Featured Post

WIZARA YA AFYA ZANZIBAR NA BOHARI YA DAWA (MSD) WASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO

 Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD),  Laurean Rugambwa Bwanakunu (kulia), na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar,  Asha Ally Abdullah wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano mjini Zanzibar leo. Wengine wanaoshuhudia ni wanasheria wa taasisi hizo mbili.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD),  Laurean Rugambwa Bwanakunu, akielezea namna MSD ilivyojipanga kwenye majukumu yake.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD),  Laurean Rugambwa Bwanakunu, akimkabidhi,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar,  Asha Ally Abdullah , mpango mkakati wa MSD, 2017-2020, ripoti ya maboresho ya MSD na kitini cha bei za bidhaa za MSD (MSD price catalogue)
Kabla ya kusaini makubaliano hayo Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD),  Laurean Rugambwa Bwanakunu (kulia) na timu yake walitembelea ghala la kuhifadhi dawa la Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar (CMS)

Na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Afya ya Zanzibar na Bohari ya Dawa (MSD) wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa MSD kuipatia wizara hiyo huduma ya kuwasambazia dawa,vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kupitia Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar (CMS)

Hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuhakikisha wananchi wake wanapata dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Asha Abdulla amesema changamoto ya upatikanaji wa dawa ilikuwa kubwa, zikipatikana kwa gharama ya juu na kiwango kidogo  walichohitaji ilikuwa inaleta shida wanapoagiza wenyewe.

Ameongeza kuwa hatua hiyo ni muungano shairi,na kuipongeza Bohari ya Dawa (MSD) na Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar (CMS) kwa kutekeleza taratibu zote kwa haraka hadi kufika kusaini makubaliano hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Laurean Rugambwa Bwanakunu amewahakikishia kuwa watawapa huduma nzuri,zenye viwango na kwa wakati na bei nafuu kutokana na kushuka kwa bei ya dawa kwani wananunua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji.

Ameongeza kuwa pamoja na maboresho ya kiutendaji yanayoendelea kufanyika MSD,taasisi hiyo pia imeteuliwa kuwa mnunuzi Mkuu wa dawa,vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa Jumuiya ya nchi za Ukanda wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) hivyo huduma zake zinakubalika kimataifa,hasa katika mnyororo mzima wa ugavi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa CMS Zanzibar , Zahran Ali amesema licha ya makubaliano yaliyofikiwa na kusainiwa, wamekuwa wakishirikiana na MSD kwa huduma mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa watalaam wa kuwasaidia kuboresha mnyororo wa ugavi na masuala ya maoteo sahihi ya mahitaji ya wateja.

(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712727062)

Comments