- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Veronica Kazimoto,
Dar es Salaam,
28 Machi, 2018.
Serikali imeanza maadalizi ya kutengeneza Mfumo wa Pamoja wa Kielektroniki wa Uondoshaji Shehena Bandarini, Viwanja vya Ndege vya Kimataifa na Mipakani kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na ufanisi.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Serikali wanaohusika na udhibiti wa mizigo katika maeneo hayo na wadau mbalimbali wa sekta binafsi, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere amesema lengo la kuwashirikisha wakuu hao ni kujenga uelewa wa pamoja wa utekelezaji wa mfumo huo.
“Uwepo wenu katika mkutano huu ni muhimu sana kwasababu mtaweza kupitia mahitaji yote ya mfumo yaliyoandaliwa na watalaamu wetu ikiwa ni pamoja na maeneo ya kisheria, kiufundi na kibiashara ili muweze kuuboresha zaidi”, alisema Kichere.
Kichere alieleza kuwa, uwepo wa wakuu hao na wadau wa sekta binafsi katika mkutano huo ni kiashiria cha kuunga mkono adhma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga mazingira bora ya kufanya biashara ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Kamishna huyo Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania aliongeza kuwa, Serikali imelenga kuwawezesha wadau wote wanaohusika na biashara za kimataifa na usafirishaji wa mizigo kutumia Mfumo wa Pamoja wa Kielektroniki wa Uondoshaji Shehena kwa lengo la kuwezesha uwasilishaji wa nyaraka mahali pamoja ili wadau wote waweze kushughulikia nyaraka hizo kwa wakati.
Naye Mratibu wa Mfumo wa Uondoshaji Shehena kutoka TRA Felix Tinka amezitaja faida za mfumo huo kuwa ni pamoja na kurahisisha na kuwezesha biashara, kuongeza ufanisi wa matumizi bora ya rasilimali na kuongeza uhiari wa ulipaji ushuru na tozo mbalimbali kwa waingizaji na waondoshaji wa mizigo.
“Mfumo huu una faida nyingi, mbali na hizo nilizozitaja awali, pia kuna kuimarisha usalama, kuimarisha uadilifu na uwazi katika utendaji kazi, kupunguza biashara haramu, kupunguza gharama, kupunguza muda wa uondoshaji mizigo katika vituo vya forodha pamoja na kurahisisha ufuatiliaji wa mizigo kwa wakati”, Alisema Tinka.
Utekelezaji wa Mfumo wa Pamoja wa Kielektroniki wa Uondoshaji Shehena Bandarini, Viwanja vya Ndege vya Kimataifa na Mipakani umegawanyika katika maeneo makuu matano ambayo ni eneo la usimamizi wa mapato, uwezeshaji wa usafiri na uchukuzi, utekelezaji wa sera na biashara, pamoja na usimamizi wa afya na usalama wa umma, usalama wa uchumi pamoja na ugawaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Hamza Johari akitoa mchango wake wakati wa mkutano huo. |
Katibu Mtendaji wa Chama cha Wakala wa Meli Tanzania (TASAA), Abel Urono akitoa mchango wake katika mkutno huo. |
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere (kulia) akibadilishana mawazo na Nibu Kamishna wa TRA, Zanzibar Mcha Hassan baada ya kuhudhuria mkutano huo. |
Mshauri wa Tehama, Abdulrahman Mbamba akitoa mada kwa washiriki wa Mkutano huo. |
Sehemu ya washiriki wa mkutano huo wakifuatilia mijadala kwenye mkutano huo. |
Comments
Post a Comment