Featured Post

WAFUGAJI WAITAKA SERIKALI KUWAMULIKA MAOFISA WANAOJINUFAISHA NA MIFUGO YA WANANCHI

Baadhi ya wafugaji wakimsikiliza kwa makini Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati wa kikao cha pamoja akizungumza na wafugaji Jimboni kwake Bukombe, Leo 4 Machi 2018.

Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akiwaeleza bwafugaji namna serikali ilivyo jipanga kwa ajili ya kutenga maeneo ya malisho wakati akizungumza na wafugaji Jimboni kwake Bukombe, Leo 4 Machi 2018.

Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akisisitiza jambo wakati akizungumza na wafugaji wa Jimbo la bukombe walioshiriki kwenye kikao cha kujadili namna ya kuwa na ufugaji wenye tija katika jamii, Leo 4 Machi 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog

Na Mathias Canal, Geita

Baadhi ya wafugaji wamemlilia Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko kwa kumtaka kuwafikishia kilio chao kwa Waziri wa Wizara ya maliasili na Utalii Mhe. Dkt Khamis Kigwangala juu ya kuwafichua baadhi ya maofisa wa serikali wanaojinufaisha na mifugo ya wananchi hifadhini.

Manufaa ya maofisa hao na askari wa wanyamapori yanajili kipindi wanapowakamata Ng'ombe wa wafugaji wanaoingia katika maeneo ya hifadhi ya Taifa ambapo huwakamata na kuwapiga mnada kwa bei yakutupa tofauti na thamani ya wanyama hao.

Wananchi hao wametoa malalamiko hayo leo 4 Machi 2018 mbele ya Mbunge huyo wakati wa kikao na wafugaji wa Jimbo hilo la Bukombe kilichofanyika katika eneo la shule ya msingi Shibingo katika kata ya Yogelo ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara ya Mbunge huyo katika Jimbo hilo la uchaguzi tangu ateuliwe kuwa Naibu Waziri wa Madini.

Akizungumza katika kikao hicho Mbunge Biteko alisema kuwa wananchi wanapaswa kutoa taarifa Mara kwa Mara kwa uongozi wa vijiji ili kuwabaini maofisa hao wanaofanya kazi kinyume na matakwa ya taratibu na sheria.

Aidha, alisema kuwa wananchi wanapaswa kutambua kuwa kumekuwa na athari nyingi katika jamii kutokana na kukamatwa Ng'ombe wengi kwa ukiukaji wa taratibu kwa kuwaingiza kuchunga katika maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya hifadhi.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha muda mrefu wananchi walijisahau na kupeleka mifugo yao katika maeneo yasiyoruhusiwa kwa ufugaji hivyo kutokana na usimamizi hafifu wa sheria wananchi wakadhani kuwa wapo sahihi kwa kila wafanyalo kumbe sivyo.

Mhe Biteko alisema hakuna kilichobadilika badala yake kumekuwa na usimamizi madhubuti wa sheria katika kila sekta jambo ambalo linawaumiza kwa kiasi kikubwa wananchi kwani hawakutegemea jambo hilo katika kipindi hiki.

Akijibu kuhusu serikali kuwatengea maeneo ya malisho wafugaji hao Mhe Biteko alisema kuwa tangu serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli iingie madarakani imekuwa na kazi kubwa ya kuondoa mifugo holela kutoka nchi jirani jambo ambalo limeifanya serikali kushindwa kutenga maeneo hayo ya malisho.

Sambamba na hayo aliongeza kuwa wakati Tanzania inapata Uhuru 1961 kulikuwa na Ng'ombe wasiozidi milioni 10 lakini kwa hivi Sasa kumekuwa na Ng'ombe zaidi ya elfu 40 hivyo serikali inatumia busara kubwa kutenga maeneo kwani kumekuwa na wingi wa mifugo lakini maeneo hayajaongezeka bado ni yale yale.

Alisema serikali imedhamiria kwa kauli moja kuwatoa wananchi katika ufugaji holela usiokuwa na tija na kuhamia katika ufugaji wenye tija ili kuwa na faida ya ufugaji huo kwa wananchi wenyewe.

Katika hatua nyingine Mhe Biteko alisisitiza kuwa wakati serikali inaendelea na utaratibu wa manufaa kwa wakulima kwa kuwatengea maeneo kwa ajili ya malisho, wakulima hao wanapaswa kuwa wavumilivu sambamba na kushirikiana na serikali katika zoezi la upigaji chapa mifugo.

Comments