Featured Post

SEED TRUST YAPOKEA VITABU1000 VYA MALENGO YA DUNIA KWA WASIOONA


Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Alvaro Rodriguez (katikati) akimkabidhi Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Mambo na Sheria, Mh. Amon Anastazi Mpanju (wa pili kushoto) sehemu ya nakala 1,000 za vitabu vya taarifa za Malengo ya Dunia kwa wasioona katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia tukio hilo ni Mwenyekiti wa Bodi ya SEED Trust Tanzania, Mh. Stephen Mashishanga (wa pili kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa SEED Trust Tanzania, Mh. Margaret Mkanga (kushoto) na Meneja Programu wa SEED Trust Tanzania, Peter Mwita (kulia).

Umoja wa Mataifa umetoa nakala 1,000 za vitabu vya taarifa za Malengo ya Dunia vilivyochapishwa kwa herufi nundu (braille)(hizi ni herufi zilizovimbishwa na ambazo watu wasioona au wenye uoni hafifu husoma kwa kugusa na kidole) kwa taasisi ya Seed Trust Tanzania katika jitihada za kuwafikia wasioona. 
 Kuna takribani watu milioni 39 wasioona na wenye uoni hafifu kote duniani leo; miongoni mwao takribani milioni 5.8 wako Afrika. 
Nchini Tanzania, kuna taarifa kwamba takribani asilimia 1.2 ya watu wenye ulemavu huu walitoa taarifa kwamba wana matatizo ya kuona. 
Msaada huu kwa shirika la Seed Trust, ambalo ni asasi inayojishughulisha na uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi wa watu wenye ulemavu nchini Tanzania, ni juhudi za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa za kutomwacha mtu yeyote nyuma katika utekelezaji wa Malengo ya Dunia kama wito unavyotolewa kupitia Agenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030. 
Vitabu hivyo vya taarifa vilikabidhiwa leo na Mratibu Mkazi wa UN, Bw. Alvaro Rodriguez, kwa shirika la Uwezeshaji wa Kijamii na Kiuchumi Tanzania (SEED Trust Tanzania). 
Msaada huu unaendelea kujenga uelewa kuhusu Malengo ya Dunia ulianzia na semina iliyoandaliwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu mwaka janana Bw. Rodriguez na Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, kwa kushirikiana na Seed Trust Tanzania. 
Ushirika huu kati ya UN na Seed Trust unalenga kuwajengea uwezo wenye ulemavu kujumuishwa katika jitihada za kufikia Malengo ya Dunia nchini Tanzania.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Alvaro Rodriguez akizungumzia kuhusu Umoja wa Mataifa kuwafikia watu wenye ulemavu katika kuhakikisha taarifa za Malengo ya Dunia zinawafikia watu wote wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam.
Akibabidhi vitabu hivyo vya taarifa, Bw. Rodriguez alizungumzia umuhimu wa msaada huo: “Bila kujali kama ni mitandao ya kijamii au ni matini yaliyochapwa, kujenga uelewa tulioufanya kuhusu Malengo ya Dunia kunahusisha kusoma,” alisema. 
“Kutoa msaada wa vitabu hivi vya taarifa vilivyochapwa kwa herufi nundu ni hatua ya kwanza kuhakikisha kwamba watu wenye matatizo ya uoni wanaweza kuchangia katika kufikiwa kwa Malengo ya Dunia kwa sababu vitawasaidia kuyaelewa malengo hayo.”
Akisisitiza umuhimu wa kuwajumuisha wenye ulemavu katika shughuli za maendeleo, Bi. Margaret Mkanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Seed Trust Tanzania na Mbunge wa zamani wa Viti Maalumu akiwakilisha wenye ulemavu alisema: “Malengo ya Maendeleo Endelevu ni ajenda ya dunia itakayodumu hadi mwaka 2030.
"Malengo haya ni zaidi ya ajenda ya kawaida, shabaha zake na viashiria vinatoa fursa ya kufanya marejeo katika ngazi tofauti katika ratiba ya utekelezaji wake. Ushiriki wa watu wenye ulemavu ni muhimu katika kufanikiwa kwa ajenda hii. 
"Vitabu hivi vya taarifa tunavyovipokea leo ni hatua nyingine kuelekea katika ushirikishwaji wa watu wenye matatizo ya kuona katika ajenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu.”
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Mambo na Sheria, Mh. Amon Anastazi Mpanju, akitoa salamu za serikali na kupongeza juhudi za Umoja wa Mataifa kuwafikia wenye ulemavu kwa kutoa nakala 1,000 za vitabu vya taarifa za Malengo ya Dunia kwa wasioona katika hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Umoja wa Mataifa, Masaki jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo ya makabidhiano iliyofanyika katika ofisi za UN ilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Mambo ya Sheria, Mh. Amon Anastazi Mpanju.
Akizungumzia juhudi za UN kuwafikia wenye ulemavu, Mh. Amon alisema: “Lengo la 4 la Malengo ya Dunia linahusu elimu bora iliyo jumuishi na usawa wenye haki na kuhamasisha upatikanaji wa fursa za kujifunza za kudumu kwa wote. 
"Lengo la 10 linahusu kuhakikisha kupungua kwa tofauti ndani na kati ya nchi nanchi. Lengo la 17linahusu kuimarisha njia za utekelezaji na kuhuisha ushirika duniani ili kufikia Maendeleo Endelevu. 
"Shabaha hizi kwa namna ya pekee zinataja ulemavu kama kitu kitakachosaidia kuhakikisha ushirikishwaji na ushiriki wa watu wenye ulemavu katika utekelezaji, usimamizi na tathmini ya Malengo ya Maendeleo Endelevu. 
"Ujumuishwaji kwa hakika utahakikisha kwamba hakuna yeyote anayeachwa nyuma."
Kujumuishwa kwa watu wenye ulemavu kunatoa fursa kwao kushiriki na kutoa dukuduku zao pia.
Mwenyekiti wa Bodi ya SEED Trust Tanzania, Mh. Stephen Mashishanga akizungumza jambo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya nakala 1,000 za vitabu vya taarifa za Malengo ya Dunia kwa wasioona iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Umoja wa Mataifa, Masaki jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu pia aliongeza, “Serikali ya Tanzania imejizatiti kuunga mkono utekelezaji wa Malengo ya Dunia katika ngazi zote. Vitabu hivi vya taarifa vitasaidia sana watu wenye matatizo ya uoni nchini Tanzania katika kupata taarifa zinazohusu malengo ya dunia na vitawasaidia nao kutoa mchango wao katika utekelezaji wake.”

Comments