Featured Post

WANYAKYUSA-7: BINTI ANAYEVUMILIA VIKWAZO HUSIFIWA

Mapishi ya asili ya Kinyakyusa.

Na Innocent Nganyagwa
NI siku nyingine tena ndugu zangu, nawakaribisha kwenye mambo yetu ya kijadi kupitia safu hii ya Asili na Fasili.
Tunaingia katika sehemu ya saba ya ziara yetu kwa ndugu zetu Wanyakyusa, tukikaribia mwisho wa uchambuzi wa mambo yao lakini sio kukamilisha kabisa kuchambua mambo yote ya kabila hilo, maana bado ni mengi na hatuwezi kuyaeleza yote.

Kwenye ziara zetu kwa hawa Wanyakyusa, tumekuwa pia tukijibu maswali na maoni yenu na kukumbushana kabla ya kuendelea mbele na uchambuzi wa sehemu tuliyonayo, hivyo kusaidia kupunguza maswali kwa waliokosa sehemu hizo.
Ni rahisi kuwianisha maswali mliyoyauliza ndani ya mtiririko wa uchambuzi tunaoendelea nao, kuliko kusubiri hadi uchambuzi ufike mwisho.
Basi tuendelee na ujadi wetu kwa kukumbushana tuliyoyachambua jana kabla ya kutopea kwenye ujadi wa leo.
Kwanza niliwakumbusha ubainishaji wa mambo yaliyofuatia sehemu zinazofuata za uchambuzi huu, kwamba mwanzo waliitwa Wasokile, Wangonde au Wankonde na nchi yao ya Unyakyusa inaanzia Kaskazini mwa Malawi hadi Kusini mwa nchi yetu huko mkoani Mbeya.
Lugha yao ni tanzu ya Kibantu yenye mashiko yasiyo ya Kibantu, kama ulivyo muundo wa sehemu kubwa ya lugha za Kibantu.
Utofauti huo, ni hata kwa baadhi ya matamshi ya Wabantu wengine wanaowiana nao. Pia tuliona kwamba hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990 asilimia 75 ya watu wa jamii ya kabila hilo wako Tanzania, na asilimia 25 wamebakia Malawi.
Mgawanyo huo ni kwa idadi yao ya awali ipatayo milioni moja na ushei, ambayo imeongezeka tangu wakati huo hadi sasa.
Lakini licha ya muelemeo huo wa wingi kwa pande mbili za nchi yao, waliobaki Nyasaland (Malawi) kupita Mto Songwe ndiyo waliobakia na jina la Wankonde na walioko upande wetu ndiyo Wanyakyusa.
Nyasaland ilikuwa chini ya Waingereza na upande wetu ulikuwa chini ya Wajerumani, waliotatanishwa na kupaita Konde kutokana na ule ufanano wa karibu mno, kumbe wasijue hiyo ni jamii moja iliyotenganishwa kwa mipaka yao.
Mipaka ya utawala usio wa kijadi hutatiza sana watu wengi, hata baadhi yenu wajadi mnafungwa na fikra za mgawanyo wa maeneo uliofanywa na wageni.
Hata dhana kuwa kabila fulani linapatikana mkoa fulani tu, si sahihi sana japo yapo makabila yaliyo katika maeneo ya kiini cha mkoa.
Lakini kuna sehemu kubwa ya makabila ambayo kutokana na yalikoanzia hata kufika mahali yalipo kijiografia, si sahihi sana kuyatambulisha kuwa yanapatikana katika mkoa mmoja.
Kwamba yapo kwenye uwanda mzima na hata zaidi ya mkoa mzima, ndiyo maana kwenye ujadi wetu tuna ramani zetu za kijadi na mara nyingi huwa tunatamka ‘nchi ya kabila fulani.’
Tulitolea mfano wa Wakimbu ambao nchi yao inamega mikoa saba, wanapatikana Iringa, Mbeya, Tabora, Katavi, Songwe, Rukwa na Singida.
Kwa hiyo huwezi kusema kuwa Wakimbu wote ni wa mkoa fulani, Wakimbu saba tofauti wanaweza kuwa wanatokea kwenye mikoa tofauti kila mmoja kati ya ile iliyomegwa maeneo yake na nchi yao ya Ukimbu.
Ufafanuzi mwingine tulioufanya ni kuwa licha ya kuoa kwa mitala lakini kiwango chao cha mahari ni cha kutosha.
Kwa hiyo wapo waliolipa nusu nusu na ndiyo maana wale waliovuka ukomo wa ustahimilivu wa kucheza na wachumba zao, walilazimika kumalizia kulipa mahari na kuchukua binti aliyemvusha daraja na kuwa mke kabla ya muda husika.
Tulizungumzia pia utumwa uliosalia kule Konde-Karonga, uliofanywa na wageni dhidi ya wenyeji. Waliposogea Unyakyusani hakukuwa na matukio hayo, japo kulikuwa na sehemu ya utumwa wa ndani.
Kuna tofauti ya utumwa wa ndani na wa kigeni, lakini pia tulizungumzia utopevu mkubwa wa imani za kigeni kwa watu wengi wa kabila hilo hivi sasa.
Lakini wana mambo yao ya kiimani ya kijadi kama tulivyoeleza kwenye sehemu zilizopita, imani ambazo ni za tangu mababu na mababu zao japo kuna baadhi ya mambo hayawekwi wazi.
Tulielezea pia mabadiliko mengine ambayo ni urithi wa Uchifu, kukiwa na utaratibu ulioanzia Konde wa watoto kurithi moja kwa moja kutoka kwa baba yao.
Kwenye himaya ndogo ndogo za Kichifu, Chifu alirithiwa na watoto wake wawili wa kiume wa kwanza kuzaliwa kwa mke mkubwa na aliyefuatia kwa daraja.
Urithi huu si lazima utokee Chifu anapofariki, bali akishafikia umri wa uzee kiasi cha kutoweza kutimiza majukumu ipasavyo, wakati watoto wake hao wameshafikia umri wa kuweza kukabili majukumu hayo.
Katika kukabidhi majukumu yake kwa mfumo huo, Chifu huagwa kwa sherehe ambayo pia huitumia kugawanya eneo la himaya yake kwa wanawe wawili na kuzalisha himaya mbili.
Kwa mtindo huo utitiri wa zile himaya ndogo ndogo uliibuka na kutokuwa na Uchifu Mkuu. Maana wale watoto wawili pia wakishajiuzulu Uchifu nao hutumia mfumo huo, kwa mfumo huo kama ililazimika, himaya za zamani za Machifu waliojiuzulu zilizipisha himaya mpya za warithi kwenye sehemu kubwa ya eneo hilo.
Huu ni mfumo tofauti kidogo na ule wa ‘Mafumu’ (wasaidizi wa Chifu) kuwa na sauti zaidi, kama tulivyoeleza sehemu zilizopita.
Katika hayo niliyoyasimulia sehemu iliyopita ambayo tulifafanuliana Jana tulizungumzia mabadiliko mengi ya kimsingi kutoka Konde hadi Unyakyusani japo pia kuna mashiko ya zamani yanayodumu hadi sasa.
Kuna baadhi ya mambo yaliyotendeka Konde-Karonga sikuyasema na sitayasema, ili kuepusha taharuki. Maana licha ya safu hii kuitwa ‘Asili na Fasili’ mengine yalivyo hayaandikiki ukurasani, huwa tunayachuja na kuyaweka kando.
Huo ulikuwa muhtasari wa sehemu iliyopita, ambapo tulichanganya muendelezo na ufafanuzi wa ujadi wa Kinyakyusa ambao baadhi yenu hamkuuelewa.
Basi sasa tutopee kwenye ujadi wa leo, tulipowapigia hodi kwa mara ya saba ndugu zetu hawa, nilieleza kuhusu kigoli kujizoesha majukumu ya nyumba yake kwa mumewe mtarajiwa.
Nadhani moja kati ya ujadi uliowatatanisha baadhi yenu wajadi, tuliposema kujizoeza kujamiiana japo pia tulifafanua kuwa si kwa ukamilifu hasa bali ni kama aina fulani ya michezo.
Katika vyanzo nilivyonavyo jambo hilo limeelezwa kwa kina, lakini katika namna ambayo nami naweza kuwaeleza kwa kustahi ujadi wetu.
Lakini kimsingi ni kuwa, kama nilivyosema yule amvushaye mchumba wake kwenye ngazi ya uchumba na kumuingiza kwenye daraja la mke kikamilifu kabla ya muda, alipaswa kulipia sehemu ya mahari iliyosalia maana ameharakisha mambo.
Pia ingekuwa vigumu kwake kujua uaminifu wa mchumba wake kujizuia tendo hilo kwa mtu mwingine, kwa kumuwekea uaminifu yeye aliye mtarajiwa halali.
Kabila hilo lina muelemeo wa ukiritimba mwingi wa kiumeni, kama tulivyodhihirisha ile hulka ya wanaume kujikusanyia wake wengi ilivyosababisha uhaba wa wake kwa vijana waliotaka kuoa.
Kutegemeana na eneo husika na jamii husika ndani ya kabila hilo, binti alichunguzwa kuhakikisha kuwa ameweza kustahimili na kujitunza licha ya ukaribu na mumewe mtarajiwa.
Jukumu hilo lilitekelezwa na shangazi yake, shangazi wa mchumba wake au mama yake. Baba nafasi yake ni kupewa taarifa tu kuhusu maendeleo yake, ndiyo maana ukomo ukikiukwa basi huamuru mahari iliyosalia ilipwe na kutimiza alichokiharakisha mume mtarajiwa.
Na si kwamba kuvuka ukomo kulichukuliwa kirahisi tu, bali kulikuwa na adhabu zake kwa binti husika maana kama tulivyoeleza mwanzoni kuwa, kama aliridhia mwenyewe matakwa ya mchumba wake basi hakukuwa na matatizo sana.
Lakini kama alilazimishwa, basi licha ya kumalizia mahari lakini kuna adhabu kwa binti na faini kwa mchumba wake.
Ila kwa mabinti waliovuka kikwazo hicho salama, hufanyiwa sherehe na kupelekwa kwa mumewe kwa vishindo vya nyimbo na sifa nyingi kutokana na alivyoweza kujihimili.
Mahari ya binti wa aina hii huwa na nyongeza ya mambo tofauti kidogo, kulinganisha na ya binti ambaye hakufaulu hatua hiyo.
Unaweza kuona kuwa katika simulizi hizi kuna baadhi ya mambo ambayo yanabadilika kimaelezo.
Lakini ukweli ni kuwa kabila lenyewe lina mabadiliko mengi, mchanganyiko wa mambo yake na hata baadhi ya mambo ambayo yalibadilika kutoka sehemu moja hadi nyingine ya hatua za maeneo ya kabila hilo.
Nikudokeze kuwa hata kubadilika jina kutoka Wankonde na kuwa Wanyakyusa, kunatokana na mabadiliko hayo.
Tukubaliane jambo moja, kwamba tusimalizie yote kwa leo kwa kuwa Jumamosi ijayo ndiyo sehemu ya mwisho, kuna mambo ya kina zaidi ambayo sikuwa nimewaeleza kuhusu hawa Wanyakyusa ambayo nitayaeleza.
Ili marudio yetu yawe mafupi na ujadi mpya wa sehemu ijayo uwe mrefu, basi tukomee hapa kwa leo na tukutane tena kesho kumalizia kuwatembelea ndugu zetu hawa wenye mambo ya kuvutia.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Septemba 05, 2009.

Comments