomoni, Kange na
Mkulumuzi) na Kyerwa (Kaborishoke) umeonesha uwepo wa tani
403,056,469 za miamba chokaa yenye
ubora
wa
zaidi ya asilimia 48 ya chokaa (calsium); na tani
1,409,742.15 za bati sawia. Maandalizi
ya ujenzi wa Vituo hivyo yanaendelea. Aidha,
matokeo ya utafiti huo yatatumika kuainisha njia bora
za uchenjuaji kwenye kila eneo na kuwasaidia wachimbaji wadogo kupunguza
upotevu wa madini wakati wa uchenjuaji.
44. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Mgodi wa Mfano wa Lwamgasa unaendelea kujengwa
ambapo
kwa
sasa umefikia asilimia 70. Gharama za mgodi huo ni Dola za Marekani 584,800. Mgodi huu utawezesha
Chama cha Washirika wa Kijiji cha
Lwamgasa na wachimbaji wanaozunguka Mgodi huo kuchimba na kuchenjua dhahabu
kwa kutumia teknolojia sahihi na yenye
gharama nafuu. Vilevile, mafunzo
mbalimbali yamekuwa yakitolewa kwa
wachimbaji wadogo ambapo kwa
Mwaka wa Fedha wa 2017/18. Jumla ya wachimbaji
wadogo 4,468 walipatiwa mafunzo
katika Mikoa 13 ambayo ni Manyara, Morogoro, Tanga,
Pwani, Shinyanga, Geita, Mara, Katavi,
Singida, Dar es Salaam,
Mbeya, Lindi na Mtwara. Vilevile, STAMICO kwa kushirikiana na Tanzania Gender Network Program (TGNP)
na
Women
in
Mining
Association
(WIMA) ilitoa mafunzo kwa
wachimbaji wadogo katika eneo la Mwalazi mkoani Morogoro ambapo jumla ya
wachimbaji 37 walipatiwa mafunzo kuhusu namna ya
kuchakata madini ya dolomite kwa
kuzingatia matumizi na
mahitaji ya soko.
45. Mheshimiwa Spika, mafunzo mengine yalito- lewa na Ofisi ya Madini Mirerani kwa kushirikiana na Wakala wa Usalama
Mahali pa Kazi (OSHA) katika
eneo la Mirerani; Ofisi ya Madini Geita kwa
kushirikiana na OSHA katika
Mkoa wa Geita;
Ofisi ya Madini
Shinyanga kwa kushirikiana na OSHA na TRA katika Mkoa wa Shinyanga; Ofisi ya
Madini Chunya kwa kushirikiana
na Kampuni ya PAULSAM katika Wilaya ya Chunya; Ofisi ya Madini Singida
kwa kushirikiana na Vyama vya Wachimbaji Wadogo na Shirikisho la Vyama
vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) katika Mkoa wa Singida;
Ofisi ya Madini Mpanda katika Wilaya ya Mpanda; Ofisi ya Madini Songea; Ofisi ya Madini Musoma katika Wilaya za Butiama, Tarime na Bunda; Ofisi ya Madini Mtwara katika
Mikoa
ya
Lindi
na
Mtwara; na Ofisi
ya Madini Dar es Salaam
katika Mikoa ya Morogoro,
Tanga na Pwani. Mafunzo hayo yalihusu
usalama na afya mahali pa kazi.
(l) Sera, Sheria na
Miongozo mbalimbali kuhusu Rasilimali Madini
46. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha
wa 2017/18, Serikali chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa Rais, imefanya
mageuzi makubwa na ya msingi kwenye Sekta ya Madini.
Tunalishukuru Bunge lako Tukufu
kwa kuridhia na kupitisha Marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kupitia Marekebisho
ya Sheria mbalimbali yaliyofanywa na Sheria ya Marekebisho Na.7 ya Mwaka
2017. Katika kuwezesha utekelezaji wa Sheria
hiyo, Wizara ya Madini
ilitengeneza Kanuni za Madini zipatazo saba ambazo ni:-
(i)
Kanuni za Madini
(Haki Madini) za Mwaka 2018;
(ii) Kanuni za Madini (Biashara ya Madini na
Makinikia) za
Mwaka 2018;
(iii)
Kanuni za Madini (Huduma na Bidhaa Madini zinazotolewa na Watanzania) za Mwaka 2018;
(iv) Kanuni za Madini
(Madini
Mionzi)
za
Mwaka
2018;
(v)
Kanuni za Madini (Uongezaji Thamani
Madini) za
Mwaka 2018;
(vi)
Kanuni za Madini (Utafiti wa Kijiolojia) za Mwaka
2018; na
(vii)
Kanuni za Madini
(Ukaguzi na Uchunguzi wa
Nyaraka) za Mwaka 2018.
47. Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 105 (1) na (2) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na
Marekebisho yake ya Mwaka 2017
kinamtaka mmiliki wa leseni ya utafutaji na uchimbaji wa madini kuandaa
Mpango wa Mwaka wa
Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR). Mpango
huo lazima ukubalike kwa pamoja na Mamlaka
ya Serikali ya Mtaa husika au Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kushauriana na Waziri anayehusika na Serikali za Mitaa na Waziri anayehusika na masuala
ya fedha. Aidha, Kifungu cha 105(4) kinaitaka kila Halmashauri ya Serikali ya
Mtaa kuandaa Mwongozo wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii, kusimamia
utekelezaji wa Mpango
Kazi wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa
Jamii na kutoa elimu kwa umma kuhusu miradi iliyopo katika maeneo yao. Hivyo, Wizara ya Madini inawahimiza wadau
wote wa Sekta
ya Madini wazingatie Sheria ya Madini
wanapotekeleza majukumu yao.
(m) Uimarishaji wa Usimamizi wa Sekta ya
Madini
48. Mheshimiwa
Spika,
Marekebisho ya Sheria
ya Madini ya Mwaka 2017 yamewezesha kufanyika kwa
mabadiliko katika usimamizi wa Sekta ya Madini ambapo majukumu ya iliyokuwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na baadhi ya majukumu ya Kamishna wa Madini yamehamishiwa Tume ya Madini. Pia, Ofisi zilizokuwa za
Kanda na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi
zipo chini ya Tume ya Madini. Kutokana na mabadiliko hayo, kila Mkoa utakuwa na
Ofisi ya Afisa Madini Mkazi na kila mgodi mkubwa na wa kati utakuwa na Afisa Mgodi Mkazi. Mabadiliko hayo yamelenga kuongeza ufanisi katika
utekelezaji wa majukumu ya Wizara
hususan kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali;
kuondoa
muingiliano
wa
majukumu na kuimarisha usimamizi wa rasilimali madini ili kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
(n) Uongezaji Thamani Madini
49. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea na jitihada mbalimbali za
kuhakikisha shughuli za uongezaji
thamani madini zinafanyika
ndani ya nchi ikiwa
ni pamoja na
kusimamia ipasavyo zuio la kusafirisha madini ghafi nje ya nchi.
Wizara ilitoa matangazo ya
kukaribisha uwekezaji katika ujenzi wa vinu vya uchenjuaji kwa ajili ya kusafisha na kuongeza
thamani madini ya metali - smelter na refineries hapa nchini. Jumla ya maombi
27 ya uwekezaji kwenye smelter na refineries yaliwasilishwa na uchambuzi unaendelea kufanyika ili kupata mwekezaji
atakayekidhi vigezo.
50. Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa madini
ya vito, Wizara imeendelea kukijengea uwezo Kituo cha
Jimolojia Tanzania (TGC) kilichopo Arusha kwa kuimarisha miundombinu yake.
Vilevile, Kituo kimepata usajili
wa kudumu kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa namba
ya usajili REG/SAT/033 wa kutoa mafunzo ya Diploma in Gem
& Jewellery
Technology mwezi Oktoba, 2017.
Mafunzo
hayo yatakuwa ya muda
wa miaka 3 na yanatarajiwa kuanza
mwezi Agosti, 2018.
Katika kuwajengea uwezo wakufunzi wazawa, Wizara iliingia
Mkataba na Kampuni ya Centre
for Development of Gem & Jewellery
Technology kutoka nchini India
kuleta wakufunzi saba (7) ambao watatoa mafunzo mbalimbali
ya vito na usonara katika Kituo
hiki wakishirikiana na wakufunzi
wazawa. Aidha, Kituo kimeendelea kutoa mafunzo ya usanifu wa madini ya vito (lapidary) katika ngazi ya Astashahada
ambapo jumla ya wanafunzi wanawake
18 walidahiliwa chini
ya ufadhili wa Wizara ya Madini
pamoja na Kamati ya maonesho ya Madini ya Vito
ya Arusha (Arusha Gem Fair).
(o) Kazi zilizotekelezwa kupitia Mradi wa
Usimamizi Endelevu
wa Rasilimali Madini
- SMMRP
51. Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka
wa Fedha wa 2017/18 kazi
zilizotekelezwa kupitia Mradi wa
Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP)
ni pamoja na upatikanaji wa Washauri Waelekezi kwa ajili ya kusanifu na kusimamia ukarabati na upanuzi wa Ofisi 7 za Madini za Mikoa kuwa Vituo vya Umahiri ambazo ni Bariadi, Bukoba (Tazama Picha Na.1),
Chunya, Mpanda, Musoma, Tanga na
Songea. Pia, Mradi uligharimia upatikanaji wa Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya
upanuzi wa miundombinu ya Chuo cha Madini
Kampasi ya
Dodoma. Michoro ya
majengo
hayo imekamilika na makadirio ya gharama za ujenzi yanaendelea kufanyika. Kazi
nyingine iliyofanyika ni kusimamia ujenzi wa Mgodi wa Umahiri katika eneo
la Lwamgasa - Geita ambao utagharimu Dola
za Marekani 584,800 kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo
ambapo ujenzi wa shimo la uchimbaji (mining shaft) umefikia asilimia
70 (Tazama Picha Na.2); kuiwezesha GST kufanya utafiti wa
kijiolojia kwa ajili ya ukadiriaji wa mbale katika
maeneo yanayokusudiwa kuanzishwa Vituo vya Mfano. Maeneo hayo ni Bukombe
(Katente); Chunya (Itumbi); Mpanda (D-Reef na Kapanda); Musoma (Buhemba);
Kyerwa (Kyerwa); na Tanga (Kiomoni, Kange
na Mkulumuzi). Taarifa ya utekelezaji
wa utafiti huo imebainishwa kwa kina katika sehemu ya taarifa ya utekelezaji wa kazi zilizofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafutaji Madini Tanzania.
(p) Ajira na Maendeleo ya Watumishi
53. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka
wa Fedha wa 2017/2018, Wizara
imepata Kibali cha Ajira Mpya chenye jumla ya nafasi 16 katika kada za Katibu
Mahsusi 3, Jiokemia 1, Mjiolojia 1, Wahandisi
Migodi 2, Watunza Kumbukumbu Wasaidizi
2, Madereva 6 na Mkutubi Msaidizi 1. Vilevile, katika Ikama ya Watumishi kwa Mwaka wa Fedha wa
2017/18, Wizara imeidhinishiwa nafasi za ajira mpya
53, kuwapandisha vyeo watumishi 196, kubadilisha kada watumishi
7 na nafasi za uteuzi 3. Aidha, katika Ikama
ya Watumishi kwa Mwaka
wa Fedha wa 2017/18,
STAMICO iliidhinishiwa nafasi 36 za kuwapandisha vyeo watumishi. Pia, GST
imeidhinishiwa nafasi 36 za kuwapandisha vyeo watumishi, kuwabadilisha kada
watumishi 3 na nafasi 6 za uteuzi.
54. Mheshimiwa Spika,
Wizara imeendelea kuwajengea uwezo watumishi
wake 44 katika fani mbalimbali ikiwemo Jiolojia na Utafutaji wa Madini; upimaji wa ardhi
(jomatikia); Sayansi ya Mazingira;
Uhasibu; Utawala; Sera za Uchumi; Takwimu
na Uhazili. Kati ya hao, watumishi 40 wamehudhuria mafunzo ya muda mrefu
katika ngazi za Stashahada, Shahada na Shahada
za Uzamili. Watumishi 4 walipata
mafunzo ya muda mfupi kuhusu
utafiti wa kijiolojia na usimamizi wa rasilimali madini yaliyofanyika nchini China.
55. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa huduma ya lishe, chakula na malipo ya dawa zilizo nje
ya orodha ya dawa zinazogharamiwa na
Bima ya Afya kwa watumishi wanaoishi na virusi vya UKIMWI na UKIMWI, ikiwa ni utekelezaji wa Waraka wa Watumishi
wa Umma Namba 2 wa Mwaka 2006 na Mwongozo wa Kudhibiti UKIMWI Katika
Utumishi wa Umma wa Mwaka 2007.
KAZI ZILIZOTEKELEZWA NA TAASISI ZILIZO CHINI
YA WIZARA
56. Mheshimiwa Spika,
Wizara ya
Madini inasimamia jumla ya Taasisi 6. Taasisi hizo ni Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti
Madini Tanzania, Shirika la Madini la Taifa, Chuo cha Madini, Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji
katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia na Kituo cha Jimolojia
Tanzania.
(a) Tume ya Madini
57. Mheshimiwa Spika, Tume ya Madini imeundwa
kwa mujibu
wa
Kifungu
cha
21
cha
Sheria
ya
(Marekebisho ya Sheria
mbalimbali) ya Mwaka 2017 iliyorekebisha
Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, na
ilianza kutekeleza majukumu
yake tarehe 30 Aprili,
2018. Kazi zilizotekelezwa na Tume ni pamoja na kupitia,
kuchambua na kuhakiki maombi ya leseni za utafutaji,
uchimbaji na biashara ya madini yaliyowasilishwa na waombaji wa leseni baada ya
tarehe 4 Julai, 2017. Uhakiki
uliofanywa na Tume umebaini kuwepo kwa jumla
ya maombi 4,394
ya Leseni za Uchimbaji Mdogo (PML) yaliyokuwa
yamependekezwa kupewa leseni. Pia,
kulikuwa na maombi
549 ya leseni
za biashara ya madini
yaliyokidhi vigezo vya kupewa leseni hizo. Maombi hayo yote yanaendelea
kuandaliwa leseni husika.
58. Mheshimiwa Spika,
vilevile, Tume ilichambua
na ilihakiki maombi ya leseni
za utafutaji na uchimbaji
wa kati wa madini yaliyowasilishwa baada ya tarehe
4 Julai, 2017. Uhakiki huo ulibaini uwepo wa jumla ya
maombi 150 ya
leseni za utafutaji
wa madini na
15 za uchimbaji
wa kati za madini. Aidha, uchambuzi
wa maombi ya leseni ulibaini
kuwepo kwa migogoro
4 katika maeneo yaliyoombewa leseni;
taarifa za upembuzi yakinifu
zisizojitosheleza; kutokuwepo kwa taarifa za Mpango
wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa
Jamii katika kutoa huduma (Corporate Social
Responsibility – CSR);
kutokuwepo kwa Mpango wa Ushirikishwaji wa Wazawa katika miradi ya madini (Local Content Plan); na kutokuwepo
kwa tamko la kiapo cha uadilifu – “Integrity Pledge”. Waombaji wa leseni wamejulishwa kupitia Vyombo vya Habari kuhusu mapungufu hayo ili
wawasilishe taarifa hizo zinazohitajika kwa mujibu wa Sheria.
(b) Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Madini
Tanzania – (GST)
59. Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi
ya
Taasisi ya Jiolojia
na Utafiti wa Madini Tanzania ni:-
(i) kukusanya, kuchambua, kutafsiri na
kutunza takwimu na taarifa mbalimbali
za jiosayansi (jiolojia, jiokemia na jiofizikia) na za upatikanaji madini;
(ii) kutengeneza na kusambaza ramani mbalimbali za
jiosayansi; kufanya uchunguzi
wa maabara kwa sampuli mbalimbali za miamba, madini, maji, mimea na udongo kwa ajili ya tafiti mbalimbali;
(iii) kutoa idhini
ya maandishi
kwa sampuli
za miamba,
udongo na sampuli zilizo katika hali ya
vimiminika kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi;
(iv)
kusaidia wachimbaji wadogo hasa
katika kubaini umbile na
aina
ya
mbale, kutambua
aina
na
ubora wa madini pamoja na namna bora ya uchenjuaji;
(v) kuratibu majanga asilia
ya jiolojia
(kama vile matetemeko ya ardhi, milipuko ya
volkano, maporomoko ya ardhi) na kutoa ushauri wa namna bora ya kujikinga;
(vi) kuboresha kanzidata ya Taifa ya jiosayansi
na madini;
(vii) kufanya tafiti maalum za jiosayansi;
(viii) kufanya tafiti za jioteknolojia na kutoa ushauri unaostahili katika
masuala ya ujenzi wa miundombinu na makazi; na
(ix) kutoa ushauri wa jiosayansi na utafutaji madini kwa wadau.
60. Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka
wa Fedha wa 2017/18, GST
ilipanga kukusanya maduhuli ya Shilingi 350,000,000
kutoka kwenye vyanzo vyake
mbalimbali. Vyanzo hivyo ni ada ya
ushauri elekezi, tozo za ramani au machapisho ya jiosayansi na tozo
za huduma za maabara. Hadi kufikia tarehe 31 Machi,
2018 GST
ilikuwa
imekusanya
jumla
ya
shilingi
294,700,000. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 84.2 ya
lengo ililowekewa kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18.
61. Mheshimiwa Spika,
katika kutekeleza majukumu yake, GST imepima
na kuchora ramani za jiolojia
na jiokemia za mfumo wa QDS kwa skeli ya 1:100,000 kwenye maeneo mapya
(QDSs 264, 265) yaliyoko Wilaya ya Mahenge na Malinyi; na kufanya ugani (field checks) wa jiolojia na jiokemia ili kuboresha ramani 2 za QDS 64 na 65 za Wilaya
ya Shinyanga. Vilevile, kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo,
GST ilifanya tafiti mbalimbali
za jiosayansi. Katika kipindi husika, GST kwa kushirikiana na Geological Survey
of China ilifanya
utafiti wa kina wa jiokemia katika maeneo ya Mbeya (QDS 244 na 245) na utafiti wa awali (Regional Scale Surveys) katika mikoa
ya Mtwara, Lindi,
Dar- es-Salaam na Morogoro
(Tazama Picha Na.3), Pwani, Tanga, Kilimanjaro,
Manyara, Arusha na Mara kwa lengo la kutafuta madini mbalimbali. Kwa ufadhili
wa Serikali ya Marekani, GST
ilikusanya taarifa na sampuli
katika maeneo ya Wilaya za Kondoa na
Chemba ili kupata vyanzo vya nishati ya joto ardhi
kwa ajili ya maeneo ambayo yako mbali na gridi ya Taifa.
62. Mheshimiwa Spika, vilevile, GST na Serikali ya Jamhuri ya Korea Kusini ilisaini Hati ya Makubaliano kwa ajili ya kufanya utafiti kwa kutumia teknolojia ya kisasa
ya kuainisha maeneo yenye uwepo wa madini kwenye maeneo ya Tunduma
na Mtwara (QDS 257,
312, 313, 319, 320) yanayopakana na Zambia na Malawi. Aidha, GST ilitengeneza ramani
mbalimbali za jiosayansi na kuzisambaza kwa wadau mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji
katika Sekta ya Madini pamoja na matumizi mengine.
63. Mheshimiwa Spika, GST iliendelea kuboresha
huduma za maabara ambapo mfumo wa kompyuta kwa
ajili ya kuratibu uchunguzi wa sampuli kwenye maabara uliandaliwa na
kusimikwa (Laboratory
Information Management System - LIMS). Pia, GST imeendelea kutengeneza Internal
Reference Standards za limestone,
phosphate na dhahabu. Vilevile,
GST ilifanya uchunguzi wa kemia,
petrolojia, minerolojia, uchenjuaji
madini
na jioteknolojia kwenye sampuli
13,633 za miamba choronge, udongo na madini. Pia, vyungu (cupels) 4,558 na
crucibles 4,626 vilitengenezwa kwa ajili
ya kutumika kuyeyushia sampuli za dhahabu ambapo hapo awali vilikuwa
vinanunuliwa nje ya nchi kwa gharama kubwa. Vilevile,
GST ilifanya uchunguzi wa kimaabara wa jumla ya sampuli 361 za udongo, madini na miamba
na taarifa zake ziliandaliwa ambapo ziliwasaidia wateja kupata vibali (export
permits) vya kusafirisha sampuli
nje ya nchi kwa uchunguzi zaidi.
64. Mheshimiwa Spika, GST iliendelea na kazi ya kuratibu majanga asilia ya jiolojia
ambapo takwimu kutoka vituo 8 vya kudumu
vya kupimia matetemeko ya ardhi vilivyopo
Dodoma, Mbeya, Arusha,
Mtwara, Geita, Singida,
Babati na Kibaya – Manyara zilikusanywa, kuchakatwa na kuhifadhiwa kwenye kanzidata. Kwa kutumia takwimu hizo, GST
iliainisha maeneo yenye vitovu (epicentres) vya
matetemeko na kuboresha ramani inayoonesha maeneo yenye vitovu
vya matetemeko ya ardhi. Aidha,
taarifa kuhusu matetemeko ya ardhi
yaliyotokea katika maeneo mbalimbali ya nchi katika kipindi cha mwezi Oktoba,
2017 hadi Machi, 2018 ilitolewa kwa wananchi
na kwenye vyombo
vya habari. Matukio hayo
yameainishwa kwenye Jedwali Na.1.
65. Mheshimiwa Spika,
vilevile, GST ilifanya utafiti
maalum wa kuangalia ubora
na wingi wa madini ya
jasi katika maeneo ya Makanya na Bendera (Same), Mwanga (Mwanga),
Itigi (Manyoni), Msagali
(Mpwapwa) na Manda (Chamwino), Mpindiro,
Mandawa, Mbaru, (Kilwa-Lindi) na Mkomole (Sumbawanga); utafiti maalum katika Wilaya ya Mufindi, Kijiji cha Isalavanu
kwa maombi ya Serikali ya Wilaya ili kubaini
uwepo wa madini yaliyofichwa katika maeneo hayo wakati wa Utawala wa Wajerumani kama ilivyokuwa inadhaniwa na wana kijiji hicho;
utafiti wa jiosayansi ulifanyika katika mahandaki yaliyopo katika Kijiji cha
Gibeshi Mkoani Simiyu ili kujua kama
ni mahandaki ya asili au yamechimbwa
na binadamu; utafiti wa jiosayansi katika
eneo la Nholi
- Dodoma ili
kubaini chanzo na uwepo wa madini
ya dhahabu katika eneo hilo; uchunguzi wa malikale
katika Wilaya
ya Same Kata ya Lugulu na Kitongoji cha Vumba pamoja na Mkoani Tanga katika Kata ya Pongwe; kukusanya
taarifa za uwepo wa madini na utafiti wa miamba katika Mkoa wa Iringa,
Wilaya za Mufindi, Iringa Vijijini
na Kilolo; na pia
GST ilishiriki katika
ukaguzi wa taarifa
zilizotumika kupata kiwango cha almasi kilichopo kwa sasa katika Mgodi wa almasi wa Mwadui na
kuhakiki uwepo wa kiwango hicho cha almasi na kutoa mapendekezo kwa Serikali.
66. Mheshimiwa Spika, Pia, katika tafiti
nyingi zilizofanywa na wataalam wa jiosayansi ya uchenjuaji zimebainisha
kuwa madini mengi hubakia kwenye
visusu (tailings) baada
ya
kuchenjuliwa.
Sababu
za madini kubakia kwenye mabaki ni
kutokana na kutofikiwa kwa kiwango cha ukubwa wa chembe (particle
size) za mbale kinachotakiwa baada ya mwamba
kuvunjwa na kusagwa; matumizi yasiyo sahihi ya kemikali zitumikazo kuchenjua na
utumiaji wa vifaa visivyostahili. Hii inatokana na wachimbaji
wadogo kutofahamu tabia tofauti za miamba na mbale
hivyo kupelekea kutotumia njia bora za uchenjuaji. Ni vyema wachimbaji wadogo
wakafahamu njia bora za uchenjuaji kwa kufanya
majaribio ya sampuli
za mbale katika maabara
mara kwa mara ili kutambua
mtiririko mzuri, aina ya miamba, kiwango cha usagaji, njia na mbinu za
uchenjuaji.
67. Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa wachimbaji
wadogo, kama hawajui tabia za mbale ya sehemu wanayochimba, kabla ya kuanza
uchenjuaji wapeleke sampuli za mbale (bulk
samples) kwenye maabara za
GST kwa ajili ya uchunguzi ili waweze kutambua njia bora za uchenjuaji. Lengo ni kupunguza
madini kubaki kwenye visusu (tailings), kuongeza
wingi wa uvunaji wa madini, kipato na faida kwa wachimbaji wa madini.
68. Mheshimiwa Spika, GST ilifanya kazi ya
kuboresha Kanzidata ya jiosayansi na madini, ambapo jumla ya machapisho 412 yalibadilishwa kutoka katika
mfumo wa karatasi na kwenda kwenye mfumo wa digitali; ramani 93 za jiosayansi zilikuwa
‘‘scanned’’ na
kuhaririwa na kuwekwa kwenye mfumo wa utunzaji wa taarifa na machapisho (GMIS); Ramani 17 za jiolojia za mfumo wa QDS zimebadilishwa kutoka
mfumo wa karatasi kwenda
mfumo wa digitali (digitization) kwa
lengo la kurahisisha usambazaji na utumiaji. Aidha, GST ilisambaza ramani na machapisho mbalimbali kwa wadau wa Sekta ya Madini kwa matumizi mbalimbali. Vilevile,
GST imepokea na kuhakiki taarifa
205 kutoka kwa wamiliki
wa leseni za utafutaji na uchimbaji madini kwa ajili ya kujua uhalisia wake
na kuzitunza kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Madini
ya
Mwaka
2010 na Marekebisho
yake ya Mwaka 2017.
69. Mheshimiwa Spika, GST ilifanya utafiti
wa uchenjuaji mbale za madini ya dhahabu katika
maeneo ya Londoni na Sambaru (Singida) kwa ajili ya kusaidia
wachimbaji wadogo; na
kukamilisha uchakataji wa taarifa za awali za jiosayansi (Geotechnical and seismological) ili kuainisha maeneo hatarishi na salama kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika Jiji la Dodoma ikizingatiwa kuwa
maeneo hayo yapo katika ukanda wa matetemeko ya ardhi. Aidha, GST ilitoa ushauri elekezi wa jiosayansi
kwa
kampuni
10 za utafutaji na uchimbaji madini ya metali na ya viwandani. GST pamoja na hayo ilipokea
taarifa zenye jumla ya leseni 247 za utafutaji madini (Prospecting
licences), leseni 12 za
uchimbaji wa kati wa madini (Mining licences) na
leseni 6 za
uchimbaji mkubwa kwa ajili ya kuhakiki ili kujua uhalisia
wake na kutunza kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017. Kati ya taarifa za leseni zilizofanyiwa tathmini zimebainisha kuwa taarifa
za kampuni 10 hazikidhi
vigezo vilivyotolewa na GST na vilivyoainishwa kwenye Sheria. GST imezielekeza
kampuni hizo kuziboresha taarifa hizo.
(c) Chuo cha Madini – (MRI)
70. Mheshimiwa
Spika, Chuo cha Madini kimeen- delea na majukumu yake ya
kutoa mafunzo
ya muda mrefu ya utaalam wa kada ya kati (Ufundi
Sanifu) katika fani za madini, mafuta
na gesi asilia;
kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wachimbaji wadogo wa
madini hasa katika nyanja za jiolojia na utafutaji madini, uhandisi uchimbaji
madini, uhandisi uchenjuaji madini, uhandisi
na usimamizi wa mazingira migodini;
kutoa
mafunzo maalum (tailor-made courses) kwa
wadau kulingana na mahitaji yao; kufanya tafiti katika Sekta za Madini,
Mafuta na Gesi; na kutoa ushauri elekezi (consultancy) katika Sekta hizo.
71. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka
wa Fedha wa 2017/18,
Chuo kimedahili jumla
ya wanafunzi 542 katika mafunzo ya muda mrefu katika fani za Jiolojia na Utafutaji Madini; Uhandisi Uchimbaji Madini;
Uhandisi Uchenjuaji Madini; Sayansi za Mafuta na Gesi; Uhandisi na Usimamizi wa
Mazingira Migodini; na Upimaji wa Ardhi na Migodi.
Katika kutoa mafunzo ya muda mfupi, Chuo kimeweza
kufundisha na kutoa vyeti kwa wafanyakazi 33 wa migodini ili kuwajengea uwezo
wa kufanya kazi kwa ubora. Aidha, katika kutoa mafunzo maalum,
Chuo kimeingia Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Kampuni ya Acacia North
Mara kwa ajili ya kuwafundisha wafanyakazi wake 20 kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Januari,
2018. Pia, Chuo kina Mikataba ya Makubaliano na Taasisi ya Jiolojia na Utafutaji Madini Tanzania (GST), Earth Sciences Institute
of Shinyanga (ESIS), Zimbabwe School of Mines (ZSM), Dedan Kimathi University
of Technology (DeKUT), Dar es
Salaam Marine Institute (DMI), Tanzania Geothermal Development Company (TGDC),
Chuo cha Cégep Limoilou – Canada, Chuo Kikuu cha Montpellier – Ufaransa, Mgodi wa Dhahabu wa Acacia – North
Mara na Baraza
la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
72. Mheshimiwa Spika, Vilevile, Chuo cha Madini kimeanzisha mafunzo ya fani mpya
ya Upimaji wa Ardhi na Migodi
(Land and Mine Surveying) kwa ngazi ya
Astashahada na Stashahada. Jumla ya wanafunzi
24 wamedahiliwa na kuanza masomo ya Astashahada mwezi Januari,
2018. Mafunzo haya yatazalisha Mafundi Sanifu wa kupima ardhi na migodi.
73. Mheshimiwa Spika,
katika kuhakikisha
mafunzo yatolewayo na Chuo cha Madini yanakidhi matakwa ya mtaala na mfumo wa ufundishaji, Serikali imeboresha maabara za Jiolojia, Uhandisi Uchimbaji na Uhandisi
Uchenjuaji kwa kutoa vifaa vya maabara (Tazama Picha Na.8) kupitia mradi wa SMMRP
ulio chini ya Wizara vyenye thamani ya Dola za Marekani
514,924.81 Maabara hizi zitakiwezesha Chuo kutoa mafunzo
kwa vitendo na kufanya tafiti mbalimbali. Aidha, kupitia Mradi
wa
Improving Skills
Training for Employment Program (ISTEP) unaotekelezwa kwa kushirikiana kati
ya Chuo cha Madini na Chuo cha Cégep
Limoilou kilichopo nchini Canada, Chuo kimepata vifaa vya kisasa (Tazama Picha Na.9)
vya kusaidia kutoa mafunzo ya vitendo katika fani mpya ya Upimaji Ardhi na Migodi. Vifaa
hivi vimegharimu jumla ya Dola za Kanada 40,000.
74. Mheshimiwa Spika, katika kusaidia wachimbaji wadogo Chuo kina mpango wa kufanya tafiti kuhusu kutengeneza njia mbadala ya uchenjuaji madini ya dhahabu kwa wachimbaji wadogo. Madhumuni ya utafiti huu ni kusaidia upatikanaji wa njia bora yenye ufanisi wa kuchenjua madini ya dhahabu kwa wachimbaji wadogo nchini na kuondoa matumizi ya kemikali ya Zebaki kwenye uchenjuaji wa dhahabu kama inavyotakiwa na Mikataba ya Kimataifa ikiwemo Makubaliano ya Minamata kuhusu utunzaji wa mazingira na afya za watu na viumbe mbalimbali katika mazingira yetu.
(d) Shirika la Madini la Taifa – (STAMICO)
75. Mheshimiwa Spika, majukumu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ni pamoja na kuwekeza kwenye shughuli za uchimbaji na utafutaji madini; kuwekeza katika uchenjuaji, uongezaji thamani na uuzaji madini; na kutoa huduma na ushauri wa kitaalamu na kiufundi katika Sekta ya Madini wakiwemo wachimbaji wadogo kwenye nyanja za kijiolojia, kihandisi, kimazingira na uchorongaji miamba.
76. Mheshimiwa Spika, STAMICO imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya uchimbaji wa madini nchini ikiwemo ya uwezeshaji wa wachimbaji na miradi ya ubia. Utekelezaji wa shughuli hizo unahusisha uzalishaji wa makaa ya mawe katika Mgodi wa Kabulo; uzalishaji wa madini ya Tanzanite katika Mradi wa Ubia wa TanzaniteOne; uzalishaji wa madini ya dhahabu katika Kampuni Tanzu ya STAMIGOLD; na uendelezaji wa Mradi wa uchimbaji wa dhahabu wa Buhemba.
(i) Mradi wa Makaa ya Mawe wa Kabulo, Kiwira
77. Mheshimiwa Spika, Shirika lilianza uchimbaji wa makaa ya mawe katika kilima cha Kabulo kilichopo eneo la Kiwira, Mkoani Songwe mwezi Aprili, 2017. Lengo ni kukidhi mahitaji ya makaa ya mawe nchini.
78. Mheshimiwa Spika, tangu mradi uanze mwezi Aprili, 2017 hadi kufikia mwezi Machi, 2018, Shirika limezalisha jumla ya tani 8,674 za makaa ya mawe yenye thamani ya shilingi milioni 555.1 na kiasi cha tani 2,827.7 za makaa ya mawe zimeuzwa kwa jumla ya shilingi 180,972,800. Aidha, kiasi cha tani 5,846.30 za makaa ya mawe zimehifadhiwa katika eneo la mgodi wakati jitihada za kutafuta wateja zikiendelea.
79. Mheshimiwa Spika, vilevile, Shirika lilifanya ukarabati wa maabara ya kupima ubora wa makaa ya mawe katika Mgodi wa Kiwira sanjari na matengenezo ya vifaa vya maabara ikiwemo kuweka mfumo mpya wa umeme. Ukarabati huo uligharimu kiasi cha shilingi
7,566,000. Pia, Shirika lilifanya ukadiriaji wa mashapo ya makaa ya mawe katika leseni yake ya utafiti ya Kabulo PL Na. 9963/2014 iliyopo wilayani Ileje, Mkoa wa Songwe ambapo ukadiriaji huo umeonesha uwepo
wa tani milioni 300 za makaa ya mawe.
(ii) Mgodi wa TanzaniteOne
80. Mheshimiwa Spika, migodi ya Tanzanite iliyopo Mirerani ni pamoja na mgodi unaomilikiwa kwa ubia baina ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya TanzaniteOne Mining Limited (TML). Ipo pia, migodi mingine inayomilikiwa na wachimbaji wazawa wenye leseni za uchimbaji mdogo na wa kati. Uendeshaji wa mgodi baina ya STAMICO na TML umekuwa na changamoto nyingi zilizosababishwa na kasoro katika Mkataba wa Ubia na Mkataba wa Uendeshaji. Kutokana na kasoro zilizobainishwa na Kamati Maalum ya Spika ya Kuchunguza Uchimbaji na Biashara ya Madini ya Tanzanite, Serikali iliagiza Timu ya Majadiliano ya Serikali kukutana na wamiliki wa TML na STAMICO kujadiliana ili kubaini kasoro hizo na kupendekeza namna bora ya uchimbaji, biashara na uendeshaji wa mgodi huo kwa lengo la kulinufaisha Taifa kuliko ilivyo sasa. Kufuatia kukamilika kwa majadiliano hayo, Serikali imeagiza Leseni ya Uchimbaji wa Ubia baina ya STAMICO na TML irudishwe Serikalini ili utaratibu mpya uandaliwe utakaowezesha Serikali, TML na mwekezaji wa kimkakati kushirikiana katika uchimbaji, uendeshaji na biashara ya madini ya Tanzanite katika mgodi huo kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Madini, Sura ya
123 kama ilivyorekebishwa na Bunge Mwaka 2017. Aidha, majadiliano na wachimbaji wadogo yanaendelea baina ya Timu ya Majadiliano ya Serikali na wamiliki wa migodi hiyo kwa lengo la kuleta manufaa zaidi kwa Taifa kutokana na madini ya Tanzanite. Vilevile, kwa kutambua umuhimu na upekee wa madini ya Tanzanite duniani kwamba yanapatikana Tanzania tu, Serikali inakamilisha utaratibu wa kuyatangaza madini ya Tanzanite kuwa madini maalum (specified minerals).
Utaratibu wa kuyatangaza utakamilika katika Mwaka huu wa Fedha wa 2017/18.
(iii) Mgodi wa Dhahabu wa STAMIGOLD
81. Mheshimiwa Spika, Kampuni ya STAMIGOLD ni Kampuni tanzu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) iliyoanzishwa Oktoba, 2013. Kampuni hii inamilikiwa kwa ubia kati ya STAMICO asilimia
99.98 na Msajili wa Hazina asilimia 0.02. Kampuni hii ilipewa jukumu la kuendeleza Mgodi wa dhahabu wa STAMIGOLD Biharamulo Mine (SBM) ambao ulirithiwa kutoka kampuni ya Pangea Minerals LTD iliyokuwa mmiliki wa awali kupitia Leseni ya Uchimbaji Mkubwa Na. SML 157/2003.
82. Mheshimiwa Spika, wakati STAMICO inakabidhiwa mgodi huu, gharama za uendeshaji zilikuwa juu ikilinganishwa na mapato yaliyotokana na mauzo ya dhahabu kwa kuwa katika kipindi hicho bei ya dhahabu ilikuwa chini kutokana na mdororo wa uchumi duniani hususan katika Sekta ya Madini. Pamoja na tatizo hilo, Kampuni ilijiendesha kwa hasara na kusababisha deni la takriban shilingi bilioni 64 hadi kufikia mwezi Machi, 2018. Hata hivyo, deni hili linahakikiwa na Vyombo vya Serikali ili kujua uhalali wake na namna ya kuondokana nalo.
83. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Julai, 2017 hadi Machi, 2018 Mgodi umezalisha na kuuza jumla ya wakia 3,967.92 za dhahabu na wakia 400.85 za fedha zenye thamani ya shilingi
11,459,212,821.83. Kutokana na mauzo hayo, Serikali imepokea mrabaha wa shilingi 802,144,897.53.
84. Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine Menejimenti ya Mgodi imeweza kuchukua sampuli 10 za visusu (old tailings) vilivyoachwa mgodini hapo na kupeleka kwenye Maabara ya African Minerals and Geoscience Centre (AMGC) iliyopo Kunduchi, Dar es Salaam ili kuthibitisha kitaalamu kiasi cha dhahabu kilichomo. Kiasi cha visusu kilichopo ni tani 8,600,000. Kwa mujibu wa ripoti ya maabara, visusu hivyo vya dhahabu vina wastani wa gredi ya gramu 1.15 kwa tani ambapo ni sawa na takriban wakia 300,000. Vilevile, thamani ya visusu hivyo itatambuliwa kwenye vitabu rasmi kuwa ni mali ya Kampuni kwa ajili ya kumbukumbu na udhibiti wa mali hiyo.
(iv) Mradi wa Dhahabu wa BUHEMBA
85. Mheshimiwa Spika, Mradi wa Dhahabu wa Buhemba uliopo Wilaya ya Butiama, Mkoa wa Mara unahusisha uchenjuaji wa mabaki ya mchanga wa dhahabu na uchimbaji wa dhahabu katika miamba migumu. Katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, Shirika limeendelea na utafiti kwa lengo la kuendelea kubaini kiasi kingine cha mashapo ya dhahabu kilichopo katika miamba ambapo kazi zilizofanyika zilihusisha uchorongaji wa miamba.
(v) Mradi wa Dhahabu wa BUCKREEF
86. Mheshimiwa Spika, Mgodi wa Buckreef unamili- kiwa kwa Ubia kati ya STAMICO na Kampuni ya TANZAM 2000 kwa asilimia 45 kwa 55. Katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, STAMICO kwa kushirikiana na Wizara ya Madini na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaupitia upya mkataba wa ubia. Hii ni kutokana na mbia kuchelewa kuanza uzalishaji kwa
mujibu wa makubaliano ya Mkataba. Pia, STAMICO kwa kushirikiana na mbia mwenza ilifanya tathmini ya maeneo yanayofaa kuachiwa kwa wachimbaji wadogo katika maeneo ya leseni za utafiti Namba PL 6430/2010 (Lwamgasa West); PL 6549/2010 (Nyamalimbe 2); na PL
6547/2010 (Lwamgasa South 2). Matokeo ya tathmini hiyo yalibainisha kuwa maeneo hayo yanafaa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Utaratibu unaandaliwa wa kuyaachia maeneo hayo kwa wachimbaji wadogo.
(vi) Mradi wa Kokoto - Ubena Zomozi
87. Mheshimiwa Spika, Shirika lilifanya utafiti wa wingi na ubora wa miamba katika leseni zake kumi (10) za uchimbaji kokoto zilizopo Ubena Zomozi, mkoani Pwani. Utafiti huo ulibaini uwepo wa miamba yenye kiasi cha mashapo yanayokadiriwa kufikia tani milioni 41.5 za kokoto zinazoweza kuchimbwa kwa zaidi ya miaka 50. Shirika linaendelea na taratibu za kutafuta fedha au kumpata mbia kwa ajili ya mradi huo.
(vii) Huduma kwa Wachimbaji Wadogo
88. Mheshimiwa Spika, Shirika kwa kushirikiana na Wizara limeendelea kusimamia ujenzi wa Mgodi wa Mfano katika eneo la Lwamgasa kwa ajili ya wachimbaji wadogo, ambapo hadi kufikia Machi, 2018, ujenzi wa shimo la uchimbaji (mining shaft) na usimikaji wa mitambo ya kuchenjulia dhahabu umefikia asilimia 70 (Tazama Picha Na.10 na 11). Mgodi huu utawanufaisha wachimbaji wadogo katika eneo hilo kwa kuwawezesha kujifunza teknolojia sahihi ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) ulihusika kufanya upembuzi yakinifu katika eneo la
mgodi wa mfano. Aidha, hadi sasa Mradi wa SMMRP umeshatumia jumla ya Dola za Marekani 293,881.2 katika ujenzi wa mgodi huo wa mfano.
(e) Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia – (TEITI)
89. Mheshimiwa Spika, Tanzania ni Mwanachama wa Mpango wa Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (Extractive Industry Transparency Initiative) tangu mwaka 2009. Katika kutekeleza mpango huo, Serikali ilianzisha Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) chini ya Sheria ya TEITA ya Mwaka 2015. Taasisi hii ina jukumu la kuhamasisha Serikali kuweka mifumo ya uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia ili kuongeza mapato na manufaa yatokanayo na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo.
90. Mheshimiwa Spika, Taasisi hii pia ina jukumu la kuwajengea uwezo wananchi katika kutumia takwimu zinazotokana na shughuli za uendeshaji wa kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa kuhoji na kuhamasisha mijadala kuhusu manufaa ya shughuli za rasilimali madini; utoaji wa leseni na mikataba, uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia; usimamizi na uendeshaji wa kampuni za madini, mafuta na gesi asilia; ukusanyaji wa mapato yatokanayo na madini, mafuta na gesi asilia; na mgawanyo wa mapato na matumizi yake.
91. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, TEITI ilikamilisha na kutoa kwa umma ripoti ya ulinganisho (Reconciliation report) wa malipo yaliyolipwa na Kampuni za madini, mafuta na gesi asilia na mapato yaliyopokelewa na Serikali kwa
Mwaka wa Fedha wa 2015/16. Ripoti hiyo ambayo ni ya 8 imewasilishwa kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya uchunguzi. Aidha, TEITI ilikamilisha muhtasari wa takwimu za ripoti hiyo zilizowekwa katika vielelezo (Inforgraphics) kwa lugha ya kiswahili na kiingereza. Lengo ni kurahisisha ufikishaji wa matokeo ya ripoti za TEITI kwa wadau na kujenga uwezo wa wananchi katika kutumia takwimu zinazotokana na shughuli za uendeshaji wa kampuni, kuhoji Serikali na kuhamasisha mijadala kuhusu uongezaji wa manufaa ya uchimbaji madini, mafuta na gesi asilia nchini.
(f ) Kituo cha Jimolojia Tanzania – (TGC)
92. Mheshimiwa Spika, Kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) kina majukumu ya kutoa mafunzo ya uongezaji thamani madini na miamba na utengenezaji wa bidhaa za urembo na mapambo kwa kutumia miamba (Tazama Picha Na. 12). Kituo kinatoa mafunzo katika fani za usanifu wa madini ya vito, usonara na uchongaji vinyago vya miamba.
Kazi zilizotekelezwa na Kituo hiki ni pamoja na uchongaji wa vinyago 69 vya miamba; kutengeneza marumaru (tiles) za ukutani 250, table mats 80; tiles kubwa 100 kutokana na mawe ya Tanga (Tanga stones/slates); kutengeneza bidhaa mbalimbali za mapambo kwa kutumia mawe ambazo ni vikuku (bracelets) 50, hereni 65, mikufu 89, vidani 120 na pete 60; kung’arisha sampuli za madini ya tanzanite za ubora wa chini (reject) za uzito wa kilo 6 kutoka kwa watu mbalimbali; kukata na kusanifu madini ya vito ya taasisi na watu mbalimbali. Kiasi cha madini kilichokatwa na kusanifiwa ni gramu 20 za madini ya tanzanite; gramu 30 za amethyst; na gramu 300 za quartzred aventurine. Pia, TGC imeendelea kutoa mafunzo ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito ambapo wanafunzi 38 walidahiliwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2017 hadi Mei, 2018. Vilevile, kabla ya Julai, 2017 wanafunzi 65 walikuwa wamedahiliwa na kupata mafunzo ya aina hiyo.
4.0 MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA WA 2018/19
93. Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19 umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 - 2020; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21); Malengo Endelevu ya Maendeleo 2030; Ahadi za Serikali Bungeni za Mwaka wa 2017/18; Mwongozo wa Kutayarisha Mpango na Bajeti wa Mwaka wa Fedha wa
2018/19; Maagizo ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa kwa nyakati tofauti; Ushauri na Maoni ya Kamati Maalum zilizoundwa na Mheshimiwa Rais kama zilivyoainishwa katika aya ya 12 na ushauri uliotolewa na Bunge pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti, na Ushauri wa Kamati Maalum za Mheshimiwa Spika.
94. Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kuteke- lezwa kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19 na Wizara ya Madini na Taasisi zake ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini; kuwaendeleza wachimbaji wadogo na wa kati wa madini; kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini; kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa; kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika miradi ya kimkakati ya Sekta ya Madini; kuendelea kuboresha mazingira ya kuwawezesha wananchi kufaidika na rasilimali madini; kuelimisha Umma na kuboresha mawasiliano
kati ya Wizara na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya madini; kusimamia, kufuatilia na kuboresha Sera, Sheria, Kanuni, Mikakati na Miongozo mbalimbali ili kuleta ufanisi na tija katika Sekta ya Madini; kuendeleza rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi; na kuwezesha Taasisi zilizo chini ya Wizara.
(a) Kuimarisha Ukusanyaji wa Mapato ya
Serikali yatokanayo na Shughuli za Madini
95. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na shughuli za madini ambapo kwa Mwaka wa Fedha wa
2018/19lengonikukusanyaShilingi310,598,007,000, ikiwa ni ongezeko la asilimia 59.57 ikilinganishwa na Shilingi 194,663,501,763 zilizopangwa kukusanywa kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18. Katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali yanayotokana na shughuli za madini, Wizara inatarajia kuimarisha ukaguzi wa migodi mikubwa, ya kati na ya uchimbaji mdogo ili kupata taarifa sahihi za uwekezaji, uzalishaji, mauzo na kodi mbalimbali; kudhibiti utoroshwaji wa madini katika maeneo ya uzalishaji na kutokea nchini (Exit Points); kuimarisha ukaguzi wa madini ya ujenzi na viwandani; kufuatilia taarifa za ununuzi na uuzaji (returns) kwa wafanyabiashara wa madini (Dealers & Brokers); kufuatilia wadaiwa wa tozo mbalimbali za madini kwa mujibu wa Sheria kwa wakati; kudhibiti uchimbaji na uchenjuaji haramu wa madini; na kuboresha na kuimarisha mfumo wa kutoa leseni za madini na kutunza taarifa zake.
96. Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa wamiliki wa leseni za madini kuacha kukwepa au kuchelewa kulipa kodi, kulipa mrabaha stahiki na tozo nyingine zilizopo kwa mujibu wa Sheria za nchi. Kwa wale watakaobainika kukiuka matakwa ya kisheria, Serikali itawachukulia hatua kali ikiwa ni pamoja na kufuta leseni zao na kuwafikisha mahakamani.
(b) Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo wa
Madini
97. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo, Wizara itaendelea kutenga maeneo yanayofaa ambapo jumla ya maeneo
4 yanatarajiwa kutengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Aidha, GST itabainisha uwepo wa mashapo ya madini katika maeneo yatakayotengwa. Vilevile, Wizara kupitia STAMICO, itawaelimisha wachimbaji wadogo namna ya kutumia teknolojia ya kisasa na rahisi katika kuongeza uzalishaji na tija wakati wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Pia, Wizara kupitia mradi wa SMMRP itajenga Vituo vya Mfano 4 ambavyo ni Katente (Bukombe); Itumbi (Chunya); Kona Z (Tanga); na Lindi. Vituo hivyo vitatumika kwa ajili ya mafunzo ya uongezaji thamani madini, uchimbaji salama pamoja na kuongeza uzalishaji na tija na hivyo kuongeza mapato kwa wachimbaji wadogo. Vituo hivi pia vinatarajiwa kutoa huduma za uchenjuaji wa madini kwa wachimbaji wadogo.
(c) Kuhamasisha Shughuli za Uongezaji
Thamani Madini
98. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2018/19, Wizara itaendelea kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongezaji
thamani madini na kuendelea kutoa leseni za uchenjuaji na uyeyushaji wa madini ya metali. Pia, Wizara itakamilisha kazi ya kuwapata wawekezaji katika Vinu vya uchenjuaji na usafishaji wa madini. Aidha, Wizara itaandaa Muswada wa Sheria ya Uongezaji Thamani Madini ili kukuza na kusimamia vyema shughuli za uongezaji thamani madini nchini. Viwanda vya uyeyushaji, usafishaji wa madini na shughuli nyingine za uongezaji thamani zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali, kuongeza ajira na kukuza matumizi ya teknolojia nchini.
99. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa madini ya vito, Wizara itaendelea kukiimarisha Kituo cha Jimolojia Tanzania ili kiweze kutoa wataalam kwenye fani za ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito, jimolojia na usonara watakaosaidia kufanya shughuli za uongezaji thamani madini hayo hapa nchini.
(d) Kuimarisha Ukaguzi wa Usalama, Afya, Mazingira na Uzalishaji wa Madini Migodini
100. Mheshimiwa Spika, shughuli za uchimbaji wa madini zinapaswa kusimamiwa kwa karibu kwani huweza kuambatana na athari za kiafya, usalama na uharibifu mkubwa wa mazingira. Ili kuondokana na athari hizo, Wizara itaendelea kuimarisha kaguzi migodini na maeneo ya uchenjuaji wa madini, kuongeza huduma za ugani hususan kwa wachimbaji wadogo, kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali zinazohusika na usimamizi wa masuala ya Afya, Usalama na Utunzaji wa Mazingira katika kufanya kaguzi mbalimbali migodini ikiwemo utekelezaji wa Mkataba wa Minamata wa kupunguza na hatimaye kuzuia matumizi ya Zebaki katika uchenjuaji. Pia,
Wizara itaendelea kukagua na kuhakiki kiasi na ubora wa madini yanayozalishwa na migodi mikubwa, ya kati na midogo.
101. Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa wachimbaji wa madini na wale wanaofanya shughuli za uchenjuaji hususan madini ya dhahabu kuhakikisha wanaimarisha miundombinu ya mabwawa ya kuhifadhi mabaki yenye kemikali (Tailings Storage Facility – TSF) kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka
2010 kama ilivyofanyiwa marekebisho Mwaka 2017. Pia, Wachimbaji Wakubwa na wa Kati wahakikishe wanawasilisha Mpango wa Ufungaji Migodi kwa wakati kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 206 ya Kanuni za Madini kuhusiana na Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira za Mwaka 2010. Wachimbaji wakubwa na wa kati wanapaswa pia kuweka Hati Fungani ya Uhifadhi wa Mazingira (Environmental Rehabilitation Bond) kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 207 ya Kanuni za Madini kuhusiana na Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira za Mwaka 2010.
102. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia STAMICO imekuwa ikishiriki kwenye uwekezaji katika madini mbalimbali. Katika kutekeleza jukumu hilo, STAMICO imetengewa kiasi cha shilingi
8,600,000,000 kwa ajili ya kuendeleza Mradi wa Dhahabu wa Buhemba wa kuchenjua visusu. Pia, STAMICO itaendelea kutafuta fedha kutoka taasisi mbalimbali za kifedha na wabia kwa ajili ya kuendeleza miradi ya Makaa ya Mawe ya Kiwira na Kabulo; Uchimbaji na Uuzaji wa Kokoto wa Ubena Zomozi (Pwani) na Chigongwe (Dodoma). Vilevile, STAMICO itaendelea kuimarisha usimamizi wa Mradi wa Ubia wa TanzaniteOne na Kampuni Tanzu ya STAMIGOLD;
kuimarisha biashara ya shughuli za uchorongaji na utoaji wa ushauri wa kitaalam katika Sekta ya Madini; na kuratibu uboreshaji na uendelezaji wa shughuli za wachimbaji wadogo nchini.
(e) Kuendelea Kuboresha Mazingira ya Kuwawezesha Wananchi Kunufaika na Shughuli za Madini
103. Mheshimiwa Spika, Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 pamoja na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 zinatoa mwongozo wa namna Kampuni za madini zinavyopaswa kufungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine za kiuchumi. Wizara itasimamia Sheria katika kukuza ushiriki wa Watanzania (local content) kwenye shughuli za utafutaji, uchimbaji, biashara ya madini nchini na Uwajibikaji wa Kampuni za Uchimbaji Madini kwa Jamii (Corporate Social Responsibility - CSR).
104. Mheshimiwa Spika, katika Kifungu cha
102 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 pamoja na Marekebisho yake ya Mwaka 2017, maombi ya leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini yanapaswa kuambatana na Mpango wa Matumizi ya Bidhaa na Huduma za Ndani katika maombi ya leseni husika. Iwapo bidhaa hizo hazipatikani ndani ya nchi, bidhaa hizo zinapaswa zipatikane kwa kutumia Kampuni ya ndani ya nchi iliyoingia ubia na Kampuni ya nje. Mmiliki wa Leseni anapaswa kuwasilisha katika Tume ya Madini taarifa inayoonesha matumizi ya bidhaa na huduma za ndani ya nchi katika kipindi cha siku
60 baada ya kuisha kwa mwaka wa kalenda. Wizara itaendelea kusimamia Kampuni hizo ili kuhakikisha kuwa Kifungu hicho cha Sheria kinatekelezwa.
105. Mheshimiwa Spika, vilevile, Wizara itaendelea kushirikisha jamii katika shughuli za kiuchumi ambazo jamii inaweza kuzimudu. Katika Kifungu cha 105 cha Sheria ya Madini ya Mwaka
2010 pamoja na Marekebisho yake ya Mwaka 2017, kinamtaka kila mmiliki wa leseni ya uchimbaji wa madini, uchenjuaji, uyeyushaji na usafishaji wa madini kuandaa Mpango wa Mwaka wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii. Mpango huo unapaswa kuwasilishwa kwa Mamlaka za Serikali za Mtaa husika kwa rejea na idhini. Nawasihi Viongozi katika kila Halmashauri kuandaa Miongozo ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii na kusimamia utekelezaji wake. Vilevile, Halmashauri zinapaswa kuwaelimisha wananchi katika maeneo yao kuhusiana na Mipango ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii.
106. Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa Mamlaka nyingine za Serikali hususan Mamlaka ya Serikali za Mitaa kushiriki kuziandaa jamii zilizopo katika maeneo ya migodi kushirikiana na Kampuni za madini ili kufanikisha malengo ya mipango hiyo.
(f ) Kuelimisha Umma na Kuboresha Mawasiliano baina ya Wizara na Wadau wa Sekta ya Madini
107. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itafanya mikutano ya ana kwa ana na wawekezaji na itatoa elimu kwa umma kuhusu rasilimali madini. Kwa kutambua hilo, kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19 Wizara yangu itatoa elimu kwa umma kuhusu rasilimali madini, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini kupitia vipindi mbalimbali vya redio na televisheni; majarida na machapisho mbalimbali; tovuti; mitandao ya kijamii ya Wizara; na kushiriki katika maonesho mbalimbali
ya kitaifa na kimataifa na kupitia njia nyingine za upashanaji habari kwa umma. Lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu ya kina kuhusu masuala ya rasilimali madini.
(g) Kusimamia na Kuboresha Sera, Sheria, Kanuni, Mikakati na Miongozo
108. Mheshimiwa Spika, Wizara itafanya mapitio ya Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na kuandaa Sera ya Uongezaji Thamani Madini na Dira ya Taifa ya Kuendeleza Sekta ya Madini (Tanzania Mining Vision
2019 - 2035). Vilevile, Wizara itaandaa Muswada wa kutunga Sheria ya Uongezaji Thamani Madini na Kanuni zake. Aidha, Wizara itaandaa Miswada ya Marekebisho ya Sheria zifuatazo:
(i) Sheria ya Baruti ya Mwaka 1963 na Kanuni zake za Mwaka 1964;
(ii) Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali
Madini, Mafuta na Gesi Asilia ya Mwaka 2015; na
(iii) Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017.
(h) Kuendelea Kuvutia Wawekezaji Wakubwa kwenye Sekta ya Madini
109. Mheshimiwa Spika, Katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19, Serikali itaendelea kuvutia wawekezaji kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kwa wadau kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini ikiwemo kuandaa Jukwaa la Wawekezaji katika Sekta ya Madini (Tanzania Mining Forum); kuwezesha upatikanaji wa taarifa za kijiolojia zinazohitajika
katika shughuli za utafutaji wa madini na kushiriki kwenye mikutano na warsha za ndani na nje ya nchi zinazohusu shughuli za madini.
(i) Kuboresha Utoaji na Usimamizi wa Leseni za
Madini
110. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19, Wizara yangu itaendelea kuboresha Mfumo wa Kielektroniki wa Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini ili kuendana na Marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yaliyofanyika Mwaka
2017 na Kanuni zake. Pia, Wizara kupitia Tume ya Madini itaendelea kushughulikia maombi ya leseni za madini kwa wakati na kuhakikisha kuwa maombi yote yanayowasilishwa yanashughulikiwa na kujibiwa mapema iwezekanavyo. Aidha, Wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 kwa kufuta leseni zote zinazokiuka matakwa ya Sheria hiyo ili kutoa nafasi kwa wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuyaendeleza na maeneo mengine zaidi kutengwa kwa wachimbaji wadogo.
(j) Mipango itakayotekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini – SMMRP
111. Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kuteke- lezwa na Mradi wa SMMRP kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2018/19 ni pamoja na: kuanza ukarabati na upanuzi wa majengo ya Ofisi 7 za Madini ili zitumike kama vituo vya umahiri vya masuala ya madini. Ofisi hizo ni Mpanda, Songea, Chunya, Tanga, Bariadi, Bukoba na Musoma. Vilevile, Mradi utagharimia upanuzi wa
miundombinu ya Chuo cha Madini (Dodoma) kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa shughuli za madini zinazotekelezwa na WIMA; kuendelea kukamilisha ujenzi wa Mgodi wa Mfano Lwamgasa - Geita kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kusimika mitambo ya uchenjuaji; na kuiwezesha TEITI kutengeneza mfumo wa kuunganisha na kuzijumuisha pamoja taarifa za malipo na za uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa.
(k) Kuendeleza Rasilimali Watu, Kuboresha Mazingira ya Kufanyia Kazi na Kuziwezesha Taasisi zilizo Chini ya Wizara
112. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majuk- umu yaliyopangwa, Wizara itahakikisha inajenga ujuzi wa watumishi kwenye nyanja mbalimbali na itaboresha mazingira ya kazi, na kuwapatia vitendea kazi bora na kwa wakati. Aidha, watumishi watapatiwa elimu kuhusu afya bora, uadilifu, rushwa na madhara yake katika utumishi wa umma na Taifa kwa ujumla.
113. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kuwa Wizara ya Madini ni mpya katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19 Wizara na Taasisi zake inatarajia kuajiri jumla ya watumishi 314 wa kada mbalimbali ikiwemo Wahandisi Migodi; Wajiolojia; Maafisa Rasilimali Watu; Wakufunzi wa fani za Madini; Mafundi Sanifu; Madereva na Makatibu Mahsusi. Kati ya hao, watumishi 208 ni kwa ajili ya Wizara, 28 kwa ajili ya GST na 78 ni kwa ajili ya Chuo cha Madini.
114. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya UKIMWI; na kuendelea kuwahudumia watumishi wenye ulemavu na wanaoishi na virusi vya UKIMWI na UKIMWI. Aidha, Wizara
itaendelea kuwahamasisha watumishi kupima afya zao ili kutambua hali za afya zao ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi mara kwa mara.
KAZI ZITAKAZOTEKELEZWA NA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA WA 2018/19
(i) Tume ya Madini
115. Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kutekelezwa na Tume ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19 ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa Mapato yatokanayo na rasimali madini; kutathmini na kushughulikia changamoto katika utekelezaji wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017; kutoa Mwongozo wa namna ya kutoa vibali vya kusafirisha madini nje ya nchi; kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira, utafutaji na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa; kuimarisha mfumo wa kielekroniki wa kutoa na kusimamia taarifa za leseni za madini ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa leseni na kuondoa migogoro inayotokana na leseni za madini; kuimarisha udhibiti wa utoroshwaji wa madini nje ya nchi; kuimarisha shughuli za uongezaji thamani madini; kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini na kushughulikia migogoro yote inayotokana na shughuli za madini.
(ii) Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini
Tanzania – (GST)
116. Mheshimiwa Spika, GST inatarajia kutekeleza shughuli zifuatazo kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19:
kuboresha Kanzidata ya miamba na madini ya Taifa ili kuongeza uelewa wa jiolojia ya nchi na ya upatikanaji wa madini mbalimbali nchini ili kuchochea uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini; kuratibu shughuli za utafutaji na uchimbaji madini nchini kwa kupitia taarifa za robo mwaka za shughuli hizo ili kuhakiki usahihi wa taarifa hizo na kuboresha Kanzidata ya Taifa ya madini; kufanya uchunguzi wa sampuli za madini na miamba ili kujua viwango vya madini kwenye sampuli zinazokusanywa na watafiti na watafutaji madini kwa ajili ya kutoa idhini ya maandishi ya kusafirisha sampuli hizo nje ya nchi; kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kufanya tafiti za kijiosayansi katika utafutaji, uchimbaji salama, uhifadhi wa mazingira na uchenjuaji ili kuongeza tija katika uzalishaji; kuboresha huduma za maabara kwa wadau wa Sekta ya Madini, Kilimo na Ujenzi; kuboresha Kanzidata ya majanga asilia ya jiolojia na kuelimisha wananchi kuhusu namna bora ya kujikinga na majanga hayo; kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya GST kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali; kuendeleza rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.
(iii) Chuo cha Madini – (MRI)
117. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19, MRI inategemea kutekeleza shughuli zifuatazo: kuendelea na Mpango wa kukiimarisha Chuo cha Madini; kuendelea kutoa mafunzo kwa wanafunzi ambapo udahili wa wanafunzi wapya unatarajiwa kuongezeka kutoka wanafunzi 542 hadi
850; kuangalia uwezekano wa kuanzisha kozi mpya kwenye maeneo yanayohusiana na uchimbaji mdogo, madini ya vito na madini ya viwandani; kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya Chuo kwa kujenga jengo
la wakufunzi ambalo litakuwa na ofisi za wakufunzi pamoja na Ofisi za WIMA; na kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam.
(iv) Shirika la Madini la Taifa – (STAMICO)
118. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19, STAMICO imepanga kuendeleza Mradi wa Dhahabu wa Buhemba kwa kuanza kuchenjua visusu; kufanya uchorongaji ili kujiridhisha na kiasi cha mashapo kilichopo; kufanya topographic survey ya eneo zima la mradi; na ununuzi na usimikwaji wa vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji pamoja na shughuli za uendelezaji wa mradi. STAMICO pia itaendeleza Mradi wa Kiwira wa kuchimba makaa ya mawe katika kilima cha Kabulo. Aidha, ili kufanikisha lengo la kuzalisha makaa ya mawe yatakayokidhi mahitaji ya soko, Shirika linatarajia kutafuta mtambo wa kusafisha makaa ya mawe (washing plant) katika Mradi wa Kabulo ikiwa ni sambamba na kununua mtambo wa kusaga makaa (crusher) hayo, kulingana na vipimo vya mteja husika. Vilevile, STAMICO inatarajia kuanza Mradi wa kuchimba kokoto katika eneo la Ubena Zomozi mkoani Pwani. Shirika pia litaendelea kuimarisha shughuli za kibiashara za uchorongaji na utoaji wa ushauri wa kitaalam katika Sekta ya Madini na kuratibu uendelezaji wa wachimbaji wadogo nchini.
(v) Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia – (TEITI)
119. Mheshimiwa Spika, kazi zitakazotekelezwa na TEITI kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19 ni pamoja na kutoa kwa umma ripoti ya malipo ya kodi yaliyofanywa
na kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa Serikali kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2016/17; kuendelea kuelimisha umma kuhusu matumizi ya takwimu zinazotolewa katika ripoti za TEITI kwa njia ya matangazo, vipindi vya Redio na Televisheni, makala pamoja na warsha; kufanya marekebisho ya dosari zilizobainishwa katika tathmini ya utekelezaji wa masharti ya uanachama wa EITI ili kutimiza vigezo vya uwazi vya kimataifa vya EITI vya Mwaka 2016; na kuanzisha Rejista ya taarifa na majina ya watu wanaomiliki hisa katika kampuni za madini, mafuta na gesi asilia.
(vi) Kituo cha Jimolojia Tanzania – (TGC)
120. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19, Kituo cha Jimolojia Tanzania kinatarajia kutekeleza yafuatayo: kuanza kutoa mafunzo ya Stashahada ya teknolojia ya Vito na Usonara (Diploma in Gem and Jewellery Technology); kutoa mafunzo ya muda mfupi katika fani za Jimolojia; Gem and Jewellery Appraisal; Gem and Jewellery Marketing; Gemstone Faceting; Cabochon Cutting; Utengenezaji wa bidhaa za usonara; na uchongaji wa vinyago vya miamba. Kituo pia kitaendelea na shughuli za ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito ya wateja mbalimbali yanayowasilishwa kituoni; utengenezaji wa marumaru za mawe ya Tanga (Tanga stones/slates); pamoja na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za usonara na mapambo kama vile mikufu, hereni, bangili, vidani, vikuku na pete kwa kutumia madini mbalimbali.
5.0 SHUKRANI
121. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18, Wizara ya Madini ilinufaika kwa misaada na ushirikiano kutoka kwa Washirika mbalimbali wa Maendeleo. Naomba nitumie fursa hii kuwashukuru washirika wetu wote wa maendeleo ikiwa ni pamoja na Benki ya Dunia, Umoja wa Nchi za Ulaya, Serikali za Jamhuri ya Watu wa China, Kanada, Marekani, Jamhuri ya Watu wa Korea Kusini, Misri, Japan na Australia. Serikali itaendelea kushirikiana na washirika hao na wadau wengine wa maendeleo katika kuendeleza Sekta ya Madini nchini.
122. Mheshimiwa Spika, pia, naomba kutoa Shukrani kwa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)-Taifa, UWT Mkoa wa Dar es Salaam, Viongozi na Wanachama wote wa CCM na UWT kwa kushirikiana nami na kuendelea kuniamini. Nawashukuru pia, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi kwa kuniamini kuwa mwakilishi wao katika Bunge na kwa ushirikiano wanaonipatia. Vilevile, naishukuru familia yangu kwa ushirikiano wanaonipatia katika kutekeleza majukumu yangu.
123. Mheshimiwa Spika, niwashukuru Manaibu wangu Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo (Mb.) na Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb.) kwa ushirikiano wao thabiti katika kusimamia utekelezaji wa shughuli za Wizara. Aidha, nawashukuru Katibu Mkuu, Profesa Simon Samwel Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Suleiman Kikula, Makamishna wote wa Tume ya Madini, Kamishna wa Madini na Makamishna Wasaidizi, Wakurugenzi, Wakuu wote wa Idara na Vitengo, Viongozi wa Taasisi
zilizo chini ya Wizara wakiwemo Wenyeviti, Wajumbe wa Bodi na Watendaji Wakuu na Watumishi wote kwa ushirikiano wao na kuhakikisha kuwa rasilimali madini zinanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla. Vilevile, ninalishukuru Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania chini ya uongozi mahiri wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance S. Mabeyo kwa kujitolea katika ujenzi wa ukuta wa Mirerani na kwa ulinzi wanaoutoa katika ulinzi wa ukuta huo.
6.0 HITIMISHO
124. Mheshimiwa Spika, Sekta ya Madini ni muhimu katika kukuza uchumi na kutoa mchango mkubwa kwa Taifa na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka
2025. Aidha, ili kuhakikisha Sekta hii inainufaisha Nchi ipasavyo, Wizara itaimarisha usimamizi wake na kudhibiti utoroshwaji wa madini. Vilevile, Wizara itaendelea kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na uongezaji thamani madini nchini ili kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa.
Maombi ya fedha kwa kazi zilizopangwa kutekelezwa kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19
125. Mheshimiwa Spika, baada ya kueleza kwa kina utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18 na Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19, sasa naliomba Bunge lako Tukufu likubali na kuidhinisha mapendekezo ya Bajeti ya Fungu 100 la Wizara ya Madini ya jumla ya kiasi cha Shilingi 58,908,481,992 kwa ajili ya matumizi ya Wizara na taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19. Mchanganuo wa Bajeti hiyo ni kama
ifuatavyo:-
(i) Bajeti ya Maendeleo ni Shilingi 19,620,964,000: Kati ya fedha hizo, Shilingi 16,800,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 2,820,964,000 ni fedha za nje; na
(ii) Bajeti ya Matumizi ya Kawaida ni Shilingi
39,287,517,158, ambapo Shilingi
18,334,255,000 ni kwa ajili ya Mishahara na Shilingi 20,953,262,992 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC).
126. Mheshimiwa Spika, naomba tena nitoe shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii inapatikana katika Tovuti ya Wizara kwa anuani ya www.madini.go.tz. Vilevile, Hotuba hii ina majedwali na vielelezo mbalimbali kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala na takwimu muhimu kuhusu Sekta ya Madini.
127. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Comments
Post a Comment