- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
“NIMEKUWA nasema
nchi yetu si maskini. Hii nchi ni tajiri sana, lakini wapo watu wamekuwa
wanajinufaisha wao. Wapo tayari wapokee virushwa ili waneemeke wao huku Watanzania
wengi wakiumia na kuteseka. Ndio maana nasisitiza kwamba nitaendelea kutumbua
majipu ya viongozi mafisadi na wala rushwa.''
Hii ni
kauli ya Rais John Pombe Magufuli alipokuwa akisisitiza umuhimu wa uamuzi wake
wa kutumbua majipu kwa kuwawajibisha watendaji wa umma ambao ama wametumia vyeo
vyao kuhujumu mali na rasilimali za umma kwa faida yao au wamezembea kutimiza
wajibu wao huku rasilimali hizo zikiishia kwa wajanja wachache.
Taarifa ya
mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaeleza kwamba, katika kipindi cha miezi tisa
tu cha Mwaka wa Fedha 2017/2018, kati ya Julai 2017 hadi Machi 2018, mamlaka
hiyo imekusanya kiasi cha Shs. 11.78 trilioni likiwa ni ongezeko la wastani wa
asilimia 8.46.
Mapato
hayo ni makubwa ikilinganishwa na kiasi cha Shs. 10.86 trilioni kilichokusanywa
katika kipindi kama hicho kwa Mwaka wa Fedha 2006/2017.
Mapato
haya yanatokana na kodi ambapo kwa mwezi Machi 2018 pekee serikali imekusanya
kiasi cha Shs. 1.54 trilioni ikilinganishwa na Shs. 1.34 trilioni
zilizokusanywa kwa mwezi Machi 2017, ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia
14.49.
Ukuaji wa
mapato hayo ya kodi unadhihirisha wazi kwamba, kuna juhudi kubwa zinazofanywa
na serikali katika kuhakikisha mapato yanakusanywa na fedha za umma hazipotelei
kwenye mifuko ya wajanja wachache kama ilivyokuwa zamani.
Tunaelezwa
kwamba, kwa muda mrefu serikali ilikuwa inapoteza fedha nyingi kutokana na
ukwepaji wa kodi uliokuwa ukifanywa na wafanyabiashara wakubwa pamoja na
misamaha ya kodi ambayo haikuzingatia maslahi ya taifa.
Leo hii
tunaposhuhudia kuongezeka kwa mapato haya hatuna budi kuamini kwamba kumbe
tunao uwezo wa kujisimamia wenyewe na kwa hakika kama makusanyo haya yanapanda
hivi, hatuna sababu ya kuendelea kujiita Tanzania ni taifa maskini kama
tulivyokuwa tukiaminishwa.
Tunazo
rasilimali nyingi ambazo zikisimamiwa vyema zinaweza kutuingizia mapato makubwa
na kuondokana na utegemezi unaotufanya tuwe watumwa wa misaada na madeni
yanayotokana na mikopo, mingi kati ya hiyo ikiwa imeingiwa bila kuzingatia
vipaumbele na kusababisha Deni la taifa lizidi kupaa.
Suala la
rasilimali nyingi za taifa – kuanzia kwenye maliasili kama wanyama hadi madini
– kuchotwa na wachache limekuwa likipigiwa kelele kwa miaka mingi sasa, ambapo
Watanzania wamekuwa wakishuhudia nchi ikibaki na mahandaki huku rasilimali
zikichotwa na kuondoka.
Kwamba
kuna baadhi ya wawekezaji wanahujumu rasilimali hizo kwa kuwapatia rushwa
baadhi ya watendaji wa umma, huku wengine wakihodhi vitalu vingi vya madini bila
kuviendeleza na baadaye kuvikodisha wenyewe bila serikali kupata kodi ni mambo
ambayo yanadhihirisha namna Tanzania ilivyokuwa imegeuzwa ‘shamba la bibi’
lisilo na mwangalizi.
Kugunduliwa
kwa gesi yenye ukubwa wa ujazo wa futi trilioni 2.17 katika Bonde la Mto Ruvu mwaka
2015 kunadhihirisha kuwa Tanzania inao utajiri mkubwa wa rasilimali ya gesi
asilia.
Katika
ugunduzi huo uliofanywa na Kampuni ya Dodsal Hydrocarbons and Power Tanzania
Limited ambayo imekuwa inafanya shughuli za utafutaji wa gesi na mafuta katika
Mkoa wa Pwani umezidi kuleta matumaini makubwa kwamba, miaka 10 kuanzia sasa,
Tanzania haitakuwa kwenye kundi la nchi maskini, bali zenye uchumi wa kati
kutokana na mapato ya gesi asilia yatakayoanza kuvunwa.
Ugunduzi
huo unafanya hadi sasa Tanzania kuwa na amana ya gesi yenye ukubwa wa futi za
ujazo trilioni 57.27.
Licha ya
ugunduzi huo tayari gesi imegundulika katika maeneo ya kisiwa cha Songo Songo
mkoani Lindi na eneo la Mnazi Bay huko Mtwara na katika Wilaya ya Mkuranga,
Pwani pia kumegundulika kiasi kikubwa cha gesi.
Mtendaji
Mkuu wa kampuni ya Dodsal Hydrocarbons and Power Tanzania Limited,
Pilavullathil Surendran alisema mwaka 2016 katika mkutano wa wawekezaji wa gesi
na mafuta ulioandaliwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
kuwa, thamani ya gesi iliyoko katika eneo hilo inafikia Dola za Marekani
bilioni sita sawa na Shs. 12 trilioni.
Gesi hiyo iligunduliwa
tangu Julai 2015, lakini akaeleza kuwa Serikali imechelewa kutangaza ugunduzi
huo kama inavyoagizwa na Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015 kutokana na shughuli za
uchaguzi.
Sheria
mpya inasema kabla ya waziri mwenye dhamana ya gesi kutangaza ugunduzi mpya wa
gesi na mafuta ni lazima athibitishiwe na Mamlaka ya Udhibiti wa bidhaa za
Petroli na Gesi (PURA).
Kwa gesi
iliyogunduliwa tu Bonde la Mto Ruvu inaweza kuzalisha kiasi cha Shs. 30 trilioni
baada ya kutoa gharama za uendeshaji ikiwa tutachukulia bei ya gesi asilia kwa
viwango vya Desemba 2015, ambapo serikali yenyewe inaweza kupata mpaka Shs. 7
trilioni kwa mgawanyo wa asilimia 30.
Kwa mujibu
wa bei za mwaka 2015, nchini Marekani gesi asilia ilikuwa inauzwa takriban Dola
za Marekani 10 kwa kila futi za ujazo 1,000 ambao ni wastani wa Dola 0.01 kwa
kila futi moja ya ujazo.
Rasilimali
hizo ni muhimu kwa kukuza uchumi kwa sababu siyo mapato pekee ya mauzo ya gesi
yanayoangaliwa, bali hata fursa zinazotokana na uchimbwaji wa gesi hiyo kwa
wakazi wa maeneo inakochimbwa na hata Watanzania kwa ujumla.
Maeneo
inakochimbwa gesi yatabadilika kimaendeleo kwa kutoa fursa ya kuanzishwa
viwanda baada ya kujengwa kwa miundombinu, lakini pia wananchi wanaweza kutumia
fursa hiyo kwa kuwekeza biashara mbalimbali.
Mbali ya
kutoa ajira kwa wazawa, bado wananchi wanaweza kuongeza uzalishaji wa tija kwa
mazao ya chakula kwa sababu wafanyakazi kwenye maeneo hayo watahitaji chakula
na mambo mengine kadha wa kadha.
Shughuli
mbalimbali za ujasiriamali zikiwemo ufugaji pamoja na ufundi, zitapata msukumo
mkubwa, hivyo kuonyesha ni kwa namna gani rasilimali hizo zinapotumiwa kwa
usawa zinaweza kuleta tija kwa Watanzania wote.
Uchimbaji
wa gesi katika maeneo ya Mnazi Bay mkoani Mtwara na Songo Songo mkoani Lindi
tayari umekwishaleta matunda chanya kwa sababu mbali ya gesi hiyo kutumika
katika viwanda na hata majumbani, lakini wananchi wananufaika kwa kupata
nishati ya umeme unaozalishwa katikia mtambo wa Mdimba mkoani Mtwara ambao
unatumika kwenye mikoa hiyo miwili.
Zaidi ya
hayo, halmashauri ya Kilwa imekuwa ikipatiwa gawiwo la faida ya mauzo ya gesi
hiyo ambayo ni 0.03%, ambapo inapokea wastani wa Shs. 100 milioni kila baada ya
miezi mitatu.
Haya ni
mapato makubwa kwa halmashauri ambayo yanasaidia kuhudumia miradi mbalimbali ya
maendeleo ya jamii, licha ya kwamba wawekezaji nao wanatakiwa kuchangia kwa
hiari, kwa mujibu wa sharia ya uwekezaji, miradi ya maendeleo.
Ikiwa
usimamizi kwenye sekta hiyo utaimarishwa, hakika Tanzania itanufaika kwa mapato
mengi ya kiuchumi huku Watanzania nao wakifaidika kwa fursa mbalimbali za
maendeleo.
0656-331974
Comments
Post a Comment