- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Daraja la Mto Kilombero
Na Daniel Mbega
KWA
ujumla, huhitaji hata dakika tano ili kuweza kusoma na kuzielewa akili za
wapinzani - wa kisiasa na maendeleo - nchini Tanzania.
Huu ni
ukweli ulio dhahiri kwamba, dakika moja tu inatosha kabisa kuwatambua akili zao
zikoje, kwa sababu wanachokihubiri ni tofauti na wanachokiamini ama kukifanya.
Wapinzani
wa maendeleo nchini Tanzania wako hivi, watapinga serikali kushindwa
kuwawajibisha wazembe, lakini serikali hiyo hiyo inapobadilika na kuamua
kuwashughulikia wazembe, wala rushwa na mafisadi, wapinzani hao hao wataanza
tena kupiga kelele na kupinga.
Haitoshi
tu, wapinzani hao hao kuna wakati waliwahi kuomba Tanzania ipate kiongozi
ambaye hatawaonea aibu mafisadi na ambaye atakuwa na mtazamo wa kuinua uchumi
wa nchi ikiwemo kuboresha huduma mbalimbali za jamii.
Lakini
baada tu ya Dkt. John Magufuli kuingia madarakani na kuanza kutekeleza Ilani ya
Chama cha Mapinduzi (CCM) ikiwemo kupambana na mafisadi, wala rushwa, wakwepa
kodi na watumishi wazembe, wapinzani wakaanza kupiga kelele kwamba eti ni
dikteta.
Wakati
Rais Magufuli anapoendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo, bado
wapinzani wanabeza na kutoa hoja ambazo hazina kichwa wala miguu.
Kwa muda
mrefu Tanzania ilikuwa haina ndege, hata ya kukodi, na kwa bahati mbaya Shirika
la Ndege (ATCL) lilikuwa linaingizia serikali hasara kubwa huku likiwa na
wafanyakazi zaidi ya 300.
Wapinzani
walipiga kelele, wakajitahidi kukosoa, jambo ambalo lilikuwa sahihi na
liliungwa mkono na Watanzani wengi kwa kuwa kodi za wananchi zilikuwa
zikitumbuliwa na watu ambao walikuwa hawaingizi chochote.
Rais
Magufuli, baada ya kutekeleza hatua ya serikali kuhami Dodoma ambayo ilipigwa
danadana kwa miaka 45 iliyopita, hatimaye aliamua kwa dhati kabisa kulifufua
shirika hilo la ATCL na kuhakikisha serikali inanunua ndege mpya, siyo mtumba
wala siyo za kukodi, tena kwa fedha taslimu.
Wengi
walipongeza hatua hiyo, lakini upinzani ukaanza wakati alipoamua kununua ndege
aina ya Bombardier na siyo aina nyingine.
Rais
Magufuli hakujali, akanunua ndege mbili ambazo zimekuwa zikifanya safari nchini
na kupunguza adha ya usafiri katika sekta ya anga.
Haikutosha,
akaahidi kwamba ndege nyingine ingewasili wakati wowote kabla ya mwezi Mei na
nyingine mbili zitawasili Juni mwaka huu wa 2018 zikiwa ni sehemu ya ndege sita
ambazo Serikali ya Magufuli iliahidi kuzinunua kwa fedha taslimu.
Jumatatu,
Aprili 2, 2018 hatimaye ndege ya tatu baada ya zile mbili za kwanza ya
Bombardier Dash 8 Q400 iliwasili nchini na kuzinduliwa na Rais Magufuli,
uzinduzi ambao ulishuhudiwa kila kona ya nchini na sehemu nyingine duniani kwa
kuwa ulionyeshwa mubashara.
Kabla ya
ujio wa ndege hiyo, wapinzani hao wakitumia mitandao ya kijamii walishinda na
kukesha mitandao kupinga na kukejeli ujio wa ndege hiyo, huku wengine wakifikia
hatua ya kusema kwamba, hata awali hazikununuliwa ndege mbili, bali yalikuwa ni
'mapanga boi mawili tu'!
Wapinzani
wengi wa maendeleo walisema hakukuwa na haja ya kununua ndege hiyo kwa sababu
haina maana yoyote kwa wananchi walio wengi, kwa kuwa hawatazitumia.
Wakadai
kwamba, vipaumbele vya serikali vilitakiwa kulenga kwenye afya, elimu na
kilimo, lakini wakasahau kwamba katika sekta hizo tayari serikali
imekwishafanya mambo makubwa kwa kukamilisha miradi mingi ya maendeleo kuliko
wapinzani wanavyosema.
Hizi ni
akili za wapinzani wa kisiasa na maendeleo wa Tanzania, na ndiyo maana nikasema
haihitaji utumie muda mwingi kuzijua akili zao.
Leo
wapinzani wale wale waliokuwa wakikosoa Tanzania kukosa ndege zake, wanathubutu
kusema hakuna haja kwa serikali kununua ndege! Hivi kweli hizi ni akili au
nini?
Basi na
tuseme hivi, ndege hazitufai, basi hata meli nazo hazitufai maana si wananchi
wengi wanaotumia usafiri wa majini!
Na tuseme
kwamba hata magari hayatufai kwa kuwa hatuna uwezo wa kuyanunua, badala yake
pengine turudi kule kule kwenye ukoloni tuanze kutembea kwa miguu.
Na kama
ndivyo, basi hata hatuna haja ya kujenga barabara, reli na madaraja,
miundombinu ambayo inagharimu fedha nyingi za umma.
Kwa akili
mbovu za wapinzani wa maendeleo, itafika mahali kwamba hata nguo spehseli
hazitufai kwa kuwa hatuna fedha za kununulia, badala yake tuvae mitumba, enzi
zile tukiziita 'Kafa Ulaya, mazishi Bongo'!
Tunaweza
kusema kwamba hata mchele wa kutoka nje hatuna haja nao kwa sababu tunalima
mpunga sisi wenyewe - hata kama mchele hautoshelezi mahitaji.
Si hivyo
tu, tunaweza kufika mahali - kwa kutumia akili za wapinzani wa maendeleo -
tukasema hata dawa hazitufai, kwa sababu tunao waganga wengi wa kienyeji!
Hizi
jitihada za Serikali chini ya Rais Magufuli katika kujenga na kuboresha
miundombinu zinapingwa sana na wapinzani, ambao dhahiri wanataka kukwamisha
maendeleo.
Wapo ambao
wanathubutu kusema kwamba, hata wakoloni walijenga reli na barabara, lakini
bado wazee wetu waliwakataa na kutaka kujitawala!
Wanasema:
"Hata wakoloni walijenga reli, mashule, mabarabara, na kadhalika, lakini
bado tuliwakataa na tukadai uhuru."
Ni akili
fupi na za kijinga kabisa, kwa sababu hawaelewi kwamba wakoloni walipojenga
barabara na reli walilenga kusafirisha malighafi na rasilimali zetu ili
kuzipeleka kwao Ulaya kushibisha viwanda vyao.
Barabara
na reli tunazojenga zinatusaidia sisi wenyewe kujipatia maendeleo.
Watu
wanapinga ununuzi wa ndege, treni ya kisasa, ujenzi wa barabara za juu
(flyovers) na kadhalika na wanasema eti vitu hivyo haviwezi kuwa mbadala wa
utu, haki na uhuru wa mwanadamu.
Wanaongeza
kwamba eti hizi ndege ni mzigo tu kwa mlipa kodi maskini wa nchi hii maana hawajui
hata hii ndege imekombolewa kwa gharama kiasi gani huku shirika lenyewe likiripotiwa
kuendeshwa kwa hasara.
Wanapewa
dhahabu wanatupa na kuokota mawe, siyo wapewe nini jamani!
Tazama
kule Libya yaliyowakuta, walipewa kila kitu wakasema Gaddafi amewanyima uhuru.
Sasa wanatamani hata unga wa njano hawaupati!
Niseme
ukweli tu kwamba, kuna watu wanaumia sana maana kuona maendeleo haya, na
hawafahamu kuwa katika mapinduzi ya viwanda (industrial revolution) kuna kitu kinachoitwa trinity boom, ambayo kimsingi imeegemea zaidi kwenye miundombinu,
jambo ambalo ndilo linalofanywa na Rais Magufuli, ikiwa ni awamu ya pili katika
mapinduzi hayo ya viwanda na awamu ya pili hufanywa na sekta binafsi hususan
katika ujenzi wa viwanda.
Inawezekana
hawa wapinzani wa maendeleo wana malengo yao ya siri, kwa sababu haya
yasipofanyika, na kama tutawasikiliza na kufuata akili zao, basi wataanza tena
kukosoa kwamba hiki na kile hakikufanyika.
Tuseme tu
ukweli, kwamba Tanzania ya sasa haihitaji mawazo ya kupinga maendeleo kama ya
watu wenye akili kama hizi, kwa sababu hao hawaitakii mema nchi yetu.
Tumechelewa
sana kuboresha mambo mengi kwa sababu ya sias zisizokwisha, sasa tunahitaji
kuchapa kazi na kuwapuuza wenye mawazo ya kuturudisha nyuma.
Anayepinga
maendeleo huyo hayuko upande wetu, tumwepuke kama ukoma!
0656-331974
Comments
Post a Comment