- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Swali 1: Ni taratibu zipi zinazotumika katika
utoaji wa vyeti vya hakimiliki za kimila kwa wamiliki wa ardhi za kimila ndani
ya maeneo ya vijiji?
Mfumo wa umiliki wa ardhi Tanzania ni wa aina
mbili. Kwanza, ni kwa njia ya kimila; ambapo mmiliki wa ardhi aliyeipata kwa
njia ya kurithi, kupewa zawadi, kugawiwa
na kijiji, kununua ama kusafisha pori anakuwa na haki ya ardhi
hiyo. Haki hiyo inalindwa kisheria hata bila ya kuwa na hati yoyote.
Njia ya pili ni kwa hati miliki ambapo mmiliki
wa eneo hupewa cheti au hati inayothibitisha umiliki wake wa eneo husika. Mara
nyingi ardhi ya jumla inamilikiwa na hatimiliki wakati ardhi ya kijiji
inamilikiwa kimila.
Kwa mujibu wa sheria ya vijiji ya ardhi ya
vijiji Na. 5 ya mwaka 1999, hakimiliki ya kimila inatolewa baada ya kutimiza
taratibu za awali ambazo ni pamoja na kijiji husika kupata cheti cha ardhi ya
kijiji (F.7 [7]), cheti ambacho hupatikana baada ya kutimiza masharti matatu ya
msingi.
Kwanza, kijiji kisiwe na mgogoro wowote wa
mipaka ya ardhi yake. Pili, kijiji kiwe kimejenga masijala ya ardhi kwa ajili
ya kuhifadhia nyaraka muhimu, na tatu, kijiji kiwe kimeandaa mpango wa matumizi
bora wa ardhi.
Baada ya taratibu hizo kukamilika, halmashauri
ya kijiji kupitia kwa Afisa Mtendaji wake itatakiwa kutoa taarifa kwa
halmashauri ya wilaya kwa ajili ya taratibu za kubainisha mipaka, kuchora
ramani na kuendeleza mchakato wa upatikanaji wa cheti cha ardhi ya kijiji na
baadaye vyeti vya hakimiliki za kimila ambavyo hutolewa kwa mmiliki mmojammoja
wa ardhi kwa mujibu wa kifungu cha 22(3) na 25 cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji
Na.5 ya 1999.
Angalizo: Kwa kijiji ambacho kiliwahi kupata
hatimiliki ya kijiji huko nyuma itabiti hatimiliki hiyo irejeshwe kwanza ndipo
cheti cha ardhi ya kijiji kiandaliwe. Hii inamaanisha kuwa kijiji hakipaswi
kuwa na hakimiliki ya kijiji pamoja na cheti cha ardhi ya kijiji kwa wakati
mmoja.
Swali 2:
Taratibu gani zinapaswa kufuatwa wakati
eneo linapotangazwa kuwa la mipango miji?
Wakati eneo linapotangazwa kuwa la upimaji au
mipangomiji, masharti ya sheria yaliyoko kwenye sheria ya utwaaji na sheria na
sheria za ardhi yanapaswa kuzingatiwa. Kifungu cha 3 (1)(g) cha sheria ya ardhi
Na. 4 na Na. 5 kimeeleza kwamba, umiliki wa mtu unapositishwa kwa namna yoyote
ile, usitishwaji huo unapaswa kuambatana na malipo ya fidia kamili, ya haki na
kwa wakati kwa mtu huyo.
Rachel Kilasi – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akifafanua sheria ya Ardhi na. 4 ya mwaka 1999 sambamba na Umiliki wa Ardhi
Hii ni pamoja na kumpa mtu notisi ya muda wa
kutosha wa kujiandaa kuhama kuendana na mabadiliko hayo. Fidia hii inahusisha
thamani ya mali iliyopo katika eneo hilo kwa kuzingatia gharama au thamani ya
soko kwa wakati huo. Fidia inapaswa kutolewa kwa kuzingatia misingi ya haki na
kwa wakati ingawa mara nyingi haya yamekuwa hayazingatiwi katika maeneo
mbalimbali.
Swali 3: Ni zipi haki za wakazi na wamiliki wa
maeneo yanayotangazwa kuwa maeneo ya upimaji au mipango miji?
Mara nyingi, eneo linapotangazwa kuwa la
mipangomiji au la upimaji huambatana na mabadiliko mbalimbali ya ukaaji na
matumizi ya ardhi ya eneo hilo. Kuna uwezekano mkubwa wa mmiliki wa eneo hilo
kuagizwa kuondoka kupisha shughuli husika, ama kutekeleza na kuendana na
masharti mapya ya eneo lililotangazwa kuwa na mipango miji.
Hali hii inapojitokeza bado mmiliki anazo haki
zinazoendana na uendelezaji uliofanyika mahali pale. Miongoni mwa haki hizo ni
pamoja na kupewa fidia endapo mmiliki atalazimika kuhamishwa au sehemu ya
umiliki wake katika ardhi hiyo inahamishiwa kwa mmiliki mwingine.
Fidia hii sharti iwe ya haki na itolewe kwa
wakati kama ilivyofafanuliwa hapo awali. Sheria za ardhi zinakataza watu
kuondolewa katika maeneo yao bila kulipwa fidia endapo ni wamiliki halali kwa
mujibu wa sheria mbalimbali na taratibu zilizotumika kuwamilikisha maeneo hayo.
Swali 4: Kuna tofauti gani za kimsingi kati ya
hatimiliki, cheti cha hakimiliki ya kimila na leseni ya makazi?
Hakimiliki ya
kisheria
Ni cheti kinachompa mtu umiliki wa kisheria kwa
maandishi. Cheti hiki kinatolewa kwa mujibu wa wa sehemu ya sita (6) ya sheria
ya ardhi Na. 4 ya mwaka 1999kwa mmiliki wa ardhi ya jumla na sehemu ya ardhi ya
hifadhi. Hati za namna hii hutolewa pia kwa wamiliki wa mashamba makubwa
yanayomilikiwa kwa hati hata kama mashamba hayo yako ndani ya ardhi ya kijiji
ilimradi tu yamepimwa na kukamilishwa kwa taratibu zinazotakiwa kisheria. Hati
hizi hutolewa na kamishna wa ardhi kwa kipindi cha ama miaka 33 na 99 .
Cheti cha
Hakimiliki ya Kimila
Ni cheti kinachompa mtu umilikiwa ardhi kwa
taratibu za kimila. Kwa upande mwingine, cheti hiki hutolewa kama hati ya
maandishi kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha sheria ya ardhi Na.5 ya mwaka 1999
kwa wamiliki hasa katika ardhi ya kijiji. Cheti hiki hutolewa na halmashauri ya
kijiji kwa mwanakijiji mmoja au kikundi cha wamiliki au taasisi.
Angalizo:Izingatiwe kuwa, kwa
mujibu wa kifungu cha 18(1) cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na.5 ya mwaka 1999,
hakimiliki ya kisheria kwa hali yoyote ina hadhi sawa na hakimiliki ya kimila.
Hivyo, hakuna umiliki wenye hadhi ya juu kuliko mwingine.
Ufafanuzi huu unapaswa kuondoa mazoea ya watu
kufikiri kuwa, hatimiliki ina hadhi ya juu kuliko milki ya kimila au cheti cha
hakimiliki ya kimila, mazoea mabayo husababisha wamiliki wa kimila kujiona
wanyonge na wakati fulani kupoteza haki zao kwa mazoea.
Leseni ya
makazi
Swali 5: Je, lengo kubwa la hati/cheti cha hakimiliki
ya kimila ni kuchukulia mikopo tu?
Watu wengi wamekuwa wakihusisha upatikanaji wa
cheti cha hakimiliki ya kimila na mikopo ya kibenki. Hata hivyo, ukweli ni
kwamba cheti cha hakimiliki ya kimila hakitolewi kwa lengo la kuchukulia mikopo
tu.
Badala yake cheti hiki kinalenga kutimiza azma
ya Sera ya Ardhi ya Taifa ya kuhakikisha kwamba haki zote zilizopo katika ardhi
na imilikaji wa ardhi wa kwa muda mrefu unatambilika na kulindwa kisheria. Hii
ni kwa mujibu wa kifungu cha 3 (b) cha sheria Na. 4 na 5 za 1999.
Pamoja na
faida nyingine, hati hii huboresha usalama wa kumiliki ardhi kijijini na
kuondoa uvamizi holela. Vilevile, hati hii inamfanya umiliki wa ardhi wa kimila
kuwa rasmi zaidi tofauti na ilivyo katika maeneo mengi ambayo hayana hati hizo
kwani huonekana kama ni vigumu kuthibitisha umiliki wake.
Kadhalika, pale ambapo itaonekana kuwa mifumo ya
taasisi za kifedha inakubaliana na matumizi ya hati hizo kama dhamana ya
mikopo, hati zinaweza kutumika katika taasisi husika. Wapo pia wanaozitumia hati
hizo kama dhamana mahakamani na hata katika taasisi za elimu ya juu kama
dhamana ya mkopo.
Swali
6: Umiliki wa kimila bila cheti cha
hakimiliki ya kimila una nguvu?
Kimsingi,
umiliki wa kimila tangu zamani haukuambatana na cheti au hati yoyote ya kimaandishi
kuthibitisha. Nguvu yake kubwa ipo katika mila na desturi za eneo husika na
hivyo sheria kwa kutambua mfumo wa milki ya ardhi ya kimila, imeupa hadhi sawa
na ule umiliki wa kutumia hati na unatambuliwa hivyo hata kama cheti cha
hakimiliki hakijatolewa.
Hata
hivyo, ni lazima pia kuweka bayana kuwa kumekuwepo shinikizo kubwa kubadili
mfumo wa kumiliki ardhi kimila kwa vile unaonekana kama haumpi mmiliki uhakika
wa milki ya ardhi yake pale ambapo hana uthibitisho wa cheti.
Mashinikizo
haya yanatokana na mabadiliko katika mfumo wa ardhi kidunia ambao unaweka mkazo
katika maslahi binafsi kuliko yale ya kiujumla ambayo ndiyo mhimili wa mfumo wa
umiliki ardhi wa kimila.
Lakini
katika mazizingira ya sasa, bado wamiliki wengi wa ardhi waishio vijijini na hata
walio mijini (maeneo yasiyopimwa) hutegemea mfumo wa ardhi wa kimila kwani ndio
unaoonekana kuwapa uhakika wa kumiliki maeneo yao kuliko hatimiliki ambazo
wengi huchukulia kuwa ni njia ya kuwatenga wengine kutoka katika umiliki wa
ardhi ya pamoja.
Swali
7: Je, kuna mtu akiwa na ardhi maeneo
tofauti tofauti katika ardhi ya kijiji, cheti cha hakimiliki ya kimila
kitatolewaje? Na pale mwanakijiji anapokuwa na ardhi kwenye kijiji kingine
umiliki wake unakuwaje?
Ni
dhahiri kwamba wanavijiji walio wengi wanamiliki eneo zaidi ya moja katika
sehemu tofauti katika ardhi ya vijiji. Utaratibu uliopo katika utoaji wav yeti
umezingatia hali hii. Kila eneo linapaswa kuwa nacheti chake kwa kuzingatia
matumizi ya eneo hilo nikiwa ni pamoja na mila, desturi na tamaduni za maeneo
hayo. Vilevile mtu anapokuwa na ardhi katika ardhi ya kijiji kingine anakuwa na
umiliki sawa na wakazi wa kijiji kile na cheti kitatolewa kama taratibu za
kijiji hicho ardhi ilipo kwa kuzingatia mila na desturi za kijiji husika.
Endapo inakuwa vigumu kwa kijiji kuruhusu umiliki wa aina hiyo kwasababu
mbalimbali ikiwemo uhaba wa ardhi kwa wanakijiji, basi itabidi mmiliki achague
kijiji atakachoishi na kujiandikisha kama mkazi wake japo pia haki yake ya
kumiliki na kutumia ardhi kama asiye mwanakijiji iko pale pale.
8.
Je, ardhi ya kijiji inaweza kugawiwa kwa mtu asiye mwanakijiji na kwa taratibu
gani?
Katiba
ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania ibara ya 17 (1) inatoa fursa kwa raia wa
Tanzania kuishi popote nchini ili mradi anafuata taratibu zinazotakiwa na kwa
kufanya hivyo hakiuki haki za raia wangine. Ibara ya 24 inatoa haki kwa raia
kumiliki mali ikiwemo ardhi. Kwa wananchi wengi wanaoishi vijijini, ardhi ndio
mali ambayo kila mmoja anamiliki.
Hivyo
kutokana na msingi huo, hata raia asiye mwanakijiji ana haki ya kuomba na
kugawiwa ardhi ya kijiji haki hiyo imefafanuliwa katika fungu la 22 la sheria
ya ardhi ya vijiji namba 5 1999, ambayo inatoa haki kwa mtu au kundi la watu
ambao kwa kawaida si wakazi wakijiji kuomba kugawiwa ardhi ya kijiji.
Hata
hivyo katika kufanya hivyo muombaji huyo anapaswa kufuata taratibu za kawaida za uombaji. Tarataibu hizo ni
pamoja na: kwanza,muombaji anatakiwa
9.
Ni nani mwenye haki ya kumiliki ardhi nchini Tanzania na nani harusiwi kumiliki
ardhi?
Kisheria
, raia wote wa Tanzania wana haki ya kumiliki ardhi. Haki hii inajumuisha pia
taasisi zilizosajiliwa kisheria na kutambuliwa kama mtu mbele ya macho ya
sheria. Kwa mujibu wa fungu la 20 la sheria ya ardhi na 4 ya mwaka 1999, mtu
asiye raia wa Tanzania haruhusiwi kupata au kumiliki ardhi isipokuwa tu
kwaajili ya shughuli za uwekezaji kwa kuzingatia sheria ya uwekezaji ya mwaka
1977.
Hata
hivyo kwa mujibu wa sheria hii, mmiliki wa ardhi hiyo hawi mwekezaji bali kituo
cha uwekezaji ambacho humpangisha mwekezaji huyo kama umiliki wa upangaji.
Mmiliki wa aina hii anakuwa na haki hafifu inayojulikana kama derivative right
tofauti na mmiliki wa kawaida ambaye anakuwa na haki kamili inayotolewa kwa
njia ya hati kupitia kamishna wa ardhi.
10.
Je, mwanamke ana haki gani katika ardhi ya familia? Ya mumewe? Ya jumla?Au ya
kijiji?
Kabla
ya ujio wa sheria mpya za ardhi wanawake walikuwa wakibaguliwa katika mifumo ya
umilikaji ardhi kutokana na kuzoeleka kuwa wangemiliki kupitia waume zao au
ndugu zao wa kiume kama wajomba na kaka zao. Ukiachilia mbali sheria ya
kikoloni ya mwaka 1923, sheria nyingi za kimila pia ziliwabagua na baadhi yake
bado zimeendelea kuwabagua wanawake katika umiliki wa ardhi na hata mirathi.
Sheria
mpya za ardhi za mwaka 1999, zimeleta mapinduzi makubwa katika mfumo wa milki
ya ardhi kwa wanawake. Kwa mujibu wa sheria ya ardhi na 4 fungu la 161(1)
mwanamke ana haki juu ya ardhi ya familia nay a mumewe. Katika fungu hili,
sheria imeweka wazi ardhi hiyo itahesabika kuwa chini ya umiliki wa wanandoa
wote, isipokuwa pale hakimiliki ya ardhi itakapobainisha wazi kuwa ardhi hiyo
ni mali ya mwanandoa huyo pekee.
Hata
hivyo, kifungu kidogo cha pili cha fungu hilo, kimeweka bayana kuwa hali hii
inapotokea, bado mchango wa uzalishaji, maendelezo na utunzaji wa ardhi hiyo
unaofanywa na mwanandoa mwingine (mwanamke au mwanaume) utampatia haki sawa ya
umiliki wa ardhi hiyo. Haki ya mwanamke katika ardhi ya jumla na ile ya
mwanaume katika kupata, kumiliki, kutumia, na kuuza au kuigawa ardhi kwa
viwango vilevile na masharti yaleyale, kwa mujibu wa fungu la 3(2) la sheria za
ardhi, 1999
11.
Pale ambapo sheria za kimila zinamnyima haki mwanamke au makundi mengine katika
jamii kumiliki ardhi nini kinapaswa kufanyika?
Sheria
za kimila zinapaswa kuwiana na misingi ya sera ya taifa ya ardhi na sheria
nyingine yeyote inayohusiana na ardhi ikiwa ni pamoja na katiba ya jamuhuri ya
muungano wa Tanzania. Endapo mila, desturi, au mazoea ya jamii yanaonekana
kumnyima haki mwanamke, yatahesabika kuwa batili na yasiyotambulika wala kutelekezwa
na halmashauri yoyote ya kijiji, mkutano wa kijiji, mtu au kundi lolote. Hii ni
kwa mujibu wa fungu la 20(2) la sheria ya ardhi ya vijiji na 5,1999
12.
Ni taratibu zipi zinapaswa kutumika wakati wa kutwaa ardhi kutoka kwa mmiliki
kwa ajili ya matumizi mengine au maslahi ya taifa?
Utwaaji
ni uwezo wa rais kuchukuwa sehemu yoyote ya ardhi ya Tanzania kwa kile
kinachodaiwa kuwa ni kwa manufaa ya umma, kwa mujibu wa sheria ya utwaaji na 47
ya mwaka 1967 na sheria ya ardhi na.4 ya mwaka 1999.
Hatua
hii inapochukuliwa Rais anapaswa kuzingatia taratibu zifuatazo: mosi, lazima
atoe notisi ya kusudio la utwaaji wa ardhi inayoainisha sababu za utwaaji.
Pili, anapaswa kutoa muda wa pingamizi wa siku tisini kwa wale ambao ardhi yao
inatwaliwa. Tatu, endapo hakuna pingamizi, mtwaaji anatakiwa kufanya
uthaminishaji na thamani za mali zilizo katika ardhi husika. nne na mwisho,
mtwaaji anapaswa kutoa fidia ya haki na kwa wakati kulingana na viwango vya
soko vya mali husika.
13.
Mmiliki wa ardhi ana haki gani pale ardhi yake inapotwaliwa kwa matumizi
mengineyo?
Kifungu
cha 3(1)(g) cha sheria ya ardhi na.4 na na.5 kinaeleza kwamba umiliki wa mtu
unapositishwa kwa namna yoyote ile usitishwaji kwa namna yoyote ile usitishwaji
huo utapaswa kuambatana na malipo ya fidia kamili, ya haki na kwa wakati kwa
mtu huyo ikiwa ni pamoja na kumpa mtu huyo notisi na muda wa kutosha wa
kujiandaa kwa ajili ya kuhama au kuendana na mabadiliko hayo.
Fidia
hii inahusisha thamani ya mali iliyopo katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na
maendelezo yaliyofanyika katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na maendelezo
yaliyofanyika katika eneo hilo kwa kuzingatia gharama au thaman ya soko kwa
wakati huo. Fidia inapasa kufanyika kwa haki na kwa wakati ingawa mara nyingi
haya yamekuwa yakipuuzwa katika maeneo mbalimbali.
14.
Je, unaweza kuzuia uporaji wa ardhi ya kijiji isichukuliwe kwa madai ya kuwa
ardhi tupu?
Mkanganyiko
uliopo katika tafsiri ya ardhi ya jumla katika sheria na.4 ya 1999 inayoingiza
ardhi ya kijiji isiyokaliwa, kumilikiwa wala kutumiwa katika kundi hilo
unarahisisha uporaji wa ardhi ya kijiji na pia kupunguza mamlaka ya usimamizi
wa ardhi ya kijiji kutoka kwa wanavijiji na halmashauri zao.
Ili
kuzuia uporaji huu, wanavijiji wanashauriwa kuweka mpango wa matumizi bora ya
ardhi. Mpango huu unalenga kuhakikisha kuwa hakuna ardhi inayobakia kijijini
bila kuwa na matumizi maalumu ama kwa wakati huo au wakati ujao.
15.
Kwanini wamiliki wa nyumba na mali nyinginezo zilizo kando ya barabara
hubomolewa kunapokuwa na upanuzi wa barabara hizo? Yapi ni makosa yao na kama
wanahaki ni zipi kisheria?
Ni
makosa kwa mtu kujenga ndani ya hifadhi ya barabara. Inapotokea mtu akajenga au
kufanya shughuli yoyote ndani ya eneo hilo, mara nyingi hukutana na tatizo hili
kwani anakuwa amelikalia kwa hasara yake.
Na
ni vigumu kudai fidia hata hivyo,mamlaka husika zinawajibika kutoa taarifa
kabla ya kuchukua hatua hiyo. Uzoefu unaonyesha kwamba wakati mwingine nyumba
nyingi hubomolewa pale wakazi hao wanapokaidi wito wa kuondoka kwa kutoelewa
kwamba hawana haki ya kumiliki maeneo hayo. Lakini pale inapotokea mamlaka za
upanuzi wa barabara ukavuka mipaka ya hifadhi yake na akuingilia makazi au
miliki za watu waishio maeneo hayo, basi mamlaka hizo zinawajibika kuzingatia
sheria ikiwa ni pamoja na kutoa notisi, kusikiliza na kuzingatia pingamizi
pamoja na kutoa fidia kwa wahusika.
Hitimisho
Ndugu
msomaji, bila shaka umefurahia mfululizo wetu wa maswali na majibu. Matumaini
yetu ni kwamba umeelimika na kutambua masuala mbalimbali yahusuyo ardhi, ikiwa
pamoja na kujua maana, usimamizi, matumizi na utawala wa ardhi na rasilimali
nyingine nchini Tanzania. Tunaamini pia kuwa umepata fursa ya kujua haki na
wajibu wako katika kulinda na kutetea rasili mali hizo muhimu ikiwa una maoni,
maswali au mchango mwingine wowote katika kuboresha kazi hii uandikie kupitia:
Taasisi ya Utafiti na
Utetezi wa Haki za Ardhi (HakiArdhi)
P. O Box 75885
Barua
pepe:info@hakiardhi.org
Tovuti:
www.hakiardhi.org
Comments
Post a Comment