Featured Post

MHE BITEKO AWAHAKIKISHIA WANANCHI WALIOWAHI KUWA WAFANYAKAZI WA MGODI WA KIWIRA KULIPWA STAHIKI ZAO

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wananchi waliowahi kuwa watumishi wa Mgodi wa Kiwira wakati akiwa ziarani Mkoani Songwe na Mbeya kukagua shughuli za uchimbaji wa Madini, Leo 20 Februari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-WazoHuru Blog
Baadhi ya wananchi waliowahi kuwa watumishi wa Mgodi wa Kiwira wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko alipokuwa akizungumza jambo wakati akiwa ziarani Mkoani Songwe na Mbeya kukagua shughuli za uchimbaji wa Madini, Leo 20 Februari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na wananchi waliowahi kuwa watumishi wa Mgodi wa Kiwira wakati akiwa ziarani Mkoani Songwe na Mbeya kukagua shughuli za uchimbaji wa Madini, Leo 20 Februari 2018.

Na Mathias Canal, Songwe

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko amewahakikishia baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe na Wilaya ya Rungwe na Kyela Mkoani Mbeya kuwa serikali inamalizia mchakato wa uhakiki wa madeni yote ya wadai hivyo pindi itakapomaliza mchakato huo wadai wote watalipwa madeni yao.

Naibu Waziri, Mhe Biteko ametoa kauli hiyo leo 20 Februari 2018 akiwa Kijijini Kapeta, Kata ya Ikinga Wakati akizungumza na wananchi waliowahi kuwa watumishi wa Mgodi wa Kiwira waliosimamisha msafara wake wakati akiwa ziarani Mkoani Songwe na Mbeya kukagua shughuli za uchimbaji wa Madini.

Alisema kuwa wananchi hao ndio walioiweka serikali ya awamu ya tano madarakani hivyo serikali haina haiwezi kuwasahau ama kutosimamia haki yao bali wanapaswa kuwa wavumilivu wakati serikali inajiridhisha na madeni hayo kabla ya kuanza kulipa ili kuwa na uhakika na watu wanaostahili malipo hayo.

"Watumishi lazima tukubali kwamba madeni haya tumeyarithi hayakuwa ya serikali bali yalikuwa ya muwekezaji sasa ili serikali iweze kuyalipa ni lazima ijiridhishe isije ikaingia mkenge wa kulipa watu wasiostahili kwani madeni hayo ni makubwa na yanahitaji kujiridhisha" Alisema Mhe Biteko na Kuongeza kuwa

"Sisi serikalini tunalifanyia kazi jambo lenu na tumeshafanya kazi kwa kiasi kikubwa mpaka sasa ya kuona namna ya kuwalipa na ninataka niwahakikishie kuwa kila mwenye haki anayedai lazima atalipwa lakini mtuvumilie tumepita kwenye michakato mingi ya kuibiwa fedha kwa watu kupachika madeni ya watu wasiostahili kulipwa tena wengine walishafariki"

Mhe Biteko aliongeza kuwa serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli inatambua kuwa mgodi wa Kiwira na mradi wa uchimbaji makaa ya mawe wa Kabulo ni miradi ya kimkakati katika Wizara ya Madini hivyo inatambua umuhimu wake na tayari ipo mbioni kuanzisha tena uzalishaji katika mgodi huo ambao uzalishaji wake ulisimama tangu mwaka 2009.

Alisema kuwa wananchi wamesubiri kwa muda mrefu malipo yao lakini tatizo kubwa ilikuwa ni serikali kujiridhisha na kuanisha wanufaika wa madeni hayo hivyo serikali italimaliza jambo hilo na itabaki kuwa historia.

Alisisitiza kuwa katika maeneo mengi kulikuwa na changamoto mbalimbali lakini tayari serikali imezipatia ufumbuzi changamoto hizo na wananchi wanaona utofauti.

Akijibu maswali ya wananchi hao waliotaka kufahamu ni lini mradi huo utaanza uzalishaji, Mhe Biteko alisema kuwa ili mradi uweze kuanza zipo taratibu za kisheria ambazo lazima zifuatwe ili yasijejitokeza matatizo ya kisheria baadae hivyo zitakapomalizika haraka mradi huo utaanza uzalishaji na wananchi watajipatia ajira.

Comments