Featured Post

HAKI ZA ARDHI KWA WAKAZI WAISHIO PEMBEZONI MWA BARABARA



KUTOKANA na ongezeko la idadi ya watu, kukua kwa shughuli za uzalishaji mali na ongezeko la vyombo vya usafiri, suala la miundombinu ikiwemo barabara haziwezi kubaki katika ukubwa wake wa sasa.

Ni muhimu zipanuliwe ili kukidhi mahitaji ya wakati husika katika maeneo mbalimbali nchini kama vile jiji la Dar es Salaam.

Hifadhi ya barabara
Barabara ni mojawapo ya miundombinu ambayo ipo katika kundi la ardhi ya hifadhi kama ilivyofafanuliwa hapo awali. Nchini Tanzania, hususani katika jiji la Dar es Salaam, kuna ramani (master plan) ambayo inaonesha mgawanyo wa ardhi na matumizi yake kulingana na eneo husika mfano; maeneo ya makazi, barabara, reli, viwanda na biashara, maeneo kwa ajili ya shule, vituo vya afya n.k. Kwa mantiki hiyo, kila matumizi kuna taratibu na misingi yake ili kukidhi matumizi yaliyotajwa katika eneo husika.
Kwa kawaida, ujenzi wa barabara nchini umekuwa ukitekelezwa na Wizara ya Ujenzi na hali halisi ya utekelezaji wake umekuwa ukiambatana na malalamiko kutoka kwa wananchi waishio maeneo yaliyo karibu na barabara.
Ikumbukwe ya kwamba katika awamu ya tatu ya uongozi wa nchi, maeneo ya hifadhi ya barabara yaliwekwa alama ili kuondoa malalamishi yaliyokuwepo katika kipindi cha huko nyuma.

Maendelezo ya ardhi katika hifadhi ya barabara
Wakati  Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, akiwa ameagiza nyumba zilizojengwa katika hifadhi ya barabara na shughuli hiyo ikiwa imeanza kutekelezwa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisitisha bomoa bomoa hiyo. Pinda alisema yamekuwepo malalamiko mengi kwa wananchi kwamba hawakupatiwa elimu kuhusu ubomoaji huo, na ukiendelea unaweza kuibua migogoro isiyo ya lazima.
Alisema suala hilo linarudishwa serikalini ili Baraza la Mawaziri lilitafutie ufumbuzi na baadaye lipelekwe bungeni kujadiliwa upatikane muafaka. Baada ya kauli hiyo ya kusitisha, wananchi walionesha kushangilia, hali inayotia wasiwasi kwamba walielewa kuwa kufanya hivyo si uvunjaji wa sheria.
Wananchi wanapaswa kufahamu kwamba ujenzi wa nyumba katika hifadhi ya barabara ni kosa la kisheria kwani ni kwenda kinyume na matumizi ya kundi hili la ardhi.

Haki na stahili za maeneo yanayochukuliwa katika upanuzi wa barabara
Tofauti na mwananchi anayejipatia ardhi na kuiendeleza katika kundi la ardhi ya hifadhi, kuna wakazi ambao maeneo yao yanapakana na hifadhi ya barabara. Katika jiji la Dar es Salaam na nchini kote, kumekuwepo uendelelezaji na ujenzi wa barabara ambazo hupewa hadhi ya kiwilaya na kimkoa.
Uendelezaji wa namna hii husababisha kumegwa ama kuchukuliwa ardhi za wananchi waishio pembezoni mwa barabara. Mchakato huu unapofanyika ni sharti wananchi washirikishwe na mamlaka husika na pia utaratibu wa kisheria huzingatiwa; kwa maana ya kulipwa fidia kwa mujibu wa katiba ya nchi na sheria ya ardhi ya mwaka 1999.
Manispaa ya Kinondoni ni mojawapo ya maeneo ambayo wakazi zaidi ya 532 kati ya 658 walioathirika kwa kubomolewa nyumba zao ili kupisha mradi wa mabasi yaendayo kasi, tayari walishalipwa fidia zao.
Katika mwaka wa fedha 2007/2008, serikali iliwaidhinishia sh. bilioni 10 za kuwalipa fidia waathirika wa bomoabomoa itokanayo na mradi huo. Mpaka sasa ni sh. bilioni 4.6 pekee ndizo zilizotumika ikiwa ni asilimia 46 tu.
Pia kwa wakazi wa Manispaa ya Ilala, mchakato unatarajiwa kuanza mapema mwezi ujao baada ya kukamilika kwa zoezi la utwaaji wa ardhi katika eneo la Gerezani. Baada ya kukamilika kwa ulipwaji wa fidia kwa wahanga wa manispaa hizi mbili, ujenzi wa barabara ya magari yaendayo kasi utaweza kuanza.

Hali halisi na msigano katika utekelezaji wa ujenzi wa barabara unaoendelea jijini Dar es Salaam
Tangu miaka ya tisini, Tanzania ilianza kujikita katika uboreshaji wa miundombinu hususani barabara kwa kuanzishwa mamlaka maalum kama TANROADS. Mamlaka hii ilianzishwa kupitia sheria ya vyombo vya mamlaka (Executive Agency Cap 245) mwaka 1997 na kuanza kazi rasmi mwaka 2000 nchini kote kwa mujibu wa utaratibu ulivyo katika Wizara ya Ujenzi.
Hivi karibuni, Waziri wa Ujenzi alitangaza kuwa wananchi wote waliojenga katika hifadhi ya barabara wabomoe  ili kupisha ujenzi wa barabara . Suala hili katika maeneo mengi limefanyika na kupokelewa kwa hisia tofauti na wananchi na viongozi wa serikali kuu.

Mambo ya kujadili
·         Je wananchi wanafahamu mgawanyo na matumizi ya ardhi kwa mujibu wa sheria za ardhi, 1999?
·         Mara nyingi ikitokea bomoabomoa,wananchi huuliza hivi, mbona  tuliruhusiwa na maofisa ardhi wenyewe kujenga hapa ambapo mamlaka nyingine za serikali, kama za umeme na maji zilitupatia huduma?
·         Je nini mtizamo wako kwa watendaji wanaotoa vibali vya ujenzi na hati za ardhi katika hifadhi za barabara?
·         Je watendaji wa serikali wanakuwa wapi wananchi wanapofanya maendelezo katika hifadhi za barabara kinyume na matumizi yake?

Nini kifanyike?
·         Ni jukumu la wizara ya ardhi kurejelea ramani (master plan)  nchini kote kufahamu bayana barabara za wilaya na mikoa na mikakati ya mpango wa uendelezaji wa barabara na pia kuwafahamisha wanachi
·         Kinachopaswa kufanywa na mamlaka husika  hasa wizara ya ardhi ni kusimamia kwa vitendo utekelezaji wa sheria ya maadili ya maofisa mipango miji Na.7 ya mwaka 2007 ili wananchi wawe na imani na wataaluma wa sekta hiyo muhimu.
·         Serikali iwachukulie hatua watendaji wanaokiuka utaratibu wa matumizi ya hifadhi ya barabara na kusababisha kadhia kwa wananchi. hali halisi inaonyesha kwamba wenye taaluma hii ndio wamekuwa wakipima na kugawa viwanja mijini kiholela bila kujali kama kuna umuhimu wa kuwa na maeneo ya barabara, shule, zahanati, soko, nyumba za ibada, viwanja vya michezo na matumizi mengine.
·         Serikali iwajibike na sio kufumbia macho uvunjwaji wa utaratibu uliowekwa katika hifadhi za barabara na matumizi mengine kwa manufaa ya wananchi. mfano hai ni katika miji ambayo ina hadhi ya majiji na manispaa kama Dar es salaam, Mbeya , Iringa, Mwanza, na Arusha. Mipango mikuu ya majiji na manispaa hizi hazifuatwi kabisa, hasa ukizingatia kwamba maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya makazi ya watu tu, yameruhusiwa pia kutumika kwa ajili ya karakana kubwa za magari na mashine, viwanda vyenye kemikali, sehemu  za kuegesha magari makubwa na hata kumbi za starehe zinazotoa huduma na kupiga muziki mpaka asubuhi kandokando ya barabara sanjari na ujenzi wa hoteli kubwa zenye ghorofa bila kujali eneo husika lilipangwa kujengwa nini kwa mujibu wa mpango mkuu. Aidha ujenzi wa vituo vya mafuta umeenea hata katika maeneo ya mapumziko na michezo. Kutosimamia hili kunasababisha uvunjaji wa haki za binadamu pale wananchi wanapobomolewa nyumba zao ili kupisha ujenzi kama vile barabara, wakati awali watendaji wa serikali waliwaruhusu kuweka makazi ama walipuuzia na kutowachukulia hatua wananchi wanaofanya maendelezo katika hifadhi za barabara kinyume na sheria za ardhi.
·         Mwananchi anapohitaji ardhi ni jukumu la kufanya utafiti zaidi wa eneo analohitaji katika mamlaka husika ili kujiridhisha haki na umiliki wake katika ardhi husika.
·         Maafisa mipango miji wakaguliwe utendaji wao unaotakiwa kuwa katika maadili. Hii ni kutokana na maafisa wanaolalamikiwa sana na wananchi kwa tabia yao ya kudai na kupokea rushwa.

Hitimisho
Kabla ya kuanza kutekeleza bomoa bomoa kupisha upanuzi wa barabara, Januari 13, 2011 aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Rais Dkt. John Magufuli, alitoa ilani kwa wananchi waliojenga nyumba ndani ya hifadhi ya barabara kuanza kubomoa nyumba hizo mapema na kwamba wasitegemee kulipwa fidia.
Wakati zoezi hili likiendelea waziri mkuu alitoa agizo la kusitisha zoezi la bomoa bomoa hiyo Machi 6, 2011 mpaka litakapo jadiliwa na baraza la mawaziri.
Ifahamike kwamba kwa hali hiyo, ni lazima barabara zipanuliwe na kwa kufanya hivyo wale waliojenga katika hifadhi ya barabara ni lazima kama siyo sasa basi baadae, nyumba zao zitabomolewa kwani kujengwa kwao katika hifadhi ya barabara ni kitendo kilichovunja sheria.
Ila kwa wale ambao maeneo yao yatachukuliwa na serikali katika mchakato huu ni haki yao kulipwa fidia ya haki, stahili na kwa wakati kwa mujibu wa sheria na kanuni za ardhi za mwaka 1999.

Comments