Featured Post

KATIKA MAHAFALI YA 24 YA KIDATO CHA SITA SHULE YA SEKONDARI YA JITEGEMEE JKT MGULANI WAZAZI WAAMBIWA URITHI WA WATOTO WAO NI ELIMU

 Katibu Tawala wa Wilaya ya Temeke, Hashim Komba (katikati), akihutubia kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo,  Felix Lyaviva ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 24 ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Jitegemee Mgulani JKT yaliyofanyika leo hii jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Shule hiyo, Kanali Robert Kessy na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi wa Shule hiyo, Brigedia Generali mstaafu Laurance Magere.

 Mwenyekiti wa Bodi wa Shule hiyo, Brigedia Generali mstaafu Laurance Magere akihutubia. Kushoto ni Mkurugenzi wa Elimu, Utamaduni na Michezo wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Makao Makuu Luteni Kanali Meidimi.
 Mkuu wa Shule hiyo, Kanali Robert Kessy , akihutubia.
 Makamu Mkuu wa Shule, Kapteni Benitho Lubida akiwakaribisha wageni waalikwa.
 Wahitimu wakipiga makofi.
 Wahitimu wakiwa kwenye mahafali hayo.



 Baadhi ya walimu wa shule hiyo.
 Burudani zikitolewa.
Wasoma risala wakisalimia meza kuu.

Na Dotto Mwaibale

IMEELEZWA kwamba elimu ndio urithi pekee utakao wafaa watoto wetu katika ndoto za maisha yao.

Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Temeke, Hashim Komba kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo,  Felix Lyaviva ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati akihutubia katika mahafali ya 24 ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Jitegemee Mgulani JKT yaliyofanyika leo hii jijini Dar es Salaam.

"Napenda kuwaeleza wazazi kuwa urithi pekee wa watoto wetu hawa ni elimu na si vinginevyo kwani elimu ndio kila kitu na kwenye elimu hakuna kisichowezekana' alisema Komba.

Komba alisema elimu ndio njia pekee isiyoweza kumdanganya mtu na kama mtu aliteseka wakati akiitafuta akimaliza kuitafuta na kuipata elimu hiyo itamuhudumia mtu huyo.

Katika hatua nyingine Komba aliwataka wanafunzi hao kutojiingiza katika vitendo vichafu kupitia matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii badala yake watumie mitandao hiyo kwa manufaa hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu inaingia kwenye uchumi wa viwanda kama Rais wetu Dk.John Magufuli anavyohimiza.

"Vijana wengi wamejikuta wakiharibikiwa maisha yao kwa kujiingiza katika vitendo viovu kama kuvuta bangi, kupata ukimwi na vingine vingi kutokana na matumizi mabaya ya tehama" alisema Komba.

Mkuu wa shule hiyo Kanali Robert Kessy akizungumza katika mahafali hayo alisema wahitimu wote 551 wameandaliwa vizuri na wanauhakika watafanya vizuri katika mtihani wao wanaotarajia kufanya hivi karibuni.

"Ndugu mgeni rasmi wahitimu hawa unaowaona tumewanoa vizuri na kipimo kizuri ni kushika nafasi ya sita baada ya kufanya mitihani mitatu mikubwa ya kujipima hivyo hatuna wasiwasi nao kabisa" alisema Kessy.

Mwenyekiti wa Bodi wa Shule hiyo, Brigedia Generali mstaafu Laurance Magere aliwapongeza wanafunzi hao kwa kufikia hatua hiyo pamoja na kuwa na moyo wa fadhila kwa wadau wa maendeleo walioisaidia shule hiyo kwenye maeneo tofauti ikiwemo ya kukarabati majengo.

Wakisoma risala yao kwa mgeni rasmi wanafunzi hao walisema kwamba karibu changamoto nyingi zilizokuwepo zimetatuliwa isipo kuwa ni ile ya uchakavu wa sakafu ambapo inawalazimu kutumia muda mrefu wa kufanya usafi mda ambao wangeweza kuhutumia kuwa darasani.

Komba katika mahafali hayo ametoa ahadi ya kuwalipia ada wanafunzi wawili ambao wanadaiwa ambapo mkuu wa wilaya hiyo,  Felix Lyaviva  ametoa mifuko 2000 ya saruji pamoja na shilingi milioni 1.5 ili kusaidia kukabiliana na changamoto zilizopo shuleni hapo.

Comments