- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Hii ni Reli ya Kusini iliyokuwa inakwenda Nachingwea ambapo treni la kwanza liliwasili Nachingwea Oktoba 25, 1949. Ujenzi wa Reli ya Mtwara utasaidia kuchochea huduma mbalimbali za kijamii, maendeleo na uchumi.
Na Daniel Mbega
UJENZI wa Reli ya Mtwara-Ameilia Bay katika Ziwa Nyasa pamoja na
tawi lake la kwenda Liganga-Mchuchuma itakayokuwa na urefu wa jumla ya kilometa
997, inasubiri tathmini ya fedha kabla ya kuanza kwa ujenzi wake.
Uchunguzi wa gazeti hili umeonyesha kwamba, kazi ya upembuzi
yakinifu ilikwishafanywa kitambo, lakini serikali haiwezi kutangaza zabuni za
ujenzi mpaka ipate gharama halisi za ujenzi huo.
“Upembuzi yakinifu tayari ulikwishafanyika, kinachosubiriwa tu ni
gharama halisi za ujenzi ili zabuni ziweze kutangazwa, kwa sababu huwezi
kupanga bajeti mpaka ujue gharama halisi,” alisema Catherine Moshi, Meneja
Uhusiano wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli nchini (RAHCO) wakati
alipozungumza na mwandishi wa makala haya mwishoni mwa mwaka 2017.
Reli hiyo, ambayo awali ilikuwa itoke Bandari ya Mtwara na kuishia
katika Bandari ya Mbamba Bay, sasa itaishia katika Ghuba ya Ameilia (Ameilia
Bay) baada ya njia kuhamishwa kutokana na kukwepa gharama kufuatia uwepo wa
milima mingi ya Livingstone katika wilaya za Mbinga na Nyasa mkoani Rukwa.
Ramani kuonyesha Reli itakakopita.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, eneo hilo la Ameilia Bay lipo
kilometa chache kutoka Mbamba Bay, lakini itailazimu Serikali kupitia Mamlaka
ya Bandari kuipanua bandari ya Ameilia Bay ili kuwa na uwezo mkubwa wa meli
kutia nanga pamoja na kupokea mizigo.
Kulingana na uchunguzi huo, baada ya kufanyika kwa upembuzi
yakinifu, ilionekana kwamba gharama za ujenzi hadi Mbamba Bay zingekuwa kubwa
zaidi kuliko kwenda Ameilia Bay.
Catherine Moshi alikiri mabadiliko hayo na kusema kwamba ni madogo
na yenye tija zaidi.
“Washauri waelekezi, baada ya kupokea ripoti ya upembuzi yakinifu,
walisema kujenga reli hadi Mbamba Bay kungegharimu fedha nyingi kwani
ingelazimu kupasua milima, lakini wakasema, ikiwa reli hiyo itaizunguka milima
hiyo hadi Ameilia Bay gharama yake itakuwa nafuu kidogo,” alisema bila kutaja
gharama zilizoelezwa.
Reli hiyo inaelezwa kwamba itakuwa na urefu wa jumla ya kilometa
997 ambazo zinahusisha njia kuu (main
line) pamoja na michepuko (spurs).
Moshi alisema kwamba, kipande cha reli kutoka Ameilia Bay-Songea
kitakuwa na jumla ya kilometa 293 ambazo zinahusisha kilometa 164 za njia kuu
na zilizobaki ni za michepuko.
Aidha, Songea-Tunduru kutakuwa na jumla ya kilometa 316
zinazohusisha kilometa 211 za njia kuu na 129km za michepuko, wakati kipande
cha Tunduru-Masasi kitakuwa na jumla ya kilometa 180 za njia kuu pekee.
“Kipande cha Masasi-Mtwara nacho kitakuwa na urefu wa kilometa 208
pekee,” alisema Moshi.
Umuhimu wa Reli ya Kusini ni mkubwa kwani maeneo ya kusini mbali
ya kuwa na utajiri wa mafuta na gesi, lakini pia kuna hazina kubwa ya madini
iliyoko Mchuchuma na Liganga wilayani Ludewa.
Mgodi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma unakadiriwa kuwa na hazina ya
tani 540 milioni wakati hazina ya chuma cha pua iliyopo Liganga inakadiriwa
kuwa tani 45 milioni, ambapo miradi yote pacha imepewa kampuni ya Sichuan
Hongda Corporation ya China.
Ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay unakuja takriban
miaka 45 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Reli ya TAZARA (maarufu kama Reli ya
Uhuru) yenye urefu wa 1,860km, mradi uliogharimu kiasi cha Dola za Marekani 500
milioni ambazo zilikuwa mkopo kutoka Serikali ya China, ikiunganisha miji ya
Dar es Salaam nchini Tanzania na New Kapri Mposhi, Zambia.
Uchunguzi umebaini kwamba, ujenzi wa reli hiyo utafungua fursa za
maendeleo katika Korido ya Maendeleo Mtwara (MDC) inayohusisha mikoa nane
ambayo ina idadi ya watu 9,432,285 (karibu 21.6% ya Watanzania wote), na pia
kukuza mtandao wa biashara kati ya Tanzania na nchi za Malawi, Msumbiji na
Zambia kwa kupunguza gharama za usafirishaji na kuboresha uchumi kwa bidhaa za
ndani na nje.
Malawi kwa kiasi kikubwa inategemea njia mbili za reli
zinazoiunganisha na bandari katika Bahari ya Hindi – Reli ya Trans-Zambezia
yenye urefu wa 269km ikitokea kwenye ukingo wa kusini wa Mto Zambezi hadi
kwenye reli kuu ya kutoka Beira kwenda Zambia, na reli ya kwenda bandari ya
Nacala nchini Msumbiji, hivyo endapo reli ya Mtwara-Mbamba Bay itajengwa
inaweza kuisaidia Malawi kwa kiasi kikubwa.
Madini, mafuta na gesi Kusini
Uchimbaji wa Urani katika eneo la Mto Mkuju wilayani Namtumbo ndani ya Mbuga ya Selous.
Haya ni makaa ya mawe katika eneo la Ngaka wilayani Mbinga
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia makaa ya mawe katika eneo la Ngaka yanayochimbwa na kampuni ya Tancoal.
Rasilimali za madini, mafuta na gesi katika Korido ya Maendeleo ya
Mtwara, ni nyingi kwa sasa na kwa mujibu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini
Tanzania (TMAA), korido hiyo ina hazina kubwa ya madini huku kampuni nyingi za
kigeni zikiwa zimeingia mikataba mbalimbali ya uchimbaji na utafiti.
Katika Pori la Akiba la Selous ambalo ni Urithi wa Dunia, tayari
uchimbaji wa urani kwenye Mto Mkuju wilayani Namtumbo umekwishaanza tangu mwaka
2013 chini ya kampuni ya Uranium One inayomilikiwa na kampuni ya Atomredmetzoloto (ARMZ)
iliyo chini ya Rosatom State Atomic Energy Corporation inayomilikiwa na
serikali ya Russia.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Uranium One iliyofanya utafiti katika eneo
hilo, Chris Sattler, alikaririwa Juni 21, 2011 akisema kiwango cha uzalishaji
wa urani kinaweza kuwa kati ya tani 1,900 na 2,700 kwa mwaka, lakini kwa
wastani unaweza kuzalisha tani 1,600 za urani ya manjano (yellow cake) kwa
gharama ya Shs. 34,545 kwa paundi moja, hivyo kuifanya Tanzania nchi ya tatu
kwa uzalishaji wa urani barani Afrika.
Wakati akizindua ofisi mpya za Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC)
jijini Arusha Mei 7, 2010, Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema Tanzania ilikuwa
inaingia katika orodha ya nchi zinazozalisha kwa wingi urani duniani.
"Kama akiba yote tuliyonayo itatumiwa vizuri, Tanzania
itakuwa nchi ya saba duniani kwa uzalishaji wa urani," alisema Kikwete.
Kwa ujumla, Tanzania ina akiba ya tani 20,769 za urani ghafi.
Takwimu kutoka NDC zinaeleza kwamba kuna maeneo yenye makaa ya
mawe Mbamba Bay kwenye ukingo wa Ziwa Nyasa ambayo yana hazina ya tani 29
milioni ingawa iliyothibitishwa ni tani 2.4 milioni ambazo zinaweza kuchimbwa
na wachimbaji wadogo na kuzalisha tani 75,000 za ujazo kwa mwaka, hivyo kuzalisha
Shs. 4.2 bilioni kwa mwaka.
Takwimu hizo zinathibitisha kuwepo kwa mradi wa makaa ya mawe
Namwele-Nkomolo wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa wenye tani 1.5 milioni
zilizothibitishwa na hazina ya tani 17.2 milioni ambazo zinaweza kuzalisha Shs.
19.8 bilioni kwa mwaka.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, utafiti huo ulifanywa na kampuni ya Edenville
Energy ambayo pia ndiyo iliyofanya utafiti katika maeneo ya Muze mkoani Rukwa.
Aidha, machimbo ya makaa yam awe ya Ngaka wilayani Mbinga
yanatajwa kuwa na akiba iliyothibitika ya tani 97.7 milioni na tani 200 milioni
za akiba huku yakitajwa kwamba yanaweza kuliingizia taifa kiasi cha Shs. 5.3
bilioni kwa mwaka.
“Mradi wa makaa ya mawe wa Muze ambao unaweza kuzalisha umeme
kwenye ukingo wa Ziwa Rukwa una akiba ya tani 3.41 milioni na hazina ya tani
56.59 milioni ambazo zinaweza kuzalisha 300MW za umeme. Pato la mwaka
linakadiriwa kufikia Shs. 188.4 bilioni,” takwimu hizo zinaonyesha.
Kuongezeka kwa Pato
la Taifa
Watafiti mbalimbali wanasea, endapo serikali itajenga kilometa
hizo za reli na kuboresha huduma katika Reli ya Uhuru (Reli ya Tazara) yenye
urefu wa 1,860km kutoka Dar es Salaam hadi New Kapri Mposhi kule Zambia, pato
la taifa linaweza kuongezeka kwa usafirishaji wa abiria na mizigo pamoja na
kuchochea maendeleo kwa wananchi wa Korido ya Maendeleo ya Mtwara na maeneo
mengineyo.
Enoch Ugulumu, mkuu wa Idara ya Mipango na Uchumi katika Chuo
Kikuu cha Iringa, anasema miradi hiyo haiwezi kufanikiwa bila kuwepo kwa
miundombinu bora, reli ikiwa mojawapo.
“Reli hiyo itasaidia eneo lote la kusini mwa Tanzania kwa sababu
uzalishaji utakapoanza italazimu kusafirisha mali... Kuna uwanja mpya wa ndege
wa Mbeya, lakini mbali ya barabara zinazoendelea kujengwa, tunahitaji reli ya
uhakika,” anasema.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, marehemu Said Mwambungu, aliwahi
kusema kwamba mafanikio ya uwekezaji wa Wachina kwenye migodi ya Liganga na
Mchuchuma yatachangia ongezeko la ajira mpya kwa wazawa na pia kuongeza pato la
taifa na maslahi zaidi ya kijamii kwa wananchi wa Korido ya Mtwara.
“Reli hii na uwekezaji huu ni muhimu kwa maendeleo ya korido hii,
tunakaribisha uwekezaji wowote unaokuja kwenye eneo letu na kwa upande wangu
naona Wachina wamefanya jambo jema sana,” alisema Mwambungu katika mahojiano na
gazeti hili enzi ya uhai wake.
Taarifa za uchunguzi
Uchunguzi unaonyesha kwamba, ujenzi wa reli hiyo ulikuwa uanze
tangu mwaka 2015, kwani tayari upembuzi yakinifu ulikuwa umekamilika na wakati
huo mradi huo ulikuwa katika hatua ya ubunifu wa ujenzi chini ya Mshauri
Mwelekezi kampuni ya Dong Myeong Engineering Consultant ya Korea Kusini.
Wakati huo ilielezwa kwamba, ujenzi wa reli hiyo ungegharimu Dola
za Marekani 3.6 bilioni (takriban Shs. 7.2 trilioni) na taarifa zilisema
ulitarajiwa kujengwa na kampuni ya China Railway No. 2 Engineering Group
(CREGC) ambayo ni kampuni tanzu ya China Railway Group Limited.
Mwaka 2013 aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Injinia Bernhard
Tito, alikaririwa na vyombo vya habari akisema zabuni zilikuwa zimetangazwa kwa
wawekezaji wenye sifa kujitokeza kuwekeza kwenye mradi huo kupitia uhandisi,
manunuzi, ujenzi na masuala ya fedha, zabuni ambazo zilifunguliwa Juni 21,
2013.
"Kampuni 12 ziliomba zabuni lakini sisi tumeteua kampuni sita
kuzishindanisha," alisema Tito bila kufafanua kuhusu kampuni hizo na
mahali zinakotoka.
Upembuzi yakinifu wa mradi huo ulipangwa kugharimu TShs. 8
bilioni, na kwa mujibu wa tangazo la zabuni, ulipangwa kukamilika katika mwaka
wa fedha 2013/2014 kabla ya kutathmini umuhimu wa kiuchumi na taratibu nyingine
za utekelezaji wa mradi huo.
0656-331974
Comments
Post a Comment