Featured Post

MBUNGE CHATANDA ATAKA UKAGUZI TSH. MILIONI 230, UJENZI SHULE YA JOEL BENDERA SEC


Mbunge wa Korogwe Mjini Mary Chatanda (wa tatu kulia) akisikiliza taarifa inayosomwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Joel Bendera Nasson Msemwa (wa pili kushoto). Hapo ndipo Chatanda aliliamsha 'dude' kutaka kujua kwa nini sh. milioni 150 zimeshindwa kukamilisha mabweni mawili.

Yussuph Mussa, Korogwe

IMMAMATUKIO BLOG

Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Mary Chatanda amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Jumanne Shauri kupeleka wakaguzi kwenye Shule ya Sekondari Joel Bendera iliyopo Kijiji cha Kwakombo, Kata ya Kwamsisi.


Ni kutaka kubaini ukweli kuhusu matumizi ya fedha baada ya sh. milioni 150 zilizopelekwa shuleni hapo kumalizika, kabla ya ujenzi wa mabweni mawili kumalizika, huku tena zikihitajika sh. milioni 17 kumalizia ujenzi huo.

Chatanda alibaini hilo baada ya Machi 3, 2018 kufanya ziara kata ya Kwamsisi, na kusomewa taarifa na Mkuu wa Shule hiyo Nasson Msemwa kudai sh. milioni 150 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kujenga mabweni hayo ikiwa ni pamoja na kuweka samani, fedha zake zimekwisha.

"Mheshimiwa Mbunge, Serikali ilituletea sh. milioni 230, ambapo sh. milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana na wavulana na sh. milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya manne. Fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ambapo tupo kwenye hatua za mwisho zimekwisha. Na ili tukamilishe mabweni hayo kunahitajika sh. milioni 17.

"Kwa upande wa ujenzi wa madarasa manne, bado tunakwenda vizuri, kwani pamoja na ujenzi kuwa kwenye hatua za mwisho, bado tuna sh. milioni 28" alisema Msemwa.

Chatanda alisema kwa uzoefu wake, tangu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, na sasa Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhandisi Robert Gabriel, wamekuwa wakijenga namna hiyo kazi inakamilka na fedha inabaki, iweje kwao imekwisha kabla ya kazi kumalizika.

"Sisi tuna uzoefu, kwa pesa hizi mlizoletewa na Serikali, mnapowashirikisha wananchi kuchimba msingi, kuleta mchanga na kokote, huku mkitumia mafundi wa kawaida, fedha hizi zingetosha na kubaki. Hili sikubaliani nalo, na ninamtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kuleta wakaguzi ili kubaini ukweli wa matumizi wa hizi fedha.

"Mnataka tuonekane kazi hii ya kufanya vizuri kujenga madarasa na mabweni na kudhibiti matumizi ilikuwa inafanywa na mtu mmoja Robert Gabriel (sasa Mkuu wa Mkoa wa Geita. Nina hakika Bodi ya Shule haikuwashirikisha wananchi ndiyo maana mabweni hayakuisha, lakini kama hamkushirikisha wananchi na viongozi wa vijiji na kata, ambao ndiyo wenye shule yao, maana yake kuna chembechembe za ubadhirifu" alidai Chatanda.

Diwani wa Kata ya Kwamsisi Nassor Mohamed alisema Bodi ya Shule awali wakati wanaanza ujenzi wa shule hiyo kwa njia ya msalagambo chini ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhandisi Gabriel, walishirikisha watu wote, lakini baada ya Serikali kuingiza sh. milioni 230 kwenye akaunti ya shule, mambo yalibadilika.

"Mwanzo walitushirikisha, lakini fedha zilipoingia Bodi ya Shule ilikuwa inafanya kazi peke yake bila kushirikisha viongozi wa vijiji wala kata, muulize Mkuu wa Shule huyu hapa, alikuwa mbogo pindi ninapomuulizia mambo yanayohusu fedha ama maendeleo ya ujenzi" alisema Mohamed.

Akijibu tuhuma hizo, Msemwa alisema hakuna fedha imeliwa, bali mabweni hayo ni makubwa tofauti na Shule ya Sekondari Mnyuzi, kwani kila moja linachukua wanafunzi 40, lakini yupo tayari kukaguliwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Mji Korogwe Dkt. Elizabeth Nyema, ambaye alikuwa ameambatana na Chatanda kwenye ziara hiyo, alisema amepokea maagizo hayo na watayafanyia kazi.
Madarasa mapya manne ya Shule ya Sekondari Joel Bendera, Kijiji cha Kwakombo, Kata ya Kwamsisi, Halmashauri ya Mji Korogwe. Madarasa hayo ambayo yapo kwenye hatua za mwisho kukamilika, Serikali ilitenga sh. milioni 80 kujenga madarasa hayo. (Picha na Yusuph Mussa).
Moja ya mabweni yaliyopo Shule ya Sekondari Joel Bendera Kijiji cha Kwakombo, Kata ya Kwamsisi, Halmashauri ya Mji Korogwe. Mabweni mawili yaliyojengwa shule hiyo, kila moja litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kwa wakati mmoja.

PICHA ZOTE NA YUSSUPH MUSSA

Comments