- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Nyumba ya asili ya Wanyakyusa.
Na Innocent Nganyagwa
KARIBUNI tena ndugu zangu kwenye safu yetu
ya utopevu wa kijadi. Basi tuendelee na ziara yetu ya kuwatembelea ndugu zetu
Wanyakyusa, wanaopatikana mkoani Mbeya.
Tulianza kuwatembelea jana, basi
nitawakumbusha tuliyoyachambua juu yao tulipowatembelea kwa mara ya kwanza
kabla hatujaendelea na uchambuzi wa mambo yao zaidi.
Tulisema kuwa ndugu zetu hawa ambao kwa
asili huitwa pia Wasokile, Wangonde au Wankonde, wanapatikana kwenye eneo pana
sana linaloanzia kaskazini mwa nchi jirani ya Malawi hadi kusini mwa nchi yetu
huko mkoani Mbeya.
Wanyakyusa ni Wabantu na huzungumza lugha
yao ya Kinyakyusa, japo ni watu wa jamii hiyo hiyo moja wenye majina tofauti
kutokana na mgawanyiko wa makundi ya jamii zao kwenye eneo wanalopatikana.
Wanaoishi kwenye eneo la safu ya milima
Livingstone kuanzia upande wa Mto Rukuru kaskazini, Karonga huko Malawi,
hufahamika zaidi kama Wangonde au Wankonde.
Lakini walio upande wa pili yaani huku
Mbeya hapa nchini, hufahamika kama Wanyakyusa.
Licha ya lugha ya ndugu zetu hawa kuwa
Kibantu, lakini ina miundo tofauti ndani yake kwa matamshi na silabi zake
zilivyo.
Ni lugha inayojitofautisha hata na baadhi
ya lugha nyingine za Kibantu, za jamii wanazopakana nazo kwenye eneo la nchi
yao.
Nadhani unafahamu kuwa mara nyingi
tumerudia kufafanua kwenye safu hii kuwa makabila yanayotokana na mbari moja
huwa na muingiliano wa utambulisho kwa baadhi ya mambo, yakiwemo matamshi ya
baadhi ya maneno ya lugha.
Lakini pia lugha ikiingiliwa na lugha
nyingine hasa jamii zaidi ya moja zinazowiana, lazima kutatokea mabadiliko
kadhaa madogo madogo. Mabadiliko hayo baadaye huzoelekea na kukubalika kuwa
matamshi halisi, japo ukifukua kwenye vyanzo vya utafiti utagundua mwanzoni
haikuwa hivyo.
Tukirudi kwenye mambo ya Wanyakyusa
tuliyoyaeleza, ni kwamba kundi hili la wanaoitwa Wanyakyusa zamani walipokuwa
‘Nyasaland’ yaani Malawi kandoni mwa Mto Songwe waliitwa Wangonde.
Lakini baada ya kuvuka na kuja huku ndiyo
wakawa Wanyakyusa.
Awali utamaduni wao ulikuwa ukirandana kwa
ukaribu kwa makundi yote ya pande mbili za eneo lao.
Hali hiyo iliwachanganya hata watawala wa
kikoloni, maana kwa wakati huo upande wa Nyasaland ulikuwa chini ya Waingereza
na huku kwetu tulikuwa chini ya Wajerumani.
Kutokana na kufanana mno kwa utamaduni wa
jamii za pande hizo mbili watawala wa upande huu wa pili (Wajerumani), waliamua
kupaita Konde wakifananisha na jamii za wale walio upande wa kwanza.
Lakini, kama ambavyo tumegundua mara kadhaa
juu ya jamii za kale zilizokuwa na kawaida ya kuzurura na kuhamia maeneo ya
mbali katika kutafuta maisha bora, basi hata hawa Wanyakyusa nao walikuwa
hivyo.
Tukirudi nyuma zaidi kwenye chanzo chao,
kwa asili walitokana na Malkia wa Kinubi aliyeitwa Nyanseba. Mtawala huyu
alipinduliwa na wafugaji wazururaji, waliohamisha utawala kutoka kikeni kwenda
kiumeni na kusimika Wafalme badala ya Malkia.
Lakini hila hiyo haikufaulu kufuta nguvu na
uwakilishi wa kikeni ndani ya jamii za baadaye zilizozalisha kabila la
Wanyakyusa, kutokana na mfumo wao wa utoaji majina ya watoto katika ujadi wao
wa zamani.
Ilikuwa akizaliwa mtoto wa kiume huchukua
jina la ukoo wa mama na wa kike la baba, Mjadi, tulipofahamishana jambo hilo
tulifahamishana jambo lingine linalohusiana na utamaduni wa majina ya
Kinyakyusa.
Lakini tuliona kuwa, jamii mbili za watu
hawa yaani wale Wangonde waliobaki kule kusini mwa nchi yao na hawa Wanyakyusa,
walitofautiana katika maendeleo.
Tofauti nyingine ni kuwa hawa waliofahamika
kama Wanyakyusa, waliishi kwenye mikusanyiko midogo midogo wakisimamiwa na
tawala nyingi ndogo ndogo za Kichifu.
Hata hivyo licha ya udogo na mgawanyiko wa
tawala zao, lakini waliweza kuwakabili vyema maadui wa Kisangu, Kimerere na
Kingoni waliowashambulia mara kwa mara.
Wanyakyusa hapo baadaye waliingiliwa na
utamaduni wa Wakinga, waliosambaa upande wa magharibi mwa nchi yao ya Ukinga
wanakopakana na Wanyakyusa.
Kanuni nyingi za Machifu wa awali wa himaya
ndogo ndogo za Kinyakyusa, zilitokana na mchanganyiko wao na Wakinga na
kusababisha utamaduni mchanganyiko.
Kwa kawaida watawala hao wenye nguvu za
kimiujiza waliishi kwa kujitenga, lakini upeo wa madaraka yao ulidhibitiwa na
mabaraza ya utawala.
Katika udhibiti huo kama mtawala akizeeka
sana au kuugua kupita kiasi, waliamini anaweza kusababisha mkosi kwa himaya
yake na kuisababishia janga la ukame litakalofanya mavuno yawe haba.
Ikifikia hali hiyo kwa Chifu kuzeeka na
kuugua mno, wale wajumbe wa baraza la utawala waliamua kumnyonga Chifu huyo ili
kuepusha mkosi kwa himaya yao.
Licha ya mfumo huo jambo lingine
walilolitekeleza kwa mpangilio wao wa Kijadi, ni kuishi kwenye jamii yenye
mafungu ya madaraja ya umri.
Mafungu hayo yaliyotokana na koo tofauti
tofauti na si koo zenye undugu, licha ya mfumo huo ambao kwa juu juu unaonekana
dhaifu lakini kwa ndani walikuwa imara.
Moja kati ya mambo ya kujivunia ya kabila
hilo ni kuweza kujilinda wasichukuliwe utumwa, japo wale ndugu zao waliowaacha
Konde kule Karonga walishawahi kufanywa watumwa.
Kwa hiyo, ukiangalia hata zile sababu zao
za kuogopa mkosi kutokana na Chifu kuzeeka mno au kuugua, ni kwa sababu ndugu
zetu hawa ni wakulima hodari wa mazao mbalimbali.
Kama unavyoyaona yalikuwa mengi, ndiyo
maana yamechukua nafasi kubwa. Lakini nadhani ni vyema tukumbushane ili tuweze
kuunganishia kutokea hapo.
Nafahamu kuwa ule muunganiko wa Malkia wa
Kinubi aliyeitwa Nyanseba ndiyo unawachanganya, hasa ukichukulia kuwa sehemu
kubwa ya Wanubi si Wabantu.
Jambo lingine walilokuwa na utaratibu nalo,
ni kuamua na kutatua migogoro kwa mashtaka ya kijadi.
Maamuzi ya aina hii hayakuwa ya shinikizo
la watawala au watu wenye nguvu za kijamii, mara nyingi walipenda ufumbuzi
upatikane kwa usuluhishi wa majadiliano na maelewano baina ya waliokoseana
wakisaidiwa na watu wengine.
Pia kutokana na ule mfumo wao wa kuishi
kwenye madaraja ya umri kijamii yasiyolazimu ndugu kuwa kwenye eneo moja, awali
hawakuwa na muendelezo wa majina ya ukoo kwa vizazi vitatu au zaidi mbele
kutokana na mfumo huo.
Kwa mtindo wao huo wa maisha na hata
utawala wa zile himaya ndogondogo, kimsingi hawakuwa walimbikizaji au wenye
tamaa ya kuhodhi mali nyingi.
Japo mara kadhaa mifarakano ilisababishwa
na kuingiliana kwenye mipaka ya maeneo yao waliyoishi.
Hawakuwa wawindaji na kama walilazimika
kufanya hivyo, ni kwa ajili ya ulinzi wa maisha na himaya ya maeneo yao.
Japo hilo halikuwafanya wawe wazembe, maana
walijilimbikizia silaha bora za kijadi kwa kujilinda endapo wangevamiwa.
Kwa kuwa himaya zao zilikuwa ndogo ndogo na
zilijumuisha wakazi ambao si wenye undugu wa mfululizo wa vizazi vya koo
zinazowiana, waliepuka sana kusafiri na kuondoka kwenye himaya kama hakuna
ulazima wa kufanya hivyo.
Na ikilazimu kusafiri, basi safari hiyo
huchukua muda mrefu zaidi kwa sababu mara kwa mara iliwalazimu kujificha na
kusoma mazingira wanayopita kama hayana uadui.
Safari hizi ninazozungumzia hapa ni zile za
kijadi za zama hizo za ujima zilizotumia muda kadhaa hadi kufika kituo cha
mwisho.
Katika ule mgawanyo wao wa kazi, ukamuaji
maziwa ulifanywa na wanaume tu wanawake walikatazwa kabisa kufanya hivyo.
Pia mwanamke hakupaswa kujipa kipaumbele
kwenye mambo ya mikusanyiko ya kijumuiya, walipaswa kuwa watiifu na
wanyenyekevu kwa mabwana zao, kubishana na mume ni jambo lililokatazwa kabisa.
Lakini hilo halikuondoa thamani yao,
mathalan, kwenye kuolewa ng’ombe walitozwa kama mahari na wakati mwingine kwa
idadi kubwa.
Kwa upande wa ufundi wa kijadi, ndugu zetu
hawa zaidi ya kutengeneza aina ya mikeka ya kikwao hawakuwa kama Wabantu
wengine waliotengeneza vyungu, mitungi, nguo, kufua vyuma au kuzalisha chumvi.
Hili linaweza kukushangaza, maana nadhani
unatambua ile sifa yao ya vyungu vya Mbeya vinavyopikiwa maharagwe.
Walijifunza baadaye usanii huo, japo watu
waliochanganyika nao na kujifunza kwao walikuwa na utata wa uwiano nao. Nawazungumzia
Wakinga ambao ndiyo kwa sehemu kubwa walifanya nao biashara ya mabadilishano ya
bidhaa.
Wanyakyusa waliwapa chakula Wakinga, nao
wakawapa silaha na zana za kilimo walizojivunia sana kuzimiliki.
Hata hivyo, licha ya kuwiana na kushirikiana
na Wakinga kwa kiasi kikubwa, walijizuia kabisa kuchanganyika nao kwa kuoana
nao.
Maana waliwachukulia wanawake wa Kikinga
kutokuwa wasafi kuolewa nao, kwa kuwa waliwaona duni kulinganisha na jinsi
wanawake zao wa Kinyakyusa walivyo.
Bado kuna mengi ya kuzungumzia kuhusu ndugu
zetu Wanyakyusa, lakini kwa leo tuishie hapa tutaendelea tena na simulizi zao kesho.
Makala haya yamehaririwa,
yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Tanzania Daima Julai 18, 2009.
Comments
Post a Comment