Featured Post

DK. KIGWANGALLA AAGIZA JUMUIYA YA HIFADHI YA WANYAMAPORI WAMIMBIKI IPANDISHWE HADHI KUWA PORI LA AKIBA


Na Hamza Temba - WMU-Bagamoyo, Pwani
....................................................................

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudence Milanzi kuanzisha mchakato wa kisheria wa kupandisha hadhi Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Wamimbiki kuwa Pori la Akiba ili iweze kuhifadhiwa vizuri baada ya kushindwa kujiendesha.

Ametoa agizo hilo leo mkoani Pwani baada ya kutembelea eneo la Jumuiya hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua shughuli za uhifadhi katika eneo hilo ambalo ndani yake pia kuna mapito ya wanyamapori.

Dk. Kigwangalla amechukua uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa jumuiya hiyo ikiwemo tuhuma walinzi wake kutoka katika vijiji vinavyounda jumuiya kujihusisha na vitendo vya ujangili. Hata hivyo alipokea ombi la Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Omari Tofiki ambaye aliiomba Serikali ichukue jukumu la kulinda hifadhi hiyo kwa asilimia 100.

"Sisi kama jamii tumeshindwa, tunaomba msaada wa Serikali, itusaidie kuondoa hawa wavamizi na ikiwezekana ichukue jukumu la kulinda hifadhi hii kwa asilimia 100," alisema Tofiki.

Alisema jumuiya hiyo ambayo ni muunganiko wa vijiji 24 inakabiliwa na changomoto kubwa ya ujangili uliokithiri ambao umepelekea kuuwawa kwa wanyamapori zaidi ya asilimia 90 ya waliokuwepo tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo mwaka 1997.

Alisema changamoto nyingine ni kukosekana kwa muwekezaji na mapato ya kujiendesha, uvamizi wa mifugo ndani ya hifadhi hiyo na majungu yanayosababishwa na baadhi ya wananchi na viongozi wanaonufaika na vitendo vya ujangili na uharibifu wa hifadhi hiyo.

Dk. Kigwangalla alisema jumuiya hiyo imefeli katika kila eneo jambo ambalo linalazimu kuanzishwa kwa mchakato wa kuirudisha Serikalini ili iweze kuhifadhiwa vizuri. Alitoa wito kwa viongozi wa Wilaya na vijiji kuanza kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kupandishwa hadhi jumuiya hiyo kwa faida ya pande zote.

"Nimepokea maombi mengi ya kuongeza idadi ya wanyamapori katika hifadhi ya Saadan, tatizo kubwa hapa ni kwamba wanyamapori wanapotoka nje ya hifadhi hiyo na kupita kwenye eneo la Wamimbiki wanavunwa na majangili ambao wengi wao wanasuply (wanasambaza) nyamapori Jijini Dar es Salaam," alisema Dk. Kigwangalla akielezea umuhimu wa kupandishwa hadhi hifadhi hiyo.

Kwa upande wake Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Abraham Julu amesema Serikali imekuwa ikisaidia katika ulinzi wa eneo la jumuiya hiyo kwa kushiriki kwenye doria mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kuondoa makazi ndani ya hifadhi hiyo.

Alisema eneo hilo ni muhimu sana kwa uhifadhi wa wanyamapori kwa kuwa ni moja ya eneo la mazalia ya wanyamapori na shoroba nne (mapito ya wanyamapori) zinazounganisha hifadhi ya Taifa ya Saadan, Mikumi na Pori la Akiba la Selous.

Katika hatua nyingine baada ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Saadan, Dk. Kigwangalla ameuagiza uongozi wa TANAPA kupitia hifadhi hiyo kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Bagamoyo na vijiji kuweka utaratibu maalum utakaowawezesha wananchi kupita katika barabara zilizopo ndani ya hifadhi hiyo kwa ajili ya shughuli za kijamii ikiwemo kuwatengenezea vitambulisho maalum.

Ametoa agizo hilo kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa kwake na Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwan Kikwete kuwa wananchi wake wanazuiliwa kutumia barabara hizo kwa madai ya kushiriki kwenye vitendo vya uharibifu wa hifadhi hiyo.


Amewataka pia viongozi wa hifadhi hiyo ya pekee barani Afrika ambayo ipo katika fukwe za bahari ya Hindi kuwa wabunifu zaidi kwa kuanzisha bidhaa mpya za utalii ikiwa ni pamoja na kutangaza fursa zilizopo. Alisema hifadhi hiyo ambayo ipo karibu na Jiji la Dar es Salaam na Tanga ni fursa nzuri kwa watalii kutumia ukaribu huo kuweza kuwaona wanyamapori mbalimbali wakiwemo Simba, Twiga na Tembo pamoja na utalii wa fukwe.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na uongozi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Wamimbiki wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga.

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Wamimbiki wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Jana. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na wafanyakazi wa Hifadhi ya Taifa ya Saadan wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya hifadhi katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Jana. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uhifadhi wa TANAPA, Martin Loibooki. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akioneshwa mazingira ya Hifadhi ya Taifa ya Saadan na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Stephano Msumi wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Jana. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwan Kikwete. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwan Kikwete wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya hifadhi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saadan katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Jana. Katikati ni Mkurugenzi wa Uhifadhi wa TANAPA, Martin Loibooki. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akioneshwa mazingira ya fukwe ya Hifadhi ya Taifa ya Saadan na Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwan Kikwete wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya hifadhi katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Jana.
Picha ya pamoja

Comments