Featured Post

TUCHANGIE MAENDELEO KAMA TUNAVYOCHANGIA HARUSI ZETU



Na Daniel Mbega
NI siku nyingine ya Jumamosi niko kwenye uga wa Msimbazi Centre jijini Dar es Salaam, majira ya saa 10:00 hivi jioni.
Mandhari ya eneo hili wakati huu yamebadilika mno tofauti na nyakati za asubuhi au mchana. Uwanja wote mbele ya ukumbi huu mkubwa kabisa wa Marantha umefurika watu kweli kweli, wameketi vikundi vikundi.
Awali nilidhani kuna sherehe kubwa hapa wakati wenyeji wangu waliponiambia nitawakuta pale, lakini naambiwa vikundi hivyo ninavyoviona ni vya watu ambao hawajuani, kila kimoja kina mambo yake.

“Hivi vyote ni vikao vya harusi, wala usishangae. Hao wenyeji wako wamekwambia wameketi mahali gani? Kama hawajakwambia, basi wapigie simu, maana unaweza kupotea,” mhudumu mmoja ananidokeza.
Na kweli, hapa unaweza kupotea, kwa sababu kwa hesabu ya haraka tu vinaweza kuwa vikundi zaidi ya hamsini vyenye watu wasiopungua hamsini kila kimoja, wanakula, wanakunywa na wanaendelea na mipango yao – ya kutafuta michango ya harusi.
Kwa bahati nzuri wenyeji wangu wananiona. Unajua wakati mwingine maumbile yetu haya yanasaidia, unaweza kusimama wakakufananisha na mlingoti kwa jinsi tulivyo wembamba kama tunakula saruji. Usishangae, miili mingine haina shukrani, hata uilishe vipi haifumuki bwana!
Naam. Nimeingia kwenye kikao hiki cha harusi – kutafuta michango ya shehere ya harusi. Sikwambii ni harusi ya nani hiyo, lakini tambua kwamba hii ndiyo kawaida yetu Watanzania kuchangishana linapokuja suala la kuwahalalishia watu ‘kulala bila nguo’. Ni jambo la kheri, au siyo wanajamii wenzangu?
Lakini harusi hii siyo ‘mpya’, ni kwamba wahusika hawa wanataka ‘kubariki ndoa’ yao kwa sababu ni watu wazima sana, wenye watoto na wajukuu. Wameishi muda mrefu ‘kienyeji’ na sasa wanaona siyo vyema wasishiriki ‘Meza ya Bwana’, inabidi wakabarikiwe.
Kikao hiki cha kwanza tu, kwa hesabu ya haraka vinywaji na vyakula vyake vimegharimu siyo chini ya Shs. 1 milioni, ambazo zote zimetoka mfukoni mwa Bwana na Bibi Harusi watarajiwa.
Usishangae wametoa fedha nyingi hivyo, wao wanatarajia watakusanya zaidi ya hizo. Si wanasema: ‘Ukitaka kula lazima uliwe?’ Hivyo nao wanaamini wajumbe waliohudhuria watashawishika zaidi kufungua pochi zao ili kuifanya sherehe yenyewe iwe zaidi ya hapa.
Ndiyo. Tunaisikiliza bajeti husika, kwa bahati nzuri nateuliwa kuwa Katibu wa Kamati, hivyo ndiye ninayeandika humu. Tuko jumla ya wajumbe 60. Tunaambiwa kwamba, bajeti ya awali ni Shs. 15 milioni! Unashangaa nini? Watu wanakwenda kubariki tu ndoa, fikiria kama ndiyo ingekuwa ya kwanza, bajeti ingekuwaje?
Bwana harusi mtarajiwa anaahidi Shs. 2.1 milioni na anatoka keshi Shs. 1 milioni. Bibi harusi mtarajiwa naye anaahidi Shs. 600,000 na anatoa 100,000 keshi! Wacha mchezo bwana. Ahadi za wajumbe kwa siku hiyo tu ni Shs. 10 milioni na zinazokusanywa taslimu ni Shs. 2 milioni!
Kumbe hata wangeamua wao wenyewe kuandaa sherehe wangeweza kama ahadi yao tu ni Shs. 2.7 milioni! Wangewaita watu wakaja kunywa na kucheza, wangekula na kusaza.
Siyo mara ya kwanza kuona watu wakichangia sherehe, achilia mbali harusi. Siku hizi hata sherehe ya ubarikio zinachapishwa kadi na kusambazwa, sherehe ya mahafali na bethidei mambo na hivyo hivyo. Na jamii yetu iko tayari kabisa kuchanga kwa ajili ya sherehe ya siku moja.
Ninashangazwa jinsi tulivyo na umoja huu wa kuchangishana kwenye sherehe mbalimbali, ambako wengine wetu hufanya kwa sifa ili tuonekane ‘tunazo’ na kusifiwa sana. Tunachanga ili tukale na kunywa siku moja, tunasahau.
Lakini linapokuja suala la kuchangia maendeleo, watu wale wale wanaochanga maelfu kwa mamilioni kwa ajili ya sherehe za harusi ndio huwa wa kwanza kubeza na kusema kwamba wao hawahusiki kuchangia maendeleo, bali serikali ndiyo yenye wajibu wa kuchangia.
Fikiria kijiji kina mashine ya maji, lakini mashine hii imekosa kipuri kidogo tu ambacho kikifungwa itapona na jamii itapata huduma ya maji. Wananchi hawako tayari kuchanga fedha kwa ajili ya huduma hii ya kudumu, bali wanaitaka serikali ndiyo ije iwatengenezee.
Watoto wetu wanaketi kwenye vumbi kwa sababu hakuna madawati, shule zetu nyingi za vijijini zinakosa walimu makini kwa sababu wengi wanakataa kuja kwa kuwa hakuna nyumba za kuishi walimu, watoto hawana rejea yoyote kwa kuwa vitabu hakuna, lakini mbaya zaidi, shule zetu hazina hata chaki!
Mwanajamii huyu anayaona yote haya, lakini anasema siyo jukumu lake, bali ni la serikali. Sikatai, kwamba serikali ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha huduma zinawafikia wanajamii wake. Lakini hivi hata kujenga ukuta wa choo cha shule tusubiri serikali ije itujengee? Sisi wanajamii hatuyaoni hayo?
Mbona kwenye sherehe hatusemi ‘bwana na bibi harusi’ ndio wajibu wao kutuandalia chakula na vinywaji, sisi hatuna haja ya kuchangia? Mbona tunakuwa wepesi wa kutafuta sifa ya mara moja badala ya kufikiria mipango ya maendeleo yetu?
Jamani, sisemi msichangiane kwenye harusi zenu. La hasha. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba, ikiwa kasi ya kuchangia shughuli za maendeleo ingekuwa kubwa kama tunavyochangia sherehe za harusi na bethidei, hakika jamii yetu ingekuwa imepiga hatua kimaendeleo.
Wakati mwingine, nasikitika kusema, ni ujinga kuitupia kila mzigo serikali wakati hata sisi wenyewe tunaweza kufanya kazi za maendeleo, tena kwa kiwango kikubwa kabisa.
Tubadilike wanajamii wenzangu, maendeleo yetu yataletwa na sisi wenyewe. Lazima tushiriki maendeleo yetu kwa vitendo badala ya kusubiri serikali, tutakwama.

0656-331974

Comments