- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Hili ni Ziwa Ngozi mkoani Mbeya ambalo inadaiwa lilikuwa likihama kimiujiza.
Na Innocent Nganyagwa
WAJADI wenzangu, karibuni tujumuike pamoja
kwenye utopevu wetu wa kijadi kupitia safu hii. Leo tunaendelea na ziara yetu
kwa ndugu zetu Wanyakyusa.
Rika ni kigezo muhimu sana, kwa watoto wa
kiume wa Kinyakyusa. Kwa rika hilo walilazimika kufuata utaratibu wa kulima
mashamba ya baba zao, hadi wafikie umri wa kuoa. Hilo liliambatana na kujifunza
majukumu ya maisha watakapoanza kujitegemea, kwa wakati wote huo walitegemea
mlo nyumbani kwa baba.
Lakini kundi la vijana wa rika moja
waliishi pamoja kwenye vijiji vyao mahsusi, huko walikuwa na kanuni, uongozi na
utaratibu wa maisha yao. Moja ya mambo waliyopaswa kuyazingatia, ni kujenga
ukaribu baina yao na kuepuka kabisa uchoyo.
Ilikuwa muhimu sana kwa kijana wa kiume anapoenda
nyumbani kwa baba yake kupata mlo, basi walau aambatane na vijana wenzake
wawili au watatu kupata nao mlo.
Mimi nimewahi kuishi jirani na Wanyakyusa,
kwa kweli uchoyo hauko kwenye hulka yao kabisa. Na kama ukikutana na Mnyakyusa
mchoyo, basi huyo ana matatizo yake mwenyewe au ameiga tabia hizo kwingineko.
Maana kati ya vitu wanavyovipenda ndugu
zetu hawa ni kula vizuri, ukipata nafasi tembelea mkoani kwao Mbeya ujionee
mwenyewe maakuli ya ndizi, maparachichi, mchele na kadhalika.
Kwa hiyo kama kijana akija nyumbani kula
peke yake, aliweza hata kuadhibiwa na baba yake. Kula pamoja kwa vijana wa
kiume wenye rika moja, ilichukuliwa kuwa ni baraka.
Lakini pia kwa kijana wa kiume kula peke
yake au na vijana wadogo au na wanawake, ilichukuliwa kuwa ni kujilaani. Kwa
mfumo huo, wanawake walikula peke yao na watoto wadogo na mabinti ambao bado
hawajaolewa walioko nyumbani.
Hawa ndugu zetu wana kanuni nyingi za
kijadi zilizoongoza maisha yao ya kila siku. Mathalan, kijana wa kiume
aliyepevuka lakini hajaoa bado hakupaswa kulala kwao, walitengewa vijiji vyao.
Kama wangeruhusu walale kwao, moja ya
athari ni kusikia minong’ono ya wazazi wake kwa mazungumzo yao ya faragha ya
usiku. Nadhani unanielewa namaanisha mazungumzo ya aina gani haya ya usiku.
Lakini pia kwa kijana kuwa kapera hadi
makamu ya rika kubwa kidogo kulikuwa na faida zake.
Kijana wa aina hiyo alichukuliwa kuwa
mpiganaji shupavu kuliko aliyeoa, vijana wa aina hiyo walikuwa muhimu sana
kwenye yale mapigano ya himaya moja dhidi ya nyingine.
Hata wale vijana wakorofi waliokuwa wababe
walivumiliwa na jamii bila kutengwa, maana wangetumika kama askari hodari wa
kutegemewa mapambanoni.
Japokuwa hiyo haikuwa na maana kuwa wanaume
waliooa hawakutiliwa maanani, hao walitumika kama askari wazoefu kwenye
shughuli mahsusi za uvamizi wa kuteka mifugo ya himaya pinzani.
Kwa upande wa imani walihofu zaidi
kuadhibiwa kwa mtu anayetenda uovu akiwa hapa hapa duniani, kwamba mtenda mema
hunemeeka lakini mtenda maovu hulaanika.
Mathalan, ilidhaniwa kuwa mwanamke mgumba
alipatwa na hali hiyo kutokana na maovu hasa kushindwa kutimiza majukumu yake,
hivyo siku zote aliishi na hatia hiyo.
Dawa za kijadi ni muhimu mno katika
kufanikiwa kwenye kulima, kufuga, mapenzi, mapambano, kuponya, kulinda,
kulipiza kisasi au kumdhuru adui na kujilinda dhidi ya washirikina.
Mitishamba hiyo iliweza kutumika kuadhibu
wezi, wazinzi au kulaani mashamba ya maadui yasitoe mazao kama ilivyotarajiwa.
Matumizi yake yaliweza kuwa halali au haramu, kutegemeana na dhamira ya
mtumiaji husika.
Pia niwafahamishe kuwa, kama tulivyochambua
awali tulipoanza kuwatembelea ndugu zetu hawa, tulizingumzia juu ya Chifu
kudhibitiwa na washauri wake.
Moja kati ya mambo hayo ni kuhakikisha kuwa
Chifu husika hana ndumba na hawezi kufanya jambo lolote bila kuwashirikisha hao
washauri wake ‘mafumu.’ Lakini msisahau kuwa, Chifu alikuwa na nguvu zake za
kubariki himaya kwa kilimo na mambo mengine kama tulivyowahi kueleza.
Imani za kuwepo kwa ushirikina zina mashiko
sana ndani ya kabila hilo, tena pengine ni tofauti na jamii nyingine ambazo
tunafahamu baadhi ya mambo yao ya kishirikina.
Mathalan, naamini umewahi kusikia
masimulizi ya watu wanaoruka na ungo au pembe, lakini kwao kuna wachawi
wanaoruka na chatu. Usiogope, ni ujadi wa kishirikina huo! Aina hii ya wachawi
wanaoruka na chatu, ndiyo walioogopwa zaidi kutokana na kudhuru watu na mifugo
nyakati za usiku.
Wengi kati ya hawa walirithi ushirikina huo
kutoka kwa wazazi au ndugu; waliutumia kwa dhamira mbaya ya kuwadhuru wenye
mafanikio ya mifugo na mazao.
Mlo wa chatu hao wa kishirikina waliotumiwa
na wachawi hao walioruka wakiwa watupu migongoni mwa chatu wao, ni nyama na
maziwa yaliyotumiwa na waombolezaji wa wahanga wa ushirikina huo.
Tufundishane jambo moja japo lisikutishe
nikikutaarifu jambo hilo, ni muhimu pia ukilifahamu. Mara nyingi mtu anapokufa
kwa ulozi, wale walozi wake huwa si watu wanaotoka mbali na makazi ya mhanga,
wanaweza kuwa hata majirani zake.
Na kama wamemuua kwa kifo cha bandia, yaani
wamemchukua msukule, basi katika kusanyiko lenu waombolezaji msukule huyo
huweza kuletwa na hao walozi ili wamtese tu hisia zake.
Kwa kushuhudia jinsi watu wanavyomlilia,
wakati kiukweli ni kuwa hajafa. Lakini atakapokuja hapo, ninyi waombolezaji
hamuwezi kumuona isipokuwa dalili kubwa ni kuongezeka kwa kilio hasa kwa nduguze
wa karibu.
Mathalan, kama mama kafiwa na bintiye basi
ndugu jamaa na majirani wanapokuja kumfariji atalia. Lakini kuna wakati anakuwa
ametulia tu, lakini ghafla akianza kuangusha kilio kikubwa cha uchungu mkali
naye alishalia mno tangu mwanzo, basi muda huo bintiye aliyechukuliwa msukule
ameletwa eneo hilo.
Naye hulia sana muda huo sio kwa kuwa
amemuona, bali ni ule muunganiko wa hisia za kiroho baina yake na mwanaye.
Basi hata hao chatu wa kishirikina
niliowaeleza punde, wanapokuja kwenye mkusanyiko wa msiba wa aliyeuliwa na
washirikina wao, hawaonekani kwa macho ya kawaida.
Isipokuwa kwa wachache wenye uwezo huweza
kuwaona, hawa katika kabila hili huaminiwa kuwa walinzi. Wengi wao huwa wakuu
wa vile vijiji vya mikusanyiko, nguvu za walinzi hawa na wale walozi ziko sawa.
Isipokuwa namna na matumizi yake ni
tofauti, walozi ni waovu wanaodhamiria kudhuru na wale walinzi huzuia uovu kwa
wema.
Kwa kawaida wale waliokuwa na uwezo wa
kudhibiti walozi, waliwaadhibu na kulinda mifugo na mashamba. Waliweza kuwafanya
walozi na watoto wao waugue, wakitumia nguvu ya chatu au laana iliyotamkwa kwa
kunuizia pumzi.
Kunuizia kwa pumzi ni sawa na kwenye
makabila mengine wanavyotumia mavumba ya ulozi, kwa kusema maneno ya
kishirikina kisha kuyapulizia kwenye mwelekeo wa yule anayedhamiriwa kudhuriwa.
Lakini yote haya ya uwezo wa walozi au wale
walinzi kutumia nguvu za chatu, si mambo yaliyowekwa hadharani. Maana kufanya
hivyo ni kujisifu na kujivuna, jambo ambalo halikukubalika.
Wakati mwingine si wachawi tu walioadhibiwa
kwa kutumia nguvu hizo, hata wale waliokuwa na tabia zisizokubalika kwenye
jamii yao waliadhibiwa pia.
Mathalan, waliowakaidi wazazi wao kwa
kiwango cha kukiuka au kuwadharau wakwe waliadhibiwa.
Mwanamke aliyemfokea mumewe au kumpiga,
mwanamke aliyeendelea kuzaa huku binti mkwewe akiwa naye anazaa naye
aliadhibiwa. Maana mwanamke wa aina hii alichukuliwa kutojua ukomo wake, hasa
kama mwanaye wa kiume ameshaoa na sasa mkwewe anazaa naye bado anazaa, hiyo
haikuonekana kama picha nzuri.
Lakini unielewe kuwa, adhabu za wakosaji wa
kawaida na walozi zilitofautiana kwa viwango maana walozi hawakuvumiliwa
kabisa. Ila hawa wakosaji wengine waliadhibiwa ili wajirekebishe, mara nyingi
adhabu zao ilikuwa ni kufanywa waugue kwa kipindi kifupi ili wajirekebishe.
Inawezekana hata baadhi ya Wanyakyusa
wenyewe hawajawahi kuyasikia haya. Lakini haya ni mambo yaliyoanzia tangu
walipokuwa kule Konde-Karonga, hata walipoingia walipo sasa.
Kwa hiyo ushirikina upo kwenye kabila hilo
tangu zamani na ulihofiwa sana, ndiyo maana walibuni namna za kuukabili ikiwemo
kutumia nguvu zile zile za washirikina kuwadhibiti.
Pia waliwatenga waliobainika kuwa
washirikina, kwa kuwafukuza kwenye vijiji au hata kwenye himaya kabisa. Kwa
wanawake waliogundulika kuwa walozi, wengi waliachwa na waume zao.
Japokuwa kuna ajabu moja, mlozi hakuuawa
kwa kuwa endapo ingetokea vita baina ya himaya anayotoka na nyingine, basi
ufundi wake ulihitajika kushinda vita hiyo.
Haya ni mastaajabu ya kijadi hayo! Na
katika kumtuhumu mtu kwa ulozi kama kulikuwa na mashaka yoyote basi walitumia ‘umwafi’ kwa kumnywesha, kama hakutapika
basi ana hatia.
Familia zilizotuhumiwa kwa ulozi bila
kujulikana ni nani hasa mlozi husika ndani ya familia hiyo, zilikuwa na hila ya
kumchagua mtu wa familia yao ambaye akinyweshwa hiyo dawa angetapika kirahisi.
Maana iliaminika kuwa yeyote katika familia
hiyo angepewa dawa hiyo, kama kuna mlozi ndani ya familia hiyo lazima
ingebainika.
Masimulizi yetu ya utopevu wa kijadi
yanazidi kunoga lakini nafasi yetu nayo imeishia hapa. Tukutane tena kesho ili
tuendelee na ujadi wetu.
Makala haya yamehaririwa,
yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Agosti 15, 2009.
Comments
Post a Comment