Featured Post

UJANGILI NCHINI WAPUNGUA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 50 - DK. KIGWANGALLA


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma jana ambapo walijadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya uhifadhi na maendeleo ya utalii.

Na Hamza Temba-Dodoma
..................................................................
Serikali imefanikiwa kudhibiti vitendo vya ujangili hapa nchini kwa zaidi ya asilimia 50.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma.

Mazungumzo hayo yalilenga kujadili mambo mbalimbali ikiwemo kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika sekta ya uhifadhi na maendeleo ya utalii.

Dk. Kigwangalla alisema katika kipindi cha miezi sita iliyopita hakuna mauaji mapya ya wanyamapori yaliyoripotiwa na kwamba nyara zinazokamatwa hivi sasa ikiwemo meno ya tembo na ngozi za wanyamapori ni masalia ya zamani.

Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kudhibiti vitendo vya ujangili ikiwemo doria za mara kwa mara za kiitelijensia ambazo zimekuwa zikishirikisha vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama pamoja na raia wema. 

Alisema Serikali itaendelea kudhibiti vitendo hivyo kwa kuimarisha ulinzi katika maeneo ya hifadhi nchini ikiwa ni pamoja na kuanzisha jeshi maalum la usimamizi wa Misitu na Wanyamapori, Sheria ya wanyamapori na za taasisi za uhifadhi zimeanza kufanyiwa marekebisho kuwezesha mabadiliko hayo.

Katika hatua nyingine Dk. Kigwangalla amemueleza balozi Cooke kuwa, Serikali kupitia Wizara yake inaendelea kuimarisha  vivutio vya utalii hapa nchini kwa kupanua jeografia ya maeneo ya utalii sambamba na kuongeza vivutio ili kuongeza idadi ya watalii na mapato.

Amesema Serikali itajenga makumbusho ya Marais Wastaafu wa Tanzania mjini Dodoma pamoja kuanzisha makumbusho ya meno ya tembo katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Iringa na Dodoma.

Sambamba na hayo amesema Serikali itaanzisha mwezi maalum wa maadhimisho ya urithi wa Mtanzania ambao utafanyika mwezi Septemba kila mwaka pamoja na kuendeleza utalii wa mikutano.

Amesema Serikali pia itaanzisha Mamlaka ya Usimamizi na Uendelezaji wa Fukwe nchini ili kuimarisha utalii wa fukwe pamoja na kutambua barabara iliyokuwa ikitumika katika biashara ya utumwa wakati wa ukoloni ili iweze kutumika kiutalii.

Akizungumzia migogoro ya mipaka iliyopo baina ya wananchi na maeneo ya hifadhi, Dk. Kigwangalla alisema Serikali itatatua migogoro hiyo kwa kushirikisha wananchi sambamba na kuwasaidia kutatua changamoto za msingi ambazo ni kuimarisha maeneo ya malisho ya mifugo, upatikanaji wa maji kwa ajili ya wananchi na mifugo, mpango bora wa matumizi ya ardhi na uendelezaji wa kilimo na ufugaji.

Kwa upande wake balozi Cooke alisema nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano inaoutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kudhibiti mtandao wa uhalifu wa madawa ya kulevya, rushwa na ujangili.

Alisema kwa sasa watalii zaidi ya 75,000 wa Uingereza hutembelea Tanzania kila mwaka na wengine wamewekeza katika sekta utalii hapa nchini, hivyo akaiomba Serikali kurekebisha baadhi ya changamoto chache zilizopo katika sekta hiyo kwenye mtiririko wa kodi. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma jana ambapo walijadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya uhifadhi na maendeleo ya utalii.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla.
 Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiaga na balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma jana baada ya mazungumzo yaliyolenga walijadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya uhifadhi na maendeleo ya utalii.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiagana na msafara wa balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma jana ambapo walijadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya uhifadhi na maendeleo ya utalii.

Comments