Featured Post

MPRU YAPATA MTENDAJI MPYA




Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina(aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati Ndogo ya Kutathmini Utendaji wa Sekta ya Uvuvi katika Ziwa Victoria baada ya kukabidhi taarifa hiyo mjini Dodoma hivi karibuni.Waliokaa kuanzia kushoto Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Bonaventure Baya Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi, Dk Yohana Budeba, aliyesimama kuanzia kushoto John Komakoma Kaimu Meneja wa MPRU.

Na John Mapepele, Dodoma

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina amemteua John David Komakoma kukaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu nchini (MPRU) baada ya kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa awali Dkt. Milali Machumu kutokana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kubaini dosari katika usimamizi wa Kitengo hicho.

Pia Waziri Mpina amevunja Bodi ya Wadhamini ya MPRU iliyokuwa chini ya Uenyekiti wa Profesa John Machiwa ambayo ilikuwa na Wajumbe nane.

Mpina alisema ameamua kuvunja bodi na kumsimamisha Mtendaji huyo kwa mamlaka aliyonayo kulingana na Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Na 29 ya mwaka 1994.

Aidha Mpina amemwagiza Katibu Mkuu wa Uvuvi kuunda Kamati ya kuchunguza utendaji wa kazi wa Mtendaji wa awali.

Akizungumza mara baada ya uteuzi huo Komakoma ambaye ni mtaalam wa Bailojia ya Baharini amesema atahakikisha kuwa maeneo yote ya bahari yaliyotengwa yanahifadhiwa kikamilifu ili kuleta Mchango mkubwa katika taifa letu.

“Nina imani kwamba maeneo haya ni muhimu sana kwa uhifadhi wa raslimali za bahari na utalii endelevu hivyo hatuna budi kuyasimamia kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo” alisisitiza Komakoma.

Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kiliundwa na sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu  Mwaka 1994 ambapo baadhi ya majukumu yake makuu yameanishwa katika sehemu ya VI kifungu cha 10 ambayo ni pamoja na kulinda na kuhifadhi maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa bioanuai pamoja na mifumo ya ikolojia ya baharini na mwambao wa pwani.

Kuhamasisha wananchi kutumia kwa busara raslimali ambazo hazitumiki kabisa au hazitumiki kikamilifu kwa sasa, kusimamia maeneo ya bahari na mwambao wa pwani ili kuwezesha matumizi endelevu ya raslimali na ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa.

Kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi wanashirikishwa katika nyanja zote za upangaji,uendelezaji na usimamizi wa raslimali.

Hadi sasa kuna Hifadhi za Bahari tatu na Maeneo Tengefu 15 hapa nchini katika mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Mtwara.

Kabla ya uteuzi huu Komakoma alikuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi katika Kitengo cha Udhibiti Ubora, Usalama, Viwango na Masoko ya Mazao ya Uvuvi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Comments