Featured Post

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AHAMISHIA OPERESHENI YA KUWABAINI WAAJIRI WANAOKIUKA SHERIA ZA KAZI MKOANI MOROGORO

 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Antony Mavunde, akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha Tumbaku Alliance One Mkoani Morogopro leo Machi 9, 2018. Mhe. Mavunde ameagiza waajiri 242 Mkoani Morogoro ambao hawajajisajili na Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF) kufikishwa mahakamani mara moja.

NA K-VIS BLOG, Morogoro
OPERESHENI ya nchi nzima kuwabaini waajiri ambao hawatekelezi sheria ya ajira na mahusiano kazini na wale ambao bado hawajajisajili na Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF), inayoongozwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde, imeingia Mkoani Morogoro leo Machi 9, 2018, ambapo waajiri wamechukuliwa hatua mbalimbali za kisheria ikiwa ni pamoja na kutozwa faini.
Operesheni hiyo iliyoanzia jijini Mwanza Februari 26, 2018 inafuatia agizo alilolitoa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, jijini Mbeya mwishoni mwa mwaka jana ambapo aliagiza waajiri ambao bado hawajatekeleza Sheria ya Fidia Kwa Wafanyakazi, Sura 263 marejeo ya mwaka 2015, ambayo inamtaka kila mwajiri kutoka sekta ya umma na binafsi Tanzania bara awe amejisajili na kuwasilisha michango kwenye Mfuko huo, wafikishwe mahakamani.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF), Bi. Rehema Kabongo, ambaye anafuatana na Mhe. Mavunde kwenye ziara hiyo ya kushtukiza, kuna jumla ya waajiri 536, na kati ya hao ni waajiri 294 tu ndio waliojisajili na Mfuko huku wengine 242 bado hawajatekeleza takwa la kisheria la kujisajili na Mfuko.
“Naagiza waajiri hawa ambao bado hawajajisajili na Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, wanaofikia 242 wafikishwe mahakamani mara moja ili wakajibu mashtaka kwanini hawajatimiza wajibu wao wa kisheria.” Aliagiza Mhe. Mavunde.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mara baada ya ukaguzi huo wa kushtukiza, mjini Morogoro, Mhe. Mavunde ameiagiza WCF kuwafikisha mahakamani mara moja, waajiri wa kampuni ya Sengo 2000 Tanzania Limited, na Midland Inn Lodge kutojisajili na Mfuko.
Huku kampuni za Hood Transport Company Limited na Alliance One, wao wamekiuka sheria ya kazi na mahusiano kazini.
“Lakini pia naagiza waajiri hawa 242 ambao bado hawajajisajili na Mfuko nao wafikishwe mahakamani mara moja ili wakajibu mashtaka kwanini hawajatimiza wajibu wao wa kisheria.” Aliagiza Mhe. Mavunde.
Mhe. Mavunde pia ameagiza waajiri hao kufanya mawasiliano na watendaji wa Mfuko haraka iwezekanavyo ili kuweza kubaini kiwango cha riba kila mwajiri anachopaswa kulipa kutokana na kuchelewesha michango katika Mfuko.
“Ni kosa la jinai kwa mwajiri kutotekeleza takwa hilo la kisheria na kifungu cha 71(4) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi kimeweka wazi kuwa mwajiri wa aina hii, anaweza kutozwa faini isiyozidi shilingi milioni 50,000, kifungo kisichozidi miaka 5 jela au adhabu zote kwa pamoja, kwa hivyo nitoe wito kwa waajiri hao, hakuna sababu ya kushurutishwa kutekeleza sheria.­­
Aidha Mhe. Mavunde amerejea kauli yake kuwa nia ya serikali sio kuwanyanyasa waajiri au kuwapeleka mahakamani.
“Serikali inataka ninyi waajiri mfanye shughhuli zenu za biashara na uwekezaji na kazi ya kuwahudumia wafanyakazi wenu wanapopatwa na madhara wakati wakitekeleza wajibu wao wa kazi, jukumu hilo lisimamiwe na Serikali kupitia Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF).” Alisisitiza Mhe. Mavunde.
Naibu Waziri pia amebaini kuwa waajiri katika viwanda hivyo hawatekelezi sheria ya ajira na mahusiano kazini ambapo ukiukwaji mkubwa wa sheria hiyo umedhihirika ambapo amewakuta wafanyakazi wakifanya kazi bila ya vifaa vya kujihami, (protective gears), kufanya kazi kwa masaa mengi kupitia kiasi, lakini pia wengi wao hawana mikataba ya kazi.
“Tumebaini kuna mapungufu makubwa sana ya sheria za kazi hasa sheria namba 6 ya mwaka 2004, sheria hii inaelekeza mwajiri azingatie muda wa masaa ya kazi, atoe mikataba kwa wafanyakazi wote,” alisema Mheshimiwa Mavunde.
Aidha Kamishna wa Kazi, Bi.Hilda Kabisa, amesema, Waajiri ni sharti watoe mikataba kwa wafanyakazi inayoonyesha ni muda gani wa kufanya kazi, likizo kwa mfanyakazi, na hata kama mfanyakazi analipwa kwea siku ni sharti mambo hayo yazingatiwe.Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF), Bi. Rehema Kabongo, amesema Mfuko umjiandaa kabisa, na maagizo ya Mheshimiwa Naibu Waziri yatatekelezwa haraka na tayari baadhi ya maeneo hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa dhidi ya waajiri ambao wameshindwa kutekeelza takwa la kisheria.
“Operesheni hii ni endelevu tutahakikisha waajiri wote tunawafikia na nitoe rai tu kwa wale ambao bado hawajajisajili, wasisubiri kupelekewa hati za mashtaka, kwani lengo la Mfuko ni kuwasidia waajiri kuondokana na jukumu la kuwahudumia wafanyakazi wao wanapopatwa na madhara mahala pa kazi kwani jukumu hilo kwa sasa kwa mujibu wa sheria ni la Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi WCF na si mahala pengine popote.” Alifafanua Bi. Rehema.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Antony Mavunde, (kushoto), akizungumza na Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi, kiwanda cha Tumbaku Mkoani Morogoro, Ujaicy Kayera leo Machi 9, 2018 wakati wa ziara yake ya kushtukiza aliyoifanya Mkoani humo ili kubaini waajiri ambao bado hawajajisajili na Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF), na wale ambao hawatekelezi Sheria ya Kazi na Mabhusiano Kazini. Mhe. Mavunde ameagiza waajiri 242 ambao hawajajisajili na Mfuko kufikishwa mahakamani mara moja.
  Naibu Waziri Antoni Mavundeakizungumza na Meneja wa Kampuni ya Hood, Faisal Hood. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF), Bi.Rehema Kabongo

  Naibu Waziri akiwasli kwenye Kiwanda cha kusindika Tumbaku cha Alliance kilichopo Kingolwira, ambapo alizungumza na wafanyakazi na kubaini makosa ya kiutendaji kwa muajili.

  Naibu Waziri akiwasli kwenye Kiwanda cha kusindika Tumbaku cha Alliance kilichopo Kingolwira, ambapo alizungumza na wafanyakazi na kubaini makosa ya kiutendaji kwa muajili.

  Naibu Waziri akiwasli kwenye Kiwanda cha kusindika Tumbaku cha Alliance kilichopo Kingolwira, ambapo alizungumza na wafanyakazi na kubaini makosa ya kiutendaji kwa muajili.

  Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu, Blasius Lupenza akielezea baadhi ya mikataba ya wafanyakazi wake kwa Mhe Naibu Waziri katika Kiwanda cha kusindika Tumbaku cha Alliance kilichopo Kingulwira.


  Naibu Waziri akiangalia Salary slip ya mmoja wa wafanyakazi wa Kiwanda cha Tumbaku.



Comments