Featured Post

NAIBU WAZIRI MADINI ATUA MKOANI SONGWE KWA ZIARA YA KIKAZI

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza mara baada ya kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Songwe kwa ajili ya ziara ya siku mbili ya kikazi katika mkoa wa Songwe, Leo 22 Februari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akisisitiza jambo mbele yaKamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya songwe, na Kamati ya  siasa ya CCM Wilaya hiyo mara baada ya kuwasili Mkoani Songwe kwa ziara ya kikazi, Leo 22 Februari 2018.
Mkuu wa wilaya ya Songwe Mhe Samwel Jeremiah akieleza changamoto za wachimbaji wadogo katika Wilaya hiyo mbele ya Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati akisoma taarifa ya Mkoa wa Songwe kwa niaba ya mkuu wa Mkoa huo Mhe Chiku Galawa, Leo 22 Februari 2018.


Na Mathias Canal, Songwe

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko leo 22 Februari 2018 ameanza ziara ya kikazi katika Mkoa wa Songwe ambapo pamoja na mambo mengine atatembelea na kukagua eneo la mgodi tarajiwa wa Bafex linalotarajiwa kuanza uchimbaji wa Madini ya dhahabu.

Maeneo mengine atakayotembelea ni pamoja na mgodi wa uchimbaji dhahabu wa Shanta Gold Mine uliopo katika kata ya Saza, Wilayani Songwe ambapo atazungumza pia na wafanyakazi wa mgodi huo.

Sambamba na hayo pia Naibu Waziri wa Madini atazungumza na wachimbaji wadogo kwenye mkutano ulioandaliwa Mara baada ya kutembelea maeneo ya uchimbaji.

Mara baada ya kuwasili katika Mkoa wa Songwe Mhe Biteko amesifu juhudi za mbunge wa Jimbo la Songwe Mhe Philiph Mulugo kutokana na uwajibikaji mkubwa katika kuwasemea wananchi wa jimbo hilo hususani katika kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia sekta ya Madini.

Alisema kuwa mbunge huyo amekuwa mstari wa mbele katika kuwatetea wananchi wake katika katika kuchochea shughuli za maendeleo ili kuongeza ufanisi wa maendeleo endelevu ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla wake.

Aidha, Mhe Biteko alimuhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Songwe kuwa Wizara ya Madini Kupitia sheria mpya ya madini kutakua na Tume ya Madini ambayo kimuundo itakua na Afisa madini wa Mkoa wa Songwe ambapo utapelekea kuwa na Ofisi hiyo ya Madini.

Mhe Biteko aliutaka uongozi wa Wilayani na Mkoa wa Songwe kuongeza zaidi ushirikiano na Chama Cha Mapinduzi kwani ndicho Chama chenye dhamana ya kuisimamia na kuikosoa serikali pindi inapoenda mrama.

Alisema kuwa baadhi ya watumishi wanapaswa kutambua kuwa wanatekeleza wajibu wa matakwa ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2015-2020 hivyo haijalishi kuwa wanaipenda ama wanaichukia wanatakiwa kutekeleza ilani pasina kuogofya.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Songwe Mhe Philiph Mulugo alisisitiza kuwa ujio wa Naibu Waziri wa Madini utakuwa chachu ya mwanzo mzuri wa maendeleo ya wananchi kupitia sekta hiyo.

Awali akisoma taarifa ya Mkoa wa Songwe kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe Samwel Jeremiah ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Songwe alizitaja changamoto zinazoukabili Mkoa huo katika sekta ya madini kuwa ni pamoja na kukosekana Ofisi ya Madini ya Mkoa.

Changamoto zingine ni pamoja na ukosefu wa Vifaa pamoja na elimu ndogo juu ya sheria zinazosimamia shughuli za uchimbaji Madini, pamoja na wachimbaji wengi kutokuwa waaminifu katika ulipaji wa maduhuli ya serikali yatokanayo na shughuli za uchimbaji wa Madini.

Naibu Waziri wa Madini atakuwa katika ziara ya kikazi Mkoani Songwe kwa siku mbili kuanzia leo 22 Februari 2018 na kufika ukomo hapo kesho 23 Februari 2018 ambapo ataelekea mkoa wa Rukwa.

Comments