Featured Post

MAGUFULI ALIPOAHIDI WALISEMA AHADI NYINGI, SASA ANAZINDUA WANAMKEJELI!



Na Daniel Mbega
IJUMAA, Aprili 6, 2018 Rais Dkt. John Pombe Magufuli, alizindua rasmi ukuta wenye urefu wa kilometa 24.5 kuzunguka eneo la Mgodi wa Tanzanite huko Mirerani wilayani Simanjiro katika Mkoa wa Manyara.

Huo ulikuwa ni moja ya uzinduzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano, ikiwa ni katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ahadi alizozitoa kwa Watanzania katika kulinda rasilimali za taifa, yakiwemo madini.
Ujenzi wa ukuta huo uliogharimu Shilingi 5,645,843,163, umefanywa na vijana wetu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) pamoja na makamanda wao wakiwemo wahandisi kutoka JKT.
Licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kama ujenzi kwenye miamba na makorongo na uwepo wa mito ya misimu, lakini ujenzi huo uliokuwa utekelezwe kwa kipindi cha miezi sita sasa umeweza kukamilika ndani ya miezi mitatu tu.
Kujengwa kwa ukuta huo kutasaidia sana ulinzi wa eneo hilo, hasa kutokana na uvamizi pamoja na wizi holela wa madini ya vito ya Tanzanite ambayo duniani kote yanapatikana Tanzania peke yake.
Pamoja na jitihada hizo njema za serikali katika kulinda rasilimali, lakini mitandao ya kijamii imeendelea kujawa na kejeli za wapinzani ambao wanahoji manufaa ya ujenzi wa ukuta huo.
Wengine bila haya wala aibu, wanahoji kwa nini akazindue yeye badala ya kuwaachia wasaidizi wake, mawazo ambayo hayana maana yoyote.
Kama hiyo haitoshi, wapinzani wa maendeleo wanaendelea kubeza jitihada hizo ambapo wapo wanaosema kwamba kelele za utekelezaji na uzinduzi wa miradi zimekuwa nyingi na wengine wanafikia mahali kusema kwamba eti hakuna kipya kilichofanywa na serikali ya sasa kwa kuwa "mambo yote yanayofanyika ilikuwa ni mipango ya watawala waliotangulia!"
Haya ni maneno yasiyo na maana kwa wapinzani hawa ambao daima wamekuwa wakipinga kila jambo na kujeli hata mambo ya msingi.
Jumapili, Agosti 23, 2015 Chama cha Mapinduzi (CCM) kilizindua rasmi kampeni zake za uchaguzi mkuu na Dkt. John Magufuli, wakati huo akiwa ndiye mgombea mteule wa urais kupitia chama hicho, alianza kwa kutoa ahadi mbalimbali.
Kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele, ahadi mbalimbali zilitolewa kulingana na changamoto na mahitaji ya jamii, kubwa zaidi zikiwa kuwaletea Watanzania maendeleo, kuinua uchumi, kukomesha rushwa na ufisadi na mambo mengine kadha wa kadha.
Katika kipindi kile, wale wapinzani walikejeli na kusema kwamba Magufuli alikuwa anaahidi vitu vingi ambavyo kwa mawazo yao walisema "havitekelezeki".
Alipoanza kuwashughulikia mafisadi na kukomesha uzembe, walisema hiyo ilikuwa nguvu ya soda, kwamba kasi yake ingefikia ukomo.
Sasa anapoendelea kuzindua miradi inayotekelezwa na serikali, ikiwemo ile aliyoiahidi mwenyewe wakati wa kampeni, watu wale wale wanaanza kusema "anazindua sana". Jamani hivi Watanzania, na hasa nyie wapinzani wa maendeleo, mnataka nini?
Na kwa bahati mbaya zaidi ni kwamba, mitandao ya kijamii imewageuza baadhi ya watu kama mavuvuzela na kuuelezea wivu wao, wakikesha na kushinda humo kupinga kila jambo.
Kwa bahati nzuri ni kwamba, gharama ya kuperuzi mitandao hiyo ni ndogo na inawapa kiburi walio wengi kuropoka maneno ya hovyo, lakini kama ingalikuwa kubwa, naamini hakuna ambaye angeweza kuingia na wangekimbia kama wanavyoishia kusoma vichwa vya habari vya magazeti kwenye mbao za matangazo.
Kama wanapinga sasa, hebu waeleze wao zile ahadi zao wangezitekelezaje? Wangekaa majumbani ama maofisini mwao kuagiza utekelezaji bila kufika sehemu husika kukagua kama anavyofanya Rais Magufuli?
Kama wanasema ipo miradi ambayo ilibuniwa katika awamu zilizopita na yeye anatekeleza, je, huko siyo kustahili pongezi kwa sababu amefanya kile kilichowashinda wengine?
Tutaendelea kuwakumbusha wapinzani pale wanaposahau, au kama hawaoni tutawaeleza kwa mdomo na ikibidi tutawasogeza karibu ili walau wapapase tu ili kutambua kilichofanyika.        
Leo mtu anapinga kununuliwa kwa ndege zetu wenyewe! Hivi kweli mtu wa aina hiyo ana akili sawa sawa? Na iweje ahimize kufufuliwa kwa shirika la ndege wakati hataki ndege zinunuliwe? Hilo shirika litawezaje kuwepo bila ndege?
Watu wanapinga kujengwa kwa ukuta, lakini ni hao hao waliokuwa wakilalamika kwamba madini ya Tanzanite yanaibwa holela, watu wanaingia holela na kuyazoa huku serikali ikiwa haipati kitu. Leo hii kila chembe ya Tanzanite itakayotoka mgodini lazima itamulikwa na tutapata kodi yetu kama inavyostahili.
Wengi wanakejeli ununuzi wa radar, siyo kama akili zao zinawatosha, kwa sababu haiwezekani anga letu likaongozwa na nchi nyingine kwa kuwa tu sisi tumekosa vitendea kazi. Hiyo ni hatari hata kwa usalama wetu.
Narudia tena, wapinzani msiwe na magubu na kejeli kama ndugu wa mume, mnakwamisha maendeleo kwa sababu za kisiasa na kiharakati.
Tunafahamu umuhimu wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa taifa letu, lakini kamwe wapinzani hamwezi kuwadanganya Watanzania kwamba serikali ama imekosea au hicho siyo kipaumbele.
Tena basi wengi tunatambua kwamba, ujenzi wa reli hiyo unafanyika kwa vipande vipande, yaani kwa awamu, na kila kipande kina mkandarasi wake kwa mujibu wa mkataba na zabuni zilivyotangazwa, mmoja anatoka Dar es Salaam hadi Morogoro, mwingine anatoka Morogoro hadi Dodoma.
Vivyo hivyo, kutakuwepo pia na vipande vipande kutoka Dodoma hadi Tabora, Tabora hadi Kigoma, Tabora hadi kufika Mwanza, na hata mpakani na Rwanda ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
Kwahiyo, haishangazi kuona Rais Magufuli akizindua ujenzi kwa awamu kwa sababu reli hiyo haijengwi kwa mara moja.
Hoja kwamba kazi hizo zingeweza kufanywa na wasaidizi wake nazo hazina mashiko kwa sababu hata hao wasaidizi - Makamu wa Rais na Waziri Mkuu - nao wana majukumu mengine ya kufanya.
Haya mnayoyafanya yanaonekana kwa wananchi hao hao mnaodai mnawatetea na kwamba eti wanataka mabadiliko.
Mabadiliko ya kweli wananchi wanayaona, wameona utendaji wa watumishi wa umma umebadilika, wanaona vita dhidi ya ufisadi ilivyopiganwa, wanashuhudia jinsi serikali ilivyosafisha watumishi hewa, na zaidi wanaona namna changamoto zao za maendeleo zinavyotatuliwa kutokana na miradi hiyo ya maendeleo ambayo nyie mnaikejeli.
Hakika hii ndiyo inayoitwa 'bumper to bumper' na wapinzani wataendelea kupiga kelele mitandaoni huku siku zinayoyoma wakiwa hawajafanya lolote la maana kwa kuimarisha vyama vyao.
Mwisho wa siku, sanduku la kura ndilo litakuja kuhukumu kama anayoyafanya Rais Magufuli ni sahihi au la, vinginevyo wapinzani wanatakiwa kukaa kimya!
0656-331074

Comments