Featured Post

SERIKALI YAAGIZA OPERESHENI YA KUONDOA WAVAMIZI WA KIGENI KATIKA KISIWA CHA IZINGA MKOANI KAGERA


.........................................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ametoa siku 7 kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA  kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Karagwe kufanya Operesheni ya kuwaondoa wavamizi wa nchi jirani wanaodaiwa kulima na kufiga ndani kisiwa cha Izinga kilichopo ndani ya Pori la Akiba la Kimisi mkoani Kagera.
Ametoa agizo hilo jana wakati wa ziara yake wilayani Karagwe mkoa wa Kagera muda mfupi baada ya kupokea taarifa na malalamiko ya kukamatwa kwa mifugo ya Watanzania ndani ya kisiwa cha Mubali huku kukiwepo mazao yanayodaiwa kulimwa na wananchi wa Rwanda katika kisiwa kingine cha Izinga.

“Ndani ya siku saba hicho kisiwa cha Zinga msafishe kila kitu, Mkuu wa Wilaya msaidie mtengeneze kikosi kiende kule kitoe takataka zote zilizoko kule, inakua ngumu kuadministrate (kutawala) wengine wa kwetu tunawatoa alafu wa nchi nyingine wamekaa, unatawalaje?”. Aliuliza kwa mshangao Dk. Kigwangalla.

Alisema watanzania wakienda upande wa Rwanda kuvua samaki ziwa Ihema wanauawa mara moja bila mjadala, wakati kwa upande wa Tanzani raia wa nchi hiyo wapo wengi na wengine wamepewa Uraia wa Kuasili (Citizenship by Naturalisation, CN) na huwa hawafanyiwi vitendo vya unyanyasaji wala mauaji  jambo ambalo alisema  ipo haja kama nchi kuchukua hatua ili kukomesha vitendo hivyo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, David Kenyata alisema atatekeleza agizo hilo la Waziri Kigwangalla kwa haraka ndani ya muda uliotolewa ili kumaliza mgogoro huo.

Katika hatua nyingine Waziri Kigwangalla alikataa ombi la Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashugwa la kuiomba Serikali iwamegee wananchi wa vijiji jirani sehemu ya eneo katika Pori la Akiba Kimisi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.

“Ardhi mimi sitatoa, sjui mlima sjui nini, siwezi kwenda kupeleka hilo ombi kwa Mhe. Rais, kabisa, hicho ni kitu ambacho hatuwezi kufanya kwa sasa’,” Alisisitiza Dk. Kigwangalla.

Mbunge huyo pia aliiomba Serikali kuweka uzio wa waya kwa ajili ya kutenganisha mpaka wa hifadhi hiyo na vijiji kwa madai ya kuepuka ukamataji wa mifugo ya wananchi unaofanywa na askari wa wanyamapori kwenye ardhi za vijiji na kuingizwa hifadhini na kutozwa faini, hoja iliyopigwa vikali na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Godfrey Mheluka.

Hata hivyo, Dk. Kigwangalla alikataa ombi hilo na kusema kuwa mipaka ya hifadhi hiyo ni mikubwa kuwezesha utekelezaji wa ombi hilo. Alisema Serikali itatengeneza mtandao wa barabara zinazounganisha hifadhi hiyo na vijiji kwa ajili ya kuimarisha doria na shughuli za utalii pamoja na kujenga ofisi ndogo za pori hilo katika kila wilaya inayohusika na pori hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Godfrey Mheluka aliwataka wananchi wanaofanya vitendo vya kuingiza mifugo kwenye pori hilo wakati wa usiku kuacha mara moja kwa kuwa wakimatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Alisema malalamiko ya wananchi hao kuwa askari wa wanyamapori wanakamata mifugo yao kwenye maeneo ya vijiji na kuiingiza hifadhini kwa lengo la kuwatoza faini kuwa sio ya kweli na kwamba malalamiko yanakuja kwakuwa hukamatwa asubuhi wakiwa wameshatoka kulisha mifugo hifadhini.

Kisiwa hicho cha Izinga ambacho kipo katika wilaya ya Karagwe mkoani Kagera kina ukubwa wa Kilomita za Mraba 12 na kinapakana na nchi Rwanda.
Pori la Akiba Kimisi liliqnzishwa mwaka 2003 kwa Tangazo la Serikali na 116 na lina ukubwa wa kilomita za mraba 1,030. Pori hilo lina wanyamapori mbalimbali wakiwemo Tembo, Twiga, Simba na Chui. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozana na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashugwa kukagua Pori la Akiba Kimisi wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera jana. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na baadhi ya viongozi wa kijiji cha Mwisheni alipofika kukagua Pori la Akiba Kimisi wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya hiyo mkoani Kagera jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozana na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashugwa kukagua Pori la Akiba Kimisi wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera jana. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Godfrey Mheluka wakati akikagua Pori la Akiba Kimisi akiwa kwenye ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya hiyo mkoani Kagera jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akionyesha mpaka wa Pori la Akiba Kimisi wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya hiyo mkoani Kagera jana. Kulia ni Mkuu wa Karagwe, Godfrey Mheluka na Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa (kulia kwake).
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Lut. Col. Michael Mutenjele (kushoto) wakati wakivuka kivuko cha Ruvuvu wakati wa ziara yake ya kutembelea na kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya hiyo mkoani Kagera jana. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia baadhi ya mifugo iliyokamatwa ndani ya Pori la Akiba Kimisi wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya Ngara mkoani Kagera jana. (Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii).

Comments