- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NDOA na mahusiano ya familia ni mambo
yanayowahusu watu wengi katika jamii; ndoa ni kiungo kikubwa katika mahusiano
ya familia.
Msingi mkubwa wa familia ni ndoa,
ambao unatokana na mahusiano ya kimapenzi kati ya mwanaume na mwanamke.
Katika makala haya tunaangalia
mahusiano ya kimapenzi kati ya mwanamke na mwanaume yanapoweza kubeba dhana ya
ndoa kisheria; jambo la kujiuliza ni je kila mahusiano ya mwanaume na mwanamke
ni ndoa?
Katika Tanzania ipo sheria moja ya
ndoa ya mwaka 1971 Sheria hii inatambua ndoa zote zilizofungwa kwa kuzingatia
taratibu zinazoainishwa kwa sheria mbalimbali kama vile, sheria za kimila,
sheria za kidini na sheria za
kiserikali.
Katika jicho la sheria ndoa zote
katika makundi yanayotajwa zina hadhi sawa, ufungaji wa ndoa ni tofauti lakini
sheria ya ndoa inawatambua wanandoa kuwa wako sawa.
Ndoa ni mahusiano huria kati ya
mwanamke na mwanaume pia ni mkataba ama makubaliano huria yanayopelekea
wahusika kupata hadhi ya ndoa ambayo inatambulika kisheria.
Sheria ya wanandoa ya mwaka 1971
inayatambua makundi mawili ya ndoa kutokana na makubaliano ya wanandoa. Kundi
la kwanza ni ndoa za mke mmoja au zenye makusudio ya kuwa mke mmoja, kama
zilivyo ndoa za Kiserikali na za Kikristo.
Sheria ya ndoa ya mwaka 1971
inasisitiza kuwa ndoa kati ya Wakristo iliyofungwa kanisani, haiwezi kugeuzwa
kuwa ndoa ya mitala.
Mwanamke au mwanaume aliyeoa ndoa ya mke mmoja au mume
mmoja hataruhusiwa kufungua ndoa nyingine ila tu kama atakuwa mjane au mgane au
amepata amri ya mahakama ya kuibatilisha ndoa yake ya awali ama baada ya amri
ya Mahakama. Chombo pekee kinachoweza na chenye mamlaka ya kutoa talaka ni
mahakama pekee.
Kundi la pili la ndoa ni ndoa za
mitala au zinazoweza kuwa za mitala, kama zilivyo ndoa zilizofungwa kiislamu au
kimila, ndoa yenye madhumuni ya kuwa na zaidi ya mke mmoja au ya mitala
haitaweza kugeuzwa kuwa ya mke mmoja, kwa mfano mwanaume aliyefunga ndoa ya
mitala hawezi tena kufunga ndoa ya Kikristo kama hajabatilisha ndoa ya awali.
Nikiwa mwanafunzi wa chuo kikuu
wakati huo, niliona mambo kadhaa katika maisha ya chuo; Jambo majawapo ilikuwa
ni wanachuo wa jinsia mbili kuishi katika nyumba moja kama mume na mke.
Nilijiuliza ambapo hata wewe unaweza
kujiuliza je walikuwa mke na mume? Pia wakati mwingine niliwakuta watu wakisema
“…huyu mwanaume kaishi na huyu mwanamke miezi mitatu (3) hawa ni mume na mke tayari, lazima wagawane mali zao…” Mpendwa
msomaji ukweli ni upi? Bila shaka utajua baada ya maelezo yangu mafupi hapa
chini.Moja ya ndoa zinazoweza kutambuliwa ni ndoa dhania (presumption of
marriage), Kulingana na sheria ya ndoa ya mwaka 1971,endapo itathibitishwa
kwamba mwanaume na mwanamke wenye sifa ya kufunga ndoa, wameishi pamoja
mfululizo kwa miaka miwili au zaidi, katika hali ya kupata heshima ya mke na
mume, basi watachukuliwa kuwa mume na mke, hata kama hawakujaliwa mtoto.
Jambo la msingi hapa ni kwamba jamii
inayozunguka ndoa dhania hiyo iweze kushuhudia. Ikumbukwe kwamba kama ndoa
dhania itavunjika, mahakama inaweza
kutoa amri ya kugawana mali kama ilivyoamriwa na mahakama ya Rufaa Tanzania
katika Shauri la Hemed S.Tamim
dhidi ya Renatha Mashayo, {1994}.
Sheria inayosimamia ndoa Tanzania ni
moja tu ambayo ni sheria ya ndoa ya mwaka 1971, hakuna ndoa inayofungwa kinyume
cha sheria hii, iwe ya kimila ,kikristo ,kiislamu au Kiserikali. Kiongozi wa
dini au kiongozi wa Serikali aliye na kibali cha kufungisha ndoa wote katika
sheria wanayo hadhi sawa aidha ndoa zote katika jicho la Sheria ni sawa.
Comments
Post a Comment