Featured Post

HAKI ZA WANAWAKE KUMILIKI, KURITHI MALI


Na Adv. Blandina Manyanda
HALI hii imesababishwa mara nyingi na mila na desturi za baadhi ya makabila hapa nchini ambazo zimekuwa zikimchukulia mwanamke kama kiumbe duni asiyepaswa kurithi mali.

Kuna baadhi ya makabila yamediriki hata kukataa kuwasomesha watoto wa kike na pia kuwarithisha mali kama ardhi kwa mtazamo kuwa mwanamke hana faida kwani akishakuolewa hana faida tena kwa ukoo au familia yake kwa kuwa anakuwa mali ya ukoo wa mume wake hivyo kumsomesha au kumrithisha mali itakuwa sawa na kufaidisha familia au ukoo  mwingine.
Pamoja na kuwepo kwa hali hiyo ya ukandamizaji dhidi ya wanawake nchini, serikali yetu kwa kushirikiana na asasi au taasisi zinazoshughulikia haki za binadamu imekuwa mbele kuhakikisha mfumo dume huu unatokomezwa, hii ni imefanyika aidha kwa kutoa elimu sehemu mbalimbali nchini juu ya haki sawa kwa wanawake  na wanaume juu ya kumiliki mali.
Pia serikali imejitahidi kutunga sheria kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zinatoa haki sawa kati ya wanaume na wanawake katika kumiliki ardhi. Sheria hizi ni pamoja na
(i)              Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Chini ya Ibara ya 24 ibara ndogo ya kwanza (i) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wanawake na wanaume wana haki sawa katika umiliki wa mali. Ambapo imeainishwa kuwa kila mtu (awe mwanamke au mwanaume) ana haki ya kumiliki mali na kuilinda mali yake hiyo kwa mujibu wa sheria.

(ii)           Sheria  ya Ardhi ya mwaka 1999.
Kifungu namba 3  kifungu kidogo cha 2 cha Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 (Sura ya 113), kinasema kuwa haki ya kila mwanamke katika kumiliki na kutumia ardhi itakuwa na kiwango sawa kama ilivyo kwa wanaume. Pia kifungu cha 161 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili  kinawapa haki sawa wenza katika ndoa katika kumiliki ardhi waliyopata pamoja au kama wameiendeleza pamoja.

(iii)        Sheria ya Ardhi ya kijiji ya mwaka 1999.
Kifungu namba 20 kifungu kidogo cha 2 cha sheria ya ardhi ya kijiji ya mwaka 1999 (sura ya 114), pia kinampa haki sawa mwanamke katika kumliki ardhi kama ilivyo kwa wanume na kimeainisha kuwa sheria yoyote ya kimila inayomnyima mwanamke nafasi ya kumiliki mali ni batili. Pia kifungu cha 35 kifungu kidogo cha pili cha sheria ya ardhi ya vijiji kinatoa haki sawa kwa watu wote (wanaume kwa wanawake) katika kumiliki ardhi. Pia kifungu namba 23 kifungu kidogo cha 2 cha sheria ya ardhi ya kijiji ya mwaka 1999 kinatoa hakisawa  katika  kuhudumiwa wakati wa kuomba kupata hatimiliki  ya ardhi ya  kimila . 
  
(iv)          Sheria ya ndoa ya mwaka 1971
Kifungu namba 56 Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inawapa wanawake walio katika ndoa haki sawa na wenzi wao katika kumiliki mali. Sheria hii imeainisha kuwa mwanamke yoyote yule aliye katika ndoa ana haki sawa na mumewe katika kumiliki mali. Pia sheria hiyo inaendelea kuwapa haki sawa wanawake katika mgawanyo wa mali na wenzi wao pale inapotokea kuwa ndoa imevunjika.

(v)             Sheria ya Mirathi ya India ya mwaka 1865.
 Sheria ya mirathi ya India ya mwaka 1865 ambayo inatumika pia hapa nchini katika            mirathi ya marehemu ambaye wakati wa uhai wake hakufuata sheria za kimila au kiislamu, inawapa wanawake haki ya kurithi mali. Sheria hii hutumika zaidi kwa wakristo ambao hawakuishi kwa kufuata sheria za mila zao. Sheria hii haijaweka tofauti kati ya warithi wanawake na warithi wanaume. Mgawanyo wa mirathi ya mtu ambaye hakuacha wosia katika sheria hii kama ifuatavyo;
·         Mali ya marehemu huenda kwa mke au mume wa marehemu(Kifungu cha 26)
·         Mali huenda kwa wototo wa marehemu( wawe wa kike au wa kiume wote wana haki sawa.)
·         Chini ya kifungu namba 27, kama marehemu ameacha mjane moja ya tatu ya mali zake huenda kwa mjane na sehemu iliyobaki huenda kwa watoto wake.
·         Kama ameacha mjane bila watoto bali kaacha ndugu wengine wa karibu nusu ya mali huenda kwa mke na nusu nyingine huenda kwa hao ndugu wenginewa karibu
·         Kama ameacha mke peke yake basi mali yote hurithi mjane huyo.
·         Kifungu cha mali kinachorithiwa na watoto hugawanywa sawa kwa watoto wote bila khjali jinsia(kifungu cha 30).

(vi)          Sheria ya mirathi ya  kimila
Urithi chini ya sheria za kimila pia unawapa wanawake haki ya kurithi mali  ijapokuwa mgawo wa mali wanaopata si sawa na ule wa wanaume. Urithi chini ya sheria za kimila umegawanywa katika vyeo vitatu na wanawake wamewekwa katika kundi la mwisho la kurithi sehemu ndogo ndogo ya mali kuliko zote.        
Angalizo: Watu wanaweza kujiuliza kuwa je, mwanamke anaweza kurithi mali pale ambapo sheria ya kimila inamkataza kurithi?

NDIYO; Mwanamke anaweza kurithi mali hata kama sheria ya kimila inamkataza hii ni kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria ya ardhi ya mwaka 1999 na sheria ya ardhi ya kijiji ya mwaka na sheria ya ndoa  ya mwaka 1971, zote zinamlinda mwanamke asiporwe haki yake na sheria za mila. Sheria yoyote ya kimila inayompora mwanamke haki yake kurithi mali inapingana na Katiba pamoja na sheria ya ardhi pia ile sheria ya ardhi ya kijiji pia sheria ya ndoa ya mwaka 1971 na katika mazingira kama hayo sheria hiyo ya kimila ni batili kwani katiba na sheria nyingine zilizopitishwa na bunge zina kipaumbele.  

Comments