- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
VITENDO
vya rushwa na ufisadi uliotamalaki, utendaji wa mazoea wa viongozi wa Serikali
na watumishi wa umma, kutowajibika kikamilifu kwa viongozi, urasimu katika
utekelezaji wa huduma za wananchi,
mishahara hewa, mikataba mibovu pamoja na deni kubwa la Taifa ni uvundo
uliokuwa umetanda nchini Tanzania kwa miaka kadhaa.
Watendaji
wa umma kufanya kazi kwa mazowea huku wakilindana hata pale wanapoharibu kazi
au mali ya umma ni mambo ambayo yalikuwa kero kubwa kwa wananchi.
Katika
kipindi cha nyuma haikuwa ajabu kuona ofisa mmoja akivurunda kazi au hata
kutuhumiwa kwa ufisadi, lakini badala ya kuwajibishwa alikuwa akihamishiwa
idara nyingine au kituo cha kazi.
Lakini
miaka miwili na miezi takriban minne tangu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
achukue madaraka, hali imebadilika na sasa wananchi wanashuhudia namna
watendaji wa umma wanavyowajibika licha ya kwamba baadhi ya huduma bado
hazijatengemaa kutokana na ufinyu wa bajeti.
Zile
kashfa za udungunaizesheni zilizokuwa zikipigiwa kelele huko nyuma, kwamba
ukiingia kwenye taasisi moja unaweza kukuta watoto wa vigogo wamejaa, hivi sasa
zimepungua au hazipo kabisa, bali wanaopewa nafasi ni wale wenye sifa sitahiki
na wanawajibika.
Tumeshuhudia
namna Rais Dkt. Magufuli anavyowatumbua viongozi wazembe na kunyoosha mambo
ambayo yamekuwa hayaendi sawa kwa muda mrefu.
Tuliona
namna wafanyakazi wa umma walivyoanza kubanwa katika suala la kuwahi kazini na
kuwajibika wakati hata mawaziri walipoonyesha mfano wa kuwahi ofisini wakiwa
wameshika madaftari ya mahudhurio na wale waliochelewa walikiona cha moto.
Hivi sasa
ile tabia ya ‘kuzowea kazi’ haipo na watu wanawajibika na huduma zinatolewa
bila upendeleo na kwa wakati.
Zamani
haikuwa ajabu kuona mama mjamzito anafika hospitali halafu nesi badala ya
kumhudumia anazungumza na mtu kwenye simu: “Shoga, mwenzio jana si nilikuwa na
yule bwege pale Kijungu Baa… basi akajilengesha nikamnywea halafu nikatimua kwa
kupita mlango wa uani…!”
Katika
maeneo mengi ya umma, hivi sasa unapofika unaweza kuulizwa hata mara tano na
watu tofauti, kila mmoja akitaka kukuhudumia. Nidhamu ya kazi imerejea.
Katika
masuala ya kuendeleza uchumi, tumeshuhudia namna serikali inavyojitahidi
kuboresha miundombinu mbalimbali pamoja na kuweka mazingira mazuri ya usimamizi
wa rasilimali.
Bandari ya
Dar es Salaam ilikuwa kama shamba la bibi ambapo watu walikuwa wakijichotea
mabilioni ya fedha watakavyo kwa kushirikiana na wafanyabiashara wasio
wazalendo kukwepa kodi na ushuru.
Makontena
mengi yalikuwa yamepitishwa bandarini bila kulipiwa ushuru, lakini
alipokabidhiwa ofisi tu, Rais Magufuli alianza kuwashughulikia wote waliokwepa
ushuru huo wakalipa.
Maofisa
waliokuwa wamehusika kwa namna moja ama nyingine nao walishughulikiwa na
wengine mpaka sasa kesi zao bado zinaendelea mahakamani.
Mikataba
mingi ilionekana kuwa na upungufu mkubwa huku wawekezaji wakizoa rasilimali
zetu huku sisi tukipiga miayo, lakini hili nano Rais Magufuli amelishughulikia
kwa kiasi kikubwa bila hata kumtazama mtu usoni.
Tuliona
namna alivyoshughulikia suala la makinikia, ambapo licha ya wahusika kupiga
kelele, bado serikali ilishikilia msimamo wake mpaka wawekezaji hao
walipolazimika kukaa mezani.
Tumeona
maendeleo mengine kufuatia ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Tanga,
ujenzi ambao siyo tu utaimarisha uchumi wa Watanzania, bali utatoa fursa kubwa
ya ajira kwa wananchi linakopitia.
Hivi sasa
ujenzi wa Reli ya Kati unaendelea kwa kasi, na endapo reli hiyo itakamilika
yote na safari za treni ya mwendokasi kuanza, sidhani kama kutakuwa na mtu
atakayepanda basi kwenda Mwanza au Kigoma, kwani safari hizo zinazotumia saa 14
sasa zitatumia saa nane tu.
Yapo mengi
ambayo Rais Magufuli ameyafanya na anaendelea kuyafanya katika kusafisha uvundo
mwingi uliotamalaki nchini ambayo kwa hakika yanaleta taswira njema ya Tanzania
yenye neema na nidhamu.
Lakini
pamoja na jitihada hizo, bado kuna watu wanaompinga na wengine wanafikia hata
hatua ya ‘kuwahurumia’ wezi na mafisadi wakati huko nyuma wao ndio waliokuwa
mstari wa mbele kusema serikali ilikuwa inalea uozo.
Viongozi
wanaotuhumiwa kwa ufisadi walipotumbuliwa, wapinzani wenye kawaida ya kupinga
kila jambo wakajitokeza na kusema hatua hiyo ni kinyume na haki za binadamu na
wakafikia mahali wakataka kuwatafutia na wanasheria ili kuwatetea mahakamani.
Unaweza
kusema Rais Magufuli hajafanya kitu kwa kuisafisha Bandari na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) ambako ndiko mapato mengi ya serikali yalikuwa yakipotelea? Au
wanaobeza waseme wazi kwamba nao ni miongoni mwa wanufaika wa ufisadi huo!
Wapinzani
hawa hawana tofauti na ndugu wa mume ambao daima huwa hawaishi visa kila
kukicha.
Tunafahamu
katika jamii zetu kwamba gubu la mawifi na kejeli ni mambo ya kawaida
yanayompata mwanamke kutoka kwa ndugu wa mumewe.
Tumeshuhudia
mara nyingi ndani ya jamii pindi ndugu wa kiume anapoamua kuoa, hasa mwanamke
anapokuwa siyo chaguo la wanandugu – wazazi ama dada zake – kwamba mkamwana
huyo hupata shida sana kuelewana na ndugu wa mumewe.
Kama
hakuambiwa mvivu, basi ataambiwa mchoyo; na kama hakuambiwa ana maringo, ndugu
wa mume watamtoa kasoro yoyote kwamba ama ni mbaya, havutii na kadhalika,
ilimradi tu hawakosi cha kuongea.
Wanawake
wengi wanapoolewa hujiandaa kwa mazingira hayo, wakati mwingine hata waume zao
huwatahadharisha kuhusu tabia za ndugu zao.
Hata
hivyo, maandalizi hayo huwa hayasaidii kwa sababu kila siku ndugu wanaibuka na
mazengwe mapya, hawakosi cha kuongea na ukarimu wa mke huwa si kitu kwao.
Kama
walivyo ndugu wa mume wasiokosa sababu, wapinzani hao walianza kwa kubeza,
kukejeli na kupinga uamuzi mbalimbali wa serikali tena katika mambo ambayo ni
ya msingi kabisa ambayo hata wenyewe walikuwa wakiyanadi kwa wananchi kwamba
wangeyatekeleza wakiingia madarakani.
Tunafahamu
kwamba, baadhi ya wanaopinga jitihada za serikali wanafanya hivyo kwa sababu
Dkt. Magufuli hakuwa chaguo lao, lakini maadam ndiye Rais, hawana budi
kumkubali.
Dkt.
Magufuli anayafahamu hayo yote na alijiandaa kwa ajili ya kuwatumikia
Watanzania walio wengi na kamwe hana muda wa kumfurahi mtu fulani ama kikundi
cha watu.
Kama
alivyopata kusema kada wa siku nyingi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Steven
Mashishanga, kwamba Rais Dkt. Magufuli ni binidamu kama binidamu wengine na
asichukuliwe kama malaika licha ya kwamba ana madaraka makubwa ya urais.
Kwa maana
nyingine, Rais Magufuli anaweza kukosea mahali na jambo hilo ni la kawaida kwa
binadamu yeyote, lakini makosa hayo yasichukuliwe kama kigezo cha kwamba
kiongozi huyo anawakandamiza wengine.
Ni wazi
kwamba katika utendaji wake wapo watakaoumia na wapo watakaonufaika – kamwe
watu hawawezi kuwa sawa.
“Hakuna
kiongozi mkuu wa nchi duniani kote ambaye anaweza kufanya kazi kama malaika
pasipo kulaumiwa na wananchi anaowaongoza, hata kama anatenda mazuri kiasi
gani.
“Magufuli
ni kiongozi mzuri sana, lakini sio malaika. Anayo mapungufu madogo madogo ukilingalinisha
na mazuri yake mengi, hata hivyo njia nzuri ya kupima utendeji wake ni mwaka
2020, huo ndio utakuwa wakati muafaka wa kupima nini amefanya na nini hajafanya
katika kutekeleza ilani ya CCM aliyonadi kweye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,”
Mashishanga alipata kukaririwa.
Kwa
ujumla, Dkt. Magufuli amekwishaonyesha njia ya wapi anataka Tanzania ifike lakini
bado anakabiliwa na masuala mengi kwa wakati mmoja na kwa kuwa ameonyesha
dhamira ya kutatua kero sugu ambazo zimekwaza maendeleo kwa muda mrefu, ni
lazima atalaumiwa na wananchi hususan wale waliozoea kuishi kwa mazoea.
“Huyu si
malaika kusema kwamba atafanya mazuri tu ambayo yatampendeza kila mmoja.
Wanaomlaumu sasa Rais Magufuli hawakosei, kama wasingemlaumu leo, ni lazima
wangelijitokeza tu.
“Kwa kuwa
Rais Magufuli ameonyesha dhamira ya dhati ya kupambana na madudu, wale waliozowea
kuvuna vipato vyao kupitia rushwa, kughushi nyaraka na wavivu kazini lazima
watamlaumu na kumuona kuwa hafai, lakini mimi nasema utendaji wa Magufuli zaidi ya asilimia 90 ni mzuri,’’
alisema.
Inaonekana
kabisa kwamba, kilichokuwa kinachangia utendaji mbovu wa serikali ni mfumo
uliokuwepo, ambao hauwezi kufumuliwa kwa ghafla kama wengine wanavyotamani.
Rais
Magufuli amejitahidi kupambana na mfumo huo kwa staili yake ya ‘kutumbua
majipu’ na hata kuwawajibisha watendaji wazembe na wabadhirifu ni sehemu tu ya
kupambana na mfumo huo.
Kitendo
cha serikali kukusanya mapato mengi kila mwezi tangu serikali ilipoingia
madarakani kinadhihirisha kwamba ni hatua kubwa kabisa iliyofikiwa na serikali
hiyo katika kuhakikisha kodi zinakusanywa kukuza uchumi wa taifa.
Wapo hata
wanasiasa wanaobeza uamuzi wa kufukuzwa ama kusimamishwa kwa watendaji wa
serikali wanaotajwa kwa ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka ambao
ndio wamekuwa kwenye mfumo huo mbovu, lakini wanaobeza wanasahau kwamba ni
vitendo hivyo hivyo vya watumishi hao vilivyoifanya serikali yote ionekane
haifai.
Ndani ya
serikali kumekuwepo na vikundi vilivyounda mfumo wa kifisadi, na hivi ndivyo
vinavyovunjwa na serikali bila kuoneana haya. Hili linastahili kupongezwa kwa
bidi.
Wanasiasa
wanasema Rais Magufuli hajafanya lolote bali anaboresha yaliyokuwepo. Nashindwa
kuelewa, hivi hawaoni kuboresha tu yaliyokuwepo ni hatua moja muhimu zaidi kuliko
kushughulikia mapya wakati yale ya zamani yanasuasua?
Ni vizuri
basi wanaomsifu ama kumkosoa Rais Magufuli wakatumia hekima na busara na wawe
na kiasi kwa kuona kwamba yako mambo mengi mema yaliyofanyika na pia kuna
mahali anaweza akawa amekosea kibinadamu.
Kumbeza
Rais kwamba hajafanya chochote ni kutomtendea haki kwa sababu utendaji wake
unaonekana hadharani, labda kama wanaombeza watakuwa na hoja nyingine.
0656-331974
Comments
Post a Comment