- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Ngoma ya asili ya Wanyakyusa.
Na Innocent Nganyagwa
NAWAKARIBISHENI kwa mara nyingine tena
kwenye safu yetu ya kina ya uchambuzi wa asili na fasili za makabila yetu.
Kwa mara ya tatu tunaendelea na ziara yetu
kwa ndugu zetu Wanyakyusa, Wabantu kutoka kusini mwa nchi yetu, mkoani Mbeya.
Waama nilipowatajia chanzo cha Malkia
Nyanseba, haikueleweka vyema kwa kuwa najua wengi wenu mnafahamu kuwa Wabantu
hutokea kusini mwa bara hili. Lakini kwa uyakini jambo hilo si kweli, hasa
ukifuatilia vyanzo vya kihistoria.
Pia mara nyingi nimewahi kuelezea juu ya
mbari zilizozalisha makabila, ambapo wakati mwingine kuna mchanganyiko wa mbari
zilizozalisha jamii mchanganyiko ambazo nazo huzalisha makabila.
Kwa hiyo, kama nilivyowaahidi kuhusu
ufafanuzi juu ya Malkia Mnubi Nyanseba na kizazi chake kilivyochanganyika na
Ubantu uliokuja kuzalisha Wanyakyusa, nitawafafanulia yote hayo kadiri
tutakavyoendelea na uchambuzi wetu.
Basi kwa sasa tuendelee na ziara yetu, kwa
kujielekeza kwenye awamu ya leo na yale tuliyoyadhamiria kuyazungumzia.
Wanyakyusa walijifunza sehemu kubwa ya
ufundi wa kutengeneza vyungu kutoka kwa Wakinga, waliowagubika kwa utamaduni
wao. Nilieleza kuwa nchi ya Ukinga na Unyakyusa zinapakana katika maeneo yake.
Kwa hiyo, uzalishaji chumvi, utengenezaji
mitungi, kufua vyuma na kutengeneza nguo za kijadi ni mambo waliyojifunza
kutoka kwa majirani zao hao wa Kikinga.
Ni majirani zao hao ndio waliofanya nao
zaidi biashara ya mabadilishano ya bidhaa, wao waliwapa chakula kwa kuwa kwao
wana nchi yenye neema na rutuba, nao Wakinga wakawapa silaha na zana za kilimo.
Lakini tulieleza pia kuwa licha ya kuwiana
na Wakinga, kwa mambo ya ndoa hawakuchanganyika nao maana kwao wanawake wa
Kikinga walikuwa duni mno kulinganisha na wanawake wao wa Kinyakyusa.
Hayo ni baadhi tu ya tuliyoyaona kwenye
sehemu ya pili, pia kwa ufupi sehemu ya kwanza ya ziara yetu kwa ndugu zetu
Wanyakyusa.
Kama tulivyoona umuhimu wa wale watawala
wao wa himaya ndogo ndogo, machifu hao walikuwa na mfumo wa kuhudumiwa kwa
kupewa sehemu ya mazao ya chakula, pamoja na mambo mengine ambayo wakiyahitaji
ilikuwa lazima wapatiwe.
Kwa hiyo, ukitazama kwa muhtasari namna yao
ya kuishi kijadi, mtawala alikuwa na ukiritimba wa baadhi ya mambo, lakini
hakuwa na hodhi kamili ya madaraka.
Maana kuna sababu zilizofanya Baraza la
Utawala kumuondoa madarakani, isipokuwa hiyo haikumuondolea umuhimu wake kama
vile kubariki nchi yake kwa ajili ya msimu wa mvua.
Kwa upande wa wakazi wa himaya, waliishi
kwenye jamii za marika za koo zisizo na undugu, lakini waliweza kulinda umoja kwa
baadhi ya tabia kuwekewa kanuni za kutekelezwa kwa pamoja.
Mathalan, kushirikiana kwenye baadhi ya
shughuli, kama vile kulima, kula na hata kunywa pombe pamoja ilikuwa ni jambo
la muhimu. Katika shughuli hizo kama vile kilimo, licha ya kusaidiana mara kadhaa,
lakini pia ilikuwa ni lazima uwezo wa kulima na kuhudumia mashamba baina ya
kaya moja na nyingine ulingane.
Kwa mfumo huo, iliwezesha himaya nzima kuwa
na uwiano wa neema ya mazao ya chakula, maana hakukuwa na waliowazidi wengine
kwenye kulima na aliyezidiwa alisaidiwa.
Lakini sehemu kubwa ya mazao yaliyopatikana
kwenye kilimo hicho kama yalifanyiwa biashara, basi ilikuwa baina ya zile
himaya na wahamiaji, na siyo baina ya himaya na himaya kwa kuwa zote zilikuwa
na aina moja ya bidhaa, hivyo isingefaa kwa biashara iliyokuwa ya
mabadilishano.
Lakini pia kuna wakati himaya hizo
zilikabiliana kwa mapiganao madogo madogo au kutishiana kupigana. Hilo
lilidhihirisha udhaifu wa kutokuwa na uchifu mkuu, hali iliyosababisha mapigano
ya mara kwa mara baina ya himaya japo yalikuwa madogo madogo. Mapigano hayo
yalikoma baada ya uvamizi wa Wangoni.
Kwa sasa kuna mengi yamebadilika kwenye
kabila hilo, lakini kuna baadhi ya mambo yalikuwa yakitendeka zamani ambayo
yalikuwa ni sehemu ya maisha yao.
Mathalan, ilikuwa mtu akifa, aliachwa
badala ya kuzikwa au akiugua hadi kukaribia kufa, hutengwa.
Usishangae mjadi, hayo ni mambo yao ya
wakati huo! Licha ya simulizi hizo za jadi zao za kizamani, lakini pia
Wanyakyusa walikuwa na mashujaa wao tangu enzi za Konde waliopigana dhidi ya
jamii za wavamizi wakiwemo wakoloni.
Katika historia yao, mapigano ya Konde ya
mwaka 1897 yaliyowahusisha Wamisionari wa Kizungu, Wajerumani, Wanyakyusa na
Wakinga yanakumbukwa sana.
Baadhi ya wapiganaji wa Kinyakyusa
walioshiriki mapigano hayo ni pamoja na Muambaneke, Chifu Masakiwande na Chifu
Makelimba.
Kwa pamoja, Wakinga na Wanyakyusa
waliwapiga vibaya mno wavamizi wa kigeni wa Kizungu kwa kutumia mfumo wa
mapigano uliokuwa maarufu sana Uheheni.
Kwa hiyo, haishangazi kutumika kwa mbinu
hizo za kivita za Kihehe, maana Wakinga waliwafundisha Wanyakyusa kwa kuwa ndio
waliowauzia silaha katika zile biashara zao za mabadilishano ya bidhaa.
Wajerumani waliokuwa wanatawala upande wa
Wakonde kuelekea Unyakyusani, walizinduka baadaye baada ya kipigo kikali na
kutumia nguvu kubwa ili kushinda vita hiyo.
Nitaendelea kuwamegea taratibu mambo ya
ndugu zetu hawa kadiri tutakavyoendelea na ziara yetu kwao.
Kesho tutazama kwenye kina zaidi, kwa
kuchambua mambo yao ya kujamiiana na baadhi ya mila za ndani tofauti na yale
tuliyoyasimulia hadi sasa. Basi nakusihi usikose kujumuika nami kwa utopevu
zaidi wa ujadi wa Kinyakyusa.
Makala haya yamehaririwa,
yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Julai 25, 2009.
Comments
Post a Comment