Featured Post

MFUKO WA FIDIA KWA WFAANYAKAZI, (WCF), WAANZA KUWAFIKISHA MAHAKAMANI WAAJIRI AMBAO HAWAJAJISAJILI NA MFUKO

  Wakurugenzi Watendaji wa Kampuni ya Spash International Co  Ltd   Shafeek  Purayil  (kulia) na Japhet Alexander  wa Kampuni ya Kamanda Security Guard Co. Ltd, wakipelekwa mahabusu ya Mahakama ya kisutu jijini Dar es Salaam leo Februari 19, 2018 baada ya kusomewa mashtaka mawili ya jinai kwa kushindwa kujisajili na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), na kuwasilisha taarifa za shughuli za Makampuni wanayoyaongoza kwa Mfuko huo. Washtakiwa wakipatikana na hatia wanakabiliwa na kifungo kisichopungua miaka mitano (5), jela au faini isiyozidi shilingi milioni hamsini au vyote kwa pamoja.
K-VIS BLOG

MFUKO wa Fidia Kwa Wafanyakazi (WCF), umewafikisha mahakamani waajiri wanne (4) kwa kushindwa kujisajili na Mfuko huo.
Waajiri hao ambao ni Wakurugenzi Watendaji, wamefikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijinin Dar es Salaam, leo Februari 19, 2018 wakikabiliwa na makosa mawili kila mmoja.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka wa Serikali Bw. Emilly Kiria, washtakiwa ni pamoja na Bw.Riziki Silas Shemdoe na Bw. Deusdedit Samwel Kibassa ambaye hakuwepo mahakamani na aliwakilishwa na wakili na wote wanatoka Kampuni ya ENCC CONSULTANTS na wengine ni Wakurugenzi Watendaji wa Kampuni ya SPASH  INTENATIONAL CO. LTD, Malakkara P, Semis na Shafeek M. Purayil. Wengine ni Wakurugenzi Watendaji wa LASAR LOGISTIC, Abshir Farah Gure na Farhiya Hersiwarsame, wakati Mshtakiwa mwingine ni Bw.Josephat Alexander ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya KAMANDA SECURITY GUARDS CO. LTD.
Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, Bi.Victoria Nongwa, Mwendesha Mashtaka wa Serikali Bw. Emily Kiria, alisema waajiri hao wametenda makosa  mawili ambayo ni  kushindwa kujisajili na kuwasilisha taarifa za shughuli wanazozifanya kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, ambapo ni kinyume cha Kifungu  cha 71 (1) (a) na 71 (4) cha Sheria ya Fidia Kwa Wafanyakazi Sura ya 263 marejeo ya mwaka 2015.
Kosa la pili ni kushindwa kutoa taarifa kwa Afisa wa Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi ambapo ni kinyume na Kifungu cha 8 (5) (c), kikisomwa pamoja na Kifungu cha 96 cha Sheria ya Fidia Kwa Wafanyakazi Sura ya 263 marejeo ya mwaka 2015.
Kabla ya Mfuko  kuchukua hatua hii ya kuwafikisha  mahakamani, washtakiwa walipewa taarifa ya kutekeleza takwa hilo la kisheria katika tarehe mbalimbali, kati ya Septemba 2017 hadi Januari 2018 lakini walishindwa kutekeleza.
Washtakiwa hao endapo watapatikana na hatia wanakabiliwa na kifungo kisichozidi miaka 5 jela au faini isiyozidi shilingi milioni 50 au vyote kwa pamoja.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo, Meneja Matekelezo (Compliance Manager),  wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Victor Luvena alisema hatua hii ya kuwapandisha kizimbani waajiri hao ni mwanzo tu na kwamba Mfuko utachukua hatua kama hiyo kwenye mikoa yote Tanzania Bara.
“Ninawaasa waajiri kutoka sekta ya umma na binafsi, Tanzania Bara, kutekeleza takwa hili la kisheria kwa kujisajili na Mfuko ili kutimiza wajibu wao ili kuepuka shuruti.” Alisema.


Shafeek  Purayil(mbele) na Japhet Alexander wakitoka mahakamani baada ya kusomewa mashtaka na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Bibi Victoria Nongwa 
 
 Shafeek  Purayil

 Meneja Matekelezo (Compliance Manager),  wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Victor Luvena akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo. Alisema washtakiwa wengine Zaidi watapandishwa kizimbani Jumanne Februari 20, 2018 kwa makosa hayo hayo. Kulia ni Mwanasheria wa WCF, Bw. Deo Ngowi.
Meneja Matekelezo (Compliance Manager),  wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Victor Luvena akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo. Alisema washtakiwa wengine Zaidi watapandishwa kizimbani Jumanne Februari 20, 2018 kwa makosa hayo hayo.

Comments