Featured Post

MBEYA YATEULIWA KWA UMAHIRI WA VIAZI MVIRINGO



Na Mwandishi Wetu, Mbeya
MKOA wa Mbeya umeteuliwa kuwa miongini mwa vituo vya umahiri wa kilimo cha zao la viazi mviringo hapa nchini, yaani Centre of Excellence.
Kutoka na kuteuliwa huko, serikali kwa kuwatumia wataalam wa kilimo hicho wa ndani na nje ya nchi itatengenezwa Programu maalum ya kuliendeleza zao hilo kibiashara.
Ujenzi wa kituo hicho unafuatia utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo Uyole na wataalamu wa zao hilo kutoka Uholanzi ambao Juni 2016 walitembelea maeneo kadhaa yanayolima viazi na kujiridhisha kuwa zao hilo likitiliwa mkazo linaweza kuongeza uchumi wa wakulima, mkoa na Taifa.

Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Uchumi na Uwezeshaji mkoani Mbeya, Nyasebwa Chimangu, amesema ujenzi wa kituo hicho utafanyika katika eneo la Uyole wakati wowote kuanzia sasa.
Nyasebwa alikuwa akitoa ufafanuzi juu ya mkakati wa mkoa katika uendelezaji wa kilimo cha bustani, mboga mboga na matunda ambacho licha ya kulimwa kwa wingi, wakulima mkoani humo hawajawekewa mazingira rafiki ya kukiendeleza kibiashara hasa katika suala la ubora, uhifadhi na uongezaji wa thamani.
"Uwepo wa Uwanja wa Ndege cha Kimataifa cha Songwe ni fursa nyingine ya kuboresha kilimo hiki baada ya kupatikana wawekezaji walioonyesha nia ya kuwekeza kwenye usafirishaji na uhifadhi wa mazao haya uwanjani hapo.
"Ninazikumbusha tu halmashauri zote mkoani humu kuandaa maeneo yatakayojengwa vituo vya kuhifadhia mazao hayo kabla ya kwenda sokoni," alisema.
Mkoa wa Mbeya ni wa pili katika uchangiaji wa Pato la Taifa baada ya Dar es salaam, huku sekta ya kilimo ikichagiza sifa hiyo huku mazao ya bustani yanachangia wastani wa asilimi 31 ya pato la mkoa ambapo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017 jumla ya tani milioni 3.6 za mazao hayo zilizalishwa.


Comments