- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Innocent Nganyagwa
KARIBUNI kwa mara nyingine tena ndugu zangu,
katika utopevu wetu wa kijadi kupitia safu hii. Leo tunapiga hodi kwa mara ya sita
katika ziara ya kuwatembelea ndugu zetu Wanyakyusa.
Basi kwa tuendelee na mambo ya ndugu zetu
Wanyakyusa kwa kuanzia na muhtasari wa tuliyoyaona jana.
Katika ndoa za umri mdogo za mabinti wa
kabila hilo, tulieleza jinsi binti alivyoanza kujizoesha baadhi ya majukumu ya
nyumba yake tarajiwa.
Kufanya usafi wa nyumba, kupika, kuchota
maji na kusafisha zizi la ng’ombe ni baadhi ya majukumu aliyoyatekeleza kwa
mume mtarajiwa.
Pia kuna lile la kujizoesha kujamiiana japo
si kwa ukamilifu, hili lilizua maoni kutoka kwa baadhi ya Wajadi wa Kinyakyusa
waliowasiliana nami, nitafafanua zaidi hapo baadaye.
Lakini kwa mume mtarajiwa aliyepitiliza
kwenye tendo hilo, hataweza kuwa na uthibitisho kama mchumba wake huyo hajawahi
kujamiiana na mwanaume mwingine zaidi yake kabla ya ndoa.
Hilo likitokea kwa ridhaa bila yule binti
kulazimishwa, halizui tatizo kubwa.
Lakini kwa kipindi hicho ieleweke kuwa
binti husika huangaliwa kwa ukaribu na wazazi wake, kiasi kwamba hukaguliwa
kubaini kama hajavuka ukomo wa mchezo na mume mtarajiwa.
Ukomo ukivukwa basi kwa amri ya baba yule
aliyemvusha ukomo hutakiwa kumalizia kulipa ng’ombe wa mahari na kumchukua
kigoli huyo, kwa kuwa amemharakisha yeye mwenyewe kuwa mke kamili kabla ya
wakati.
Huo ni wakati huyo binti akiwa kigoli
kuelekea kuvunja ungo, hebu sasa nifafanue kama nilivyowaahidi awali.
Mwanzo kabisa wakati tulipoanza
kuwatembelea ndugu zetu hawa, nilifafanua juu ya nasaba na muingiliano wa
Kinubi ndani ya Ubantu wao.
Tulielezea juu ya Malkia Nyanseba, japo
kuna baadhi walitatanishwa na mchanganyiko wa mbari.
Nililazimika kurudia tena ufafanuzi wa
maeneo ya mbari na kuchanganyika kwake, pia kufafanua kuwa kinachodhaniwa kila
mara kuwa Wabantu kwao ni Kusini tu mwa Afrika si kweli.
Bali historia zinaonyesha kuwa walitoka
katikati ya Afrika ya Kati na Magharibi, baadaye wakaja kusini kabisa na
kusogea kutoka Kusini kuja Mashariki.
Ndiyo maana ukifika kuanzia maeneo ya Congo
ya Brazaville, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Cameroon, kuna idadi kubwa ya
Wabantu.
Kama unaifahamu vyema ramani ya bara hili
na historia ya kuzurula kwa makundi ya kijamii kuingilia Kaskazini Mashariki
mwa Afrika, kisha kuelekea Kati na kutoka Kati kwenda Kaskazini hadi Mashariki
pia kutoka Magharibi kupitia Kati, ndiko kulikosababisha muingiliano wa mbari za
Kibantu, Kinailotiki, Kikushi na Kihamitiki.
Kwa hiyo kwa Wabantu hawa wa Kinyakyusa
kutokea kule Konde-Karonga-Malawi, walikuwa na mashiko ya Kibantu
yaliyoingiliana na nasaba za Unubi wa Nyanseba kutoka eneo la Kaskazini
Mashariki kuelekea katikati.
Hata baadhi ya mambo yao tuliyoyaeleza
kwenye sehemu zilizopita za ziara yetu kwao, kwa kawaida hayatendwi na Wabantu
wengi baada ya kufika Kusini.
Mojawapo ni hilo la kujizoesha kujamiiana
japo si kikamilifu, ambalo ni mashiko ya Kinailotiki zaidi kuliko Ubantu.
Lakini pia kutoka kule Konde hadi Mbeya, kuna mengi yaliyobadilika taratibu na
kukumbatia mashiko ya Kibantu zaidi.
Nitaendelea na ufafanuzi huu baadaye kidogo
lakini nikikukumbusha tena kuhusu tuliyoyaona juma lililopita, niliwafafanulia
kuhusu historia zinazoonyesha kuwa Wanyakyusa ni mabaki ya Wangoni na Wapogoro
waliopigwa kutoka Kusini hadi milima ya Upogoroni.
Kutoka hapo milima Upogoroni wakarudi
kinyumenyume hadi milima ya Ukinga, hadi wakaishia mahali walipo hivi sasa.
Kuna majina mengi ya vijiji vya Upogoroni
yanayofanana na majina yaliyoko Unyakyusani, nilifafanua msingi wa jambo hilo.
Kwamba kutoka Konde-Karonga hadi
Unyakyusani ya sasa ni kutoka Kusini zaidi, hadi kuja Mashariki japo kwa
kuishia njiani.
Kusini (Malawi) kwenye uwanda wa safu ya
milima Livingstone, ni mapito ya makabila mengi yaliyotokea Kusini kabisa
kuingia hapa nchini.
Wangoni (Wanguni) ni mojawapo ya makabila
hayo, Waluguru pia walipita njia hiyo wakati jamii zao za awali zilizotokea
Angola zilipoingia hapa nchini.
Mapigano yaliyozikumba baadhi ya jamii za
awali za Wakonde ambazo ni jamii tanzu za awali za Wanyakyusa walipokuwa
Karonga, yaliwakimbiza hata kupitiliza eneo waliloko sasa.
Majina ya Kinyakyusa yaliyopo Upogoroni
yalianzia tangu Konde-Karonga na yapo Mbeya hivi sasa, kama mtakumbuka
tulieleza kuwa hata wakati wa ukoloni hali ya kurandana kwa jamii mbili
zilizogawanyika kutokana na jamii moja kuliwachanganya hata wakoloni.
Wajerumani waliokuwa upande wa Mbeya
mpakani na Konde, walitaka kupaita Konde kutokana na lugha na baadhi ya mambo
kufanana mno na upande wa pili (Malawi) uliokuwa chini ya Waingereza.
Kwa hiyo makala iliyopita tulimalizia kwa
kutoa tahadhari, juu ya fungamano tofauti baina ya makabila tuliyoyatembelea
muda mrefu upande wa Kaskazini na haya ya Kusini.
Nilifafanua pia kuhusu uwiano wa Unyakyusa
na milima ya Ukinga, maana mwanzoni kwenye ziara yetu kwa Wanyakyusa
tulifafanua kwa kina ushirikiano wa makabila hayo.
Na kuhusu fungamano tofauti za makabila ya
Kusini na ya Kaskazini, niliwatahadharisha mshangao utakaowakumba
tutakapowafikia Wasangu kabila litakalofuatia baada ya uchambuzi wa hawa
Wanyakyusa.
Wana fungamano fulani na Wahehe, kiasi
kwamba kuna koo za Kihehe zenye mashina yake Usanguni.
Kwa hiyo haishangazi kukuta Wasangu
wanaoongea Kihehe kama Wahehe, kutokana na kuwa matawi ya jamii moja.
Niliwakumbusha tena kuwa Wahehe ni kabila
linalotokana na mchanganyiko wa Wangazija, Wahabeshi na Wabantu.
Na baadaye kabila hilo nalo lilizalisha
makabila ya Wakinga, Wabena, Wabena-Manga na sehemu ya Wagogo.
Basi tukiendelea, mtakumbuka mwanzoni
kabisa tulipoanza ziara yetu kwa hawa Wanyakyusa niliwatajia baadhi ya mambo
yaliyobainisha yaliyofuata kwenye sehemu za mbele za uchambuzi huu.
Kwanza hawa waliitwa Wasokile, Wangonde au
Wankonde na wanapatikana kuanzia Kaskazini mwa Malawi hadi Kusini mwa nchi
yetu, eneo lote hilo ndilo nchi ya Unyakyusa.
Lugha yao ni lugha tanzu ya Kibantu, yaani
ina mashiko na lugha nyingine ambazo kwa asili si za Kibantu.
Matamshi yao ukiyasikiliza hayaweki
msisitizo wa mvunjiko wa silabi, kama sehemu kubwa ya Kibantu kilivyo. Hata
baadhi ya misamiati yake si kama ya lugha nyingi za Kibantu, hata za Wabantu
wengine wanaowiana nao.
Hadi kwenye miaka ya mwanzoni mwa 1990
walikuwa takriban milioni moja na ushei hivi, huku asilimia 75 ya idadi hiyo
wakiwa upande wa nchi yetu ya Tanzania.
Asilimia kama 25, ndiyo waliosalia upande
wa Malawi lakini kwa sasa idadi hiyo imeongezeka kutokana na kupita takriban zaidi
ya miongo miwili na nusu (miaka 27).
Na kupita Mto Songwe kwenye iliyoitwa
Nyasaland zamani (Malawi kwa sasa), ndiko walikobakia wakiitwa Wankonde na
upande wa pili ndiko wanakoitwa Wanyakyusa.
Nyasaland ilikuwa chini ya Uingereza na
upande huu ulikuwa chini ya Wajerumani, ambao walitumia sana kupaita
Unyakyusani kuwa Konde kutokana na ufanano wa ukaribu na Wankonde.
Ambacho hawakukijua ni kwamba, hiyo ni
jamii moja iliyotenganishwa na mipaka ya kikoloni na kule kuhama.
Wengi wenu hutatizwa sana na mipaka ya
kimikoa na nchi katika kutopea kina cha ujadi.
Ndiyo maana mara nyingi huwa
nawatahadharisha kuwa, mkitaka kufaidi kina cha uhondo wa ujadi msikubali
kufungwa na fikra za maamuzi ya watu wa kuja waliosababisha fikra za sasa.
Kwamba kabila fulani ni la mkoa fulani
kweli yapo baadhi ya makabila ya aina hiyo, lakini kwa sehemu kubwa kuna
makabila ambayo si ya mkoa mmoja.
Unaweza kuyakuta makabila hayo kwenye
uwanda mzima, au hata ndani ya zaidi ya mkoa mmoja. Mtakumbuka tulipowatembelea
Wakimbu, tuliona kuwa wanapatikana Iringa, Mbeya, Tabora, Katavi, Songwe, Rukwa
na Singida.
Sasa sijui ukitaka kulipanga kabila hilo
kwenye mkoa mmoja, utasema wao ni watu wa wapi?
Nchi ya Ukimbu inamega maeneo ya mikoa hiyo
saba, kwa hiyo usishangae ukikutana na Wakimbu watano tofauti na kila
utakayemuuliza kwao ni wapi akakutajia mkoa tofauti na wenzake katika ile saba.
Kwa hiyo Wajerumani hawakuweza kutofautisha
hadi kwenye miaka ya 1930, kwamba huku upande wa pili kwa sasa sio Konde ni
Unyakyusani.
Ufafanuzi mwingine Mjadi ni kuwa, hawa
ndugu zetu kama tulivyoona kuwa wana ndoa za mitala ya wake wengi.
Lakini kiwango chao cha mahari ni cha
kutosha hasa, ndiyo maana kwenye kukiuka ukomo wa ustahimilivu nilisema kuwa
mkiukaji hutakiwa kumalizia kulipa mahari na kumchukua binti aliyemvusha daraja
la mke kabla ya muda kubaliwa.
Unaweza kuona hilo kutokana na kiwango
chenyewe cha mahari, pia tulisema awali kuwa utumwa ulisalia kule Konde
Karonga.
Mkutano wa kiji katika eneo la Konde nchini Malawi, taswira inayoonyesha nyumba ambazo zinapatikana pia Unyakyusani.
Huo ulikuwa utumwa kwa jamii ile uliofanywa
na jamii za wageni, lakini taratibu walivyosogea Unyakyusani mambo hayo
yaliisha taratibu japo kulikuwa na sehemu ya utumwa wa ndani.
Jambo lingine ambao usipolifahamu
litakutatanisha, kuna utopevu mkubwa wa kiimani za Kigeni mkoani kwao hivi
sasa.
Lakini ukweli ni kama tulivyoeleza sehemu
mbili zilizopita, mambo yao ya kijadi ya kiimani yana mashiko makubwa.
Na imani hizo ni tangu mababu na mababu
zao, japo kuna baadhi ya mambo hayawekwi wazi zaidi. Mabadiliko mengine ni
urithi wa uchifu; kulikuwa na mifumo miwili: wa awali ni tangu Konde wa urithi
wa moja kwa moja kwa watoto.
Ambapo kwenye zile himaya zao ndogondogo za
kichifu, chifu aliweza kurithiwa na watoto wake wawili wa kiume wa kwanza
kuzaliwa na mke mkubwa na anayefuatia.
Na urithi huu si lazima chifu afariki bali
akishafikia uzee kiasi cha kutoweza kutimiza majukumu ipasavyo, huku watoto
wake hao wakiwa wameshafika umri wa kuweza kukabili majukumu hayo.
Chifu huagwa kwa sherehe, ambayo pia
huitumia kugawanya eneo la himaya yake kwa wanawe wawili na kuzalisha himaya
mbili.
Hilo ndilo lililosababisha utitiri wa
himaya ndogo ndogo zisizo na uchifu mkuu, maana kama hao wanawe wawili
wakishakuwa machifu na wakijiuzulu nao watatumia mfumo huo.
Kwa mfumo huo kama ililazimika, himaya za
zamani hasa za machifu waliojiuzulu, huzipisha himaya mpya za warithi kwenye
sehemu kubwa ya eneo hilo.
Mfumo huo ni tofauti na ule ambapo wale ‘Mafumu’ (wasaidizi wa Chifu) huwa na
sauti zaidi, kama tulivyoona sehemu zilizopita.
Kuna mabadiliko mengi ya kimsingi kutoka
Konde hadi Unyakyusani, japo pia kuna mashiko ya zamani yanayodumu hadi sasa.
Nikisimulia baadhi ya mambo hayo
yaliyotendeka Konde yanaweza kusababisha taharuki, lakini kwa kuwa huwa
tunachuja basi tunayaweka kando na hatuyaaniki hapa ukurasani.
Leo tulikuwa na ufafanuzi zaidi
uliochanganyika na muendelezo wa ujadi wa Kinyakyusa.
Basi tukomee hapa na tutaendelea tena kesho.
Makala haya yamehaririwa,
yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Agosti 29, 2009.
Comments
Post a Comment