Featured Post

CHADEMA YAANZA 'KUMLILIA' MAGUFULI


Calist Lazaro Bukhai, Meya wa Jiji la Arusha

* Meya amwandikia meseji Rais

Na Mwandishi Wetu, Arusha
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza 'kumlilia' Rais John Magufuli huku kikionekana kufurahishwa na utendaji wake.
Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro Bukhai maarufu kama 'Bush', amekuwa kiongozi wa Chadema ambaye ameonyesha kukubali utendaji  kazi wa Rais John Pombe Magufuli kiasi cha kufikia hatua ya kumwandikia ujumbe mfupi wa maneno (sms)  kumwalika afike  nyumbani kwake.

Rais Magufuli akizungumza na wananchi wa Jiji la Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini humo mwishoni mwa wiki, baada ya kuzindua nyumba za askari jijini humo alieleza kufurahishwa na mtazamo wa meya huyo aliyemwita kuwa ni mzalendo na mpenda maendeleo.
"Tanzania ni moja, tusichanganye na vyama, na ndiyo maana hata Meya aliniandikia sms kunikaribisha kwake, nikamwambia nikienda watakufukuza.
"Huyu Meya anapenda maendeleo na mimi napenda sana watu wanaopenda maendeleo," alisema Dkt. Magufuli na kuibua kelele za shangwe  na vifijo kutoka kwa wananchi waliofika uwanjani hapo kushudia maonyesho ya kazi zinazofanywa na polisi.
Rais Magufuli alisema pamoja na kupokea ujumbe huo wa simu, lakini kila mara amekuwa akimuahidi kwamba atafika kwake, huku akimtaka atulie ili ujio wake usije 'ukamharibia' kwa chama chake.
"Maendeleo hayana itikadi ya siasa wala dini, lazima tuweke kando itikadi zetu kwa sababu maendeleo haya ni ya Watanzania wote," alisema Dkt. Magufuli.
Lazaro, ambaye ni Diwani wa Kata ya Sokoni katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, alikuwepo uwanjani hapo na kutambulishwa na Rais Magufuli.
Aidha, Lazaro ambaye ni Mwenyekiti wa Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri zinazoongozwa na Chedema na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa na Mjumbe wa Baraza la Uongozi la Mkoa, mwaka 2017 alijiuzulu nafasi yake ya ukatibu wa chama mkoa ili kupunguza majukumu.
Jitihada zinazofanywa na Serikali chini ya awamu ya tano chini ya Rais  Dkt. Magufuli ndizo zinazoonekana kuwakuna wananchi wengi  wakiwamo wapinzani kama Meya Lazaro ambaye alikuwepo uwanjani hapo huku kukiwa hata mbunge mmoja wa Chadema wa Mkoa wa Arusha.
Itakumbukwa kwamba, tangu Januari 2017 viongozi wa Chadema pamoja na madiwani na wabunge kadhaa wa upinzani waliamua kujivua nyadhifa zao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Katika kipindi hicho, Chadema ilipoteza madiwani takribani 21, ambapo 15 kati yao ni wale waliojiuzulu na kujiunga na CCM.
Madiwani 15 kati ya waliojiuzulu walitokea mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, ambako ni ngome kuu ya chama hicho.
Baadhi ya madiwani waliohama kutoka mkoani Arusha na kata zao zikiwa kwenye mabano ni Prosper Msofe (Daraja Mbili), Obeid Meng'oriki (Terrat), Elirehema Nnko (Olsunyai), Credo Kifukwe (Muriet), Greyson Ngowi (Kimandolu) na Solomon Laizer (Ngabobo).
Akihutubia mamia ya wananchi walioshiriki uwanja hapoa, Rais Magufuli alisema kamwe hataweza kugawa ng'ombe kwa wananchi wa Longido kama alivyoombwa na Mbunge wa Jimbo hilo, Dkt. Steven Kirushwa, katika hadhara hiyo.
Awali Dkt. Kirushwa alisema kwamba, kwa kuwa wananchi hao waliahidiwa na serikali  kupatiwa ng'ombe kama fidia kutokana na ukame uliowakumba miaka mitatu iliyopita, anamuomba Mheshimiwa Rais aangalie uwezekano wa kuwapatia ng'ombe hao.
Mbunge huyo alisema kwamba ahadi hiyo ilitolewa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, ili kuwaokoa na janga la ukame lililosababisha vifo vya ng'ombe  hao.
"Mimi sigawi ng'ombe, najua JK watu waligawiwa ng'ombe, lakini mimi sigawi, huu ndio msimamo wangu na huyu ndiye Magufuli.
"Kama leo nikigawa ng'ombe kwa wafugaji wa Longido, kesho korosho zikikauka tutawafidia pia wakulima, na pamba ikikauka itabidi tugawe pamba kwa wakulima, jamani lazima tuwe wakweli, hatuwezi kwenda kwa utaratibu huo," alisema.
Akaongeza: "Mimi sikuahidi kugawa ng'ombe, hivyo mambo ya kugawa ng'ombe hayapo tena."
Alihoji kwamba, ikiwa wananchi hao wanakwenda kuuza ng'ombe wao katika mnada huko Kenya, iweje sasa waombe tena kupewa ng'ombe wengine.
"Hao ng'ombe mnaokwenda kuwauza Kenya mnao, sasa mnataka kupewa ng'ombe wengine wa nini? Kwanza malisho sasa yapo ya kutosha kwa sababu mvua inanyesha," alisema.


Comments