Featured Post

WANANCHI WAITAKA SERIKALI KUFANYIA KAZI TATIZO LA KUKATIKA UMEME KWENYE VITUO VYA USAJILI VITAMBULISHO VYA TAIFA- MTWARA

Mwenyekiti wa Mtaa wa Chiputaputa Bw. Juma Hamisi Chambeya akiwagongea muhuri wakazi wa eneo lake kwenye fomu za maombi ya Vitambulisho kuthibitisha makazi ya wananchi hao wakati wa zoezi la kuwasajili Vitambulisho vya Taifa likiendelea. Kabla ya wananchi kugongewa muhuri wa Serikali ya Mtaa wananchi kwanza wanatakiwa kujaza fomu ya maombi yenye vipengele 72 na kutoa nakala ya viambatisho vyao msingi vinavyowatambulisha kabla fomu hiyo haijapitiwa kugongwa muhuri wa Serikali ya Mtaa/Kijiji anakoishi.

Kushoto ni Bi. Sharifa Said akiwa na Bi. Zubeda Abdallah ( katikati) na Bi.Rahma Ally (kulia) wakijaza fomu za maombi ya Vitambulisho vya Taifa katika kituo cha Usajili kilichopo  Shule ya Msingi Lilungu mkoani Mtwara, wakati zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu lenye kulenga utoaji wa Vitambulisho vya Taifa likiendelea Wilaya ya Mtwara.
Bi. Asha Bakari (kushoto) na Bi. Asha Yasini (mwenye mtoto) wakazi wa Kata ya Mbaya Mashariki wakitafuta fomu zao walizojaza mwaka 2014 waliposhiriki zoezi la uandikishaji Vitambulisho  vya Taifa; ili wakakamilishe hatua ya mwisho ambayo ni kuchukuliwa alama za kibaiolojia, Picha na Saini ya Kielektroniki.
Hawa ni baadhi ya wananchi wa Mbaya Mashariki wakisubiri kujaziwa fomu za maombi ya Vitambulisho vya Taifa ili wakapigwe picha, kuchukuliwa alama za kibaiolojia na saini ya kielektroniki wakati zoezi la Usajili likiendelea kwenye Kata yao. Wakitoa huduma hiyo ni Bi. Moza Mohamedi Lukwekwe (kulia) Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbaya na Bi. Asia Abdallah Nachuma (kushoto) ambaye ni mjumbe wa Mtaa wa Mbaya. Huduma hiyo ya kuwajazia wananchi fomu za maombi ya Vitambulisho imekuwa ikitolewa kwa wananchi wote wanaofika kwenye vituo kusajiliwa na hawajui kusoma na kuandika ili kurahisha zoezi.

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeendelea na Usajili wananchi Vitambulisho vya Taifa mkoani Mtwara ambapo katika Wilaya ya Mtwara Idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza kushiriki zoezi hilo huku baadhi wakilalamikia kukaa muda mrefu kwenye vituo vya Usajili na baadhi ya mashine kutokufanya kazi.
Bwana Athumani Salum mkazi wa Kata ya Magomeni amesema “zoezi kama zoezi ni zuri ila changamoto kubwa ni kukatika kwa umeme na hivyo kusababisha wananchi tusubiri muda mrefu kiasi cha kukatisha tamaa. Kwakuwa hili ni zoezi la kiserikali kwanini Serikali isisaidie  umeme kutokatwa kwenye vituo? ”
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Bi Rose Mdami ambaye alikuwepo kituoni hapo ameeleza changamoto ya umeme ni kubwa katika vituo vingi vya usajili hata hivyo kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya wameshachukua  hatua za kutafuta magenereta ili kazi ziendelee kama kawaida.
“ si kweli kwamba mashine zote hazifanyi kazi katika mashine tulizonazo zipo baadhi ambazo zinatunza umeme muda mrefu na kwahizi ambazo hazifanyi kazi kwa kukosa umeme tunaendelea kuharakisha kupata magenereta ili kuamsha mashine ambazo zimeshindwa kufanya kazi ili wananchi wasisubiri muda mrefu” alisisitiza
Katika kituo cha Magomeni kilichopo shule ya Msingi Lilungu wananchi pia wamekutwa wakihangaika kutafuta fomu zao za usajili walizosajiliwa mwaka 2014 ambapo zoezi hilo lilifanyika kwa mara ya kwanza kwa hatua ya  kujaza fomu tu bila kupigwa picha.
Akifafanua kuhusu wananchi  hao  Bi. Rose amesema kwa wale wananchi wanaofika kwenye vituo vya Usajili na ambao walisajiliwa mwaka 2014 na kujaza fomu za maombi ya Vitambulisho vya Taifa,  pindi wanapofika kwenye vituo vya Usajili wanachukuliwa alama za kibaiolojia, picha na saini ya kielektroniki na kisha kuruhusiwa kuondoka kwakuwa taarifa zao msingi tayari zilishaingizwa kwenye mfumo tofauti na wale ambao ndio kwanza wanaanza Usajili.
Mkoa wa Mtwara unakusudiwa kusajili wananchi zaidi ya 800,000 kwa Wilaya za Mtwara, Tandahimba, Nanyumbu, Masasi na Newala. Usajili ambao unakusudiwa kumalizika mapema mwezi Machi, 2018 na kuwezesha wananchi katika mkoa huo kuanza kutumia Vitambulisho vitakavyozalishwa  katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na uzalishaji mali.


Comments