Featured Post

MAKAMU WA RAIS KUONGOZA HARAMBEE YA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA YA MUHEZA

 Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi Mwanasha Tumbo (kulia) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu maandalizi ya Harambee ya uchangiaji wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga. Kutoka kushoto ni Katibu wa Kamati ya Harambee hiyo, Hassan Msumari na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hamis Mgoda. 


Na Mwandishi Wetu
MAKAMU  wa Rais, Samia Suluhu Hassan, kuongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari, jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Mwanasha Tumbo alisema kuwa hafla hiyo itakayoanza Kesho Ijumaa saa 12 jioni  kwenye Hoteli ya Golden Tulip ya Masaki, Dar es Salaam itaambatana na chakula cha usiku kwa wageni waalikwa.

Hivi sasa Wilaya hiyo haina Hospitali ya Wilaya na wananchi wanaohitaji huduma za afya wamekuwa wakitumia hospitali teule ya Kanisa la Anglikana ambayo imeingia mkataba na Serikali na kutokana na idadi ya wananchi wa wilayani hapo hospitali hiyo imezidiwa.

Hayo yamesemwa leo na Mhandisi Tumbo wakati akizungumzia harambee ya kuchangisha fedha inayotarajia kufanyika kesho jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufanikisha ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya hiyo.

Mhandisi Tumbo amesema kutokana na Wilaya ya Muheza kutokuwa na Hospitali ya Wilaya tangu kuanzishwa kwake mwaka 1974, wananchi wamekuwa wakiteseka pindi wanapohitaji huduma za afya na hivyo wakaamua kuchanishana fedha ili kuanza ujenzi wa hospitali hiyo.

Amefafanua tayari wananchi na wadau wa maendeleo wilayani Muheza mkoani Tanga na Watanzania kwa ujumla wameanza kuchingiaa ujenzi huo na hadi kukamilika kwake zinahitajika fedha Sh.bilioni 11.1, hivyo wakati wakisubiri fedha za Serikali Kuu na zile za kwenye bajeti wameamua kuanza kwa kuchangisha fedha hizo.

"Kesho tutakuwa na harambee itakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia saa 12 jioni ambapo wananchi wa Wilaya ya Muheza wanaoishi Dar es Salaam pamoja na watanzania wengine tunaomba wajitokeze kuchanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya.

"Mgeni rasmi kwenye tukio hilo la harembee ya kuchangisha fedha atakuwa Makamu wa Rais ,Mama Samia Suluhu Hassan. Kwa wachangiaji ambao tumewapa kadi ya kuja kwenye harembee hiyo kila mchangiaji atachangia kuanzia Sh.milioni moja kwa walio na kadi.Na wote ambao tumewaalika kesho wana kadi za mualiko,"amsema.

Amefafanua kwa wale ambao wanahitaji kadi ni vema wakawasiliana naye kwa kutumia namba yake ya simu ya mkononi ya 0713 341937 ili wapatiwe kadi huku akifafanua pia mbali ya wale ambao watafika kesho kwenye harambee hiyo pia wameandaaa utaratibu mwingine wa kuchangia ujenzi huo.

Mhandisi Tumbo amesema ili kufanikisha ujenzi huo wanapokea mchango wa kiasi chochote cha fedha na hao wachangie kupitia Tigopesa au M-pesa kwa kutumia namba 395533 ambayo kumbukumbu namba ya kampuni ni 123.

"Tunatambua jitihada za Serikali katika kutatua changamoto kwenye sekta ya afya, na hasa Muheza lakini kwa upande wetu tumeamua kuanza kwa kuchangishana, wapo wanaotoa fedha, wapo wanaochangia kokote, mchanga , saruji na vifaa vingine vya ujenzi.Tumeanza vizuri kwani tayari msingi wa wadi ya akina mama na watoto umejengwa na lengo letu hadi Oktoba mwaka huu tuwe tumekamilisha ili wananchi wapate huduma za afya.

"Tukifanikiwa kuwa na Hospitali ya Wilaya Muheza mwananchi anayehitaji huduma za matibabu ya afya atakuwa na nafasi ya kuchagua aende kwenye Hospitali ya Anglikana au ya Wilaya.Niishukuru Hospitali ya Anglikana kutokana na kutoa huduma za tiba kwa wananchi wa Muheza,"amesema Mhandisi Tumbo.

Pia amesema wakati wanaendelea kutafuta fedha kujenga Hospitali ya Wilaya ya Muheza, wanaendelea na jitihada za kujenga zahanati na ujenzi huo unaendelea kwa kasi kutokana na wananchi kuhamasika kuchangia ili kuondoa changamoto ya uhaba wa zahanati za vituo vya afya.
 Baadhi ya waandishi wa habari walihudhuria mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya 
Golden Tulip katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Katikati ni Adam Ngamange Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Kijani Kibichi Tanzania (Mkikita), ambaye kwa asilimia kubwa alisaidia kuaandaa mkutano huo.
 Sehemu ya wanahabari hao
 Mkuu wa Wilaya, Tumbo akifafanua jambo ambapo aliwaomba wananhi kujitokeza kutoa michango kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo. Kulia ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Desderia Haule.
 Waandishi wa habari wakiwa kazini wakati wa mkutano huo
 Mkuu wa Wilaya ya Muheza akijibu maswali ya wanahabari
 Wajumbe wa Kamati ya Harambe hiyo wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa mkutano na wanahabari kwenye Hoteli ya Golden Tulip, katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Juma Mgazija,  Mwenyekiti wa Kamati, Hamis Mgoda, Mkuu wa Wilaya, Mhandisi Mwanasha Tumbo, Katibu Tawala wa Wilaya, Desderia Haule na Katibu wa Kamati, Hassan Msumari.

Comments