- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
MENGI kati
ya magari 50 ya kutema maji ya kuwasha (washawasha) yaliyotumika wakati wa
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 yametelekezwa baada ya kukosa shughuli ya kufanya.
Taarifa za
ndani zinaeleza kwamba, ingawa ilipendekezwa kuwa magari hayo yatumike katika
Kikosi cha Zimamoto ili kupunguza uhaba wa magari katika kitengo hicho kilicho
chini ya Jeshi la Polisi, lakini uamuzi huo bado haujapitishwa.
Mnamo Mei
18, 2016, Serikali, kupitia kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Yusufu
Hamad Masauni, ilisema ilikuwa katika mchakato wa kuangalia uwezekano wa kubadili
matumizi ya magari ya polisi ya washawasha ili yaweze kutumika kuzima moto.
Naibu
waziri huyo alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa
Mbozi (Chadema), Pascal Haonga, aliyeuliza ni kwanini Serikali inanunua magari
ya washawasha yasiyo na tija ambayo hutumika nyakati za uchaguzi tu badala ya
kununua magari ya zimamoto.
Uchunguzi
unaonyesha kwamba, magari hayo 50 ya washawasha yalikuwa sehemu ya magari 777
yaliyoingizwa nchini kwa ajili ya kupatiwa Jeshi la Polisi, ambapo siku tano
kabla ya Uchaguzi Mkuu, yaani Jumanne, Oktoba 20, 2015, Rais (mstaafu) Dkt.
Jakaya Kikwete, alikabidhi kwa jeshi hilo magari 399, tukio lililofanyika katika
Chuo cha Polisi Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Magari
20 kati ya 399 yaliyokabidhiwa siku hiyo yalikuwa ya washawasha na mengine ya
kawaida ambayo lengo lake lilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kufanya doria na
shughuli zingine za kipolisi.
Magari kununuliwa kwa
mkopo
Uchunguzi
unaonyesha kwamba, magari yote 777 yaligharimu jumla ya Dola 29,606,100
(takriban Shs. 60 bilioni), ambazo ni fedha za walipa kodi. Taarifa za ndani
zinasema, hata kampuni iliyouza magari hayo, Ashok Leyland ya India, haijalipwa
fedha zake zote zaidi ya kupokea kiasi cha Dola 10,362,135 (takriban Shs. 21
bilioni) sawa na asilimia 35 ya gharama licha ya mkataba wa malipo kusainiwa
Juni 19, 2015 na magari ya kwanza kukabidhiwa Oktoba 20, 2015 kwa Polisi.
Uchunguzi
unaonyesha kwamba, ukiacha magari madogo aina ya Toyota Land Cruiser na Leyland
Vans, magari ya washawasha ‘yametelekezwa’ kutokana na kukosa shughuli za
kufanya kwa sasa.
Wataalam
wa masuala ya vyombo vya moto wanaeleza kwamba, yakiachwa kwa muda mrefu bila
kutumika yanaweza kuharibika baadhi ya vipuri, hali ambayo itaitia hasara kubwa
serikali.
Hata
hivyo, wanashauri kwamba, kwa kuwa kazi kubwa ya magari ya washa washa ni
kutuliza ghasia na kwa vile ghasia hazipo, ingalikuwa jambo la busara kama
Wizara ya Mambo ya Ndani ikayapeleka kwa muda magari hayo kwenye Jeshi la
Zimamoto, ambapo kwa kuyafanyia marekebisho kidogo, yangeweza kusaidia kuokoa
amali pale ajali za moto zinapotokea.
Aidha,
wengine wanashauri kwamba, wizara hiyo pia inaweza kuyapaleka magari hayo
kwenye Jeshi la Magereza kwa ajili ya kusaidia kumwagilia mbolea za maji maji
kwenye mashamba ya jeshi hilo nchini.
“Kwa
kuwa yana uwezo wa kumwaga maji kwa kunyunyiza, nashauri serikali ingeweza
kuyapaleka hata Magereza ambako yanaweza kutumika kumwagilia mbolea za majimaji
na yatakapohitajika yanaweza kurudishwa polisi kuliko kuyaacha yameegeshwa,”
anashauri Mohammed Mtandika, mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Mohammed
anasema, katika baadhi ya nchi zilizoendelea, magari ya aina hiyo hutumika
kumwagilia hata mbolea za asili hasa zinazotokana na kinyesi cha nguruwe baada
ya kuzichakata katika hali ya majimaji.
Ujio
wa magari hayo katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi ulijenga taswira kwamba
Chama Tawala kilikuwa kinaliimarisha Jeshi la Polisi ili kiweze kulitumia
kujiokoa na wimbi la mageuzi lililokuwa linaendelea nchini, ambapo kila
Mtanzania alitaka kuona ‘mabadiliko’ ya uongozi.
Ingawa
Rais Mstaafu JK alikanusha vikali kwamba magari hayo hayakuletwa kwa ajili ya
‘kuwadhibiti wakorofi’ wakati wa uchaguzi, lakini ukweli ni kwamba ulikuwa ni
mkakati wa serikali kupitia Jeshi la Polisi kujidhatiti ili kukabiliana na fujo
zozote ambazo zingaliweza kutokea.
“Siyo
kweli kwamba magari haya yamekuja kwa ajili ya uchaguzi, lakini ninakuomba IGP
(Ernest) Mangu usiogope maneno ya watu kwani kusema ni kawaida yao. Jambo la
kushukuru ni kwamba, kampeni za mwaka huu kila mgombea amekuwa akipanda
jukwaani na kutoa ahadi zao kwa amani na usalama, hii yote ni kutokana na kazi
nzuri ya Jeshi la Polisi,” alisema Rais Mstaafu Kikwete.
Akaongeza:
"Endeleeni kufanya kazi kwa weledi katika kipindi hiki cha kuelekea
uchaguzi mkuu, nafurahi kumaliza muda wangu madarakani huku nikiwa nimetimiza
ahadi ya kuwapatia magari Jeshi la Polisi ili kuongeza ufanisi wenu.”
Naibu
Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki, akimshukuru Rais Kikwete kwa
kuungana nao, alisema: "Vifaa hivi tulivovipata tutahakikisha tunatumia
kwa uangalifu na utaratibu uliopo ili vilete tija kwa sababu tunatambua kwamba
ni kodi za watanzania zimetumika kupata magari haya na vifaa vingine.”
Naye
IGP Mangu aliongeza wakati huo kwamba, magari mengine 378 yaliyokuwa yamesalia
yalitarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwaka 2015 huku akimshukuru JK kwa kutimiza
ahadi ya kuwapatia magari ambayo
yatawawezesha katika kufanya kazi kisasa.
Wachunguzi
wa masuala ya siasa na uchumi wanaeleza kwamba, uamuzi wa serikali kuliwezesha
Jeshi la Polisi kiutendaji ni mzuri hasa kutokana na kukabiliwa na uhaba wa
vitendea kazi, lakini wanahoji ni kwa vipi magari hayo yaliletwa wakati wa
uchaguzi.
“Hizi
ni fedha za walipa kodi maskini wa Tanzania, ingekuwa na kipindi kingine
tungesema sawa wanaliwezesha jeshi, lakini kitendo cha kununua magari mengi
kiasi hicho kilikuwa ni kama kuwatisha wananchi hasa katika kipindi ambacho
kila Mtanzania alitaka kuona mabadiliko ya kweli ya uongozi kutokana na wimbi
la kashfa za ufisadi, rushwa pamoja na matumizi mabaya ya madaraka,” anasema
Jovin Mwakyambiki, mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Kilichotokea
Baada
ya Ashok Leyland kushinda zabuni hiyo mwaka 2013, mkataba ulisainiwa Septemba
5, 2013 kati ya Ashok Leyland Limited na Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuleta
magari hayo kwa Jeshi la Polisi.
Magari
hayo ya aina tofauti yalinunuliwa kwa kati ya Shs. 150 milioni na Shs. 400
milioni.
Nyaraka
mbalimbali ambazo gazeti hili limeziona zinaonyesha kwamba, hadi Oktoba 20,
2015 wakati Rais (mstaafu) Kikwete anakabidhi magari hayo – Toyota Land
Cruiser, Leyland Vans na magari ya washawasha – kwa Jeshi la Polisi yalikuwa
hayajalipiwa hata senti moja, ambapo malipo ya asilimia 35 (Dola za Marekani
10,362,135) yalilipwa Machi 2016 baada ya Katibu Mkuu wa Hazina kumwagiza
Meneja Mkuu wa Benki ya Exim India.
Sehemu
ya nakala ya barua ya idhini kumruhusu Meneja Mkuu wa Exim India kuilipa
kampuni ya Ashok Leyland inasomeka hivi:
“Buyer Credit of USD
29,606,100 Under Buyer Credit Agreement dated 19th June 2015 Signed
between Ministry of Finance and Exim Bank of India for Contract Valued at USD
29,606,100 Between Ashok Leyland India (SELLER) and Ministry of Home Affairs (BUYER).
We wish to inform you
that Seller has presented us its claim for Advance Payment duly authorized by
the Buyer for an amount of US$ 10,362,135 (US Dollars Ten Million Three Hundred
Sixty Two and One Hundred Thirty Five Only), in respect of 35% advance payment
under the contract.
We hereby irrevocably
authorize Exim Bank of India to make payment of the said amount of US$
10,362,135 (US Dollars Ten Million Three Hundred Sixty Two and One Hundred
Thirty Five Only) being 35% of the contract value to the designated account of
the Seller to Exim Bank. We agree that the amount so paid by Exim Bank to the
Seller shall deem as an Advance Payment made by Exim Bank to us out of the
Credit and date on which Exim bank shall remit the amount from Mumbai shall be deemed
date of such advance,
We request Exim Bank to
advice us the date and the amount of the advance payment soon after the Exim
Bank makes the payment aforesaid.”
Idhini
ya malipo hayo ilifanywa kufuatia barua kadhaa za ufuatiliaji kutoka Ashok
Leyland India iliyoshinda zabuni hiyo Namba ME/014/PF/2012/2013/G/40, ambapo
barua ya kwanza ilisainiwa Februari 3, 2016 na Nivedh Shetty, Meneja wa
Operesheni za Kimataifa ikimtaka Katibu Mkuu Hazina kuwatumia taarifa mara
malipo ya awali yatakapokuwa yamefanyika.
Baada
ya ukimya wa barua ya kwanza, kampuni hiyo iliandika tena barua nyingine Machi
7, 2016 iliyosainiwa na Nivedh Shetty pia kukumbushia malipo hayo hayo na ndipo
baadaye Hazina wakaamua kuidhinisha.
0656-331974
Comments
Post a Comment