Featured Post

KIGWANGALA ATUMIA NGORONGORO MARATHON KUWATUMIA SALAMU MAJANGILI

PICHANI: Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala (fulana nyekundu) akiwa na uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) pamoja na baadhi ya washiriki wa mbio za Ngorongoro Marathon zilizofanyika leo Aprili 21, 2018. Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA Profesa Abiud Kaswamila (namba 002), Mhifadhi Mkuu wa NCAA Dkt. Fred Manongi (namba 003) na Meneja Mahusiano wa NCAA Joyce Mgaya (kulia waliosimama). (Picha na Yusuph Mussa Immamatukio Blog).

Na Yusuph Mussa, Karatu
Immamatukio Blog

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala ametuma salamu kwa majangilli wanaojihusisha na uwindaji haramu wa wanyama kwenye Hifadhi za Taifa ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).


Amesema Serikali na wadau wengine wamejipanga kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa kwa kudhibiti ujangili wa wanyama na viumbe hai vyote vinavyotokana na maliasili yetu ya asili kwenye hifadhi za Taifa.

Dkt. Kigwangala alituma salamu hizo kupitia Mbio za Ngorongoro Marathon zilizofanyika leo Aprili 21, 2018 kwa kuanzia Lango Kuu la kuingilia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuishia Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu mkoani Arusha.

Pamoja na kuwa mgeni rasmi kwenye mbio hizo, Dkt. Kigwangala pia alikimbia kilomita 21 kuanzia saa 3.30 asubuhi na kumaliza saa 6.20 mchana, na kusema hiyo ni ishara tosha ya kujipanga na kukabiliana na majangili. Dkt. Kigwangala alisema kwa kumaliza mbio hizo, sio tu anawatishia majangili kuwa yupo vizuri kukabiliana nao, bali anataka askari wote wa wanyama pole wawe wakakamavu na asimuone askari yeyote mwenye kitambi.

"Moja ya malengo ya mbio za Ngorongoro Marathon kwa mwaka huu ni kupambana na ujangili na majangili. Na sikumaliza mbio hizi za kilomita 21 kwa bahati mbaya, bali ni kuwadhihirishia majangili na watu wote wenye nia mbaya na rasilimali zetu kuwa nipo fiti.

"Lakini sio kwa majangili, hata kwa askari wetu, nataka kuwaeleza kuwa kuanzia sasa sitaki kuona askari anakuwa na kitambi. Hatuwezi kupambana na majangili kama askari wetu wana vitambi na wapo legelege... Na nataka kuwaeleza askari kama wanataka twende nao pamoja kwenye hili basi wajipange" alisema Kigwangala.

Dkt. Kigwangala alisema nia nyingine ya NCAA kudhamini mbio hizo ni kutangaza shughuli za utalii ndani na nje ya nchi, kwani anaamini kupitia waandishi wa habari na washiriki wa mashindano hayo kutokea ndani na nje ya nchi, itawezesha kuongeza watalii na hifadhi hiyo kujulikana zaidi.

Naye Rais wa Chama cha Riadha nchini (RT) Anthony Mtaka, alisema moja ya mambo yanayotushinda nchini ni kujitangaza, lakini hapo hapo kushindwa kupenda vya kwetu, kwani pamoja na kuwa Mlima Kilimanjaro upo Tanzania, lakini matangazo yake mengi yapo Kenya.

Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu alisema amefurahishwa na uongozi wa NCAA kudhamini mashindano hayo, kwani yatawezesha Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kufahamika duniani kote.

"Kwenye Serikali ukiwa na mtu kama Dkt. Fred Manongi (Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro) mambo yatakwenda vizuri. Tumempa taarifa wiki mbili kabla ya mashindano kumuomba atudhamini, lakini akawa amekubali na mambo yamekwenda vizuri.

"Hiki cha kukubali kudhamini mashindano haya ni kikubwa sana. Sasa anatufanya Watanzania tuanze kujitangaza na kupenda vya kwetu. Hili tatizo la kushindwa kujitangaza ni kubwa ndiyo maana kila siku kuna malalamiko kuwa Kenya wanajitangaza Mlima Kilimanjaro ni wa kwao. Sisi sasa tujitoe na kuonesha rasilimali hizi za utalii ni za kwetu" alisema Mtaka.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala akionesha medali yake kwa waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mbio za Ngorongoro Marathon (kilomita 21). Alimaliza mbio hizo saa 6.20 mchana. Mbio hizo zilizoanza leo Aprili 21, 2018 saa 3.30 asubuhi kwenye lango kuu la kuingia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), zimehitimishwa kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu. NCAA ndiyo wadhamini wakuu wa mbio hizo. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala akihutubia wananchi wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha mara baada ya kumalizika mbio za Ngorongoro Marathon leo Aprili 21, 2018 na kuhitimishwa kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu. Wa pili kulia ni Rais wa Chama cha Riadha (RT) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA Profesa Abiud Kaswamila. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Fred Manongi (kulia), Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Jubilate Mnyenye (kushoto) na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha Cecilia Pareso (katikati) wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala (hayupo pichani) kwenye kilele cha mbio za Ngorongoro Marathon zilizohitimishwa kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu leo Aprili 21, 2018. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).

Comments