Featured Post

WANYAKYUSA-5: KIGOLI HUMSAIDIA MUMEWE MTARAJIWA

Vyakula vinavyopatikana kwa Wanyakyusa.


Na Innocent Nganyagwa
NAWAKARIBISHENI kwa mara nyingine kwenye safu hii ambapo tunaendelea kuwatembelea Wanyakyusa. Katika makala yaliyotangulia, matembezi yetu yalihusiana na imani, ushirikina na baadhi ya miiko ya Machifu.
Wao huamini kuwa maovu huadhibiwa hapa hapa duniani, japo haina maana kuwa hawaamini katika maisha baada ya kifo.

Ni dhana hiyo ya adhabu hapa duniani iliyowafanya wanawake wagumba wadhaniwe kuwa wanatumikia adhabu hiyo, kutokana na kushindwa kutimiza majukumu yao.
Kama tulivyoona, mwanamke wa Kinyakyusa si tu alipaswa kumnyenyekea mumewe lakini pia alikuwa na mpangilio wa majukumu tangu maisha yake ya ukigoli, kama ambavyo nitaainisha pia kwenye uchambuzi wa leo.
Pamoja na watu wengi wa kabila hilo kugubikwa sana na imani za kidini hivi sasa, lakini wana mambo ya dawa za kijadi zinazowezesha mafanikio ya kilimo, ufugaji, uwezo wa kimapenzi, vita, kutibu magonjwa, kujilinda, kulipiza kisasi kwa maadui na kujilinda dhidi ya washirikina.
Mara nyingi wezi na wazinzi waliadhibiwa kwa nguvu hizo za dawa, ikiwa ni pamoja na kulaani mashamba yao yasitoe mazao ya kutosha.
Uhalali na uharamu wa matumizi ya nguvu hizo, hutegemea dhamira husika. Mathalan, machifu hawakuruhusiwa kuwa na nguvu za kishirikina. Waliohakikisha kuwa chifu hana uwezo huo, ni wale washauri wake ‘mafumu’ japo chifu alibakiwa na zile nguvu za kubariki himaya yake kwa kilimo.
Kuhusu washirikina, wachawi waliotumia chatu kusafiria kwa kupaa nyakati za usiku ndiyo walioogopewa zaidi.
Hawa mara nyingi walidhuru watu, mifugo na mashamba nyakati za usiku, wengi wao walirithi ushirikina huo kutoka kwa wazazi au ndugu. Mjadi, kama ilivyo kwa motokari kutumia mafuta ili iweze kufanya kazi basi chatu hawa waliotumiwa na washirikina kuruka nyakati za usiku, walilishwa nyama na maziwa.
Tulisema kuwa, nyama na maziwa hayo ni chakula cha waombolezaji kwenye misiba ya wahanga waliouliwa na wachawi hao.
Tunazungumzia misiba ya kijadi ya Kinyakyusa, hasa katika enzi hizo za utopevu wa kijadi kwenye kabila lao. Maana kutokana na kuwa na mifugo mingi, ng’ombe kuchinjwa misibani na watu kunywa maziwa ilikuwa kawaida japo pombe hazikukosekana pia.
Ndugu zangu, makala iliyopita katika kufafanuliana vyema kuhusu mambo haya ya ulozi, niliwasimulia kidogo juu ya mambo ya misukule. Maana tulishawahi kuzungumzia mambo hayo, katika kufahamishana baadhi ya misukosuko ambayo Mjadi mwenzenu hukumbana nayo katika kutafiti ujadi.
Kwenye kutafiti ni kawaida kukumbana na ‘mengineyo’ japo ninayowaletea hapa ni yale yananayohusika zaidi na ujadi muafaka. Mara kadhaa nikigusia tu mambo hayo ya kishirikina, hutokea watu wengi wenye kuvutiwa nayo na kutaka kujua zaidi.
Bahati nzuri au mbaya, kwa kuwa Mjadi mwenzenu si mganga wala mlozi, nachelea kuwaeleza sana juu ya mambo hayo msije mkavutiwa zaidi na kujiingiza kwenye vitendo halisi.
Maana nikiri kuwa katika ujadi wangu wa kufukua mambo, nimeshawahi kukumbana na mambo yanayotia hofu kama nilipowahi kualikwa kupaa na ungo, japo sikupokea mwaliko huo! Nilichukua yale niliyohisi yananifaa tu, ili niyafanyie kazi.
Naam, ni ujasiri wa kijadi katika kufukua utopevu wa kijadi!
Tukirudi kwenye wale chatu wa kishirikina, wanapokuja kwenye msiba kupata mlo huwa hawaonekani kwa macho ya kawaida. Kuna wachache tu wenye uwezo wa kuwaona chatu hao, hawa ni wale walinzi wa kuzuia ulozi ambao mara nyingi ni wale wakuu wa vijiji vya mikusanyiko tulivyowahi kuvitaja awali.
Nguvu za walinzi hawa na wale walozi hulingana kwa vyanzo vyake, tofauti ni kwenye matumizi. Walozi hutumia kwa kudhuru, walinzi hutumia kukinga madhara. Walinzi hulinda mashamba na mifugo kwa kuwaadhibu walozi, wakitumia nguvu ya chatu na kusababisha walozi na familia zao waugue.
Lakini mambo yote haya ya nguvu za ulozi na ulinzi dhidi ya ulozi huwa hayasemwi hadharani kwa kuwa kufanya hivyo ni kujivuna, jambo ambalo halitakiwa kabisa kwa wanaohodhi nguvu hizo.
Nguvu hizo hazikutumika kuadhibu wachawi tu, bali pia hata wale waliokuwa na tabia zisizokubalika zilizovuka mipaka ya heshima ya kijamii.
Watoto waliowakaidi wazazi wao kupindukia na kudharau wakwe zao, wanawake waliowafokea waume zao na kuwapiga nao waliadhibiwa kwa nguvu hizo. Hiyo ni pamoja na wanawake ambao wake za watoto wao huzaa nao bado huzaa sanjari nao, hawa walichukuliwa kutojua kiasi cha ukomo wao.
Lakini adhabu za hawa wa kundi la mwisho, hazikulingana na za walozi maana walozi hawakuvumiliwa kabisa. Hawa wakosaji wengine waliadhibiwa kidogo ili wajirekebishe, adhabu zao mara nyingi ni kuuguzwa kwa muda mfupi tu.
Ulozi si mambo yanayofahamika kwa wazi ndani ya kabila hilo kwani ni mambo waliyotoka nayo tangu huko Konde-Karonga, Malawi.
Kwa ufupi ushirikina upo kwenye kabila hilo tangu zamani, tena ulihofiwa sana na ndiyo maana walitafuta mbinu za kuudhibiti. Mbinu moja ya kuwadhibiti washirikina hao ni kuwafukuza kwenye vijiji na himaya, wanawake waliogundulika kuwa walozi waliachwa na wanaume zao.
Lakini washirikina hawakuuawa, kwa kuwa ujuzi wao ulitumika kusaidia ushindi kwenye vita endapo himaya aliyofukuzwa iliingia mapambanoni dhidi ya himaya nyingine.
Kama kuna mashaka yoyote juu ya mtuhumiwa wa ulozi, basi alinyweshwa ‘umwafi’ na asipotapika basi ni mlozi. Kama familia nzima ilituhumiwa kwa ulozi, basi mmoja kati yao hunyweshwa dawa hiyo na hata kama si yeye mchawi ila kuna mchawi kwenye familia hiyo, basi hatotapika.
Ila baadhi ya familia za kilozi zilikuwa na hila ya kumchagua mwakilishi ambaye wanaelewa ni mtapishi kirahisi, ili wajioshe na hatia hiyo ya kishirikina.
Hapo ndipo tulipoishia kwa mara ya mwisho, lakini tukiendelea mbele hebu tutopee kwenye mambo mengine ya ujadi wao badala ya haya ya ulozi.
Kuna mawili, kwanza ni zile ndoa za umri mdogo za vigoli wa Kinyakyusa. Tulishaona jinsi mtoto wa kiume alivyokuwa na baadhi ya taratibu zake, hata wa kike pia walikuwa na taratibu zao. Mojawapo ni kwa binti kuanza kujizoesha maisha ya ndoa tangu angali mdogo, kwa kumtembelea mume mtarajiwa na kutimiza majukumu mbalimbali.
Baadhi ya majukumu hayo ni kufanya usafi wa nyumba, kuchota maji, kupika na kusafisha zizi la mifugo. Lakini la muhimu zaidi ni kuanza kujizoeza kujamiiana, japo si kwa ukamilifu kabisa. Nadhani mnanielewa, japo kuna baadhi ya waume watarajiwa hawakuwa na uvumilivu hasa binti anapokaribia kuvunja ungo.
Hutenda ngono kamili, lakini hasara ya hilo ni kwamba hataweza kuwa na uthibitisho kuwa mchumba wake huyo hajawahi kujamiiana na mwanaume mwingine zaidi yake kabla ya hajamuoa.
Katika mfumo wao wa maisha ya kijadi, hilo halikuwa tatizo kama lilitendeka kwa ridhaa na si kulazimishwa. Namaanisha lile la mwanaume kujamiiana kikamilifu na mchumba wake.
Lakini ifahamike kuwa wakati huu binti huyo huangaliwa kwa ukaribu na wazazi wake. Hutokea mara kadhaa mama humkagua bintiye kujua kama hajavuka ukomo wa mchezo wa kujamiiana na mchumbawe, ikitokea kavuka ukomo huo basi baba hutaarifiwa.
Hapo kinachofuatia ni kwa mwanaume kutakiwa kumalizia ng’ombe wa mahari waliosalia, kisha kumchukua binti maana ameshamharakisha kuwa mke kamili kabla ya muda.
Huu ni ule wakati wa uchumba kuelekea kuolewa kabisa, japo awali tuliona kuwa mabinti kwenye kabila hilo huolewa wakiwa wadogo. Wakati tunaouzungumzia hapa ni kati ya udogo (kigoli), hadi kukaribia kuvunja ungo.
Jambo la pili ambalo nitawafafanulia kwenye uchambuzi wa leo, kuna historia zinazoonesha kuwa Wanyakyusa ni mabaki ya Wangoni na Wapogoro waliopigwa kutoka Kusini hadi milima ya Upogoroni.
Kisha wakarudi kinyume nyume hadi milima ya Ukinga, na kuishia mahali walipo sasa. Kwa majina mengi ya vijiji vya Upogoroni kufanana na majina yaliyoko Unyakyusani, msingi wake ni kuwa kutoka Konde-Karonga kuja Unyakyusani ya sasa ni kutoka Kusini zaidi kuja Mashariki japo kwa kuishia njiani.
Kusini (Malawi) kwenye uwanda wa safu ya milima ya Livingstone, ni njia na mapito ya makabila mengi yaliyotokea Kusini kabisa na kuingia hapa nchini.
Wangoni (Wanguni) ni mojawapo ya makabila hayo, hata Waluguru walipita upande huo wakati jamii zao zikitokea Angola.
Katika kukumbwa na mapigano kuna jamii za Wakonde ambazo ni jamii za awali za Wanyakyusa walipokuwa Karonga, zilizosombwa hata kupitiliza eneo walilopo sasa.
Kwa hiyo majina hayo ya Kinyakyusa yaliyopo Upogoroni, ni yale yale yaliyotokea Konde na kuwapo Mbeya hivi sasa. Ndiyo maana tuliwahi kueleza tulipoanza ziara yetu kwa Wanyakyusa, kwamba hata watawala wa Kijerumani waliokuwa upande wa Mbeya mpakani na Konde, walishawishika kuita eneo hilo jina la Konde kutokana na lugha kuwa moja na upande wa pili (Malawi) uliokuwa chini ya Waingereza.
Niwatahadharishe kuwa kuna aina fulani ya fungamano tofauti baina ya baadhi ya makabila ya upande huu wa Kusini tulikoingia hivi sasa, na Kaskazini.
Kuhusu uwiano na milima ya Ukinga hakuna tatizo maana tulishafafanua mahusiano ya Wakinga na Wanyakyusa, lakini utashangaa tutakapowafikia Wasangu.
Utakachoshangazwa nacho ni fungamano zao na Wahehe, kiasi kwamba kuna koo za Kihehe ambazo mashina yake yako Usanguni.
Usishangae ukikutana na Msangu anayeongea Kihehe kama Mhehe, kwa kuwa ni matawi ya jamii moja baada ya kufika eneo hilo na kujiunda kwenye hali tofauti na mwanzo.
Wahehe ni mchanganyiko wa Wangazija, Wahabeshi na Wabantu.
Lakini baada ya mchanganyiko huo wa jamii na kuwa Wahehe, wakazalisha makabila ya Wakinga, Wabena, Wabena-Manga na sehemu ya Wagogo. Mimi nina ndugu zangu Wasangu ambao tuna shina moja la ukoo, japokuwa wengi kati ya Wahehe na Wasangu hao hawafahamu hivyo.
Ni fungamano za aina hiyo ninazomaanisha, ambazo tutakutana nazo mara kadhaa upande huu wa kusini.
Haya, utopevu wetu wa kijadi unazidi kuzama kina cha ujadi. Lakini kwa leo tuishie hapa, tutaendelea tena na ujadi wetu kesho.


Makala haya yamehaririwa, yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Agosti 22, 2009.

Comments