- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Innocent Nganyagwa
NDUGU zangu, nawakaribisha kwa mara
nyingine kwenye utopevu wetu wa ujadi, ambapo leo tunamaliza ziara yetu kwa
Wajadi wenzetu wa Kinyakyusa.
Lakini licha ya kukamilisha ziara yetu ya
kijadi kwao haimaanishi kuwa tumemaliza kuchambua kila kitu kinachowahusu.
Maana kama ambavyo siku zote huwa
naainisha, mambo ya makabila ni mengi kihistoria na yana mchanganyiko mwingi wa
jadi mbalimbali.
Kwa hiyo si rahisi kusimulia kila kitu,
hasa kutokana na muundo na mfumo wa makabila yenyewe kwa kuzingatia historia
yake, mafungu yanayounda kabila husika, mbari ambayo kabila linatokea, lilipo
sasa na mabadiliko yaliyotokea ndani ya kabila husika kutokana na kuhama kwenye
chanzo chake cha asili.
Katika hayo niliyoyataja, Wanyakyusa nao
wana mambo yanayowahusu ambayo ni ya kina na ya kihistoria yasiyofahamika vyema
hata na baadhi ya Wajadi wa kabila hilo.
Lakini yana mashiko na uthibitisho mwingi
wa kutosha, kama ambavyo tumefafanua kwa takriban awamu kumi tulizowatembelea.
Basi kwa utaratibu wetu tuliojiwekea ambao
tunautumia sasa, tutazame japo kwa ufupi makala yaliyopita kabla ya kuendelea
na uchambuzi wa leo niliowatayarishia.
Katika kufafanua jambo mojawapo ambalo
halikueleweka, niliwaeleza kwa kina kuhusu kigoli kujizoeza majukumu ya nyumba
yake kwa mumewe mtarajiwa.
Utata ulitokana na maelezo yaliyohusu
kujizoeza kujamiiana, japo tulisema si kwa ukamilifu, yaani ni aina fulani ya
mchezo. Kuna maelezo ya kina ya jambo hilo, lakini kwenye staha ya ujadi wetu
tulielezea kwa namna ya kulinda heshima ya ujadi wa ukurasa huu.
Lakini tuliona kuwa mume mtarajiwa
aliyeshindwa kustahimili michezo kiasi cha kupitiliza, huwa amemvusha mchumba
wake huyo kutoka daraja la uchumba hadi kuwa mke kamili kabla ya muda husika
haujawadia.
Ikitokea hivyo basi alipaswa kumalizia
sehemu ya deni la mahari anayodaiwa kwa kuharakisha kwake mambo, lakini athari
itakayompata ni ugumu wa kujua kama mchumbawe huyo amejizuia kujamiiana na mtu
mwingine zaidi yake. Kwa kuwa ameshamuanzisha na hataweza kuona ishara, nadhani
naeleweka nikisema hivyo.
Lakini hayo yote yanatokana na kabila hilo
kuwa na muelemeo wa ukiritimba mwingi wa kiumeni, kama tulivyoona ile hulka ya
wanaume kujikusanyia wake wengi na kusababisha uhaba wa wake kwa vijana
waliotaka kuoa.
Ningependa uelewe kuwa, kutokana na maeneo
husika na fungu la kijamii husika ndani ya kabila hilo, ndiyo maana utaona
kunakuwa na mabadiliko kuhusiana na baadhi ya mambo yao kama lilivyo suala hili
la ndoa na mahusiano ya kijinsia.
Kuna jambo jingine nitawafahamisha kwenye
ujadi wa leo, linalohusu mabadiliko yao ya kimafungu na kimaeneo.
Kwa hiyo, licha ya ule uhuru wa kucheza na
mchumba wake lakini binti hukaguliwa kuhakikisha kuwa ameweza kujitunza na
kustahimili kulinda ukomo.
Jukumu hilo la ukaguzi lilitekelezwa na
shangazi wa mchumba wake, au mama yake mzazi. Nafasi ya baba katika jambo hilo
ni kupewa taarifa tu, hasa ukomo ukikiukwa maana akishafahamu hali hiyo
hulazimika kuamuru mahari iliyosalia ilipwe kama tulivyoeleza awali.
Ieleweke kuwa ukomo ukivukwa si kwamba hali
hiyo ilichukuliwa kwa urahisi tu, kulikuwa na adhabu husika kwa binti kama
aliridhia mwenyewe matakwa ya mchumba wake katika kuvushana ukomo.
Lakini kama yule mchumba ndiye
aliyeshinikiza basi naye alihusika kupata sehemu ya adhabu hiyo, mojawapo ikiwa
kuharakishwa kumalizia mahari iliyosalia.
Lakini kwa mabinti waliostahimili na kuvuka
kikwazo cha kukiuka ukomo wa kucheza, wakithibitika kuwa hivyo husifiwa sana na
hupelekwa kwa mume kwa vishindo vya nyimbo na sifa nyingi kutokana na kuweza
kujihimili.
Kutokana na thamani ya binti wa aina hii
mahari yake huwa na vitu vya nyongeza, tofauti na yule ambaye hakufaulu
kuhimili kuvuka ukomo.
Mjadi, kutokana na maelezo hayo utaona kuwa
kuna baadhi ya mambo kama hilo la mahusiano, yanabadilika sana kimaelezo mara
kwa mara. Lakini ukweli ni kuwa kabila lenyewe lina mabadiliko mengi, kutokana
na mchanganyiko wa baadhi ya mambo yake kutoka eneo moja hadi jingine. Hata
kule kubadilika jina kutoka Wankonde na kuwa Wanyakyusa, ni sehemu ya
mabadiliko hayo.
Makala iliyopita tulichambua kwa kifupi
zaidi, ili tupate nafasi ya kutosha kuelezea baadhi ya mambo ambayo mlikuwa na
maswali nayo tangu tulipoanza uchambuzi wa kabila hili, ambayo sikuwa
nimeyaeleza.
Sasa tujielekeze kwenye ujadi
niliowatayarishia leo, mtakumbuka tulisema kuwa nchi ya Unyakyusa inaanzia huko
Konde-Karonga kwenye uwanda wa milima ya Livingstone nchini Malawi hadi Kusini
mwa nchi yetu huko mkoani Mbeya.
Pia tuliona jinsi ukiritimba wa kiume
ulivyogubika kabila hilo, lakini hali hiyo ikishindwa kufuta kabisa ile alama
ya kikeni kutokana na kuchukua majina ya kikeni.
Nilipoeleza awali juu ya Malkia Nyanseba
mwenye asili ya Kinubi, kuna baadhi yenu hamkunielewa. Kwa kuwa hawa Wanyakyusa
ni Wabantu, lakini pia nilifafanua kuwa kwa asili Wabantu walitoka Kaskazini
wakaja hadi Kusini kabisa kabla ya wengine kurudi tena Katikati.
Hapo nazungumzia Bara la Afrika, pia kuna
masalia yao kwenye vipito takriban vitatu kutoka Kaskazini kuja Kusini, viwili
kati ya vipito hivyo vikiwa Afrika Kati na Kaskazini-Mashariki kwenye eneo la
Unubini.
Kwa hiyo katika yale mabadiliko yao ya mara
kwa mara, baadhi ya tabia zao zina athari za Kinubi kwa damu ya Malkia Nyanseba
huku nyingine zikiwa na athari za Kibantu zaidi na nyingine zipo kati kwa kati.
Tabia nyingine ni kutokana na athari za
mgawanyiko kutoka Konde hadi Unyakyusani, na kama mtakumbuka tulifafanua kwa
nini baadhi ya vijiji vya Upogoroni vina majina yanayoshabihiana na ya
Unyakyusani; kwamba kuna Wankonde waliopitiliza kutokana na kukimbia mapigano
ya wababe wa Kingoni, ambao ni tawi tanzu la Wazulu kutoka kusini.
Hawa Wangoni (kwa asili hasa wanaitwa
Wanguni), walidhamiria kupiga jamii zote kutoka Kusini walikoingilia hadi
maeneo ya Mashariki (Uluguruni).
Lakini walisimamishwa na mbabe wa kivita wa
Wahehe, Mtwa Mkwavinyika (Mkwava), aliyewazungukia kutoka Kalenga na kuanza
kuwarudisha nyuma kutoka Tanangozi.
Vita havikuwa na mshindi zaidi ya Mkwawa na
jeshi lake kuishia mpakani mwa Iringa na Ruvuma, na baada ya hapo utani baina
ya makabila haya ulianza.
Pia msisahau zile fungamano za Wanyakyusa
na Wakinga, huku hao Wakinga wakiwa fungu tanzu lililotokana na Wahehe.
Unaweza kujiuliza, kwa nini nakueleza yote
hayo? Nataka kukukumbusha ili nikueleze sasa chanzo hasa cha kuitwa Wanyakyusa,
kutoka kule Konde-Karonga Malawi walikokuwa Wangonde au Wankonde.
Soma kwa makini sehemu inayofuata, ili
akili yako itopee vizuri kwenye ujadi ninaotaka kukufahamisha.
Nimewahi kueleza sana kuhusu Wabantu mara
kadhaa, Bantu ni moja kati ya mbari kuu tano za Waafrika. Ambapo kila mbari
huzalisha makabila kadhaa, pia kuna makabila yanayotokana na mchanganyiko wa
mbari.
Makabila mawili au zaidi yanayotokana na
mbari moja, hufanana kwa baadhi ya mambo yake hata kama yako maeneo mbalimbali.
Kwa Kibantu, neno ‘Banya’ linamaanisha ‘wanaotokana na’ au ‘wanaotoka kwa’.
Mathalan, Banyamwezi (ambayo kwa Kiswahili
hutamkwa Wanyamwezi) ni ‘wanaotoka kwa’ sio kwenye mwezi, ila inamaanisha
upande wa magharibi.
Kwa jiografia ya kijadi Wajadi wa maeneo ya
pwani walifahamu fika kuwa, Wanyamwezi wanatoka upande wa Magharibi mkoani
Tabora na upande huo ndiko mwezi mpya (mwandamo) hutokea.
Kalenda ya kijadi inahesabu miezi kwa
kufuata kutokea na kupotea kwa mwezi, unaweza kushangaa na kuhisi mbona
inafanana na Kalenda ya Kiislamu?
Hujakosea, sehemu kubwa ya makabila yenye
Ukushi, Uhamitiki na Unailotiki, yanatokea Mashariki ya Kati na Mashariki ya
Mbali ambako ustaarabu ulianzia na kuna kiini kikubwa cha imani ya Kiislamu.
Tuliona jinsi Warangi walivyotoka Mashariki
ya Mbali, eneo la Uhamitikini na wao ni Wahamitiki.
Sasa turudi kwa Wanyakysusa maana katika
kukufafanulia nikikuzamisha sana kwenye kina cha utopevu wa ufafanuzi wa
kijadi, nachelea nitakuchanganya.
Jina la Wanyakyusa kwa kabila hilo
walilipata kwa nyanya (Bibi Mzee), kwa ule utaratibu wao wa kuchukua majina
kikeni.
Kyusa ni jina la huyo bibi ambaye aliishi
Kabale kwenye msitu wa tambiko kwenye Kijiji cha Suma, njia ya kuelekea mji
mdogo wa Mwakaleli.
Kwa hiyo kusema Wanyakyusa (Banyakyusa)
maana ni wale watokanao na huyo Bibi Kyusa, japo hiyo Kyusa pia ina maana yake
pia.
Kwa hiyo kuna baadhi ya Wanyakyusa ambao
hujitambua kuwa wanatoka eneo hilo, japo kwa uhakika Bibi Kyusa anatokana na
kizazi cha waliokuja kutoa Konde-Karonga.
Kama tulivyoona awali ndugu zetu hawa ni
wajasiriamali wa kijadi. Maana zamani kabisa kwenye miaka ya sitini kurudi
nyuma, vijana wengi wa kabila hilo waliokosa uwezo wa kulipa mahari ya kutosha,
walienda kutafuta maisha kwanza huko Zimbabwe Kusini na Kaskazini kwa kufanya
kazi ya vibarua kwenye migodi.
Lakini endapo hawakufanikiwa waliwarubuni
wazazi wa mabinti waliotaka kuwaoa kwa kutoa pesa kidogo na ng’ombe mmoja,
kisha walifanya utekaji wa binti anayetakiwa.
Yaani mposaji wa ile mahari kidogo huwatuma
vijana wenzake kumvizia binti husika mathalan akienda kuteka maji, kisha
humnyakua na kumpeleka kwa aliyewatuma.
Kinachofuata ni kutuma ujumbe wa mshenga
kwa wazazi, kuwataarifu alipo binti yao ili wasihangaike kumtafuta.
Hali hii huonesha taswira tofauti, binti
anaweza kuvunga kutokukubaliana na hali hiyo au hata wakwe nao kuonesha
kutopenda hali hiyo.
Lakini kwa familia ambazo mabinti
hawakuposwa, ilionekana kama nafuu ya kuondoa mkosi kwa ahueni ya kupata mtu
aliyemchukua.
Lakini lazima kijana husika atozwe faini, hili
linaakisi mabadiliko mengine ya hulka tofauti za kabila hili.
Ndoa za kusombana tuliziona tulipotembelea
baadhi ya makabila yaliyopita eneo la Afrika Kaskazini Mashariki wakati
yanakuja hapa nchini, au ndani yake yana mchanganyiko wa jamii zilizotoka eneo
hilo.
Lakini licha ya athari za mbari nyingine
kwenye kabila hilo, bado wana sehemu kubwa ya mambo ya Kibantu hasa kwa ngoma
zao kama ile ya Ipenenga na Ing’oma.
Ipenenga huchezwa na watu wazima
hasa wale ‘Mafumu’ wasaidizi wa Chifu
ambao ni wajuzi wa uganga. Ngoma hii huchezwa pamoja na wake zao siku za
sikukuu kubwa, au kumalizia arobaini ya msiba wa mtu mkubwa au Chifu
aliyefariki.
Na ile ing’oma
huchezwa zaidi na vijana wakitumia fimbo na vibuyu, hii huchezwa wakati wowote
haina muda mahsusi. Kama nilivyochelea awali kuwa hata tukiendelea kwa awamu
ngapi hatuwezi kumaliza mambo yao ndugu zetu hawa.
Basi tuishie hapa kwa leo, nawashukuru
Wajadi wenzangu wa Kinyakyusa tulioshirikiana vyema muda wote nilipokuwa
nachambua mambo yao.
Makala haya yamehaririwa,
yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Septemba 12, 2009.
Comments
Post a Comment